Wiki hii kumekuwa na mzozo miongoni mwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa Simba baada ya timu hiyo ya soka kufungwa mabao 5-1 na wapinzani wao wa jadi, Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC.
Ni matokeo ya kawaida katika mchezo wa soka, lakini ambayo huja kwa nadra sana hasa kwa wababe hao wawili wa Kariakoo ambao mara nyingi mechi zao huisha kwa sare au ushindi wa tofauti ndogo.
Na kwa sababu matokeo kama hayo ya mabao mengi ni ya nadra sana, kila yanapotokea huambatana na mambo mengine kama tuhuma dhidi ya wachezaji kuwa wamehujumu timu, kelele za kutaka viongozi wawajibike kwa kushindwa kuimudu timu, na wakati mwingine hata tuhuma dhidi ya viongozi, au wafadhili, kuwa wameihujumu timu.
Haya ni mambo ambayo yamekuwepo miaka na miaka na ambayo wengi walidhani baada ya klabu hizi mbili kubadili muundo wa uendeshaji, labda yatapungua na uwajibikaji uende kwa waliokabidhiwa majukumu tu.
Muundo wa uendeshaji
Simba na Yanga zimebadili muundo wa uendeshaji lakini ni Simba pekee iliyoanza utekelezaji, huku Yanga ikiendelea na muundo wa uongozi wa zamani uliofanyiwa marekebisho machache tu, hasa katika idadi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu.
SOMA ZAIDI: Mamelodi Wametoa Somo kwa Yanga, Simba
Lakini Simba inasema imeenda mbali hadi kubadili muundo wa umiliki wa klabu na tayari imeshauza asilimia 49 ya hisa zake kwa mmoja wa wanachama wake maarufu, Mohammed Dewji.
Na katika uongozi, Simba imechukua muundo wa mashirika, au corporate governance kwa kimombo, ikiwa na Bodi ya Wakurugenzi kama chombo muhimu cha uongozi wa pamoja kati ya wamiliki, yaani mwekezaji na wawakilishi wa wanachama.
Katika hali isiyo ya kawaida, mwekezaji, ambaye anamiliki asilimia 49 tu za hisa, ndiye amechagua Mwenyekiti wa Bodi, huku Mwenyekiti wa Klabu, iliyo na asilimia 51, ni mjumbe tu wa bodi hiyo.
Ni vizuri kwamba mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage, ameieleza kasoro hii alipozungumza na Clouds FM wiki hii.
Salim Abdallah, maarufu kama Try Again, ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi aliyeteuliwa na mwekezaji, wakati Murtaza Mangungu ndiye mwenyekiti aliyechaguliwa na wanachama katika Mkutano Mkuu wa uchaguzi kusimamia maslahi ya klabu katika uendeshaji.
SOMA ZAIDI: Kanuni za Ridhaa Zinaondoa Ushindani wa Haki Kwenye Soka. Bodi ya Ligi, TFF Ziziondoe
Ungetegemea Mangungu ndiyo ateue Mwenyekiti wa Bodi kwa kuwa anawakilisha klabu inayomiliki asilimia 51 za hisa, halafu asiwe Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi. Lakini huyu Mangungu ndiyo alikashifiwa kuwa kazi yake ni “kufungua na kufunga vikao” na hana nguvu yoyote. Leo ndiyo anatuhumiwa kuhusika na uendeshaji mbovu.
Menejimenti dhaifu?
Na kwa kuwa pande hizo mbili zina maslahi ya kiuchumi, ni lazima chombo huru cha uendeshaji wa shughuli za kila siku kiwepo ambacho ni menejimenti. Menejimenti ya Simba inaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu ambaye kazi yake kubwa ni kuhakikisha mipango yote ya bodi na maelekezo yake yanatekelezwa kadri yalivyokusudiwa.
Bodi ndiyo inapitisha bajeti ya klabu na kuiachia menejimenti itekeleze. Na kwa maana hiyo, ni nadra sana katika uendeshaji wa mashirika, kusikia mmoja wa wanahisa ameongeza fedha kwa ajili ya kufanikisha shughuli za kila siku, wakati bodi ilishakaa na kukubaliana kupitisha bajeti ya kipindi husika.
Lakini mfumo wa Simba unamruhusu mwekezaji kuandika, mara kwa mara, katika akaunti yake ya X, zamani Twitter, kuwa ametoa mabilioni kwa ajili ya usajili, lakini anaona kuna ubabaishaji kwa baadhi ya viongozi. Mara kadhaa amekuwa akitoa kauli zinazoonyesha kuwa kuna tatizo katika uongozi na anatishia kujiondoa.
Katika siku za karibuni, aliyekuwa CEO wa Simba, Barbara Gonzalez, ambaye alijiondoa au kuondolewa, ameungana na mwekezaji kuponda viongozi kuwa wanatumia fedha vibaya.
SOMA ZAIDI: AFL Yaanza kwa Kishindo Huku Ikiacha Maswali Mengi
Hali hii imejenga picha mbaya kwa wanachama kiasi kwamba wanakuwa tayari wana jibu pale timu inapofanya vibaya.
Ndiyo maana leo hii kuna kilio kikubwa cha kutaka Mangungu aondoke kana kwamba alishushwa tu kwenda kuongoza Simba, kumbe alichaguliwa kwa kura nyingi kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama.
Kilio dhidi ya Salim Try Again kutaka aondoke si kikubwa sana, lakini kipo na kama kilivyo kwa Mangungu, tuhuma zake ni kushindwa kuimudu timu na kutosajili vizuri.
Kwa hiyo, unapofuatilia kwa kina uendeshaji wa klabu, kauli za mwekezaji za mara kwa mara na sauti za wapenzi, mashabiki na wanachama, unaona dhahiri kuwa kuna tatizo la kutotekeleza vizuri maamuzi ya kufanya mageuzi ya kiuendeshaji ili klabu iendeshwe kisasa.
Tatizo la uelewa
Kuna tatizo kubwa kwa wanachama, wapenzi na mashabiki kutouelewa mfumo mpya wa uendeshaji na umiliki na pili mwekezaji kutoka hadharani kutuhumu kuwa baadhi ya viongozi wanafuja mali na kuhujumu mabadiliko. Haya yote yanatengeneza bomu ambalo cheche zake zimeanza kuonekana baada ya Simba kufungwa mabao 5-1 na Yanga.
SOMA ZAIDI: Makosa ya Waamuzi ni Tatizo la Soka Siyo Klabu Zinazolalamika
Hakuna mwanachama jasiri anayeibuka kuzungumzia hadharani kasoro hizo, isipokuwa Mbunge wa Nzega Vijijini (Chama cha Mapinduzi – CCM) Hamisi Kigwangalla ambaye amefikia hadi hatua ya kuhoji kama fedha za mwekezaji zilizotakiwa kuwa Shilingi bilioni 20 zimeingizwa kwenye akaunti za Simba.
Majibu kwake yamekuwa ni matusi!
Kama Simba inataka kuendeshwa kisasa, ni lazima kasoro hizi ziwekwe bayana na kusahihishwa.
Ni lazima fungu la bajeti ya usajili lijulikane japo kwa bodi pekee, kuliko mwekezaji kutamka nje ya vikao kuwa ametoa mabilioni kufanikisha usajili na hivyo kuweka matumaini kuwa klabu itasajili nyoa yeyote barani Afrika wakati uwezo huo bado haujafikiwa.
Ungetegemea fedha hizo ziingie kwa CEO na halafu likitokea tatizo katika usajili, ndiyo awajibike. Lakini inaonekana CEO hapewi fedha hizo, bali viongozi wengine ‘watu wa mpira.’
SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga
Ni lazima CEO, ambaye ni Imani Kajura, awe na mamlaka kamili ya kufanya shughhuli za kila siku za klabu bila ya kuingiliwa na awajibike kwa bodi kila baada ya kipindi fulani kilichowekwa kikatiba au kisheria. Kama bodi inafikia hatua hata ya kujadili mwenendo wa mchezaji, menejimenti inafanya nini?
Kocha wa zamani wa Manchester United, Jose Mourinho, alikaririwa hadharani akionyesha tofauti zake na Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Ed Woodward, kuhusu usajili wa beki wa kati.
Lakini baadaye Woodward alisema alilazimika kukataa usajili wa beki huyo kutokana na idara ya usajili ya klabu kukataa. Alichokifanya ilikuwa ni kumwambia Mourinho kuwa haitawezekana na hivyo kocha huyo Mreno kuchukulia kuwa ni uamuzi binafsi.
Leo hii husikii Kajura akilaumiwa kuhusu usajili kwa sababu kazi hiyo, ambayo ilitakiwa iwe mikononi mwake, inafanywa na wengine, maarufu kama ‘watu wa mpira.’ Ni lazima Kajura anafurahia kikombe hicho kumpita.
Lakini ni kwa sababu klabu imebadili mfumo, lakini watu walewale wameshika nafasi mpya na hivyo kuendelea na utamaduni uleule wa mfumo wa zamani!
SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Hazina Haja Tena ya Kuhofia Yeyote Ligi ya Mabingwa
Ndiyo maana leo hii kilio cha kutaka Mangungu aondoke ni kikubwa kwa kuwa hakuna mwanachama anayejua mwenyekiti huyo anahusika na nini katika uendeshaji wa klabu.
Kilio kinatoka wapi?
Wote wamekaririshwa kuwa muhusika mkuu ni Mangungu. Anayepewa fedha kwa ajili ya usajili, kama kweli, si Mangungu. Anayeandaa kambi si Mangungu. Anayeahidi bonasi si Mangungu.
Anayelipa mishahara si Mangungu wala Salim Try Again. Anayeshughulikia maisha ya kila siku ya wachezaji si Mangungu na hata anayelipa makocha na kutoa maelekezo si Mangungu. Kilio hiki kinatoka wapi?
Ni lazima kilio hiki kinatokana na wanachama, wapenzi na mashabiki kutoelewa nani ni nani katika mfumo mpya wa uendeshaji na umiliki wa klabu.
Pia, kinaweza kuwa kinatokana na uongozi na wawekezaji kutotekeleza vyema mabadiliko na hivyo kuendelea na utamaduni wa zamani, unaoonyesha anayetoa fedha ndiyo mwenye nguvu zaidi na hawezi kuwa na kosa kwa kuwa majukumu yake ya kutoa fedha ameyatimiza.
Ni lazima masuala haya yaeleweke vizuri kwa wote ili inapofikia suala la kuwajibisha, basi kila mtu ajue kuwa tatizo fulani limesababishwa na majukumu fulani kutotekelezwa na si kukaririshwa kuwa fulani ndiye muhusika mkuu bila ya kujua majukumu yake.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.