The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mahakama Imdhibiti DPP Kuondokana na Kero ya Futa Kesi, Kamata, Shitaki Upya

Kufuta mashitaka na kumkamata mtuhumiwa papo kwa papo, na baadaye kumshitaki upya kwa kosa lilelile, chini ya mamlaka ya kipekee na yasiyohojiwa, kumepelekea kesi za jinai kuchukua muda mrefu zaidi kukamilika.

subscribe to our newsletter!

Kumekuwa na manung’uniko ya dhati kuhusu mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP) kuondoa kesi za jinai Mahakamani na kuwashitaki watuhumiwa upya kwa kosa lilelile. Hali hiyo imepelekea kuchelewesha utoaji wa haki, na inaibua hoja kuhusu nafasi ya Mahakama katika kusimamia utoaji wa haki. Ninashauri Mahakama iimarishwe kimamlaka, na imdhibiti DPP.

DPP anapata mamlaka ya kuondoa kesi mahakamani kupitia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) (kif. 91), Sheria ya Mashitaka ya Taifa (kif. 9(1)), Sheria ya Mahakama za Mahakimu (kif. 33, kikisomwa pamoja na kif. 3(2)(c)) cha CPA) na Sheria ya Kuzuia Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupagwa (kif. 29(6)), katika mazingira tofauti tofauti. 

DPP atafanya hivyo kesi ikiwa katika hatua yoyote kabla ya hukumu. DPP hatakiwi kutoa sababu, isipokuwa hati ikielezea ‘hana nia ya kuendelea na kesi’ husika. DPP ameondoa kesi nyingi mahakamani kwa kanuni hiyo maarufu kama nolle prosequi, au kwa kifupi kama nolle.

DPP anaondoa kesi mahakamani kwakuwa ana dhamana ya mashitaka ya jinai ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hati ya nolle haibishaniwi endapo DPP amefuata utarabitu wa kuiwasilisha. Kwa hiyo, kuondoa kesi mahakamani kunaongeza ufanisi katika utekelezaji wa sheria. 

Pia, kulinda uhuru wa mtuhumiwa na kuondoa mashitaka ya hila. Kwamba, baada ya upembuzi, DPP asitishe mashitaka fulani kwa maslahi ya umma au haki. Hii ni kwa kuwa kesi za jinai zinafunguliwa wakati upelelezi haujakamilika. Kwa hiyo, nolle ni nafuu muhimu kimantiki.

SOMA ZAIDI: Rasimu ya Warioba Ina Majibu Yote Samia Anayahitaji Kuhusu Mfumo wa Haki Jinai

Utekelezaji wa sheria kupitia kanuni ya nolle, hata hivyo, umesababisha dosari zinazohujumu shabaha ya upatikanaji wa haki kwa wakati. Japo DPP anatakiwa kuwa na nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya mifumo ya haki, na kujali maslahi ya umma anapoendesha mashitaka ya umma, sawa na Ibara ya 59B(4) ya Katiba ya nchi, kuna walakini endapo azma hiyo inatimizwa katika matumizi ya nolle.

Futa kesi, kamata upya

Mathalani, kufuta mashitaka na kumkamata mtuhumiwa papo kwa papo, na baadaye kumshitaki upya kwa kosa lilelile, chini ya mamlaka ya kipekee na yasiyohojiwa, kumepelekea kesi za jinai kuchukua muda mrefu zaidi kukamilika. 

Vipo visa vya watu waliokaa muda mrefu gerezani, angalau miaka mitano hadi kumi na mbili. Wengi wao wameonja joto la nolle. Kesi inafutwa, unaachiwa huru, unakamatwa upya. Kesi itaonekana –ina namba– mpya, sawa na chai iliyotengwa katika kikombe kilekile.

Marekebisho ya CPA ya mwaka 2022 katika matumizi ya nolle yalitarajiwa kuleta unafuu. Sheria Nambari 1 ya mwaka 2022 ilirekebisha kifungu cha 91 cha CPA kwa kuongeza aya ya (3) yenye takwa la mtu anayeachiwa kwa nolle asishitakiwe isipokuwa panapokuwa na ushahidi wa kutosha kesi hiyo kuanza kusikilizwa mara moja. 

Vilevile, marekebisho yaliongeza kifungu 131A katika CPA chenye takwa la kuzuia kufungua kesi kabla upelelezi haujakamilika. Marekebisho hayo ya CPA, hata hivyo, hayakutoa majibu ya maswali kadhaa.

SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo Serikali Inavyoweza Kuuboresha Mfumo wa Haki Jinai Tanzania

Mosi, kwamba, watuhumiwa washitakiwe wapi? Suala hili ni muhimu sana. Linagusa mamlaka ya Mahakama. Na kimsingi, Mahakama za Mahakimu hazina mamlaka ya kusikiliza kesi ambazo zinasikilizwa kiupekee na Mahakama Kuu. 

Mfano, kesi zinazohusiana na makosa ya mauaji, uhaini, utakatishaji fedha, usafirishaji haramu wa binadamu, madawa ya kulevya, nakadhalika. Ukiachiwa ukakamatwa upya, mara zote, na sheria mpya haijaelekeza, utashitakiwa katika Mahakama zilezile ambazo hazina mamlaka ya kusikiliza kesi yako.

Pili, sheria haijaelekeza Mahakama zifanye nini ikiwa DPP hatazingatia takwa la kusababisha kesi isikilizwe mapema, au kushitaki kabla ya upelelezi. Na zaidi, hadi leo, mara baada ya kuachiwa na kukamatwa upya, watuhumiwa wanashitakiwa katika Mahakama zilezile zisizo na mamlaka ya kuwasikiliza. Wanatoswa hapo hadi pale DPP atakapoamua vinginevyo.

Kuna kisa cha mteja wangu. Alishitakiwa mwaka 2019 katika Mahakama ya Kisutu kwa tuhuma za kufanya biashara ya dawa za kulevya. Lakini mwaka 2022 aliachiwa kwa nolle kesi yake ikiwa hatua ya kusikilizwa katika ‘Mahakama ya Mafisadi.’ 

Alipoachiwa huru, alikamatwa upya akapelekwa Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam kwa siku chache. Baadaye akashitakiwa upya Kisutu kwa kosa lilelile. Tangu 2022 kumekuwa na danadana.

SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania

Awali walidai upelelezi haujakamilika. Baadaye wakadai mfumo unasumbua kufaili taarifa Mahakamani ya ama kumpeleka Mahakama Kuu asikilizwe au aachiwe huru. Hii ilichukua muda mrefu, zaidi ya miezi minne. Baadaye mwaka huu imedaiwa tena upelelezi haujakamilika. 

Haya yanatokea mteja wangu akiwa mahabusu gerezani, miaka mitano sasa. Kama kuna haki ya mtu inalindwa kwa mazingira haya, ni haki ya nani? DPP anabeba maslahi ya nani kwa kuendesha kesi namna hii?

Mzaha

DPP anafanya mzaha katika masisha ya watu kwa kufuta na kurejesha mashitaka upya kwa kosa lilelile, huku akijua Mahakama za Mahakimu hazina mamlaka ya kusikiliza (baadhi ya) kesi hizo. 

Anafahamu pia ni yeye pekee mwenye mamlaka ya kuamua kesi ipi isikilizwe na ipi iwekwe kando. Ukijaribu kwenda Mahakama Kuu kutafuta haki ni ama unamchelewesha zaidi mteja wako au utaambiwa unafanya uanaharakati. Ni ajabu!

Tatu, nafuu kwa waathirika wa matumizi ya nolle hazitolewi. Nitatoa mfano wa Enock na wenzake wawili. Waliingia mahabusu gerezani wakiwa watoto wa umri kati ya miaka 11 – 12. Wakatoka wakiwa na miaka kati ya 21-22. 

SOMA ZAIDI: Ucheleweshaji Kesi Mahakamani Unavyokwamisha Upatikanaji wa Haki

Katika miaka kumi waliyokaa gerezani, waliachiwa, kukamatwa na kushitakiwa upya kwa kosa lilelile kwa zaidi ya mara tatu. Ya nne wakaachiwa jumla, japo ilibidi ‘watoke nduki’ wakihofia kukamatwa upya. 

Lakini miaka kumi gerezani bila hatia, kwa misingi ipi? DPP alikuwa analinda maslahi, au haki, ya nani? Hakuna fidia kwa muda wote waliopotezewa wakiwa gerezani.

Na labda Mahakama, ni kwamba wanakuwa hawana historia ya shauri husika? Hapana. Hawajui wajibu wao? Hapana. Wana cha kufanya? Pengine, ndiyo. Lakini ni ajabu, na inafikirisha, kuwa na Mahakama ambazo zinatumiwa na DPP kuwatesa watu wasio na hatia kwa kesi za uongo, halafu baadaye anaielekeza Mahakama izifute. 

Kanuzi za utawala wa sheria, usawa mbele ya sheria, uhuru wa mtu, utawala bora, haziafiki tabia hii.

DPP adhibitiwe

Ninapendekeza kuwe na udhibiti wa matumizi ya kanuni ya nolle. Serikali iamuriwe kulipa fidia iwapo itaitumia vibaya Mahakama kuwaweka gerezani watuhumiwa kwa muda mrefu, na baadaye kuielekeza Mahakama iwaachie. 

SOMA ZAIDI: Je, Ni Haki kwa Serikali Kuwaweka Rumande Washtakiwa Halafu Kufuta Kesi Bila Kuwalipa Fidia?

Ninafahamu kwamba mtu aliyeshitakiwa kwa hila, akaachiwa, ana fursa ya kudai fidia. Hata hivyo, kigezo mojawapo cha kudai fidia hiyo ni lazima mtu huyo ashinde kesi. Mazingira ya nolle hayasadiki madai ya fidia.

Lakini, ni wangapi wana msuli wa kuidai fidia ya Serikali? Na je, ni kweli Serikali yetu inashitakika? Kwa waliokaa jela kiasi, uhuru huja kwanza, na kwa hiyo hawataona maana ya kusigana upya na Serikali yenye mabavu na mamlaka kupita kiasi ya kukurejesha jela na kukutelekeza huko. Watamshitakia Mola, na ndiyo mwisho wa biashara.

Haya yanatokea kwa kuwa DPP anaanzisha mashitaka – na kwa mashauri yasiyo na ukomo wa upelelezi, ndiye anaamua kesi ianze lini kusikilizwa. Katika muktadha huo, Mahakama haina lolote la kufanya ili kuharakisha upelelezi au usikilizwaji wa shauri. 

Hali kadhalika, mtuhumiwa hana chaguo zaidi ya kukaa mahabusu gerezani akisubiri huruma za DPP. Kwenye mazingira haya, kama kesi ni ya ‘maelekezo kutoka juu’ – nafahamu bado zipo – basi sahau kuhusu haki, kusikilizwa kwa wakati, au kutendewa kama binadamu. Utalazimika kukaa jela hadi DPP atakapoelekezwa afute kesi yako.

Kwa mazingira hayo, ninarejea wito wangu wa siku zote, kwamba Mahakama zirejeshewe na zitumie mamlaka yake ya kusikiliza maombi ya dhamana kwa makosa yote. Kuwe na ukomo wa upelelezi, na Mahakama itoe amri ya mtuhumiwa kuachiwa endapo upelelezi utachukua muda mrefu.

SOMA ZAIDI: Kuachiwa kwa Mbowe na Mapungufu ya Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania

Vilevile, tukaondokane na mazoea ya kuunda tume kuonesha kwamba kuna mchakato kuelekea mageuzi fulani fulani. Maana zimeundwa tume nyingi ambazo ripoti zake hazifanyiwi kazi. Inakuwa ni sawa na geresha, au kisogeza muda, au danganya toto. 

Mfano, tangu tupokee Ripoti ya Tume ya Haki Jinai ya Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, Serikali na Bunge hawajaona umuhimu wa kutekeleza mapendekezo yake ambayo kwa kiasi kikubwa ni mazuri.

Kwa hiyo, Serikali itimize wajibu wake, kuandaa Miswada inayoakisi mapendekezo ya tume hiyo. Bunge liichachafye Serikali kuelekea matarajio yetu. Vilevile, Mahakama iamke, itoke katika shimo kubwa ambalo imechimbiwa na Serikali. 

Ifike wakati Mahakama itumie mamlaka yake ya sasa, na kudai kurejeshwa katika nafasi yake ya kusimamia utoaji wa haki nchini, bila uoga wala upendeleo.

Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts