Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro ameteua kamati ya hamasa kwa timu za taifa ambazo zitakuwa zimefuzu kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.
“Kamati hii itakuwa na jukumu la kuhamasisha mashabiki wa michezo ndani na nje ya nchi kujitokeza kuzishangilia na kuziunga mkono timu za taifa pamoja na kuratibu hafla maalum ya harambee ya kuzichangia timu za taifa inayotarajiwa kufanyika tarehe 10 Januari 2024 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa hoteli ya Rotana,” inaeleza taarifa ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikitaarifu kuwa mgeni rasmi siku hiyo atakuwa Waziri Mkuu Kasssim Majaliwa.
Kamati imeundwa wakati timu ya taifa ya soka ikiwa katika maandalizi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) zitakazofanyika kuanzia Januari 13 nchini Ivory Coast. Fainali hizo zilisogwezwa mbele kutoka Juni mwaka jana kutokana na hali ya hewa ya Ivory Coast ya wakati huo.
Tofauti na kamati nyingine nyingi zinazoteuliwa kwa ajili ya timui ya taifa, hasa ya mpira wa miguu, hii ya sasa imepokelewa kwa hisia tofauti, pengine kutokana na kujumuisha wasanii wa vichekesho na watu ambao wamejitangaza hadharani kuwa ni “machawa” wa baadhi ya watu maarufu au wanasiasa.
SOMA ZAIDI: Kila la Heri Maandalizi ya Stars AFCON 2023
Lakini wapo pia ambao wamejenga hoja kuwa hamasa ya timu hujengwa na kocha, wengine wakisema cha muhimu ni kuiandaa timu vizuri kwa kila kitu kama hamasa kwao ya kurejesha walichofanyiwa.
Kamati zimekuwa zikiundwa kila mara, lakini ufanisi wake umekuwa hauonekani zaidi ya wajumbe wa hizo kamati kudai haki ya kuwa sehemu ya timu wakati zinaposafiri kwenda nje ya nchi kucheza mechi zake, au kutumia hiyo nafasi ya ujumbe kwa maslahi mengine binafsi.
Pia zipo kamati za kujitolea za waandishi wa habari, kama ile iliyoundwa mwaka 2021 ya kutaka timu ya taifa ya soka irudi tena Cameroon kucheza Afcon baada ya kufuzu kwa mara ya pili mwaka 2019.
Kamati ambayo nakumbuka ilikuwa na ufanisi mkubwa ni ile iliyoundwa na wizara katikati ya miaka ya tisini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa Stars. Kamati hiyo ilikuwa chini ya mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi na mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji, akiwa makamu mwenyekiti.
Wakati huo, mpira wa miguu haukuwa na fedha wala udhamini wa kiwango cha sasa na hivyo kamati ya Mengi na Dewji iliundwa kwa wakati muafaka wa kusaidia kuondokana na changamoto hiyo ya kkifedha na ilifanya hivyo.
SOMA ZAIDI: Michezo ni Muhimu Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa Mafanikio
Kwa timu ya taifa ambayo hata jezi ilitegemea za msaada, kamati ya Mengi ilikuwa jibu; kwa timu ambayo malazi yalikuwa hosteli ya Jeshi la Wokovu, kamati ya Mengi ilikuwa jibu; kwa timu ambayo hata viatu vya wachezaji havikuwepo, kamati ya Mengi ilikuwa jibu; kwa timu ambayo wachezaji walikuwa wakikopwa posho, kamati ya Mengi ilikuwa jibu; kwa timu ambayo ilikuwa inaokoteza makocha kutokana na ukata, kamati ya Mengi ilikuwa jibu; na kwa timu ambayo nauli ya kwenda nje ilikuwa shida kupatikana, kamati ya mengi ilikuwa jibu.
Ilikuwa ni kamati muafaka iliyopewa majukumu kulingana na kipindi na changamoto zilizokuwepo na ilitekeleza majukumu yake kikamilifu. Ni kwamba timu ndiyo iliyoshindwa kupata matokeo ya kuivusha kwenda fainali za Afrika na Kombe la Dunia.
Ipo kamati nyingine iliyofanya kazi kwa ufanisi lakini matokeo hayakuwa mazuri. Hii ni ile iliyoundwa kwa ajili ya timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa na wajumbe kama Salim Abdallah “Try Again”, Nassor Bin Slum, Abdallah Bin Kleb na wengine, ambayo ilifanya kazi kubwa ya kuhamasisha michango kwa vijana hao wadogo ambao baadaye walitolewa na Congo Brazaville.
Pengine hii ya sasa ni kamati tofauti na hizo za Mengi na Try Again au zile nyingine za akina Godson Karigo na Haji Sunday Manara kwa kuwa hii hailengi timu moja ya taifa, bali zote na ndio maana taarifa ya wizara haitaji mashabiki wa soka, bali mashabiki wa michezo.
SOMA ZAIDI: Huu ni Wakati Muafaka Kuanzisha Wakala wa Viwanja Vya Michezo
Lakini timu ambayo inaangal;iwa zaidi kwa sasa ni timu ya taifa ya soka ambayo itasshiriki fainali hizo za Afcon nchini Ivory Coast kuanzia wiki ijayo. Kama wizara ingekuwa na mawasiliano mazuri na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), basi angalau kungekuwa na mikakati ya pamoja na jinsi ya kuhamasisha mashabiki.
Kwanza timu imeshaondoka zake kwenda Misri ambako imeweka kambi kiujiandaa na fainali hizo kabla ya kwenda Ivory Coast ambako fainali zitaanza Januari 13. Ni dhahiri kuwa kamati iliyoundwa haitakuwa na mkakati mkubwa kwa ajili ya kutekeleza jukumu hilo, ikizingatiwa kuwa Ivory Coast ni mbali na hakuna jumuiya kubwa ya Watanzania au watu kutoka Afrika Mashariki wanaoweza kuhamasishwa kujitokeza viwanjani.
Pia imekuwa shida kuimilikisha timu kwa wananchi. Ni kama vile Taifa Stars ni taasisi inayojitegemea yenye majukumu yake binafsi yasiyotegemea wananchi. Yaani, mechi za kufuzu ni tofauti na hizi za fainali na hivyo mkakati wake ni lazima uwe tofauti. Ilikuwa muhimu kwa wachezaji wote wa Taifa Stars kuja kwanza Tanzania kuanzia kambi hapa na baadaye kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kuagwa rasmi.
Ni vitu vidogo lakini muhimu kwa ajili ya kuirudisha timu kwa wananchi na kuwapa wachezaji hisia za taifa wanalolitumikia. Baadhi ya wachezaji ni wale waliozaliwa na kukulia nje ila wana asili ya Tanzania. Hawa walitakiwa waletwe kwanza hapa nchini badala ya kupitiliza Misri.
SOMA ZAIDI: Tufurahie Uenyeji AFCON 2027 Tukisuka Mikakati
Hata kama walikuja, kulifanyika jitihada gani kuhakikisha wananchi wanawaona wakicheza angalau mazoezi. Mataifa makubwa kama Brazil, hutoa siku moja ya mazoezi kabla hya mashindano makubwa kwa ajili ya wananchi kwenda kuiona timu yao. Na siku hiyo huwa si mazoezi ya mbinu bali ya kawaida.
Hii ni sehemu tu ya mikakati ambayo TFF ilitakiwa iwe imeiarifu serikali, ili waziri ajue anapoiteua kamati itaingia katika programu gani ya kijamii au ya masoko ya shirikisho hilo ili kufanikisha kazi ya kamati.
Morocco ilipata sifa sana baada ya wananchi wake kushukua takriban asilimia 40 ya watu walioingia uwanjani kushuhudia mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar. Zikiwa zimesalia siku chini ya kumi kabla ya kuanza fainali hizo, hakukuwa na mkakati wowote wa kuhakikisha Watanzania wanachukua angalau asilimia 10 ya mashabiki watakaoona mechi tatu za makundi za Taifa Stars.
Huu ni mkakati ambao idara za habari na masoko za TFF zilitakiwa kuwa nao, angalau zingevuta hata wasafirishaji kujiunga kwenye mkakati huo.
Hata uhamasishaji wa ununuzi wa nakala za jezi (replica) haupo kabisa, ingawa zilitambulishwa katika moja ya sherehe za kawaida za TFF. Wahusika wako Misri wakifanya kazi ya kuwahoji wachezaji, badala ya kufikiria Watanzania wataiungaje mkono timu.
SOMA ZAIDI: Kocha Adel Amrouche Awajibike Kwa Watanzania
Bila ya mkakati wa masoko au wa uhamasishaji ulioandaliwa na TFF, kamati ya hamasa inaweza isifanye kazi kwa ufanisi na kuishia kukosolewa, kudhihakiwa na kutukanwa kutokana na aina ya baadhi ya watu waliomo kumbe hawakuwa na nyenzo ya kuwasaidia.
Bila ya shaka, kazi kubwa ya kamati itakuwa ni kuizungumzia hafla ya Januari 10 kwa kuwa Waziri Mkuu yupo, na nyingine itakuwa ileile iliyofanywa na baadhi ya kamati zilizopita ya kuitisha mikutano na waandishi wa habari eti kwa ajili ya kuwaambia Watanzania umuhimu wa mechi za timu za taifa.
Na iwapo kamati haitafanikiwa katika hatua ya kwanza, hali itakuwa ngumu zaidi huko mbele kwa timu nyingine za taifa ambazo mvuto wake umepungua. Mfano timu ya taifa ya Olimpiki ambayo itakuwa na kibarua mwakani, timu za netiboli, timu za soka za wanawake, timu za mpira wa kikapu na nyingine.
Kunahitajika mikakati ya vyama kwanza ili kamati za hamasa ziweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.