Mwaka mwingine umeanza na watoto wanatarajia kurudi shuleni kuendelea na masomo yao. Ni dhahiri kuwa kama mzazi, ulikamilisha majukumu yako kwa mwanao wakati wa likizo, kwanza kwa kuwa na muda wa kutosha nae na pia kwa kumuandalia mahitaji yake ya muhimu kwa ajili ya kurejea shule.
Hebu tuyaangazie mambo muhimu ambayo mzazi unapaswa kuendelea kufanya kwa ajili ya mtoto wako akiwa shuleni.
Kwanza, endelea kuwa na uhusiano wa karibu na mtoto. Ikiwa mwanao anasoma shule ya bweni jitahidi kumtembelea mara kwa mara kulingana na taratibu za shule, kuzungumza nae na kumjulia hali.
SOMA ZAIDI: Je, ni Upi Umri Sahihi wa Kumpeleka Mtoto Shule ya Bweni?
Kama anasoma shule za kutwa hakikisha unashiriki nae chakula cha jioni na unapata muda wa kutosha wa kumuuliza kuhusu siku yake, masomo yake na hata kumsaidia na kazi za nyumbani alizopewa shule.
Katika mazungumzo yenu mueleze mtoto wako jinsi unavyoamini jitihada zake katika masomo na kwa namna gani anapaswa kuendeleza juhudi zake ili afanye vizuri zaidi. Hii itamjengea kujiamini na uthubutu katika masomo yake. Pia, muelezee kuwa anapaswa kuchagua marafiki sahihi wanaopenda masomo na ajitahidi kuzingatia ratiba yake ya kila siku, shuleni na nyumbani.
SOMA ZAIDI: Je, Unafahamu Asilimia 80 ya Malezi ni Mahusiano Kati ya Mzazi na Mtoto?
Kama mtoto wako anasoma shule ya kutwa, basi mzazi una jukumu la kujenga mazingira yanayomhamasisha kujifunza akiwa nyumbani, unaweza kufanya hivyo kwa kuhakikisha ana sehemu inayofaa ya kusomea, vifaa vya kujifunzia, huku ukifuatilia kazi zake za nyumbani ili kuhakikisha anaelewa kile anachofundishwa shuleni.
Pia, hakikisha unaendelea kuwa na mahusiano mazuri na walimu wa mtoto wako ili uweze kufahamu maendeleo yake shuleni, kwani wao ndio hutumia muda mwingi zaidi nae kuliko wewe.
Usiache kuendelea kumtimizia mwanao mahitaji muhimu katika safari yake ya elimu. Kama anasoma shule ya kutwa unapaswa kumpa nauli na pesa ya kununulia chakula au kumfungashia chakula kila siku, kumnunulia vitabu, mavazi ya michezo, kumlipia masomo ya ziada (kama atahitaji) ili afanye vizuri zaidi.
SOMA ZAIDI: Mtoto Anapaswa Kuwafahamu Wazazi Wake, Ndugu na Familia Tandaa
Ni vizuri pia kujenga malengo na kupanga mikakati ya elimu na mtoto wako. Je, angependa kutimiza lengo gani katika masomo yake ndani ya mwaka? Je, kuna somo ambalo linamsumbua na angependa kuliongezea jitihada?
Watafiti wanaamini kuwa watoto wengi ambao wamejipangia malengo hua na motisha kubwa zaidi kutimiza malengo hayo.
Hivyo basi, unaweza kumuuliza maswali haya kisha mkapanga mikakati inayofaa ili mtoto aweze kufikia malengo yake. Pia, mnaweza mkawa na malengo ya pamoja, mfano; akipata alama flani katika masomo yake basi utampatia kitu flani, au mtafanya jambo flani pamoja. Hii itawahamasisha kuweka juhudi zaidi.
Kama mwandishi mahiri Tony Robbins alivyosema ‘’Kuweka malengo ni hatua ya kwanza katika kugeuza kisichoonekana kuwa kinachoonekana.’’
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.
One Response
Makala imenisaidia sana katika shughuli zangu za utangazaji , naomba tuwasiliane ili tuwe na mikakati zaidi ya elimu ya malezi kwa watoto wetu
Mimi ni Grace Munuo
Chombo ; Redio Sauti ya Injili Moshi
Namba 0768196582