The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tufurahie Uenyeji AFCON 2027 Tukisuka Mikakati

Ingawa miaka minne inaonekana mingi, shughuli ya maandalizi ni nzito na inahitaji kujituma sana kufanikisha hilo.

subscribe to our newsletter!

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) hapo Jumatano, Septemba 27, 2023, ilizipa nchi tatu za Afrika Mashariki —Kenya, Uganda na Tanzania—haki ya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika za 2027 (AFCON 2027) baada ya mataifa hayo kuwasilisha ombi la pamoja la kuwa wenyeji wa mashindano hayo makubwa barani.

Hii inamaanisha kuwa nchi hizo, ambazo chombo chake cha Baraza la Soka la Afrika Mashariki (CECAFA) ni kikongwe kati ya mashirikisho yote ya kikanda, zitaandaa mashindano hayo makubwa kwa mara ya kwanza tangu yaanzishwe.

Kenya, Uganda na Tanzania zimekuwa zikifuzu kwa shida sana kucheza fainali hizo hadi uamuzi wa CAF wa hivi karibuni wa kuongeza idadi ya timu zinazoshiriki kutoka 16 hadi 24, kitu kinachomaanisha kuwa karibu nusu ya nchi za Afrika zinashiriki na hivyo uwezekano wa kufuzu kufikia karibu asilimia 50 kwa kila nchi.

Hii itamaanisha kuwa Tanzania ina uhakika wa kushiriki kwa mara ya nne kwenye fainali hizo baada ya wiki mbili zilizopita kufuzu kucheza fainali za mwaka 2023 zitakazochezwa nchini Ivory Coast mwezi Januari, 2024.

CAF inataka nchi inayoandaa fainali hizo iwe na angalau viwanja viwili vinavyoweza kuchukua kuanzia watu 40,000, viwanja vingine viwili vinavyoweza kuchukua hadi watu 20,000 na vingine viwili vinavyoweza kuchukua hadi watu 15,000. Sharti hilo ni rahisi kwa nchi tatu kuandaa kwa pamoja.

Tanzania ina uwanja wa kisasa kabisa wa Benjamin Mkapa, ambao ulitumiwa kwa fainali za Afrika za vijana walio na umri wa chini ya miaka 17 miaka minne iliyopita, wakati Kenya ina Uwanja wa Kimataifa wa Moi, maarufu kama Kasarani, uliotumika kuandaa Michezo ya Afrika (All Africa Games) ya mwaka 1987, huku Uganda ikiwa na Uwanja wa Mandela, maarufu kama Namboole.

Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sasa umefungwa kwa ajili ya ukarabati ambao utauweka katika hali nzuri zaidi, wakati viwanja vya Mandela na Moi vilishafungwa mwaka 2010 kwa ajili ya matengenezo kama hayo.

Faida

Kupewa uenyeji wa fainali hizo kuna faida nyingi kimichezo na kiuchumi. Kwa mataifa 24 kupangwa katika makundi manane, ni dhahiri kuwa kila nchi itakuwa na uhakika wa angalau kuwa na makundi mawili, jambo linaloongeza umuhimu wa nchi kuwa na angalau viwanja vitatu kwa kuwa mechi za mwisho za makundi huchezwa kwa wakati mmoja.

Labda tatizo itakuwa ni kugombea mechi muhimu ambazo ni za ufunguzi na fainali. Lakini sina shaka kwamba Tanzania, kutokana na unazi mkubwa uliopo, itapewa mechi ya fainali kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam, jiji ambalo lina ushabiki mkubwa wa soka.

SOMA ZAIDI: Kocha Singida Amedokeza Tatizo Kubwa la Soka Letu

Na kitendo cha hivi karibuni cha mashabiki wa klabu za Simba na Yanga kuzifuata kwa wingi timu zao zilipokuwa zinacheza ugenini, mechi za Ligi ya Mabingwa wa Afrika, kitajenga hoja zaidi ya kupewa mechi ya fainali kama taifa lenye wendawazimu wa soka.

Kimpira, nchi hizi zitapata tiketi ya moja kwa moja kushiriki fainali hizo kama wenyeji na hivyo kuongeza uzoefu wake kwenye mashindano hayo ambayo yamekuwa yakitawaliwa na mataifa ya Afrika Kaskazini, kama Misri, Algeria, Morocco na Tunisia, pamoja na mataifa ya Afrika Magharibi, kama Nigeria, Cameroon, Senegal na Ghana.

Ni kwa nadra sana Zambia ilifurukuta na kutwaa ubingwa huo, ikiwa ni moja ya mataifa kutoka nje ya kanda hizo mbili kutwaa ubingwa.

Baada ya kushiriki fainali hizo mara nne (na Ivory Coast mwakani), hakuna shaka kwamba malengo ya Tanzania hayatakuwa kuvuka hatua ya makundi, bali kwenda juu hadi angalau fainali.

Tupange mikakati

Mbali na ushiriki, kupewa uenyeji huo kunamaanisha kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linalazimika kukaa chini kuangalia itazitumiaje fainali hizo kuendeleza soka lake, kukuza unazi na kutangaza situ soka lake, bali pia wachezaji.

Huu ni wakati wa kuanza kupanga programu hizo ambazo husaidia pia wadau wakuu kwenye soka kibiashara, kuona fursa za kuja kuwekeza nchini katika programu zitakazokuwa zimeandaliwa. Fainali za mwaka 2023 nchini Ivory Coast hazitakuwa na mwamuzi hata mmoja kutoka Tanzania, vipi wakati tutakapoziandaa?

SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga

Ni miaka minne, na hasa mitatu, kwa ajili ya kujiandaa ili kuwa na fainali zenye mafanikio zitakazoongeza kitu kwenye soka letu, ambalo linategemea sana wachezaji kutoka nje kulinogesha, wakati mataifa yanayokuja yameweka kiwango kidogo cha wageni.

Kiuchumi, tunatarajia kufurika kwa watalii ambao watakuwa wanafuatilia fainali hizo na hivyo kuchangia katika kuongeza pato la taifa. Kwa nchi 24 kuja na vikosi vyenye watu hadi 40 kila kimoja si jambo dogo. Hawa watahitaji kula, kunywa, kusafiri na kuburudika, kitu kinachoongeza uhakika wa pato.

Hao ni sehemu tu ya kundi lenye uhakika wa kuja. Bado kuna mashabiki ambao huzifuata timu zao, mashabiki wenye wendawazimu wa soka ambao hufuata mpira wenyewe, wapo watafutaji vipaji, wapo watu wa masoko na wengine wengi ambao hujazana kwenye nchi kwa ajili ya kufuatilia fainali hizo na mambo yanayoambatana nazo.

Na kwa utamaduni wa CAF, pia hualika watu maarufu kwa ajili ya kuja kutia joto kwenye michezo hiyo. Nakumbuka fainali za mwaka 2006 nchini Ghana kulikuwa na watu kama Jose Mourinho, Lothar Matheus na Marcel Dessailly ambao walialikwa kutia joto.

Watu hawa maarufu huambatana na wasaidizi na wapambe wao ambao tafsiri yake ni kipato kwa taifa. Hapa pia mchezo wenyewe unatakiwa umejiandaa kwa ajili ya kliniki ambazo zinaweza kuendeshwa na malejendari hawa kabla na wakati wa fainali hizo.

Fainali hizo pia zitaleta idadi kubwa ya waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, ambao mbali na kuripoti michezo hiyo, watakuwa pia wakiangalia mambo mengine ambayo ama yanaweza kuitangaza nchi au kuiharibia iwapo hatutakuwa tumejiandaa vizuri.

Maandalizi makubwa

Kuna faida lukuki za kuwa mwenyeji wa fainali hizo, lakini kunahitajika maandalizi makubwa na hilo litafanikiwa kama tutakuwa na kamati imara ya nchi ya kuandaa fainali hizo, au local organising committee (LOC), itakayoundwa mapema.

Uzoefu unaonyesha kuwa LOC kwa ajili ya fainali za U-17 haikufanya kazi vizuri kwa sababu nyingi na hivyo makosa yaliyotokea wakati ule hayana budi kutibiwa wakati huu.

Wakati mwingine kujaza wakuu wa taasisi bila ya kuwepo watendaji, hudhoofisha kamati na matokeo yake ni kazi za kukimbizana mwishoni mwa maandalizi.

SOMA ZAIDI: Kocha Amrouche Ametoa Majibu ya Kapombe, Tshabalala, na Fei Toto Uwanjani

Kutojiandaa vizuri pia kuna athari zake. Miaka minne iliyopita, Cameroon ilipokonywa uenyeji wa fainali hizo kutokana na kutokamilika mapema kwa matengenezo na ujenzi wa viwanja. Ni kitu kizuri kwamba Rais Samia Suluhu Hassan amepongeza kupewa fainali hizo kwa kuagiza matengenezo ya uwanja wa Sheikh Amri Abeid na ujenzi wa uwanja mpya jijini Dodoma ufanyike mapema.

Hiki ni kitu muhimu kwamba salamu za pongezi zimeambatana na maagizo muhimu. Kwetu Watanzania, kusipokuwa na maagizo kama hayo kutoka kwa kiongozi wa nchi, watu watazungukazunguka tu hadi fainali zinakaribia.

Kwa kuwa kuandaa fainali hizo kunategemea sana mkono wa Serikali, tunategemea bajeti ijayo ya 2024/2025 itaonyesha mwelekeo wa Tanzania katika kujiandaa kwa fainali hizo.

Ukiacha Cameroon, mwaka 1982 Kenya ilipewa uenyeji wa Michezo ya Afrika, lakini hadi inakaribia Uwanja wa Moi, au Kasarani, haukuwa tayari. Majaribio ya kuhamishia michezo hiyo nchini Zimbabwe na baadaye Afrika Kaskazini, hayakufanikiwa na michezo hiyo haikuchezwa hadi 1987 wakati Kenya ilipokuwa tayari.

Kwa jinsi mataifa kama Morocco, Algeria, Misri, Afrika Kusini na sasa Cameroon yalivyo na miundombinu imara ya michezo, nafasi hiyo ya kuahirisha mashindano haipo tena. Tumeona Cameroon ilipokonywa haki hiyo na Misri ikapewa.

Maandalizi ni kazi

Ingawa miaka minne inaonekana mingi, shughuli ya maandalizi ni nzito na inahitaji kujituma sana kufanikisha hilo. Haihitaji kudharau kwamba tutakuwa na mechi chache au wageni wachache. Tunahitaji kuonyesha kuwa Tanzania ni taifa la soka.

Hata kama tutafanikiwa kuwa na viwanja vizuri, bado ubora wa kuandaa fainali hizo utategemea mambo mengine kadhaa. Uwanja wa Benjamin Mkapa hauna sehemu ya kutosha ya maegesho ya magari. Ni magari machache yanayoweza kuruhusiwa kuingia. Hili litachafua taswira ya nchi, hata kama uwanja utakuwa bora sana.

Yale mambo ya kuegesha lori kubwa mwanzoni mwa Chuo cha Elimu cha Chang’ombe kuzuia magari, ni mbinu za kijima mno tunazotakiwa tuondokane nazo kwa kuandaa utaratibu bora wa kudhibiti magari.

SOMA ZAIDI: Kukosa Uvumilivu Kunaigharimu Azam FC?

Kibaya zaidi, hata ambao huamua kutotumia magari binafsi, hukumbana na tatizo kubwa. Hakuna kituo kwa ajili ya mabasi ya umma kinachoweza kuwapunguzia mashabiki usumbufu. Kituo kinachojengwa sasa kiko umbali wa takriban kilomita moja kutoka uwanjani.

Na kukiwepo na mechi maana yake ni usumbufu kwa chuo, ofisi zilizo eneo hilo na wakazi wanaoishi maeneo ya jirani.

Uwanja wa Azam, ambao umekuwa ukitumika sana siku hizi, hauna miundombinu bora ya usafiri ya kuwezesha mashabiki kufika na kuondoka uwanjani mapema. Hilo ni ombi ambalo lilitolewa na uongozi wa kampuni ya S.S Bakhresa tangu wakati ukifungiliwa mwaka 2012.

Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ndiyo kabisa hauna maegesho wala viti kwa mashabiki. Uwanja uko katikati ya mji, na hivyo jaribio lolote la kuweka maegesho litatakiwa lihusishe ulipaji wa fidia kwa biashara nyingi zinazozunguka eneo la uwanja.

Angalau uwanja utakaojengwa Dodoma unaweza kuzingatia hayo yote na nchi kuwa na uwanja mwingine bora baada ya ule wa Mkapa.

Hatuna budi kufurahia kuwa sehemu ya wenyeji wa fainali za Afcon 2027, lakini changamoto nilizozitaja hapo awali na nyingine hazina budi kuanza kushughulikiwa sasa ili Tanzania iibuke kuwa muandaaji bora kati ya mataifa matatu yaliyopewa haki hiyo!

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *