The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

AFL Yaanza kwa Kishindo Huku Ikiacha Maswali Mengi

Fedha pekee haziwezi kupandisha kiwango cha soka bila ya utamaduni wa mchezo huu kuheshimiwa.

subscribe to our newsletter!

Hakuna shaka kwamba michuano mipya ya Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) imezinduliwa kwa mafanikio makubwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao utatumiwa pia leo na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Sherehe za ufunguzi wa mashindano hayo yanayoshirikisha klabu nane zilizopatikana kutokana na mfumo wa kukusanya pointi kwa miaka mitano, zilifanyika Ijumaa na kuanza kwa mechi baina ya vigogo wa Afrika, Al Ahly na wenyeji Simba.

Nje ya uwanja alikuwepo rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) Gianni Infantino, wa Shirikisho la Afrika (CAF), Patrice Motsepe na Mkuu wa Maendeleo ya Soka Duniani wa FIFA, Arsene Wenger, wageni ambao ni nadra sana kuonekana wakati mmoja jijini Dar es Salaam.

Michuano hiyo haina tofauti na ile iliyotakiwa kuanza barani Ulaya ya Super League, ambayo ilianzishwa nje ya mfumo wa Chama cha Soka Ulaya (UEFA) na hata wa FIFA, lakini ikazuiwa kwa nguvu ya mashabiki na vyama vya soka vya nchi kutokana na kwenda kinyume na utamaduni wa mpira wa miguu wa timu kushiriki kutokana na kufuzu kuingia mashindano hayo kwa matokeo ya uwanjani.

Michuano hiyo ilianzishwa na kampuni ya kibiashara inayoitwa European Super League Company iliyokuwa na lengo la kushindana na michuano ya UEFA, hasa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, ambayo ndiyo ya juu kwa klabu barani Ulaya. Kwa upande wa ushiriki, ligi hiyo ilitakiwa ishirikishe timu zinazoteuliwa kutokana na historia ya mafanikio yake.

SOMA ZAIDI: Makosa ya Waamuzi ni Tatizo la Soka Siyo Klabu Zinazolalamika

Kwanza ingeanzishwa kwa kushirikisha klabu 20 bora, kwa mujibu wa kampuni hiyo, huku klabu 12 zikipewa heshima ya kuwa klabu asisi. Lakini baada ya kutangazwa kwake mwaka 2021, kulitokea upinzani mkubwa kutoka kwa mashabiki, makocha, wachezaji, wanasiasa na klabu nyingine za soka nchini England.

Hoja ya kupinga michuano hiyo ni kuweka mbele ukubwa wa klabu, kukosa ushindani wa jinsi ya kufuzu, yaani timu zingepatikana kutoka baadhi ya nchi ambazo zingeteuliwa na ndizo ambazo zingekuwa zikishiriki miaka yote bila ya kushuka.

Pia, kulikuwa na hoja kuwa Super League ya Ulaya ingeua ligi za ndani za nchi ambazo kwa kawaida ndizo zinazotoa wawakilishi wa kushiriki michuano kama Ligi ya Mabingwa, Europa League na Conference League.

Mashabiki hawakupenda ushindani wa klabu nyingi uondoke halafu ziwepo klabu ambazo zinashiriki ligi mpya tu hata kama zitakuwa zimeshuka kiwango.

Vurugu zilikuwa kubwa kwa mashabiki ambao walidiriki kuzuia mechi baina ya Manchester na Liverpool, hadi ikapangiwa tarehe nyingine.

SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga

Hali hiyo ilisababisha waandaaji wa mashindano hayo kutangaza nia ya kuachana na mpango huo, lakini pia suala hilo likaenda mahakamani ambayo ilizizuia FIFA na UEFA kuingilia mpango huo. Hata hivyo, hukumu bado inasubiriwa.

Maswali mengi

Hadi mechi ya ufunguzi inachezwa Ijumaa jijini Dar es salaam, bado kulikuwa na maswali mengi kuhusu ligi hiyo mpya ya AFL. Bado haijajulikana hatima yake ni nini kwa bingwa na upatikanaji wa klabu nyingine kuingia kwenye ligi hiyo utafanywa kwa uteuzi au kwa ushindani.

Kwa kawaida, utamaduni wa soka unataka timu zinazoshiriki mashindano ya daraja la juu iwe imefuzu kulingana na kiwango cha wakati huo na si mfumo uliotumiwa na CAF kupata washiriki wa AFL.

Waratibu wa mashindano hayo walitumia mfumo wa ukusanyaji pointi wa CAF ambao huangalia matokeo ya timu katika kipindi cha miaka mitano.

Kwa hiyo, hata TP Mazembe ambayo iliondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana katika raundi ya awali, na ikashindwa kuvuka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, imo AFL kwa matokeo ya huko nyuma na si kiwango chake cha sasa.

Uteuzi wa timu shiriki utasaidiaje kuendeleza soka kama hauzingatii kiwango cha wakati huo cha timu au klabu?

SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Hazina Haja Tena ya Kuhofia Yeyote Ligi ya Mabingwa

Kama hadi wakati michuano inaanza CAF haijaweka bayana upatikanaji wa timu kwa ajili ya msimu ujao, klabu zitajiandaaje ili ziwe na uhakika wa kushiriki mwakani? Haya yote yalitakiwa yawe bayana hata kabla ya kuanza kwa mashindano.

Juzi ndiyo Motsepe ameanza kufikiria hali ya baadaye ya mashindano aliposema kuwa CAF itabidi iangalie upya michuano yake, na ikiwezekana ifute mashindano mengine ili kuepuka mkanganyiko.

Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) imelazimika kurefusha awamu ya kwanza ya msimu wake baada ya kuiondoa Mamelodi Sundowns katika ratiba yake ili iweze kushiriki AFL. Hali kadhalika Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) imelazimika kufanya hivyo ili Simba iweze kushiriki.

Hapo bado kuna Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Azam, Kombe la Shirikisho na Super Eight kwa Afrika Kusini. Na Januari kutakuwepo na fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Ivory Coast, achilia mbali michuano mingine ya kufuzu kwa timu za taifa.

Mrundikano utakuwa mkubwa kiasi cha kusababisha ladha ya mashindano ya ndani kuondoka.

Kuboresha viwango

Moja ya hoja kubwa za CAF kubariki mashindano hayo ni kwamba yatasaidia kuboresha kiwango cha soka Afrika. Kivipi?

Kwa nini isitumie nia hiyohiyo kuboresha mashindano yake ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, badala yake inaanzisha mashindano mapya? Kwa nini fedha ambazo zinapatikana kwenye AFL zisingeingizwa kwenye Ligi ya Mabingwa?

SOMA ZAIDI: Huu ni Wakati Muafaka Kuanzisha Wakala wa Viwanja Vya Michezo

Ukijiuliza sana swali hilo, ndipo unapoanza kushawishika kuwa CAF si muandaaji wa mashindano hayo, bali imetumiwa tu na kampuni binafsi kuhalalisha baada ya mpango wa barani Ulaya kuvurugika.

Na ndiyo maana PSL walihoji sababu za barua za mawasiliano ya mashindano hayo kutumwa kutoka Kigali, Rwanda badala ya Cairo, Misri, ikisema ina wasiwasi na mashindano hayo.

Na wanaposema CAF imeipa kampuni moja ya Italia kuratibu mashindano hayo na kampuni hiyo kuamua kuweka ofisi zake jijini Kigali badala ya Cairo, ndipo unapozidi kuamini kuwa AFL ni mpango tofauti na CAF.

Hata unapoangalia tovuti ya CAF huoni kitu kama AFL na hata kwenye orodha ya mashindano ya CAF, hakuna AFL. Na angalia tovuti ya AFL hutaweza kuiona CAF popote, labda pale wanapomtaja rais wake tu.

Suala la fedha

Kwa hiyo, bado kuna maswali mengi kuhusu AFL kuliko majibu. Lakini kwa sababu suala la fedha zinazopatikana kwenye mashindano hayo ndilo limewekwa mbele, inakuwa vigumu kwa viongozi na mashabiki wa soka Afrika kuhoji zaidi kuhusu mashindano hayo.

Super League ya Ulaya ingekuwa na fedha nyingi kwa timu shiriki na hata vyama vya nchi, lakini kutokana na upeo mkubwa wa viongozi na mashabiki kuhusu soka na utamaduni wake, michuano hiyo ilipingwa kila kona na ikapotea.

SOMA ZAIDI: Kocha Singida Amedokeza Tatizo Kubwa la Soka Letu

Na hii si mara ya kwanza kwa suala hilo kuibuka barani Ulaya. Liliwahi kuibuka katikati ya miaka ya tisini, lakini likapingwa na UEFA na ndipo ilipozaliwa Ligi ya Mabingwa.

Kwa hiyo, fedha pekee haziwezi kupandisha kiwango cha soka bila ya utamaduni wa mchezo huu kuheshimiwa. Ni lazima viongozi wetu wahoji mambo mengi kabla ya kukubali mashindano hata pale yanapoonekana yanaweza kuingiza fedha nyingi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *