Search
Close this search box.

CHANETA Imetufikirisha Kuhusu ‘Goli la Mama’

Je, Serikali inajihusisha zaidi na mchezo wa mpira wa miguu kwa kuwa ndiyo maarufu na hivyo wanasiasa wanaweza kuutumia kujijenga?

subscribe to our newsletter!

Habari iliyosambaa wiki hii kuhusu kushindwa kwa Timu ya Taifa ya Netiboli kwenda Afrika Kusini kutokana na ukosefu wa fedha zimenifanya kutafakari upya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika kuweka hamasa michezoni.

Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kiasi kikubwa, amefanikiwa sana kutia hamasa wachezaji, timu na mashabiki wa mpira wa miguu kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. ‘Goli la Mama’ limekuwa chachu kubwa kwa timu zetu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kuanzia ngazi ya klabu hadi timu za taifa.

Na si tu zimewahamasisha wachezaji na timu, bali zimeamsha ari kwa watu wengine, wakiwemo wanasiasa, kufikiria wafanye nini kusaidia ushiriki wa timu zetu kimataifa, katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia kusaidia michezo.

Na si tu ‘Goli la Mama,’ ambalo timu hujipatia kuanzia Shilingi milioni tano hadi Shilingi milioni 10 kwa kila bao kutegemea na hatua ya mashindano, bali Rais Samia amekuwa akilipia viingilio kwa mashabiki ili waingie kwa wingi uwanjani kuziongezea nguvu timu zetu kwa kushangilia.

‘Goli la Mama’ likawa sehemu ya mafanikio ya Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka jana na pia limechangia klabu za Simba na Yanga kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu mbili kufikia hatua hiyo kwa wakati mmoja.

SOMA ZAIDI: Waziri Pindi Chana, Wizara Wasitekwe na Umaarufu wa Soka

Pia, timu ya taifa ya soka imefanikiwa kufuzu tena kushiriki fainali za soka za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) zilizosogezwa hadi Januari 2024, huku safari hii ‘Goli la Mama’ likigeuzwa kuwa zawadi ya Shilingi milioni 500 kwa kufuzu, ahadi ambayo Samia aliitoa mwanzoni mwa michuano ya kufuzu.

Rais Samia pia amekuwa akitoa usafiri wa ndege kwa timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa barani Afrika, kitu ambacho kimekuwa kikizipunguzia klabu mzigo wa gharama za usafiri na hivyo kujikita katika kugharimia mambo mengine muhimu.

Mchango wa Rais pia umeonekana kwa timu ya soka ya walemavu ambayo ilifuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka jana, huku Waziri wa Michezo na Mkurugenzi wa Michezo wakiwa sambamba na timu wakati wote wa mashindano hayo.

Yapo mengi ambayo Rais Samia ameyafanya tofauti na watangulizi wake ambao nao walikuwa na mbinu zao za kuchochea mafanikio katika michezo. Na kwa kweli anastahili pongezi nyingi kwa kushikilia mpango wake bila ya kutetereka wala kuubadili. 

Tayari wizara imeshasema mpango wa ‘Goli la Mama’ utaendelea wakati Simba na Yanga zikishiriki Ligi ya Mabingwa wa Afrika mwaka huu.

Maswali

Lakini hili la Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) limeleta maswali kidogo kuhusu ushiriki wa Serikali katika kuchochea mafanikio kwa michezo yote.

SOMA ZAIDI: Huu ni Wakati Muafaka Kuanzisha Wakala wa Viwanja Vya Michezo

Kiongozi wa CHANETA aliongea na waandishi wiki hii na kuwaeleza kuwa timu ya taifa ya netiboli, mchezo maarufu kwa wanawake Tanzania kuliko mingine, haitaweza kwenda Afrika Kusini baada ya kushindwa kupata nauli na fedha za malazi wakati timu ikiwa Afrika Kusini.

Kiongozi huyo alifafanua kwamba chama kiliwasiliana na Wizara ya Utamaduni na Michezo na kuahidiwa kuwa Serikali ingegharamia safari hiyo, lakini baadaye wakaandikiwa barua kuwa wizara imekosa fedha hizo na kuishauri CHANETA ijitoe katika mashindano hayo. Walikuwa wameomba Shilingi milioni 20 kwa ajili ya safari.

Nadhani CHANETA watakuwa wanajisikia vibaya kwa Serikali kushindwa kuwasaidia, hasa wakiona hamasa kubwa inayowekwa katika mchezo wa mpira wa miguu ambao ni maarufu kuliko michezo mingine Tanzania.

Ni dhahiri kwamba timu za mpira wa miguu huweza kujimudu kwa gharama za ushiriki, ikiwa ni pamoja na safari, malazi na posho kutokana na fedha nyingi zinazoingizwa kwenye mchezo huo na hivyo inakuwa rahisi kwa Serikali kuongeza chachu kwa kuweka vitu kama ‘Goli la Mama.’ 

Ni wazi kuwa Serikali ikisema igharimie kila kitu kwa timu za taifa, kila chama kilichosajiliwa kwa msajili kitaibuka na kusema kina mashindano ya kimataifa na hivyo kinaomba msaada wa Serikali wa kusafirishwa hadi kituo cha mashindano na kulipiwa gharama nyingine kama malazi na posho za wachezaji na hivyo mzigo kuwa mkubwa kwa Serikali.

Vigezo maalum

Ni kwa jinsi hiyo, inabidi kuangalia upya hamasa hiyo na pengine kuiwekea vigezo, au sifa, zinazotakiwa ili timu ya taifa inayoshiriki kimataifa ifuzu kupata msaada wa Serikali kama ule wa ‘Goli la Mama.’ Maana kwa netiboli ukisema ‘Goli la Mama,’ utakuwa umejitwisha mzigo mkubwa kwa kuwa timu hufungana hata mabao 20-29.

SOMA ZAIDI: Ni Fedheha Klabu Zetu Kushtakiwa FIFA

Kwa hiyo, ni lazima kuwepo kwa vigezo kwamba timu inayoweza kupata msaada wa Serikali ni ipi? Ile ambayo inajimudu kwa gharama za safari? Kwa soka ni rahisi kwamba timu inapewa ndege ambayo huisafirisha na kuisubiri imalize mechi na kuondoka muda unaofaa siku inayofuata na hata usiku, ikiwezekana.

Kwa kwenda kushiriki mashindano labda ya wiki mbili, ndege haiwezi kuegeshwa uwanja wa udege kwa wiki mbili ikisubiri timu imalize mashindano. Na ukisema ndege irudi nyumbani na kwenda kuichukua timu mwishoni mwa mashindano ni gharama mara mbili.

Lakini pia ni katika hatua gani ya mashindano Serikali inaweza kushawishika kuchangia gharama? Tumeona ‘Goli la Mama’ sasa si katika hatua ya awali, bali hatua ya juu. Kwa netiboli, mashindano ya Afrika Kusini yalikuwa ni ya kutafuta nafasi ya kusonga mbele na si fainali au hatua ya juu ya mashindano.

Labda Serikali inajihusisha zaidi na mchezo wa mpira wa miguu kwa kuwa ndiyo maarufu na hivyo wanasiasa wanaweza kuutumia kujijenga? Kama ndivyo, basi hapo pia ndipo ulipo umuhimu wa netiboli.

Hamna gharama 

Mchezo wa kwanza kwa mtoto wa kike wa Kitanzania kukutana nao na kuushiriki ni mchezo wa netiboli. Kama ulivyo mpira wa miguu, netiboli ni mchezo usio na gharama kubwa na ndiyo maana ni rahisi kuchezwa na wengi. 

SOMA ZAIDI: Kelele kwa Mangungu ni za Kukariri, Tatizo ni Kubwa Simba

Na karibu kila shule ya msingi, ina uwanja wa mpira wa miguu na netiboli. Viwanja vya michezo mingine ni ziada. Na hata uchaguzi unapokaribia, mashindano ambayo wanasiasa wangependa kuyadhamini ni yale ya mpira wa miguu na netiboli kwa kuwa ndiyo michezo maarufu.

Tatizo kwa netiboli labda ni viongozi wa chama hicho kushindwa kuutangaza vizuri na kutokuwa na programu za kuuendeleza kiasi cha kurudisha ule umaarufu wake wa enzi za akina Yondo Sister, Judith Ilunda, Judith Chifupa, Happy Nzunda na wengineo wa nyakati tofauti zilizovuta mashabiki na wanasiasa pale Relwe Gerezani na Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Kama soka inavyopata kipaumbele, ndivyo netiboli ingepata kipaumbele kutokana na umaarufu wake kwa wanawake.

Na kwa maana hiyo kungekuwepo na jicho fulani kwa ombi la CHANETA kuhusu ushiriki wao Afrika Kusini, huku likiwekwa sharti kwamba safari nyingine ni lazima kwanza wao watafute japo nauli tu, halafu vitu vingine vichangiwe na Serikali au ihamasishe wadau waichangie.

Hii ni mara ya pili CHANETA inashindwa kutuma timu Afrika Kusini. Mara ya kwanza karibu miaka mitatu iliyopita, chama hicho kilikosa fedha za kulipia Shilingi Milioni moja. Huwezi kueleza ilishindikanaje!

SOMA ZAIDI: Mamelodi Wametoa Somo kwa Yanga, Simba

Pengine ni viongozi wa netiboli kulala. Kama wamelala, ni jukumu la Baraza la Michezo la Taifa kuwaamsha kwa kuwa ni sehemu ya majukumu yao kama yanavyoelezwa katika uanzishwaji wa chombo hicho.

Lakini cha msingi ni kuweka sifa za ‘Goli la Mama’ au hata ‘Ndege ya Mama’ ili kuondoa dhana kwamba Rais anashughulikia soka pekee kwa sababu ni mchezo unaopendwa na wengi na ameisahau michezo mingine. 

Inawezekana kabisa viko vigezo ambavyo Rais anatumia, lakini ni muhimu vikawekwa bayana ili kuondoa manung’uniko yanayoweza kuibuliwa na vyama vingine.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *