Kila mtu ana mipaka yake binafsi yaani kwa kimombo tungeweza sema personal boundaries, ikiwemo watoto. Kuelewa na kuheshimu mipaka hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya watoto. Mipaka inaweza kuwawezesha watoto kujifunza kufanya maamuzi binafsi na sahihi, kujieleza, na kuwasiliana vizuri na wengine.
Mipaka inawaongoza watoto kujenga uwezo wa kusema ndiyo au hapana kwa mambo anayokubaliana nayo au asiyokubaliana nayo, na hivyo kujenga ujasiri na hali ya kujiamini na kujithamini. Kwa kujua mipaka yao, watoto wanaweza kujisikia salama na kuzitetea haki zao.
Watoto wanapaswa kuelewa jinsi ya kucheza na jinsi ya kusihirikiana na wenzao, wanapaswa wawe na uwezo wa kutambua mipaka yao wakiwa na rafiki zao wa kike au wa kiume. Wazazi au walezi tuna wajibu wa kuwafundisha watoto jinsi ya kutambua na kulinda mipaka hii.
SOMA ZAIDI: Unawezaje Kutambua, Kumlinda Mtoto Wako Dhidi ya Kuonewa na Wenzake?
Wengi wetu hudhani kwamba mipaka ni ile ya kimwili tu ndio tunapaswa kuwafundisha watoto, lakini kuna mipaka ya aina nyingi, kama ifuatavyo;
Mipaka ya kimwili; Mipaka hii huhusisha vitu vingi ikiwemo kumkumbatia, kumbusu, au kumshika mtu au mtoto bila ya ridhaa yake. Mipaka ya kimwili ni muhimu katika kuheshimu haki za kibinafsi, za watu wengine na kuzuia ukiukaji wa faragha zao.
Ni muhimu kumfundisha mtoto kuwa, kila mtu ana haki ya kusema ndio au hapana pale mtu akitaka kuvuka mipaka hii. Hii itamsaidia kuelewa na kuheshimu mipaka yake ya kimwili na ya wenzake, ili kujenga mahusiano yenye afya, salama na amani.
Mipaka ya kihisia; Hii inahusisha kutambua na kuheshimu kwamba kila mtu ana hisia, na hisia hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kuheshimiwa. Kuheshimu mipaka ya kihisia kunajumuisha kutoa nafasi kwa watu kuelezea hisia zao bila kuingiliwa, kudhalilishwa au kubezwa.
SOMA ZAIDI: Kama Mzazi, Umejiandaaje Kuimarisha Uhusiano na Mtoto Wako 2024?
Watoto wanapaswa kujisikia huru kuelezea jinsi wanavyojisikia juu ya mambo mabalimbali bila hofu ya kukosolewa, kubezwa au kutokuaminiwa. Kuheshimu mipaka ya kihisia kwa watoto kunajumuisha kuwasikiliza kwa makini, kuwapa nafasi ya kueleza hisia zao, na kuwasaidia wanapohitaji msaada. Hivyo mfundishe mtoto kuelewa na kuthamini hisia zake na za wenzake.
Mipaka ya muda; Hii inahusisha kuheshimu ratiba na mipango ya mtu iliyowekwa ndani ya muda flani. Kwa mtoto, kuheshimu mipaka ya muda ni kama kujua wakati gani wanapaswa kufanya mambo tofauti na kuwa tayari kwa mabadiliko.
Kwa mfano, wanaweza kujua kwamba baada ya kucheza kwa muda fulani, itabidi waendelee na shughuli nyingine na wasiwaburuze wenzao kwa kuwalazimisha au kuwashawishi kufanya mambo yaliyo nje ya ratiba zao.
Ni muhimu kuwafundisha watoto kuheshimu ratiba zao na kutokulazimisha mambo kwaona kwa wenzao bila sababu za msingi. Wanapojifunza kuheshimu mipaka ya muda, wanaweza kuwa na ufanisi zaidi na wanaweza kujisikia huru kufanya mambo wanayopenda ndani ya muda wao.
SOMA ZAIDI: Vitu Muhimu vya Kufanya Kwa Ajili ya Mtoto Wako Akiwa Shuleni
Mipaka ya kifedha: Watoto wanapaswa kuwa na nidhamu juu ya matumizi kwa kufundishwa kwamba hawawezi kupata kila wanachotaka . Wanapaswa kuelewa thamani ya pesa na jinsi ya kuweka vipaumbele katika matumizi yao.
Mzazi unaweza kumfundisha mtoto jambo hili kwa kumuelezea thamani ya vitu mnavyonunua kama familia na kwa vitu vyenye thamani kubwa anaweza kuweka akiba ili aweze kupata kitu hicho.
Kama tulivyosema hapo awali, jukumu la kuwafundisha watoto mipaka hii ni la mzazi na mlezi. Inatupasa kujitahidi kuwezesha na kusaidia watoto kuelewa umuhimu wa mipaka katika maisha. Kufanya hivyo kunaweza kuwasaidia kuepuka madhara ambayo wanaweza kukutana nayo wanapovuka mipaka.
Kufundisha watoto kuheshimu na kuelewa mipaka kutajenga msingi imara wa mahusiano bora na kuleta amani katika maisha yao ya sasa na huko mbeleni.
Anza kwa kujenga mazingira ya kuheshimiana nyumbani ili watoto waweze kujifunza kwa vitendo umuhimu wa kuheshimu na kutambua mipaka yao na ya wengine.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.