Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupitia taarifa yake kwa umma, imeeleza kwamba kuanzia Januari 2024 imebadili mfumo wa kusimamia sera ya fedha, au monetary policy, kutoka mfumo wa kudhibiti mzunguko wa fedha kupitia ujazi wa fedha kwenda mfumo wa riba ili kudhibiti mfumuko wa bei nchini.
Kupitia taarifa hiyo, mfumo huo, kwa Tanzania, utatambulika kama Mfumo wa Riba wa Benki Kuu.
Ieleweke kuwa moja ya jukumu la msingi la Benki Kuu ni kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi. Kwa kipindi kirefu, ili kudhibiti mfumuko wa bei, BoT imekuwa ikitumia mfumo wa kudhibiti ujazi wa fedha kwenye uchumi.
Kwa mfano, fedha zikiwa nyingi katika mzunguko ikilinganishwa na uzalishaji mdogo wa bidhaa na huduma kwenye uchumi husababisha bei za bidhaa kuongezeka. Hivyo, Benki Kuu hulazimika kutumia mbinu mbalimbali kupunguza ujazi wa fedha katika mzunguko ili kudhibiti mfumuko huo wa bei.
Katika mfumo mpya wa kutumia riba, iwapo kutakuwa na mfumuko wa bei, Benki Kuu itapandisha riba yake, na pakiwa na mdororo wa uchumi itashusha riba.
SOMA ZAIDI: Yetu Microfinance Yafilisika, Yawekwa Chini ya Uangalizi wa Benki Kuu
Hivyo, mfumuko wa bei utadhibitiwa kwa kupandishwa na kushushwa kwa kizio cha Riba ya Benki Kuu (CBR) ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kizio cha Riba ya Benki Kuu, pamoja na vigezo vingine, vitatumika katika kuchakata riba katika benki za biashara. Hivyo, benki za biashara zitatumia riba hiyo kama kizio cha kukokotoa riba ya kumtoza mteja wao kwa kuzingatia vigezo na masharti ya mkopo husika.
Kizio cha riba ya Benki Kuu kikiwa juu, maana yake riba ya benki za biashara zitakuwa juu, hali itakayopunguza hamu na shauku ya wananchi kukopa vivyo hivyo, kwa kiasi cha mikopo inayotolewa. Hatua hii itapunguza ujazi wa fedha katika mzunguko na itashusha mfumko wa bei.
Iwapo uchumi utadorora, kwa kutumia mfumo huu, BoT itashusha kizio chake cha riba, suala ambalo litazilazimu benki za biashara pia kushusha riba zao. Kwa sababu riba zitakuwa chini, hii itachochea watu kukopa sana na kuweka fedha katika shughuli za uzalishaji wa uchumi.
Ieleweke kuwa mfumo huu haulengi kulazimisha benki za biashara kutoa kiwango fulani cha riba katika mikopo na amana, bado zitatumia njia zingine, kwa kuzingatia kizio cha riba cha Benki Kuu kupanga riba zake.
SOMA ZAIDI: Gavana Benki Kuu: Ni Muhimu Kuwa Makini Na Mikopo Ya Kibiashara
Kwa upande mwingine, mfumo huu utakuwa na athari za moja kwa moja katika ununuzi wa hati fungani za Serikali na zinazouzwa katika masoko ya pili mitaji na dhamana kwani thamani halisi ya ukwasi inategemea kizio cha riba cha Benki Kuu kilichowekwa kwa wakati huo.
Pia, mfumo huu hauondoi dhana zingine za lazima katika shughuli za kuongeza uzalishaji ili kukuza uchumi.
Oyuke Phostine Filemon ni mtaalamu wa mawasiliano na masuala ya fedha. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia phofiotho@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
3 responses
In practice, central banks often use a combination of CBR adjustments and money supply manipulation to achieve their inflation targets. The choice of which tool to prioritize depends on various factors like the specific nature of the inflation, the state of the economy, and the central bank’s overall monetary policy framework
Somo zuri Sana Ahsante kwa Somo. Hii ya Riba sikuwa naijua zaidi ya regulators zingine kama government bonds etc.
Ni lini riba za mabenki zitashuka na kufikia “Single digit”?