Search
Close this search box.

Usajili Dirisha Dogo Ni Kwa Ajili ya Kuziba Mapengo Tu

Ni lazima timu zetu ziwe na picha halisi ya nini zinakwenda kufanya wakati wa dirisha dogo. Haitakiwi kumwendea kila mchezaji anayeonekana kung’aa kwa sababu tu muda unaruhusu kusajili.

subscribe to our newsletter!

Wakati Mbwana Samatta anahamia Ligi Kuu ya England, Watanzania wengi walifurahia, si kwa sababu amepata timu kubwa, bali kijana wao kipenzi alikuwa anakwenda kwenye moja ya ligi kubwa duniani na maarufu kuliko zote.

Hakuna aliyeangalia mustakabali wa maisha yake England, bali nafasi finyu aliyopata na ambayo ni nadra kwa mchezaji kutoka kanda yetu ya Afrika Mashariki kuipata. Na mtu aliyeonekana kuwa na mawazo tofauti na mpango huo alionekana shetani, asiyemtakia mema nyota wetu.

Nilikuwa mmoja wa waliofurahia Samatta kupata timu England lakini ambao hawakupenda mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba ajiunge na Aston Villa wakati wa dirisha dogo.

Ndiyo. Ni kwa sababu dirisha dogo limewekwa kwa ajili ya kuziba nafasi zilizotokea baada ya mikikimikiki ya duru la kwanza la msimu. Kwamba mchezaji aliyekuwa akitegemewa katika safu ya ushambuliaji amepata jeraha litakalomuweka nje kwa takriban miezi mitatu na hivyo asajiliwe wa kuziba pengo hilo.

Ni kweli kwamba anayesajiliwa kuziba pengo kwa wakati huo anaweza kufanya vizuri kiasi cha kumzuia aliyekuwa majeruhi arejee kikosi cha kwanza moja kwa moja baada ya kupona, na ikiwezekana ampore namba kabisa.

Nadra

Lakini mara nyingi, hiyo hutokea kwa nadra sana. Ndiyo maana usajili wowote mkubwa hufanyika mwanzoni mwa msimu. Mipango yote ya msimu husukwa kwa kuangalia wachezaji waliotafutwa mwanzoni mwa msimu na kusajiliwa ili wabebeshwe mikoba ya klabu hadi msimu unapoisha.

SOMA ZAIDI: Waamuzi Zanzibar Wametia Doa Kombe la Mapinduzi

Ndiyo maana kwa wenzetu huwezi kusikia majina makubwa yakitajwa wakati wa dirisha dogo, bali wakati wa usajili mkubwa. Leo Kylian Mbappe anaelekea kumaliza mkataba wake na Paris Saint Germain, lakini si kipindi hiki cha dirisha dogo. Kuhama kwake kunazungumziwa mwishoni mwa msimu.

Kwa hiyo, haikuwa sahihi kwa Samatta wakati ule kuharakisha kwenda Aston Villa kuziba kwa muda nafasi ya mshambuliaji ambaye alikuwa majeruhi kwa kuwa huyo ndiye aliyekuwa kwenye mipango ya muda mrefu ya kocha wa klabu hiyo. Ndiyo maana alipopona tu, Samatta hakuwa muhimu tena kwa sababu kazi yake ya kuziba nafasi ilishaisha.

Ndiyo maana nasema dirisha dogo si kipindi cha kufanya usajili mkubwa, bali kuziba mapengo yaliyoonekana awamu ya kwanza ya msimu, la sivyo klabu zetu zitakuwa zinayumba kila mara kwa sababu wachezaji wanapoanza kuelewana ndipo viongozi wanapoleta wapya wengine na hivyo kuanzisha upya kazi ya wachezaji kuelewana.

Hekaheka

Ukiangalia usajili wa dirisha dogo ulivyokuwa na hekaheka hapa nchini, utafikiri kuwa msimu ndiyo kwanza unaanza. Timu hazikuwa zinaziba mapengo, bali zinasajili upya kana kwamba kipindi cha usajili mkubwa cha katikati ya mwaka jana hakukuwa na usajili wowote.

Kati ya klabu zilizofanya makubwa kipindi cha usajili mdogo ni Ihefu FC ya mkoani Mbeya, ambayo ilitangaza kuachana na wachezaji watano, Simba iliyotangaza kuacha wachezaji sita, wakiwemo washambuliaji wawili wa kigeni, Moses Phiri na Jean Baleke.

SOMA ZAIDI: Kamati ya Hamasa Bila ya Mkakati wa TFF

Kana kwamba haikuwa na mshambuliaji iliyekaa naye angalau kwa miaka miwili, Simba ilitangaza kusajili washambuliaji wapya wawili, Freddy Michael Kouablan wa Ivory Coast na Omar Jobe wa Gambia. Pia, imemsajili kiungo wa pembeni, Saleh Karabaka, ambaye alijaribishwa katika Kombe la Mapinduzi.

Singida Fountain Gate ndiyo imetia fora, ikiwa imewaweka sokoni wachezaji saba na kuwatoa kwa mkopo wengine wawili.

Yanga, ambayo haikuwa imepata mshambuliaji sahihi wa kati baada ya kuondoka kwa Fiston Mayele, imesajili washambuliaji kutoka Cameroon na Nigeria, kiungo kutoka JKU Zanzibar na kumpandisha beki mmoja aliyeng’ara Kombe la Mapinduzi.

Ukiangalia klabu hizo na nyingine kama Namungo, Mashujaa, Coastal na KMC, utaona kuwa hekaheka za usajili zilikuwa kubwa kana kwamba ndiyo kwanza zilikuwa zinaanza usajili mpya, kumbe ni kuziba nafasi ambazo zilijitokeza kama mapungufu wakati wa awamu ya kwanza ya msimu huu.

Kuyumbisha timu

Kwa maana nyingine, rasilimali kubwa sana zinatumika wakati wa dirisha dogo kiasi cha kuziyumbisha timu, huku makocha kwa baadhi ya timu wakiingia na kutoka.

SOMA ZAIDI: Simba Iongeze Muda wa Maoni Marekebisho ya Katiba

Ni malengo ya mamlaka za mpira duniani kuwa klabu ziwe na timu zenye wachezaji wanaokaa pamoja kwa muda wa kutosha ili kujenga vikosi imara, lakini kwa utamaduni kama huu wa kuhangaika kila wakati wa usajili ni wazi kuwa ni vigumu kujenga timu yenye uimara unaotokana na wachezaji wake kukaa pamoja na kocha kuweka mikakati yake ya muda mfupi na mrefu.

Ni lazima timu zetu ziwe na picha halisi ya nini zinakwenda kufanya wakati wa dirisha dogo. Haitakiwi kumwendea kila mchezaji anayeonekana kung’aa kwa sababu tu muda unaruhusu kusajili. 

Ni muhimu kuwa na maelewano naye ya muda mrefu ili aanze na timu msimu mpya na si ajiunge na timu kwa sababu tu anapatikana wakati hakukuwa na nafasi kwake kupata muda wa kucheza.

Kama ni mchezaji mwenye kipaji ameonekana na kuna umuhimu wa kuwa naye, basi awe ni yule wa malengo ya muda refu, au kwa maana nyingine, mchezaji chipukizi ambaye hatarajiwi kuingia kikosi cha kwanza mapema, bali anatarajiwa kukuzwa na kupata uzoefu kutoka kwa wabobevu kabla ya kuanza kupata muda wa kucheza.

Mchezaji wa aina hii aweza hata kununuliwa na kupelekwa timu nyingine kwa mkopo ili apate nafasi kikosi cha kwanza kwa lengo la kumkomaza na kumpa uzoefu. Ndivyo walivyofanya Arsenal kwa Saliba walipomchukua kutoka Real Madrid na moja kwa moja kumpeleka Ufaransa ambako alipata nafasi Olympique Marseille na aliporudi Arsenal alikuwa ameshakomaa.

SOMA ZAIDI: Kila la Heri Maandalizi ya Stars AFCON 2023

Fedha nyingi zinazotumika kusajili nyota wa nje na kuwalipa fidia wakati wanapoachwa, zingetumika kwa busara zingeweza kukuza vijana wetu badala ya rasilimali hizo kupotea bure kwa sababu ya ufahari, huku kukiwa hakuna mipango madhubuti kwenye klabu.

Ni muhimu kwa wamiliki na viongozi wa klabu kuanza kutumia dirisha dogo kwa busara kuliko linavyotumika hivi sasa. 

Kama timu itajielekeza kuziba nafasi mbili au tatu zilizotokana na wachezaji kuumia, au kutofikia matarajio, ni wazi itatumia rasilimali chache kusaka wachezaji wanaofaa kuliko hekaheka kubwa kutafuta mchezaji yeyote anayeweza kupatikana bila ya kufikiria mahitaji halisi ya timu na kocha.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *