The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hongera Hersi Said, Kazi ni Kuziamsha Klabu Afrika

Hersi atapaswa achore ramani ya wapi Chama cha Klabu Afrika kielekee, kuwa na maono ya changamoto zinazoweza kutokea na njia ya kuzitatua, na kuonyesha chama kitakuwa wapi miaka mitano ijayo.

subscribe to our newsletter!

Wakati tuko kwenye mchakato wa kuanzisha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kuna viongozi wachache sana wa klabu walikuwa wanajua umuhimu wa chombo hicho na mara nyingi walisisitiza hata kuzunguka kwenye vyombo vya habari kuzungumzia hilo.

Unaweza kusema pengine walikuwa na maslahi binafsi ya kuchukua uongozi wa chombo hicho baada ya kuundwa kwa jinsi walivyokuwa mstari wa mbele. Lakini pia walijua umuhimu wa klabu kuendesha wenyewe ligi na kuondokana na uendeshaji unaofanywa na Shirikisho la Soka (TFF) ambao mara nyingine hutawaliwa na siasa.

TPLB ilikuwa ni chombo kilichotazamiwa kuwa mwokozi wa klabu katika uendeshaji wa mashindano na mipango ya maendeleo, lakini kimekuja kuwa chombo mithili ya kamati ya kusimamia ligi na si chombo huru chenye mipango yake mingi ya kuendeleza klabu katika uongozi, programu za maendeleo kwa vijana, wanawake na watoto, ualimu, usimamizi wa fedha, stadi za masoko na zaidi ya yote kuwa sauti kuu na pekee ya klabu za Tanzania katika kupigania maslahi ya klabu.

Pengine muundo wa uongozi uliokubaliwa ndiyo ulirudisha nyuma baadhi ya watu waliojipa jukumu la uanaharakati wa kupigania chombo huru cha kuendesha ligi. 

Sharti kwamba mgombea wa nafasi za uongozi wa TPLB ni lazima awe mwenyekiti wa klabu au mtu mwenye wadhifa wenye mamlaka yanayolingana na mwenyekiti ndilo lililorudisha nyuma wale waliokuwa mstari wa mbele kudai chombo huru cha kuendesha ligi.

SOMA ZAIDI: CHANETA Imetufikirisha Kuhusu ‘Goli la Mama’

Na tangu hapo ile misuli ambayo TPLB ilitazamiwa kuwa nayo ikasinyaa ghafla na hadi leo chombo hicho hakionekani kama kina nguvu zozote.

Sababu kubwa yaweza kuwa ni kutokana na chombo hicho kuanzishwa na TFF badala ya msukumo wa klabu zenyewe. Baada ya Azimio la Bagamoyo la mwaka 2007, klabu zilikubaliana kuunda chombo hicho. Lakini hadi wakati wa kupitia upya maazimio ya bagamoyo mwaka 2011, hakuna kilichofanyika. 

Klabu zilipoulizwa, zikasema kila zikijaribu kuitisha kikao, hakuna anayehudhuria na ndiyo maana hakuna kilichofanyika.

Klabu zikamuomba rais wa TFF aunde kamati ambayo ingepewa jukumu la kuunda TPLB na ndipo ilipoundwa Kamati ya Mashindano iliyokuwa na uwakilishi mzuri wa klabu na ilichukua mwaka mmoja kuunda chombo hicho ambacho sasa ni TPLB.

SOMA ZAIDI: Ni Fedheha Klabu Zetu Kushtakiwa FIFA

Lakini TPLB inasimama kama sauti ya klabu? Au nayo iko juu kama chombo ambacho mamlaka yake hayatokani na ridhaa ya klabu? Hapa ndipo tatizo lilipo. TPLB imegeuka kuwa chombo kilicho juu ya klabu na ambacho kimeundwa na TFF na si kwamba kimeundwa na klabu zenyewe. Sauti ya TPLB haitofautiani na TFF na hivyo klabu hazina kimbilio.

Kuanzishwa kwa ACA

Mazingira hayo ndiyo yameunda Chama cha Klabu za Afrika (ACA) ambacho uanzishwaji wake umetokea ndani ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Hakukuwa na klabu zilizoona umuhimu wa kuunganisha sauti zao kutetea maslahi yao katika uendeshaji wa soka hadi CAF ilipoona kuna haja ya kuziunganisha.

Inaonekana rais wa CAF, Patrice Motsepe, ambaye ni mmiliki wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ndiye amekuwa chachu kubwa ya kuanzishwa kwa ACA, pengine ni kutokana na jinsi alivyoshuhudia uendeshaji wa mpira wa miguu wakati akiwa msimamizi wa moja kwa moja wa Mamelodi kabla ya kuiachia familia yake majukumu.

Kama klabu hazikuona umuhimu wa kuwa na sauti moja na hata kujua umuhimu wa kushirikiana katika maendeleo, ni dhahiri kuwa rais wa kwanza wa chama hicho, Hersi Said, ambaye ni mwenyekiti wa Yanga, atakuwa na kazi ngumu ya kuziamsha klabu kuona umuhimu wa ACA na kuiunga mkono.

Klabu za Afrika hazina mwamko mkubwa katika kuhakikisha nguvu yao inatambulika kwa waendeshaji wa soka. Nyingi zinasubiri kama zawadi maamuzi ya CAF au Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) na si kusimama kupigania haki zao.

SOMA ZAIDI: Kelele kwa Mangungu ni za Kukariri, Tatizo ni Kubwa Simba

Katika mechi za kwanza za makundi za Ligi ya Mabingwa wa Afrika, baadhi ya klabu ziliathirika kutokana na wachezaji wao kuwa na mechi za timu zao za taifa karibu siku tatu kabla ya kurudi klabuni kucheza mechi za kimataifa. 

Baadhi ya wachezaji walikosa kabisa mechi kwenye klabu zao, wengine kutumika mwishoni mwa mchezo, huku wale waliocheza muda mwingi wakicheza chini ya kiwango.

Haya ni mambo ambayo CAF na ACA ni lazima iyaangalie mapema ili klabu ziwe kamilifu zinaposhiriki mashindano yake. Pia, upo mgawanyo wa fedha, hasa kwa klabu ambazo wachezaji wake hufanikisha michuano ya CAF. 

Mfano, klabu zinastahili asilimia fulani ya mapato pale wachezaji wake wanapoziwezesha timu zao za taifa kufika hatua za juu za fainali za AFCON. 

Chama cha Soka Ulaya (UEFA) kimeingia makubaliano na Chama cha Klabu Ulaya (ECA) kuwa klabu ambazo wachezaji wake wataziwezesha timu zao za taifa kufika hatua za juu kama robo fainali, nusu au fainali kupata malipo ya siku ya kila mchezaji aliyeshiriki hatua hiyo. Yaani mfano mshahara wa Dola za Kimarekani 4,000 kwa siku kwa kila mchezaji.

SOMA ZAIDI: Mamelodi Wametoa Somo kwa Yanga, Simba

Hii hukata makali ya kiuchumi kwa klabu na kuwafanya waendeshaji soka kutambua umuhimu wa klabu katika uendeshaji wa michuano yao.

Majukumu ya Hersi

Hersi Said atakuwa na jukumu la kupambana na CAF kuhakikisha klabu zinanufaika na faida ambayo shirikisho hilo la soka Afrika hupata katika mashindano yake ya timu za taifa.

Hersi pia atakuwa na jukumu la kuhakikisha ACA inakuwa na programu za mafunzo ya uongozi, uongozi wa shule za soka, utafutaji masoko, usimamizi wa fedha na zaidi ya yote kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya soka, hasa viwanja vya mechi na mazoezi, jambo ambalo ndio ahadi yake kuu kwa wanachama wa Yanga.

Si picha nzuri kuona mechi nyingi za klabu na timu za taifa zinachezwa nje ya mataifa yao eti kwa sababu nchi hizo hazina viwanja vinavyofikia viwango vya CAF na FIFA. Hii inaua kabisa unazi na inaondoa ile dhana kwamba shabiki ni mchezaji wa 12.

Mechi nyingi za michuano ya klabu zinachezwa Uwanja wa Mkapa na licha ya kwamba wachezaji wengi nyota wanakuja kucheza na watu maarufu wanazifuata, uwanja unakuwa mtupu kwa sababu timu zote ni ngeni kwenye Uwanja wa Mkapa.

SOMA ZAIDI: Kanuni za Ridhaa Zinaondoa Ushindani wa Haki Kwenye Soka. Bodi ya Ligi, TFF Ziziondoe

ACA haiwezi kuhusisha klabu zote Afrika kuwa wanachama wake, bali kutengeneza mfumo ambao utawezesha kila nchi kuwa na wanachama kulingana na mafanikio yake katika mashindano ya kimataifa. 

Yaani Tanzania haiwezi kuwa na wanachama wanane ACA, wakati timu zake zinaishia robo fainali ya mashindano ya Afrika. Ni lazima utengenezwe utaratibu wa kuziwezesha nchi kuongeza idadi ya wanachama kulingana na mafanikio kimataifa.

Ni vizuri kwamba Hersi amechukua uenyekiti wa ACA mwanzoni na hivyo ndiye anayetakiwa kuchora ramani ya wapi chombo hicho kielekee, kuwa na maono ya changamoto zinazoweza kutokea na njia ya kuzitatua, na kuonyesha chama kitakuwa wapi miaka mitano ijayo.

Yapo mengi ya kuzungumza na najua Hersi ameshayaona mapema. Cha muhimu ni kumpongeza Hersi kuwa mwenyekiti wa kwanza wa Chama cha Klabu Afrika, kuwa Mtanzania wa kwanza kushika wadhifa huo. 

Kazi ni ngumu na ina changamoto kubwa. Hivyo, kazi yake ya kwanza ni kuziamsha klabu za Afrika kuona umuhimu wa chombo hicho ili atakapoanza harakati nyingine, Afrika imuelewe na ielewe kuwa klabu ndiyo nguzo ya maendeleo ya soka na hivyo zinastahili zinachokipigania.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *