The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Demokrasia ni Sharti Au Matokeo ya Maendeleo ya Kiuchumi?

Baadhi wanaweza kusema ni sharti lakini mimi ningepinga, nikisema demokrasia ni matokeo ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi husika.

subscribe to our newsletter!

Kuna utofauti katika utekelezaji wa kanuni za kidemokrasia katika nchi na muktadha tofauti. Ingawa demokrasia, kwa kawaida, inachukuliwa kama mfumo wa utawala unaopendelea haki za binafsi, ushiriki wa kisiasa, na uwajibikaji, mfumo huo wa kujitawala pia unakabiliwa na changamoto na utata mwingi katika utekelezaji wake.

Lakini inabaki kwamba kiini cha demokrasia ni mapenzi ya wengi, huku haki za wachache zikilindwa. Tahadhari ni kwamba demokrasia inahitaji muktadha. Huwezi kuchukua mfano mmoja wa demokrasia na kuutumia kama kiwango cha nchi zote bila kuweka katika muktadha wa historia, utamaduni na maendeleo ya kiuchumi ya nchi husika. 

Baadhi wanaweza kusema kwamba demokrasia ni sharti la maendeleo ya kiuchumi lakini mimi ningepinga, nikijenga hoja kwamba demokrasia, kimsingi, ni matokeo ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi husika. 

Huku kwetu Tanzania, na sehemu kubwa tu ya Afrika, tunapenda kutumia nchi za Magharibi kama mifano mikuu ya demokrasia, lakini mara nyingi tunapuuza ukweli kwamba nchi hizo hizo hazikufuata kanuni sawa za demokrasia wanazohubiri leo hii wakati zilipokuwa zinaendeleza uchumi wao.

SOMA ZAIDI: Mwenezi Khamis Mbeto: CCM Ndiyo Baba wa Demokrasia Tanzania

Tukiwa wakweli, tutakubaliana kwamba demokrasia, katika mfumo wake safi kabisa, inaweza kuwa kikwazo kwa maendeleo. Hii ni kwa sababu kwenye uamuzi wowote, mamlaka husika itahitaji kufuata mapenzi ya wengi, hata wakati ambapo wengi hao hawapo sahihi!

Tuchukulie mfano wa taifa la Marekani, ambalo wengi wetu hulitumia kama kielelezo cha ukomavu wa demokrasia, na kuona ni namna gani demokrasia yao imekuwa ikibadilika kadiri historia na uchumi wake unavyobadilika.

Mnamo Julai 4, 1776, Waasisi wa Taifa la Marekani, ambao wao ni wengi kuliko hapa kwetu Tanzania, wanaoitwa kwa kimombo Founding Fathers, walitoa hati iitwayo The Declaration of Independence, au Tamko la Kujitawala. Kwenye hati hiyo, kuna maneno yasemayo:

We hold these truths to be self-evident, that all men are created equal, that they are endowed by their Creator with certain unalienable Rights, that among these are Life, Liberty and the pursuit of Happiness.

Kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, maneno haya yanamaanisha: Tunasimama kwa ukweli huu kuwa wazi, kwamba watu wote wameumbwa sawa, kwamba wamejaaliwa na Muumbaji wao Haki fulani zisizoweza kuondolewa, miongoni mwa hizi ni Maisha, Uhuru na harakati ya Furaha.

SOMA ZAIDI: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Miaka 63 ya ‘Uhuru wa Migogoro’

Lakini tujiulize, “watu” waliokuwa wanazungumziwa kwenye tamko hilo ni watu gani? Ilikua inahusu raia wa Kimarekani, ndiyo, lakini je, ni nani kwa wakati huo alikua anahesabika raia mwenye haki zote za kiraia? Jibu ni wale wanaume weupe wanaomiliki mali. 

Katika majimbo mengi ya Marekani, tunasoma katika historia, uraia kwa kawaida ulikuwa unawahusu wamiliki wa mali weupe wa kiume. Hii inamaanisha kuwa wanaume weupe tu ambao walimiliki kiasi fulani cha mali, au walikutana na sifa maalumu za mali, walitambuliwa kama raia wenye haki kamili ya kushiriki katika mchakato wa kisiasa.

Wanawake, hata wale weupe na wanaomiliki mali, hawakupewa haki zote za kiraia ambazo ni pamoja na haki ya kupiga kura na kuchaguliwa. Watu weusi hawakua na haki zozote za kiraia na walichukuliwa kama mali za kumilikiwa. 

Baadhi ya majimbo yalikua yanataka mtu awe na kigezo cha ziada cha kua Mprotestanti ili kupewa haki zote za kiraia. Kwa muda mrefu, watu Weusi walitumika kama mali za Wazungu ili kukuza uchumi wa nchi. 

Ikumbukwe kwamba mara pekee katika historia ya Marekani waliopigana vita ya wenyewe kwa wenyewe, iliyoanza mwaka 1861 na kuisha mwaka 1865, ilikuwa ni kati ya majimbo ya Kusini yaliyotaka kulinda “haki” yao ya kumiliki watumwa na majimbo ya Kaskazini yaliyotaka kuondokana na utaratibu huo!

SOMA ZAIDI: Je, Matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Yanakinzana na Yale ya Demokrasia ya Vyama Vingi?

Hapa Tanzania, kwa hiyo, ukiangalia tulipo leo ni dhahiri kuwa tuko mbali zaidi kuliko Marekani ilivyokuwa mwaka 1776 na kwa miongo mingi baada ya hapo. Sisemi kwamba tusiige mazuri ya wenzetu, la hasha! Ninachojaribu kuhimiza ni kwamba tutambue pia demokrasia ni hatua. 

Ni rahisi kusema kwamba hizi nchi za Magharibi ziliendelea kwa sababu ya demokrasia, ila uhalisia ni kwamba demokrasia na utawala kwenye nchi hizo ulikua unabadilika kutokana na hatua za kimaendeleo walizokua wanapitia. 

Kwa nchi kama Tanzania, ambayo inaendelea, itatuwia vigumu kubeba demokrasia kama inavyopatikana kwenye nchi za Ulaya. China, kwa mfano, imeweza kupiga hatua ndani ya miongo michache kwa kuchagua utaratibu tofauti wa kiutawala, ule wa kua na Serikali yenye nguvu na uwezo wa kufanya maamuzi.

Nihitimishe safu hii kwa kusema tu kwamba demokrasia nayo ni utamaduni. Hata tulazimishe vipi hatuwezi kuwa na mfumo wa kiutawala ambao ni kinyume na jinsi sisi wenyewe tulivyo kwenye ngazi za chini, yaani ngazi za mtu mmoja mmoja, familia, na jamii. 

SOMA ZAIDI: Afrika Na Demokrasia Bado Mguu Ndani, Mguu Nje

Viongozi wanatokana na jamii zetu hizi hizi na si malaika wanaoshushwa kutoka mbinguni. Hivyo, tutambue kwamba mifumo tuliyonayo haiwezi badilika mpaka sisi kama jamii tubadilike. 

Na madaliko siku zote, hususani yale ya kiutamaduni na kimawazo, hayaji kwa haraka ile tunayoitegemea sisi. Mwisho wa siku tunarudi palepale, kwamba demokrasia ni utawala wa wengi na jinsi wengi walivyo ndivyo demokrasia yetu itaenda.

​​Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au Twitter kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *