The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mamelodi Wametoa Somo kwa Yanga, Simba

Wametuonyesha jinsi ya kuvaana na Al Ahly na hakuna shaka kwamba yapo mengi zaidi ya kujifunza kutoka kwa timu hiyo.

subscribe to our newsletter!

Timu kutoka Afrika Kaskazini, yaani nchi kama Misri, Algeria, Tunisia na Morocco, zimekuwa kikwazo kikubwa kwa klabu zetu kusonga mbele katika mashindano ya Afrika.

Hata timu yetu ya taifa, Taifa Stars, huonekana imefikia mwisho pale inapokutana na timu kutoka mataifa hayo katika mashindano ya mtoano, labda iwe ni katika makundi ambako tunaweza kusonga mbele tukiwa nyuma ya moja ya mataifa hayo.

Pamoja na kuwa kikwazo kikubwa, si kwamba klabu za Tanzania hazijawahi kuzitoa timu kutoka mataifa hayo. Simba iliiondoa Zamalek iliyokuwa ikitetea ubingwa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2003. 

Tena iliitoa katika ardhi ya Misri baada ya kila timu kushinda bao moja nyumbani na hivyo mechi kuamuliwa kwa njia ya matuta.

Mwaka jana, 2022, Yanga ilifanikiwa kuondoa mkosi huo ilipoiondoa Club Africain ya Tunisia katika mechi ya mtoano ya kutafuta timu zinazoingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. 

SOMA ZAIDI: Kanuni za Ridhaa Zinaondoa Ushindani wa Haki Kwenye Soka. Bodi ya Ligi, TFF Ziziondoe

Na haikuishia hapo, ilifanikiwa kushinda kwa bao 1-0 mbele ya US Alger nchini Algeria katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya vigogo hao wa Kariakoo kukubali kufungwa mabao 2-1 nyumbani katika mchezo wa kwanza.

Al Ahly haigusiki?

Lakini mafanikio hayo hayajawahi kuigusa Al Ahly, klabu ya karne inayoshikilia rekodi ya kutwaa ubingwa wa Afrika mara nyingi. Hata timu zetu zinapopata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani, huwa vigumu kulinda ushindi huo katika mechi za marudiano ambazo mara nyingi hufanyika jijini Cairo, Misri.

Na imekuwa ni nadra vigogo hao wa Misri kutolewa hata na timu kutoka kanda nyingine. Mara nyingi inaposhindwa kutetea ubingwa inakuwa imekutana na timu kutoka mataifa kama Morocco, Algeria, na wakati fulani Congo na Nigeria.

Hivi karibuni, Al Ahly iliburuzwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, wakati fulani ikicharazwa mabao 5-2, kipigo kikubwa kwa wababe hao wa soka Afrika.

Ushindi wa hvi karibuni wa bao 1-0 na sare ya bila kufungana uliowaondoa mabingwa hao wa Afrika kwenye michuano mipya ya Ligi ya Soka ya Afrika umewafanya vigogo hao wa Afrika Kusini kuwa wababe wa Al Ahly.

SOMA ZAIDI: AFL Yaanza kwa Kishindo Huku Ikiacha Maswali Mengi

Timu hizo zimeshakutana mara 13, huku Al Ahly ikishinda mara nne na kufunga jumla ya mabao 15, wakati Mamelodi imeshinda mechi tano ikifunga jumla ya mabao 19. Timu hizo zimetoka sare mara nne.

Kwa hiyo, ushindi wa Mamelodi dhidi ya Al Ahly katika mechi hizo mbili za nusu fainali si mgeni sana kwa timu hiyo inayomilikiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe.

Funzo kwa Yanga, Simba

Lakini kwa wakati huu una maana yake kwa klabu za Tanzania, hasa Simba na Yanga ambazo zimeingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, ambayo mabingwa watetezi ni vigogo hao wa Cairo.

Yanga inaanza mechi zake za makundi kwa kukutana na Al Ahly, wakati Simba inaweza kukutana na wababe hao iwapo itavuka hatua ya makundi. Yaani robo fainali, nusu au fainali.

Mamelodi waliupoza mchezo wa kwanza, lakini hawakukubali Al Ahly waumiliki mpira au wawe na nafasi na muda mwingi wa kufanya maamuzi pale wanapokuwa na mpira.

SOMA ZAIDI: Makosa ya Waamuzi ni Tatizo la Soka Siyo Klabu Zinazolalamika

Na walihakikisha wanakaa katika nusu ya timu hiyo kutoka Afrika Kaskazini sehemu kubwa ya mchezo, na hata ule ujanja wao wa kufanya mashambulizi ya kushtukiza, uliishia katikati ya uwanja.

Mchambuzi mmoja wa Afrika Kusini aliandika kuwa ingekuwa ni kosa kubwa kwa Mamelodi kujaribu kuwakimbiza Al Ahly kwa lengo la kupata mabao mengi. 

Muda mwingi, mabeki hawakuonekana kuwa na haraka ya kuutupia mpira mbele kwa washambuliaji ili wahangaike kutafuta bao, bali waliupeleka pale walipoona kuna nafasi ya kujaribu kupiga golini au kupiga krosi yenye uwezekano wa kuzaa mabao.

Kilichonifurahisha zaidi ni jinsi kila mchezaji alivyowajibika kukimbia kuongeza idadi ya wachezaji eneo ambalo lilikuwa na mpira mara tu Al Ahly walipopokonya mpira. 

Hii iliwasaidia kuziba nafasi za kupitisha mpira haraka kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza ambayo hunufaisha sana timu kutoka Afrika Kaskazini kwa kuwa zina utaalamu nayo.

SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga

Kama kocha wao alivyonukuliwa, ndivyo wachezaji walivyoonyesha uwanjani. Rhulani Mokwena aliikosoa Al Ahly kwa kuanza kutoa malalamiko baada ya kupoteza mchezo wa kwanza, wakidai upangaji wa muda wa mechi na mambo mengine.

Kocha huyo alisema malalamiko yanaufanya ukubwa wa Al Ahly uondoke kwa kuwa timu kubwa hazina tabia hiyo.

Nidhamu ya mchezo

Katika mchezo wa pili, wachezaji wake walionekana kumuelewa. Hawakuhangaika sana na mwamuzi kila alipopiuliza filimbi na hata alipotoa penati kipindi cha kwanza, haikuwatoa mchezoni. Na kipa wao alipookoa, uimara wa akili yao ukaongezeka.

Kocha huyo aliwashukuru wachezaji wake, akisema unapocheza na Al Ahly mbele ya mashabiki 50,000, lazima ujue kuwa utahangaishwa sana usipokuwa na mpira.

“Tuliwaambia wachezaji kucheza pamoja na kusumbuka pamoja,” alisema kocha huyo ambaye timu yake pia bado iko katika hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa. “Tulijua tungepata uwezekano wa kumiliki mpira na kuwa imara zaidi.”

SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Hazina Haja Tena ya Kuhofia Yeyote Ligi ya Mabingwa

Kwa walioiangalia mechi hiyo wanaweza kuyaona maneno ya kocha katika uchezaji wa timu. Na ndivyo inavyotakiwa iwe. Hawakuwa na lawama nyingi kwa mwamuzi kila filimbi ipopulizwa na ndivyo inavyotakiwa; kuwa na nidhamu ya kufuata maelekezo na kucheza kwa kujituma wakati wote.

Najua kuna mambo mengi nyuma ya pazia yaliyofanyika kupata ushindi huo, hasa maandalizi ya kimwili na kiakili, jambo ambalo ni muhimu sana unapokutana na timu kutoka Afrika Kaskazini kwa kuwa wachezaji wana ujanja binafsi wa kimpira na uwezo mkubwa wa kuvuruga akili za wachezaji wa timu pinzani.

Lakini hayo ni machache tuliyoyaona kwa macho ya kawaida na ambayo huwa hatuyaoni sana wakati timu zetu zinapocheza mechi muhimu za kuamua timu inayosonga mbele au bingwa.

Kwa kifupi ni kwamba Mamelodi wametuonyesha angalau somo dogo la jinsi ya kuvaana na Al Ahly na hakuna shaka kwamba yapo mengi zaidi ya kujifunza kutoka kwa timu hiyo maarufu kama Brazil ya Afrika Kusini iliyogeuka kuwa mbabe wa miamba ya Afrika.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *