Search
Close this search box.

Michezo ni Muhimu Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa Mafanikio

Ni wakati wa kuangalia tunaitumiaje michezo kama moja ya vitu muhimu kufanikisha mipango ya muda mrefu ya maendeleo na wakati mzuri ni huu wa kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

subscribe to our newsletter!

Ni vigumu kusikia neno “Dira ya Maendeleo ya Taifa” katika mazungumzo ya watu wa michezo, tena kwenye taifa ambalo mchezo wa mpira wa miguu una wendawazimu kwa wananchi.

Ni neno ambalo hata mchambuzi wa michezo anaweza kukwambia si lazima alijue na si wajibu wake kujua kila kitu. Kwa watu wa michezo, Dira ya Maendeleo ya Taifa ni kwa ajili ya wanasiasa kwa fikra kwamba michezo ni kitu kinachojitegemea kiasi kwamba hakiwezi kuunganishwa na kitu chochote kinachohusu uchumi, mazingira, miundombinu, afya ya jamii, utalii, nishati na mambo mengine.

Kwa hiyo, hata mwandishi wa michezo hajihusishi kufahamu wala kujua Dira ya Maendeleo ya Taifa ni nini. Na ndiyo maana, pamoja na Serikali kufanya uzinduzi mkubwa wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, hakuna mjadala wowote wa michezo uliozungumzia suala hilo. Katika michezo ilikuwa ni “kama kawa” au Waingereza wanasema, business as usual.

Yaani mijadala ileile ya kugeuzageuza habari za Simba na Yanga, leo kuchambua mechi, kesho kumzungumzia kocha, kesho kutwa kulinganisha wachezaji wawili na mtondogo kuzungumzia timu ipi ni ndogo au kubwa. Hapo tunajipongeza kuwa leo tulikuwa na mijadala mizito!

Uzoefu wa Qatar

Wakati Qatar inaandaa mkakati wake wa maendeleo ifikapo mwaka 2030, suala la michezo lilikuwa ndiyo nguzo kuu katika kufanikisha utekelezaji wa dira hiyo, maarufu kwa jina la Qatar National Vision 2030 au QNV 2030.

SOMA ZAIDI: Timuatimua ya Makocha Imekuwa Mtindo Ligi Kuu

Dira hiyo iliyozinduliwa mwaka 2008 ililenga kuigeuza Qatar kuwa jamii iliyoendelea na yenye maendeleo endelevu, ikiangazia maeneo makuu manne: maendeleo ya watu, maendeleo ya kijamii, maendeleo ya kiuchumi na usimamizi wa mazingira.

Michezo iliwekwa kama moja ya nguzo za kufanikisha dira hiyo si tu kwa ajili ya maendeleo ya michezo ndani ya nchi, bali pia kujenga taswira nzuri ya Qatar duniani. Qatar ililenga kujijenga kama kituo kikuu cha michezo, ikitambulika kimataifa kwa kutumia uandaaji wa mashindano makubwa na kuonyesha uwezo wake.

Kama nchi nyingine za Kiarabu, Qatar imekuwa ikitegemea sana mafuta na gesi kama nguzo kuu za kiuchumi, lakini dira ya 2030 ililenga kupanua zaidi wigo wa kiuchumi, ikilenga kuifanya michezo kuwa nguzo kuu ya ukuaji. 

Pamoja na mambo mengine, ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya michezo kwa ajili ya kuandaa mashindano makubwa duniani ulikuwa ndiyo mkakati mkubwa ambao ungesaidia pia ukuaji wa utalii na kukuza zaidi shughuli za kiuchumi.

Kwa hiyo, uamuzi wa kuomba kuandaa fainali za Kombe la Dunia za mpira wa miguu za mwaka 2022 haukuwa wa kukurupuka, bali ulikuwa sehemu ya mikakati ya utekelezaji wa dira yake ya maendeleo ifikapo mwaka 2030.

SOMA ZAIDI: Hongera Hersi Said, Kazi ni Kuziamsha Klabu Afrika

Kwa kuandaa fainali hizo, Qatar ilijenga miundombinu ya usafiri, viwanja vya kisasa, iliboresha viwanja vya ndege, bandari na treni za umeme, vitu ambavyo vilitumiwa wakati wa fainali hizo na vinaendelea kuwanufaisha wananchi na wageni wanaotembelea nchi hiyo, baadhi yao wakiwa ni wale waliovutiwa na nchi hiyo kutokana na kufuatulia fainali hizo kubwa za soka duniani.

Fainali hizo zikawa ni kitu kikubwa cha kuvutia wawekezaji kutoka nje na nchi hiyo inategemea kuwa fainali hizo zitatoa taswira nzuri ya hali ya baadaye ya Qatar katika uwekezaji na kuwa sehemu nzuri ya utalii katikati ya ushindani mkubwa duniani katika sekta hiyo.

Yapo mengi ya kuzungumzia Qatar na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutumia michezo, hasa fainali za Kombe la Dunia ambazo zimedhihirisha uwezo wa nchi kuandaa mashindano makubwa na pia kujenga taswira ya nchi tofauti na jinsi dunia ilivyokuwa ikiiangalia awali.

Tusipuuze michezo

Wakati huu tunaelekea mwisho wa Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 iliyoandaliwa takriban miaka 15 iliyopita na tunaelekea kwenye dira mpya ya mwaka 2050, ndiyo wa kuangalia mambo yanayoweza kufanikisha mkakati huo wa muda mrefu wa maendeleo, na kwa muktadha wa andiko langu, michezo inatakiwa iwe moja ya nguzo kuu za utekelezaji wa dira hiyo.

Sijachambua sana dira inayoisha ilizingatia vipi michezo katika utekelezaji wa malengo yake na kama suala hilo lilizingatiwa, basi ili uelewe unahitaji mzungumzaji mzuri ambaye atachukua muda mrefu kuunganisha mafanikio ya dira hiyo kwa kutumia michezo.

SOMA ZAIDI: CHANETA Imetufikirisha Kuhusu ‘Goli la Mama’

Lakini huu ni wakati wa kujua michezo inaweza kuingizwaje kwenye dira hiyo. Tumeomba na tumepewa uenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) kwa kushirikiana na majira zetu, Kenya na Uganda. Kwa kuwa tutakuwa sehemu ya wenyeji, sidhani kama tunaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa kama ambavyo tungekuwa peke yetu.

Kati ya sasa na mwaka 2050 kuna matukio mengi ya kimichezo duniani ambayo yatatokea, zikiwemo fainali za Kombe la Dunia ambazo zimeshapata wenyeji hadi wa mwaka 2030, huku Saudi Arabia ikiwa imeshageukia fainali za mwaka 2034 baada ya kukosa za mwaka 2030 ambazo zitaandaliwa kwa pamoja na Hispania, Morocco na Ureno.

Kwa hiyo, duniani kutoka 2034 hadi 2050 kuna fainali nne ambazo hazina mwenyeji, 2034, 2038, 2042, 2046 na 2050. Kwa nchi yenye malengo ya muda mrefu na yenye viongozi ambao wanaona si lazima washuhudie kitu kikifanyika wakiwa madarakani, kufikiria kuwasilisha maombi ya muda mrefu ya kuandaa fainali hizo ni jambo muhimu kwao, hasa likiambatanishwa na utekelezaji wa dira ya maendeleo.

Suala ni tunataka nchi iwe vipi ifikapo mwaka 2050 – kiuchumi, kijamii na kisiasa, kama dira ya mwaka 2025 inavyoeleza kuwa ifikapo mwaka 2025 tuwe na nchi yenye utawala bora na wa kisheria.

SOMA ZAIDI: Ni Fedheha Klabu Zetu Kushtakiwa FIFA

Kama michezo itatulazimisha kujenga miundombinu bora ya usafiri kufanikisha mashindano na baadaye miundombinu hiyo itumike kunufaisha wananchi kiuchumi na kijamii, kwa nini tusifanye hivyo? Kama itatulazimisha kujenga miundombinu bora ya afya kwa nini tusifanye hivyo? 

Kama itatufanya tujenge taswira nzuri ya nchi ili baadaye iwe kituo kikuu cha utalii barani Afrika, kwa nini tusifanye hivyo? Na kama itatulazimisha kujenga viwanja bora vya michezo ambavyo vitanufaisha wanamichezo wetu baadaye na kuiwezesha nchi kuandaa mashindano mengine makubwa, kwa nini tusifanye hivyo?

Ni wakati wa kuangalia tunaitumiaje michezo kama moja ya vitu muhimu kufanikisha mipango ya muda mrefu ya maendeleo na wakati mzuri ni huu wa kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *