The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kanuni za Ridhaa Zinaondoa Ushindani wa Haki Kwenye Soka. Bodi ya Ligi, TFF Ziziondoe

Mamlaka husika zizipitie kanuni zetu na kuanza kuondoa ule uridhaa uliojazana na kusababisha timu zicheze chini ya uwezo.

subscribe to our newsletter!

Viungo wawili wa Yanga na Azam FC, Mudathir Yahya na Feisal Salum, mtawalia, wanasubiri kutangaziwa adhabu ya kukosa mechi tatu baada ya kufanya vitendo vinavyotafsiriwa kuwa ni kukataa kushikana mkono na wachezaji wengine au imani za kishirikina.

Hii ni kutokana na kanuni ambazo zimezuia vitendo hivyo ili mchezo wa mpira wa miguu uendeleze lile kusudi lake la kuwa mchezo wa kiungwana na wa haki.

Hizi ni kanuni ambazo zinalenga kumuadhibu mchezaji, lakini zaidi zinaathiri klabu iliyotumia mamilioni ya fedha kumsajili na kumlipa mshahara, posho na bonasi.

Katika hali ya kawaida ungetegemea kuwa kanuni hizi zimlenge mchezaji pekee ili ajutie kosa na kufikiria kujirekebisha ili asiumizwe tena na adhabu kama hizo.

Lakini kwa sababu zinaumiza watu wengi, yaani mchezaji, timu na mashabiki, ule ukali na malengo ya adhabu haumuathiri sana mchezaji na pengine atafarijiwa na mashabiki na hata viongozi wake kiasi cha kujiona hakuwa na kosa kubwa au ameonewa.

SOMA ZAIDI: AFL Yaanza kwa Kishindo Huku Ikiacha Maswali Mengi

Hao ni baadhi tu kati ya wachezaji wengi wanaoathiri timu zao kwa makosa yao bninafsi. Wapo ambao eti hawakuhudhuria shughuli binafsi ya utoaji wa tuzo za msimu uliopita ambao kanuni zinataka wafungiwe hadi mechi tatu kwa kosa hilo.

Binafsi sioni sababu ya mchezaji aliyekosa kuhudhuria sherehe za tuzo binafsi kupewa adhabu ya kukosa mechi ya klabu yake ambayo haikuhusika hata kidogo kumzuia kutohudhuria hizo sherehe na isitoshe wakati huo alikuwa mapumzikoni baada ya ligi kumalizika.

Na zaidi ya hapo, msimu unaofuata anaweza kuwa amehamia klabu nyingine ambayo itaathirika na kosa hilo la ajabu.

Soka la ridhaa

Hizi ni kanuni ambazo msingi wake ni soka la ridhaa. Zimeundwa na fikra za soka la ridhaa na si soka la kulipwa ambalo linalenga kumuadhibu mchezaji ajutie kosa.

SOMA ZAIDI: Makosa ya Waamuzi ni Tatizo la Soka Siyo Klabu Zinazolalamika

Katika soka la ridhaa, mchezaji huonekana kama anacheza kwa ridhaa yake na si kulazimishwa kwa mkataba na hivyo, mchezaji huyu haishi kwa kutegemea kucheza mpira wa miguu bali shughuli zake nyingine za kiuchumi kama ajira, biashara au kilimo.

Kwa hiyo, njia pekee ya kumuadhibu ni kumzuia asipate furaha anayoitafuta kwenye mpira baada ya shughuli zake binafsi za kimaisha. Huyu hata ukimzuia kucheza miezi mitatu ni sawa tu kwa kuwa mpira wa miguu si kipaumbele kwake.

Lakini unapozungumzia soka la kulipwa unafikiria mchezo wenyewe na uchumi wa mchezaji.

Yaani akifanya vitendo vinavyoondoa uungwana, basi ni muhimu aadhibiwe kwa kuangalia ataathirikaje kiuchumi. Ndiyo maana kuna faini nyingi katika soka la kulipwa kwa kuwa mchezo wenyewe ni ajira.

Mchezaji ambaye amekataa kushikana mikono na wachezaji wengine, anazuiwaje kucheza mechi tatu na kuiathiri timu wakati kosa ni lake binafsi na wala halihusishi timu?

SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga

Tunajuaje kuwa ni mganga binafsi wa mchezaji aliyemshauri asifanye hivyo bila ya timu kujua?

Tumeona kuna shutuma nyingi miongoni mwa wachezaji wakituhumiana kurogana, iweje na hilo la kutegeana kuingia uwanjani lisiwe tatizo binafsi?

Hakuna mantiki

Silengi kutetea makosa kama hayo, lakini mantiki ya kuikosesha timu huduma ya mchezaji inayemuhudumia kwa mamilioni ya fedha ili ifanye vizuri, siioni katika ufungiaji huo.

Siku zote, waendeshaji wa ligi za wachezaji wa kulipwa hujali sana timu zicheze zikiwa timamu ili kuwapa mashabiki ile burudani wanayoifuata, na si kutengeneza mazingira kwa timu kucheza pungufu ya uwezo wake.

Wakati fulani niliandika kuhusu Ligi Kuu ya Afrika Kusini ilivyokataa wachezaji nyota wa klabu zake kujiunga na timu ya taifa iliyokuwa inakuja nchini kucheza mechi ya kirafiki na Tanzania nje ya tarehe zilizotengwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Hazina Haja Tena ya Kuhofia Yeyote Ligi ya Mabingwa

Kitendo hicho kilifanywa ili kuilinda chapa ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kwamba ni lazima timu zake zicheze zikiwa timamu na si zilizopunguzwa uwezo kwa wachezaji wake kuitwa timu ya taifa. Ndivyo ilivyo hata kwa hizi adhabu.

Nilikuwa nasoma kanuni moja ya adhabu ambazo muamuzi anaweza kutoa kabla na wakati wa mechi.

Yaani mchezaji akifanya kosa kabla ya mechi, anaweza kuonyeshwa kadi ya njano na mechi ikianza akaonyeshwa kadi nyingine ya njano, haitahesabiwa kuwa ni kadi ya pili na hivyo kutolewa nje.

Matukio ya wakati wa mechi ni tofauti na yanayotokea wakati wa mchezo, hivyo adhabu zake haziwezi kulingana kiasi cha kusababisha azuiwe kucheza mechi zinazofuata.

Isitoshe, Mudathir na Fei Toto hawakuonyeshwa hata hiyo kadi ya njano, iweje adhabu zao zifikie mpaka kuziadhibu timu zao?

Chini ya viwango

Ni muhimu sana kwa mamlaka kuzipitia kwa kina kanuni zetu na kuanza kuondoa ule uridhaa uliojazana ambao unasababisha timu zetu zicheze chini ya uwezo uliokusudiwa.

SOMA ZAIDI: Huu ni Wakati Muafaka Kuanzisha Wakala wa Viwanja Vya Michezo

Makosa yanayotokea wakati wa mchezo, hayo yanastahili kuadhibiwa kwa mchezaji kuzuiwa kucheza mechi zinazofuata, lakini si yale ya kabla ya mchezo, ambayo mengine hutokana tu na tafsiri ya wanaoadhibu.

Katika ligi ya juu ya nchi, kampuni na watu binafsi huweka fedha nyingi kwa malengo tofauti, na mashabiki huja wakitegemea kuona burudani ya hali ya juu.

Pale wanapoikosa, kama siku ile Tabora United walipolazimishwa kucheza wakiwa wanane uwanjani, ladha ya ligi huondoka na baadhi ya sifa kama za wafungaji bora au kipa kutoruhusu bao, hukosa ule utamu unaoptarajiwa.

Bodi ya Ligi (TPLB) na Shirikisho la Soka (TFF), ambalo huidhinisha kanuni hizo, hawana budi kukaa na kufikiria jinsi ya kuondokana na kanuni zinazoondoa ushindani wa haki na kupoteza ladha ya mchezo.

TPLB haina budi kufanya kila iwezalo kulinda chapa yake ili ijulikane kabisa kuwa mshindi wa Ligi Kuu si yule anayepatikana kwa ujanjaujanja, bali aliyeshindana kwa haki hadi kutwaa ubingwa.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *