The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Miaka 63 ya ‘Uhuru wa Migogoro’

Kwa kiwango fulani migogoro nchini DRC imekuwa ikichochewa na wakolini wake wa zamani na mataifa mengine ya Magharibi.

subscribe to our newsletter!

Nimefuatilia historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) tangu nikiwa shule ya msingi pasipo kupata picha kamili kuhusu chanzo cha migogoro inayoikumba nchi hiyo  kila uchao na nini inaweza kuwa suluhu yake ya kudumu. 

Katika mwongo takribani mmoja ambao nimekuwa nikitafiti migogoro barani Afrika kama sehemu ya kazi yangu ya uhadhiri, nimezidi kupata ukakasi juu ya chanzo hasa cha migogoro inayoikumba nchi hiyo ya Afrika ya Kati na Mashariki ambayo zamani iliitwa Freestate, Belgian-Kongo, Leopoldville, Kongo-Kinshasa au Zaire. 

Kuna siku nilifikia kujiuliza je, inaweza kuwa ni idadi kubwa ya wananchi wanaoishi katika nchi hiyo ndiyo inaweza kuwa tatizo? Nikawaza, ni uhaba wa ardhi ya kilimo, malisho na ujenzi? Nikasema au ni mfumo mbaya wa siasa na utawala walioachiwa na mfalme Leopold na wakoloni Wabelgiji ndiyo unaleta shida? 

Katika utafiti wangu wa hivi karibuni, nimebaini kuwa nakaribia kupata majibu ya maswali yangu ya msingi. Ingawa utafiti bado unakamilishwa, nimeamua nifanye uchambuzi wa masuala ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika kujadili hali ya kisiasa nchini DRC.

Kwa asiyejua historia ya DRC, hii ni nchi iliyopo barani Afrika katika eneo la Afrika ya Kati, ambayo kutokana na kupakana na nchi kadhaa za Afrika Mashariki pia inajitanabaisha na Afrika Mashariki kiasi cha kuamua kuomba uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukubaliwa mnamo Julai 11, 2022. 

DRC ni nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika ikizidiwa tu na Algeria. DRC ina watu wapatao milioni 108.4, idadi ambayo si ya kutisha katika taifa lenye ukubwa wa kilometa za mraba 2, 244, 858, ikiwa ni zaidi ya mara mbili na nusu ya ukubwa wa Tanzania, ambayo ina kilomita za mraba 945,087. 

Kwa jiografia na ukubwa wake, DRC imebarikiwa kuwa na nchi jirani nyingi kuliko nchi nyingi, ikipakana na takribani nchi tisa: Tanzania, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo na Angola upande wa Cabinda. 

Kwa hakika, kama ujirani huu wote ungekuwa ni mwema tupu, DRC isingewahi kupata matatizo na isipate msaada!

Kwa upande wa utajiri wa rasilimali, DRC ni kinara. Aidha, kuna madini ya kila aina yanayopatikana katika nchi hiyo. Aidha, wanayo ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo na wana uoto wa asili usiofanana na nchi nyingi duniani. 

Kwa mujibu wa taarifa za kimazingira, misitu ya DRC inapatikana katika nchi nyingine moja tu duniani na kuifanya nchi hii kuwa chanzo kikubwa cha hewa safi na mvua. 

Kunyemelewa na Wazungu

Kihistoria, eneo linaloitwa DRC hivi leo lilianza kunyemelewa na Wazungu tangu miaka ya 1800. 

Kwa mfano, mfalme Leopold II aliunda na kutuma kikosi cha kuchunguza eneo la mto Kongo katika mwaka 1876 na ikapelekea kuundwa kwa agizo lake kwa umoja wa kimataifa kuhusu Kongo kutokana na mto Kongo ambao wachunguzi waliukuta na kuupenda sana kutokana na ukubwa wake. 

Hii ndiyo sababu ilipofika wakati wa mkutano wa Berlin wa kugawana Afrika uliofanyika kuanzia mwaka 1884 hadi 1885, mfalme Leopold II wa Ubelgiji alichagua kunyakua Kongo Freestate kama eneo lake la kikoloni mahsusi kwa ajili ya kulima zao la mpira na kusafirisha likiwa ghafi kwenda Brussels. Tangia hapo, Wabelgiji hawakutaka kuiachia ardhi ya DRC mpaka mwaka 1960.

SOMA ZAIDI: Jumuiya ya Madola Imepoteza Dira, Muelekeo. Hiyo Inaiathiri Vipi Afrika?

Kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine mengi, wananchi wa Kongo walianzisha mapambano ya kuikomboa Kongo mara tu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. 

Mapambano yalipelekea mkutano kati ya mamlaka za kikoloni na viongozi wanasiasa wa Kongo mjini Brussels kati ya mwezi Januari na Februari mwaka 1960 kwa ajili ya kujadili hatma ya kisiasa ya Kongo kuelekea uhuru. Mambo makubwa mawili yalikubalika: 

Kwanza, ilijadiliwa na kupitishwa rasimu ya Katiba ya Mpito ya Kongo itakayotumika mara baada ya Wabelgiji kukabidhi nchi kwa Wakongo hadi watakapokuwa tayari kuandika Katiba Mpya ya Kongo. 

Pia, walipanga tarehe ya siku ya uhuru na kabla yake ilipaswa kufanyike uchaguzi kujaza nafasi za wabunge (137) na seneti ya watu 87. Kufikia tarehe Mei 19, 1960, Katiba ya DRC ilichapishwa na kutangazwa rasmi na kufungua ukurasa wa uchaguzi wa wabunge, Maseneta, Waziri Mkuu (ambaye ataongoza Serikali) na Rais (asiye na madaraka ya kiserikali).

Mnamo Mei 22, 1960, kulifanyika uchaguzi kuchagua viongozi wa kitaifa ambapo Wakongo wote wenye umri kuanzia miaka 21 waliamriwa kisheria kupiga kura. Kutokana na uchaguzi huo, kulionekana mpasuko mkubwa wa kijamii katika nchi ya Kongo.

Kwanza, kura ziligawanywa sana zikifuata kabila na majimbo ya wagombea kiasi kuwa hakuna chama kiliweza kupata kura za kuunda Serikali peke yake. Kutokana na hali hiyo, Chama cha Vuguvugu la WaKongo (MNC) cha Patrice Emery Lumumba kilichozoa viti 38 kati ya 137 vya ubunge kililazimika kutafuta vyama vingine kama PSA na CEREA ili kuwafanya wawe na uwingi wa viti kutosha kuunda Serikali ambapo Patrice Lumumba alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza.

Ili kuweza kukubalika katika Seneti, Lumumba alihitaji kuungana pia na mwanasiasa wa mrengo wa kulia Joseph Kasavubu ambaye alikuwa ametishia kuimega Kongo na kuanzisha taifa la watu wa Pwani ya Bas-Kongo alikokuwa anakubalika endapo asingechaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo. 

‘Ndoa’ ya Lumumba na Kasavubu iliwezesha Seneti kuipitisha Serikali ya Lumumba na kumchagua Kasavubu kuwa Rais na mkuu wa Nchi. Mwezi mmoja tu baadaye, mfalme Baudoin I wa Ubelgiji aliwakabidhi madaraka viongozi wapya wa Kongo pasipo maandalizi yoyote mnamo Juni 30, 1960. Wakati wa kupokea madaraka, wastani wa umri wa mawaziri wapya ulikuwa ni miaka 35.

Harakati za kujitenga

Akiwa amezaliwa mwaka 1925, Patrice Emery Lumumba mwenyewe alikuwa bado kutimiza miaka 34 wakati akiapa kuwa Waziri Mkuu. Hata waliokuwa na ukomavu wa umri, elimu yao ilikuwa kwa wastani ni shule ya sekondari pasipo uzoefu wowote wa kiuongozi na kiutawala. 

Mbaya zaidi, hamu ya kila Mwafrika kutaka kupigiwa saluti na mizinga 21 ilipelekea wanasiasa wengi chipukizi kuanza kutangaza uhuru wa majimbo walikozaliwa na kudai wao si sehemu ya taifa la Kongo huku kukiwa na mkono wa wakoloni katika hilo. 

Ni kwa sababu hizo, siku tano tu baada ya uhuru, Jeshi la Kongo, ambalo bado lilikuwa na maafisa Wazungu Wabelgiji, lilifanya uasi na kusababisha Serikali ya Ubelgiji kutuma vikosi kuja kulinda raia wake dhidi ya vurugu huku pia wakiunga mkono kujitenga kwa jimbo la Katanga chini ya Moise Tshombe na jimbo la Kasai Kusini chini ya Albert Kalonji.

SOMA ZAIDI: Nini Maana ya Ukimya wa Afrika Kwenye Mgogoro wa Urusi na Ukraine?

Kwa kweli, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ikifadhiliwa na Wazungu. Hata juhudi za Kasavubu na Lumumba kuomba msaada toka Umoja wa Mataifa ili kurejesha hali ya Kongo iliyo moja hazikuzaa matunda na vurugu ziliendelea na kuua watu wanaokadiriwa kufikia  500,000 kwa uchache. 

Katika harakati za Serikali ya Lumumba kuomba msaada kutoka Urusi ya wakati huo, Rais Kasavubu (ambaye alikuwa ni muumini wa itikadi ya ubepari) alimgeuka Waziri Mkuu na kutangaza kumfukuza kazi jambo ambalo Lumumba hakulikubali na kutangaza kumfukuza kazi Rais.

Ni katika hali hiyo ya vurugu kati ya Rais na Waziri Mkuu ndipo aliibuka Mkuu wa Majeshi wa wakati huo, Kanali Joseph Mobutu Sese Seko ambaye alitangaza kuwasimamisha kazi Rais na Waziri Mkuu mnamo tarehe Septemba 14, 1960. 

Badala yake, aliwaita vijana wahitimu na wanafunzi wa Chuo Kikuu na kuwapatia uwaziri ili kutengeneza baraza la mawaziri. 

Kwa upande wake, Lumumba aliwekwa kizuizini lakini akatoroka na akiwa safarini kuelekea Stanleyville kwenda kuunda vuguvugu jipya la mapambano alikamatwa, kuteswa na kutupwa jela kabla ya kuhamishiwa Katanga ambakoaliuawa kinyama mnamo Januari 17, 1961. 

Mwezi uliofuata, jeshi lilimrejesha Kasavubu katika nafasi ya urais lakini sonona, migogoro na vurugu ziliendalea kila siku zilizozidi kupita.

Hatimaye, Mobutu aliamua kutumia fursa ya ugomvi mwingine kati ya Rais Kasavubu na Waziri Mkuu mpya Moise Tshombe kujitangaza rasmi kuwa Rais wa Kongo kuanzia mwaka 1965 na baadaye kubadilisha jina la nchi na kuiita Zaire mnamo mwaka 1971. 

Rais Mobutu aliishi na jina la Zaire hadi alipotimuliwa rasmi kutoka Ikulu ya Kinshasa na Laurent Desire Kabila ambaye alisaidiwa na nchi jirani za Uganda na Rwanda kuingia Ikulu ya nchi hiyo. 

Tshisekedi na DRC mpya?

Ilikuwa ni Rais Laurent Kabila aliyerejesha jina la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa bahati mbaya walinzi wakiitwa Kadogoo waliotumwa na Uganda na Rwanda kumsindikiza Rais Kabila hadi Ikulu ya Kinshasa ndiyo waliomgeuka baadaye na kumuua mnamo January 16, 2001.

SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?

Kufuatia kifo cha Laurent Kabila, ilibidi apatikane mtu atakayeweza kuwaunganisha Wakongo na ndipo mmoja katika watoto kumi wa marehemu alipojitokeza kutoka ughaibuni alikokuwa akipatiwa mafunzo ya kijeshi na kurejea Kinshasa kuja kuchukua dola. 

Meja Jenerali Joseph Kabange Kabila alitawazwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo Januari 2001 na aliendelea kuwa Rais wa nchi hiyo pamoja na vurugu, mikasa na misukosuko hadi alipong’atuka na kupelekea kuchaguliwa kwa Felix Tshisekedi kuwa Rais wa tano wa DRC mnamo Januari 24, 2019. 

Ni katika hali hii watu wengi wanasubiri kujionea endapo Rais huyu atadumisha demokrasia ya uchaguzi na kuachia madaraka au ataendeleza ubabe wa kukataa kung’atuka muda wake wa kipindi cha urais utakapokwisha. 

DRC inapaswa kufanya uchaguzi wake mkuu ujao mnamo Disemba 20, 2023. Kwa ujumla, Kongo imekuwa katika ‘Uhuru wa Migogoro’ kwa miaka 63 tangu 1960. 

Wananchi wake hawajawahi kupata fursa ya kuchagua na kufanya kazi na viongozi wao. Je, visababishi vya vurugu na migogoro vitaisha na ni nini hasa? Mpaka lini?

Mungu ibariki Afrika na watu wake wote!

Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *