The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wanahabari Wateta Namna Ya Kupata Kipato Kwa Kuuza Maudhui Mtandaoni

Pamoja na mitandao kuonekana kuwa ni fursa lakini bado kuna changamoto kwa Watanzania kuwa tayari kulipia kununua maudhui

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wadau wa habari nchini Tanzania wamekutana kwa pamoja kuzungumza juu ya umuhimu wa kutumia fursa za kimtandao kuuza maudhui yatakayoweza kusaidia uendeshaji wa vyombo vya habari.

Haya yamezungumzwa katika mjadala uliondaliwa na kampuni ya Mwananchi Communication katika mtandao wa X zamani ukitambulika kama Twita.

Moja ya changamoto iliyoibuliwa na wadau ni ukata unaokumba  vyombo vingi vya habari, hali inayofanya wengi wasiweze kuhudumia wafuatiliaji wake kwa namna inavyofaa.

Kampuni ya Mwananchi imeelezea kwa upande wake kuwa tayari imeanza kuuza maudhui yake mtandaoni.

“Maudhui yanaweza kuwa ni biashara kwenye vyombo vya habari, tayari kampuni ya Mwananchi imeanza kuuza maudhui mtandaoni,” alieleza Victor Mushi ambaye ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi.

Ubora wa Maudhui

Wadau wengi wameelezea kuwa kuna uwezekano wa watu kununua maudhui kama yatakuwa na ubora ukilinganisha na maudhui yanayopatikana bure.

“Najiuliza je itawezekana walaji tukanunua maudhui ambayo yako kwenye mfumo wa kunukuu jambo lile lile kwa upande wa bure na upande wa kulipia?” alihoji David Kusori, mmoja wa wachangiaji katika mjadala huo.

Kusori aliendelea kusisitiza kuwa vyombo vya habari havijafanya uchunguzi juu ya aina ya maudhui ambayo yatauzwa mtandaoni, “Ni kweli maudhui mtandaoni ni biashara ila bado hakuna uchunguzi wa nini walaji wanataka kwenye vyombo vya habari.”

Kwa upande wake Dastan Kamanzi  ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation, taasisi inayohusika na kuvijengea uwezo vyombo vya habari ameeleza kuwa wengi wanaoandaa maudhui hawazingatii suala la biashara na kwamba jamii inataka nini.

 “Wakati wa kufanya hayo maudhui ni vyema kuangalia ubora wa bidhaa kwa wahusika na ukweli ni kwamba bidhaa zetu za kihabari zinaweza kununulika na je kuna maslahi ya umma kwenye hayo maudhui,” alihoji Kamanzi.

Changamoto Katika Jamii

Moja ya changamoto iliyoibuliwa ni udogo wa kipato ambao unawakumba Watanzania wengi hali iliyowajengea kuamini kuwa maudhui ni bure.

“Watanzania wengi wanaamini kuwa maudhui ni bure na wanaendelea kufikiria suala hili kama haki yao kupata bure,” alieleza Fredrick Bundala ambaye ni mmiliki wa chombo cha habari mtandaoni cha Simulizi na Sauti. “Ila hio sio sawa ni vyema nao waweze kuchangia kidogo ili kuendeleza a juhudi za kupata hayo maudhui yaliyobora,” alisisitiza Bundala.

Bundala alieleza kwa sasa sehemu kubwa ya mapato ya chombo chake anayapata mtandaoni kupitia mfumo wa matangazo ya Youtube.

Ili kutibu tatizo hili la jamii yenye ugumu katika kulipia kwa maudhui, wadau wameshauri suluhu ni kutafuta maudhui ambayo jamii haiwezi kusema Hapana, maudhui ambayo yatakata kiu ya watu kuhusu mambo yanayowazunguka, kuhusu serikali, taasisi, jamii zao na hata mambo yenye utata.

 “Tunaweza kuuza maudhui kama ambavyo Kenya na  Afrika Kusini  walivyoanza  kuwa na mfumo wa kulipia maudhui mtandaoni ambayo ni maudhui yenye ukubwa na utofautI. Sasa inalazimika kuzalisha maudhui ambayo  yatawawagusa wananchi,”alifafanua Salome Kitaomari mwandishi mkongwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa Tanzania).

Serikali kupitia Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano Nape Nauye iliwahakikishia wadau kuwa milango yake iko wazi kuzisikiliza juu ya masuala ya yanahusu maudhui ili kuwezesha uendeshaji wa vyombo vya habari.

“Niwahakikishe kwamba hakutakuwa na mgongano wa kimaslahi kwenye suala la kodi,sio kila pahali ambapo watu wanatengeneza pesa basi kutakuwa na kodi na hivyo hakutakuwa na mvutano wa kimaslahi kwenye suala la kuuza maudhui kwenye mtandao,” amesema Nnauye.

Waziri Nape alisisitiza juu ya umuhimu wa kujenga tamaduni mpya kwa Watanzania, “lazima tujenge utamaduni wa kuwaonesha watu wetu kuwa hakuna kitu cha bure na kwenye suala maudhui ni lazima tuweke wazi kwamba sio la bure,” alisisitiza Nnauye.

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *