Jumuiya ya Madola Imepoteza Dira, Muelekeo. Hiyo Inaiathiri Vipi Afrika?

Kuwemo kwa nchi zenye nguvu kiuchumi kama India, Afrika Kusini na Nigeria – kuzitaja chache – mtu ungetarajia Jumuiya ya Madola ingekuwa na uwezo wa kushinikiza mfumo mpya wa kiuchumi duniani. Hali haiko hivyo.

Mnamo Juni 24 na 25, 2022, ulifanyika mkutano wa kilele wa Viongozi Wakuu wa Serikali wa nchi za Jumuiya ya Madola, ambao kwa kimombo unajulikana kama Commowealth Heads of Government Meeting, au CHOGAM, kama ambavyo mkutano huo umekuwa ukiripotiwa na vyombo vya habari. Kwa ufupi, mkutano kama huu hufanyika kila baada ya miaka miwili.

Mkutano huo wa nchi 54 ulikuwa wa pili kufanyika katika bara la Afrika baada ya ule uliofanyika nchini Uganda mwaka 2007. Wakati sehemu kubwa ya nchi hizo ni Jamhuri, kungali na nchi kama 14 katika pembe mbali mbali za dunia ambazo kwa kuwa si Jamhuri kikatiba, Ufalme wa Uingereza, na hapa kwa maana ya Malkia Elizabeth II, anakuwa mkuu wa taifa wa nchi hizo akiwakilishwa na mtu anayemteuwa kuwa mkuu wa taifa.

Malkia Elizabeth II ametmiza miaka 70 tangu alipotawazwa kukalia kiti hicho, kufuatia kifo cha baba yake Mfalme George VI.

Wapo wanaouangalia, au waliokuwa wakiuangalia, utaratibu wa baadhi ya nchi kukataa kuwa Jamhuri kuwa sawa na kubakia na  sehemu ya mnyororo wa  ukoloni.

Nchi hizo, hata hivyo, zimekuwa zikijitetea kwamba utaratibu huo unalenga kuendeleza mafungamano yao na uhusiano mwema na Uingereza, taifa lililowahi kuzitawala nchi hizo. Baadhi ya wakosoaji, wakionesha kutokuridhishwa na utetezi huo, wameuita mtazamo huo aina fulani ya kasumba ya kutojitambua.

Barani Afrika, nchi nyingi ziliamua kuwa Jamhuri na kuwa na viongozi wao wakuu wa nchi, wakati zinapandisha bendera siku ya Uhuru au muda mfupi baadae. Miongoni mwa nchi hizo ni Tanzania na Kenya.

Uganda iliendelea kuwa na mfumo wa Ufalme lakini kiongozi mkuu wa taifa akiwa si Malkia wa Uingereza bali Mfalme wao Kabaka Mutesa II. Ufalme nchini Uganda ulifikia kikomo wakati Waziri Mkuu Milton Obote alipomuangusha Kabaka 1966, baada ya kuzuka tafauti za kisiasa. Uganda ikabadilisha Katiba na kuwa Jamhuri.

Taifa la karibuni kabisa, koloni la zamani la Uingereza, kuamua kuwa Jamhuri, ni Barbados katika kanda ya Caribbean, lililochukua hatua hiyo hapo Novemba 2021. Hisia za kuwa Jamhuri sasa zimeongezeka katika maatifa mengine yaliobakia, kikiwemo kisiwa cha Jamaica. Mataifa haya, kwa ujumla wao, hayazidi 14.

Mwisho wa himaya?

Ufalme nchini Uingereza bila shaka umeanza kutambua kwamba enzi yake ya kuendelea kuwa himaya ambayo imeendelea kuporomoka inamalizika kwa kupoteza nchi zilizobakia katika mfumo huo wa Malkia kubakia kuwa mkuu wa taifa.

Akiwahutubia viongozi wakuu wa nchi na Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, Mwana wa Ufalme (Prince) Charles alirudia tena maneno aliyoyatoa wakati wa Sherehe ya Barbados kuwa Jamhuri, kwamba ni haki ya kila nchi kujiamulia yenyewe inataka kuwa Jamhuri au Katiba inayaoupa heshima Ufalme wa Uingereza ubakie mkuu wa taifa hilo husika.

Kuna nchi kama New Zealand na Australia ambazo bado mkuu wa taifa ni Gavana akimuakilisha Malkia. Lakini  vuguvugu la kutaka kuwa Jamhuri nchini Australia limezidi kupata nguvu. Mmoja wa wanaounga mkono vuguvugu hilo ni waziri wake mkuu aliyechaguliwa hivi karibuni Anthony Albanese.

Matamshi ya Prince Charles anayetarajiwa kumrithi mama yake na kuwa Mfalme, na kupata nguvu vuguvugu la kujiengua nchi zilizobakia na kuwa Jamhuri, bila shaka yanaashiria kwamba Ufalme wa Uingereza unatambua kwamba upepo wa mabadiliko sasa umeanza kuvuma  kuelekea Kasri la Buckingham ( Makao Makuu ya himaya yake).

Hata hivyo, bado Malkia anaendelea kubaki kuwa Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

Malengo ya awali

Dhamira hasa ya makoloni ya zamani kuwa wanachama wa Jumuiya ya Madola baada ya uhuru ilikuwa ni kuwa na ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara na kiutamaduni na mkoloni wao wa zamani. Zingatio kubwa wakati huo lilielekezwa pia katika sekta ya elimu, wakati nchi hizo zikiwa bado changa.

Mvutano wa madola makubwa na kile kilichojulikana kama Vita Baridi baina ya Magharibi na Mashariki, hisia za kujikomboa baada ya karne na ushei za utawala wa kikoloni Afrika na Asia, ulisababisha nchi nyingi kujiamulia pia mrengo wao wa kisiasa baada ya uhuru. Lakini ushirikiano na mkoloni wa zamani Uingereza ukasalia, ukidumishwa na jukwaa hilo la mkusanyiko wao katika Jumuiya ya Madola.

Nchi nyingi wanachama wakati ule ziliweza kuwa  na msimamo mmoja kisiasa na kuikabili Uingereza kuhusu suala la uhuru na ukombozi wa Rhodesia (Zimbabwe) na Afrika Kusini, zikiongozwa na Tanzania.

Viongozi wa nchi wanachama walijiamini na kuikabili Uingereza ibadili muelekeo wake kuhusu utawala wa Wazungu wachache nchini Rhodesia ambapo 1965 Ian Smith alikuwa amejitangazia Uhuru na Uingereza ikashindwa kuchukua hatua yoyote. Halikadhalika, juuu ya kupigania haki ya Waafrika walio wengi nchini Afrika Kusini ambapo Uingereza ikiukingia kifua utawala wa makaburu.

Miaka ya 1980 Waziri Mkuu wa Uingereza Margeret Thacher aliitetea wazi wazi sera ya nchi yake kuelekea Afrika Kusini na kuweka mbele masilahi ya makampuni ya kibiashara ya Uingereza.

Kwa muhtasari, wanachama wa Jumuiya ya Madola walikuwa na nguvu ya kukabiliana na mkoloni wa zamani, ishara ya kuwa huru na kujiamulia kile wanachokiona ni bora kwao na kwa masilahi ya pande zote mbili. Yote yalitokana na ujasiri wa viongozi waliokuweko.

Hali ya sasa

Jumuiya ya Madola hivi sasa imepoteza dira na muelekeo. Imegeuka  kuwa Jumuiya ambapo Uingereza inatafuta njia za kuimarisha ushirikiano kwa kuzingatia zaidi masilahi yake ya kibiashara na kiuchumi badala ya masilahi ya pamoja kama Jumuiya.

Hili linaonekana kutokana na kukubaliwa kwa uanachama zile nchi ambazo hazikuwa makoloni ya Uingereza hapo kabla. Msumbiji mwaka 1995. Rwanda mwaka 2009. Na  Gabon na Togo zilizojiunga katika mkutano wa Kigali wa hivi juzi, zikiwa wanachama wapya na kuongeza jumla ya wanachama kufikia 56.

Msumbiji ilikuwa koloni la Ureno na mwanachama wa jumuiya inayoyakusanya mataifa yaliotawaliwa na Ureno na yanayozungumza Kireno, inayofahamika kama Lusophone.

Togo na Gabon ni makoloni ya zamani ya Ufaransa na ni wanachama pia wa Francophonie, jumuiya ya nchi zinazozungumza Kifaransa.

Tutaona Uingereza na Ufaransa sasa zimekuja na mkakati mwengine, nao ni kuzijumuisha nchi ambazo hazikuwa makoloni yao, ikiwemo Rwanda iliyotawaliwa na Ubeligiji, Msumbiji na Guinea ya Ikweta inayozungumza Kihispania.

Rwanda imepewa pia nafasi ya waziri wake wa zamani wa mambo ya nchi za nje Louise Mushikiwabo kuwa Katibu Mkuu wa Francophonie.

Ushirikiano wa dhati au faida za kiuchumi?

Kwa mtazamo huo, hivi sasa lengo la wakoloni hao wa zamani ni kujitanua zaidi kibiashara na kiuchumi, kwa kile kinachoitwa biashara huria na utandawazi. Lakini swali ni nani anayenufaika zaidi?

Kuna hatari ya kukosekana usawa katika uhusiano huo wa kibiashara na kiuchumi, kwa Uingereza kujadiliana na nchi moja moja kwa masilahi yake, hali inayoweza kusababisha kukosekana kwa msimamo wa pamoja wa nchi wanachama.

Kuwemo kwa nchi zenye nguvu kiuchumi kama India, Singapore, Afrika Kusini na Nigeria – kuzitaja chache – mtu ungetarajia Jumuiya ya Madola ingekuwa na uwezo wa kushinikiza mfumo mpya wa kiuchumi duniani. Hali, hata hivyo, ni tofauti sana na matarajio hayo.

Masilahi ya kibinafsi  na ukosefu wa viongozi wenye usemi ni udhaifu mwengine, hali inayoonekana pia katika jumuiya nyengininezo.

Nikitafakari inanikumbusha kupotea uzito wa awali wa jumuiya ya nchi zizofungamana na upande wowote ulioundwa 1961 mjini Belgrade, kufuatia mkutano wa mkutano wa Bandung nchini Indonesia mwaka 1955, ambayo viongozi wake waasisi – Jawaharlal Nehru wa India, Josip Broz Tito wa iliokuwa Yugoslavia, Ahmed Sukarno wa Indonesia – walikuwa sauti ya kutegemewa na nchi zinazoendelea.

Viongozi hawa baadaye waliungana na kina Gamal Abdel Nasser wa Misri, Julius Nyerere wa Tanzania, Modibo Keita wa Misri, Lee Kuan Yew wa Singapore, Kwame Nkrumah wa Ghana na Ahmed Sekou Goure wa Guinea kuipa nguvu jumuiya hiyo.

Kwa jumla, mkutano wa Jumuiya ya Madola mjini Kigali, umemalizika pakisisitizwa sula la amani na kuimarisha hali za kimaisha za wakaazi wote wa nchi za Jumuiya ya   Madola, kuipa motisha sekta binafsi ili kuunda nafasi za kazi kwa vijana wakiwa na ujuzi wa kiufundi wa hali ya juu.

Kwa mtazamo wangu, hiyo ni changamoto kubwa. Kilichoepukwa kujadiliwa kwenye mkutano huo ni suala zima la demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.

Wengi watakuwa wakisubiri kuona ni hatua gani itakuwa imefikiwa katika yale yaliopitishwa pale utakapofanyika mkutano mwengine wa kilele wa CHOGAM katika kisiwa cha Samoa, kusini mwa bahari ya Pasifik chenye wakaazi laki mbili.

Mohamed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Anuani yake ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia Twitter @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Mohammed AbdulRahman

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved