The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Timuatimua ya Makocha Imekuwa Mtindo Ligi Kuu

Tukiendelea na mtindo wa kutimuatimua makocha, tutakuwa tunalea vikundi vya wachezaji ambavyo vina wasimamizi wa mazoezi na si wataalamu wa kufundisha soka.

subscribe to our newsletter!

Moses Basena ameingia katika orodha ya makocha wa klabu za soka za Ligi Kuu ya Bara waliopewa mkono wa kwaheri hata kabla ya msimu wa 2023/24 kumalizika baada ya Ihefu kuachana naye mapema wiki hii.

Kocha huyo raia wa Uganda amedumu kwenye klabu hiyo ya mkoani Mbeya kwa siku 50, yaani takriban miezi miwili ambayo katika hali ya kawaida asingeweza kufanya makubwa kuiondoa timu hiyo katika janga la kutopata ushindi tangu ilipoishinda Yanga mabao 2-1 Oktoba 10 kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Ushindi huo pekee na vipigo na sare zilizofuata zimetafsiriwa kwa dhihaka na wapenzi wa Yanga na wengine kuwa ni laana, hasa baada ya Ihefu kuvuruga mwenendo wa Yanga wa kutoshindwa katika mechi 49 msiomu uliopita na mwaka huu kuwa timu ya kwanza kuwalaza mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.

SOMA ZAIDI: Ni Fedheha Klabu Zetu Kushtakiwa FIFA

Lakini kilicho wazi ni ukweli kwamba katika muda wa miezi miwili ambao Basena aliipokea timu ikiwa mashindanoni, ni miujiza pekee ingeweza kumpa matokeo mazuri katika ligi ambayo imeshapamba moto. Labda mkataba wa Basena na Ihefu ulijaa malengo ya kufurahisha ambayo aliyakubali bila ya kujali uhalisia.

Hata hivyo rekodi yake si mbaya sana. Katika mechi saba alizoisimamia timu, alipoteza tatu na kutoka sare nne. Matokeo hayo si mabaya kwa timu ambayo imefundishwa na makocha watatu, akiwemo John Simkoko ambaye aliisimamia katika mechi mbili tu, huku Katwila akiisimamia katika mechi nne.

Basena anaungana na makocha wengine kadhaa walioachwa na klabu zao, akiwemo Zuberi Katwila ambaye Mganda huyo alipokea mikoba yake Ihefu karibu miezi miwili iliyopita. Wengine ni Mwinyi Zahera ambaye alitimuliwa na klabu ya Coastal Union mwezi uliopita baada ya mfululizo wa matokeo ambayo hayakufurahisha.

Pia yumo Roberto Oliveira, maarufu kwa jina la Robertinho, ambaye alitimuliwa na Simba baada ya timu yake kuruhusu kipigo cha mabao 5-1 mbele ya watani wao wa jadi, Yanga Novemba 5, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Kabla ya kipigo hicho, mashabiki walionyesha kutofurahishwa na mwenendo wa timu licha ya kushinda mechi zake za Ligi Kuu, lakini uongozi ulisimama imara, ukisema cha muhimu ni ushindi.

SOMA ZAIDI: Mamelodi Wametoa Somo kwa Yanga, Simba

Pia yumo Hans van Pluijm aliyetimuliwa na Singida United mapema msimu huu baada ya matokeo mabaya. Aliyemfuata Ernst Middendorp hakudumu muda mrefu. Tofauti na wengine, Middendorp aliamua kutimka akidai kuwa alikuwa anaingiliwa katika majukumu yake. Alidai kuwa alikuwa akiulizwa sababu za kupanga wachezaji fulani na kuwaacha wengine na hivyo kuhofia kuwa itafikia muda atapangiwa kikosi.

Mwingine ni Mmarekani Melis Medo ambaye alitimuliwa na Dodoma Jiji kwa sababu kama hizo za wenzake za kutopata matokeo mazuri.

Pengine mikataba huwa si migumu sana kiasi kwamba inakuwa ni kitu chepesi tu kumtimua kocha, lakini ingekuwa ni ile inayozingatia mambo muhimu, klabu nyingi zingekuwa katika matatizo ya kifedha kwa kuwa zineshtakiwa na kupewa ile adhabu ya kufungiwa kusajili hadi zikamilishe malipo kwa wataalamu hao. Zipo zilizopelekwa Fifa na kuamuliwa ziwalipe fidia makocha ziliowatimua.

Sitaki kwenda huko sana, langu leo ni malengo ya klabu wakati wa kuajiri makocha. Ni wazi kuwa malengo ya Tabora United hayawezi kulingana na malengo ya Simba na hivyo mkataba wa kocha anayeajiriwa na klabu hiyo iliyopanda daraja msimu huu lazima uakisi suala hilo. Kwamba Tabora United inataka kuhakikisha inabakia Ligi Kuu msimu huu kwa kuwa ndio kwanza imepanda.

SOMA ZAIDI: Huu ni Wakati Muafaka Kuanzisha Wakala wa Viwanja Vya Michezo

Na ili kufikia malengo hayo, kuna mambo tutakayokuwa tunaangalia kila baada ya muda fulani kulingana na sera ya klabu hiyo. Tabora United kupoteza mechi nne kati ya kumi ilizocheza, haiwezi kuwa tatizo kubwa sana kulingana na mazingira ya michezo hiyo.

Lakini hiyo ni ngumu kwa Simba ambayo ina uzoefu kwenye ligi ya juu ya nchi na zaidi ya yote imewekeza fedha nyingi katika kupata wachezaji bora na benchi la ufundi lililosheheni wataalamu. Kupoteza mechi mbili kwao ni tatizo kubwa.

Lakini sababu za kocha anayefukuzwa Dodoma Jiji, au Ihefu au Coastal Union zinakuwa ni zilezile zilizotumika kumtimua kocha Simba au Yanga.

Ile Mtibwa tuliyozoea kuiona ikisakata soka safi huku kikosi kikiwa kimejaa vijana wanaochipukia, sasa haifurahishi tena kuiangalia. Kupoteza mechi nyumbani au ugenini imekuwa kitu cha kawaida. Ule utamaduni wa kujenga kikosi cha vijana waliokuzwa kuanzia chini, haupo tena. Ule utamaduni wa kuegemea kwa makocha waliopitia timu hiyo wakati wakicheza soka, haupo tena.

Mtibwa imeingia kwenye mtindo wa kuajiri makocha ili watimuliwe. Baada ya mechi tano za msimu huu, Mtibwa ilimtimua kocha wake Habib Kondo baada ya kumuajiri mwezi Julai. Angalau alikuwa na muda wa kuanza maandalizi ya msimu na timu iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita.

Kwa idadi kubwa ya makocha walioondoka kabla ya awamu ya kwanza ya Ligi Kuu kumalizika, ni wazi kwamba utimuaji wataalamu hao sasa umegeuka kuwa mtindo na viongozi wamepata kichaka cha kufichia ubovu wao.

SOMA ZAIDI: Kocha Singida Amedokeza Tatizo Kubwa la Soka Letu

Kwamba hatukusajili vizuri, kwamba hatukuwa na maandalizi mazuri ya msimu, kwamba maslahi ya wachezaji si mazuri na mambo mengine mengi si tatizo la viongozi. Ili kutuliza mashabiki, ni muhimu mzigo abebeshwe kocha. Ndio mtindo wa kisasa.

Kwa hali hii klabu zitakuwa zinalea vikundi vya wachezaji na wasimamizi wa mazoezi, na si walimu wa kuweza kujenga timu ya aina fulani, yenye staili fulani ya uchezaji, yenye uimara sehemu fulani. Kwa kuwa walimu hawapati muda wa kujenga timu za aina hiyo na kwa muda mfupi wanaokuwa kwenye timu, ni dhahiri kuwa wanachoweza kufanya ni kusimamia mazoezi na si kufundisha mbinu na mikakati.

Kocha ambaye atajaribisha kufundisha mbinu, halafu zikashindwa kufanya kazi kwenye mechi mbili au tatu, ni lazima atakumbana na fagio la chuma. Anachoweza kufanya ni kupanga wachezaji alioona wanamvutia mazoezini na kuwahamasisha kucheza kwa juhudi, kila mmoja kwa uwezo wake na si kulingana na mbinu za kitimu. Huo muda wa kufundisha mbinu haupo.

Ni muhimu sana viongozi wa klabu wakawa na malengo halisia wakati wa kuingia mikataba na makocha ili kutowabebesha walimu mizigo mizito inayowaweka katika mazingira magumu ya kutumia utalaamu wao.

SOMA ZAIDI: Kocha Amrouche Ametoa Majibu ya Kapombe, Tshabalala, na Fei Toto Uwanjani

Makocha wanahitaji muda kujenga timu kiufundi, kimbinu na kisaikolojia. Klabu zinazokaa na makocha kwa muda mrefu, ndizo ambazo hujenga timu imara. Yanga imefanya hivyo kwa Naredine Nabi ilipovumilia matokeo mabaya ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho msimu wa kwanza hadi ikajenga timu iliyoshika fainali msimu uliopita.

Manchester City ni timu nyingine iliyomvumilia kwa misimu mitatu kocha wake Pep Guardiola ikisubiri mafanikio katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na ikafanikiwa msimu uliopita. Lakini jirani zao, Manchester United bado wanahangaishwa na mwenendo wake unaoyumba kutokana na kutosimama imara na kocha mmoja.

Arteta ni kocha mwingine ambaye ni ushuhuda tosha wa mafanikio yanayotokana na kutoyumba katika benchi la ufundi. Aliikuta timu katika hali mbaya, lakini sasa Arsenal inazungumzwa kama moja ya timu zinazoweza kutwaa ubingwa msimu huu.

Kwa hiyo tunahitaji klabu ambazo zinajenga timu kwa kuwa na benchi la ufundi lisilobadilikabadilika bila ya sababu za msingi. Tukiendelea na mtindo wa kutimuatimua makocha, tutakuwa tunalea vikundi vya wachezaji ambavyo vina wasimamizi wa mazoezi na si wataalamu wa kufundisha soka.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *