The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Theresia Dismas: Mwanamichezo wa Kwanza Kuipatia Tanzania Medali ya Kimataifa

Theresia Dismas aliipatia Tanzania Medali ya Fedha kwenye michuano ya kwanza ya Afrika, au The Inaugural All Africa Games, iliyorindima huko Jamhuri ya Congo, au Congo-Brazzaville, mnamo mwaka 1965.

subscribe to our newsletter!

Wanamichezo nchini, waliojaaliwa na Jalali talanta za michezo, wamekuwa wakishiriki michuano anuwai ya kimataifa ambayo imekuwa ikijiri kwenye nchi mbalimbali toka tupate uhuru, huku baadhi yao wakikonga nyoyo kwa kufanikiwa kutwaa medali za dhahabu, fedha na shaba.

Hata hivyo, ombwe lililopo kwa Watanzania lukuki ni kutomfahamu Mtanzania wa kwanza kuliheshimisha taifa hili kwa kutwaa medali ya kwanza ya kimataifa. Kutokana na ombwe hilo, nimewiwa kuifinyanga makala haya kwa minajili ya kuziba ombwe hilo. 

Hivyo, makala haya inamleta kwenu, wasomaji, mwanamichezo huyo aliyeweka rekodi hiyo kuntu ambaye ni mwanamke. Mwanamke huyo si mwingine bali ni Theresia Dismas, aliyeipatia Tanzania Medali ya Fedha kwenye michuano ya kwanza ya Afrika, au The Inaugural All Africa Games, iliyorindima huko Jamhuri ya Congo, au Congo-Brazzaville, mnamo mwaka 1965.

Kwa miaka mingi, nimekuwa nikifinyanga makala lukuki za Watanzania walioifanyia mengi nchi yetu lakini hakuna makala iliyonipa shida kuifinyanga kama hii ya leo kutokana na kukosekana kwa kumbukumbu za mwanamama huyu. Hakuna ofisi yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye taarifa za Mtanzania huyu wa kipekee. 

Aidha, mitandao ya kijamii na mifumo kadhawakadha, kama vile Google, ambayo vimekuwa kimbilio la wengi kupata taarifa za namna hii, vilishindwa kufua dafu! Hata pale nilipoamua kutumia sikanu yangu kuukuu kumvutia waya Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, ambaye alikuwa Rais wa Shirikisho la Riadha nchini kwa muongo mmoja, sikufanikiwa. 

Aidha, licha ya kutumia mbinu za medani na kuwasiliana na ‘wamba’ akina Filbert Bayi, Juma Ikangaa na Suleiman Nyambui, juhudi zangu ziligonga ukuta kwani wote walinihabarisha kuwa wanajua tu kwamba mwanamama huyo wa shoka ndiye shujaa aliyeiletea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania medali ya kwanza ya kimataifa lakini hawana taarifa zake zingine zozote!

“Nchi yetu ina tatizo kubwa la utunzaji wa kumbukumbu za Watanzania walioifanyia mambo ya kipekee pamoja na kumbukumbu kuhusu historia ya nchi yetu kwa ujumla,” Cleopa Msuya, Waziri Mkuu mstaafu, aliwahi kulalamika kwenye mahojiano yake na TBC mnamo Disemba 3, 2019. 

“Iwapo juhudi za makusudi hazitafanyika, hasa kwa vile kumbukumbu nyingi zimo vichwani mwa kizazi ambacho kinazidi kupukutika, upo uwezekano mkubwa wa nchi yetu huko mbeleni kuja kukosa kabisa taarifa muhimu kuhusu Watanzania wa tasnia mbalimbali waliotoa mchango mkubwa kwa nchi yetu pamoja na Historia sahihi ya nchi yetu,” alihitimisha Msuya ambaye nakubaliana naye moja kwa moja.

Licha ya changamoto hiyo kubwa, nilijiapiza kuwa ‘lije jua, ije mvua’ lazima kitaeleweka tu na maelezo ya mwanamama huyu, hata kama ni machache, yatapatikana tu. Hivyo, juhudi kubwa na uzoefu wangu kwenye nyanja ya utafiti vikapelekea niibuke na taarifa zitakazoweza kufanya Mtanzania kumjua, walau kwa kiasi fulani, mwanamama huyu ambaye kwa sasa ni Octogenarian, yaani mwenye umri kati ya 80 na 89.

Hivyo basi, kwa heshima na taadhima, nawaalika Watanzania wote, mliopo nchini pamoja na diaspora, mfuatane nami unyo kwa unyo ili muweze kumfahamu mwanamama huyo wa kipekee. Makala haya yanaanza kwa kuivinjari historia ya ushiriki wa wanamichezo wetu kwenye michuano ya kimataifa iliyohusisha wanamichezo wa michezo mbalimbali mara tu baada ya kupata uhuru.

Michuano ya kimataifa baada ya Uhuru

Tanganyika ilipata Uhuru wake Disemba 9, 1961, na Zanzibar Disemba 10, 1963, kabla ya wazalendo kufanya Mapinduzi na kutwaa nchi Januari 12, 1964.

SOMA ZAIDI: Elizabeth Maruma Mrema: Mfahamu Mtanzania Aliyetajwa Miongoni Mwa Watu 100 Mashuhuri na Jarida la TIME

Michuano yetu ya kwanza kushiriki baada ya Uhuru, iliyoshirikisha wanamichezo wa michezo mbalimbali, ilikuwa ni michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika huko Perth, Australia kuanzia Novemba 22, 1962, hadi Desemba 1, 1962. Michezo ya Jumuiya ya Madola hushirikisha mataifa ambayo mengi yalitawaliwa na Uingereza. Michezo hiyo iliasisiwa mwaka 1930.

Kwenye michezo hiyo ya mwaka 1962, tuliwakilishwa na wanariadha wawili: Paschal Mfyomi (Marathon) na John Akhwari (5,000M & 10,000M). Hatukuambulia medali yoyote kwenye michezo hiyo.

Mnamo mwaka 1963, Kamati ya Olimpiki ya Tanganyika (TOC) iliundwa. Moja ya majukumu yake makubwa ya awali ilikuwa  kufanya matayarisho ya wanamichezo wetu kushiriki michuano ya Olimpiki ya Tokyo, Japan kuanzia Oktoba 10, 1964, hadi Oktoba 24, 1964, ikiwa ni michuano  ya kwanza  ya Olimpiki kufanyikia barani Asia. 

Ili kushiriki michuano hiyo,  TOC ilitakiwa  iwe imetambuliwa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) ili wanamichezo wetu waruhusiwe kushiriki. TOC ikatambuliwa na IOC mwaka huohuo.

Kwenye michuano hiyo, Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliwakilishwa na wanamichezo wanne: Daniel Thomas (27) (400M); Mohammed Hassan Dyamwale (23) (800M); Paschal Mfyomi (22) (10,000M); na Omary Abdallah (21) (Marathon).

Kwenye michuano hiyo tuliambulia patupu na hatukuweza hata kutoka mrisi. Daniel Thomas, mmoja wa wanamichezo wetu walioshiriki, aliwahi kutiririsha mengi kuhusu  michuano hiyo, ikiwemo jinsi walivyokuwa washamba.

“Tuliweka kambi Chuo Kikuu. Wakati ule, kila kitu kilikuwa nyara za Serikali. Suti za michezo, raba na vifaa vya mazoezi vilikuwa vya Serikali na tuliporudi tulitakiwa kuvirudisha. Tulikuwa wageni kwenye kila kitu. Tulikuwa hatujui lugha, hivyo tulipohitaji nyama tulilazimika kulia kama mnyama halisi anavyolia mfano ng’ombe au kuku. Tulikuwa washamba,” alikumbuka Thomas. 

“Mimi nilizoea kukimbia pekupeku. Kwenye michuano hiyo ilikuwa lazma uvae raba. Nilihisi zinaniumiza  hivyo nikazivua kisirisiri lakini nilibambwa, kwa hiyo nikalazimika kuzivaa,” aliendelea. “Licha ya kutorudi na medali, tuliporejea, tulialikwa Ikulu na Rais [Julius] Nyerere na kupongezwa. Kitendo cha kushikwa mkono na Rais Nyerere kilinipa ustaa mkubwa kwetu Mara nilikokuwa mwalimu.”

Mwaka 1967 ikaundwa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) na mwaka huohuo ikatambuliwa na IOC. Hii iliwezesha wanamichezo wetu kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye michezo hiyo.

Michuano ya All-Africa Games 1965

Michuano ya mwanzo ya michezo mbalimbali barani Afrika, au All-Africa Games, ilifanyika Jamhuri ya Congo (Congo-Brazzaville) kuanzia Julai 18, 1965, hadi Julai 25, 1965.

SOMA ZAIDI: Simulizi za Wapiga Debe Wanawake Stendi ya Magufuli: ‘Sisi Siyo Mateja’

Wazo la kuanzisha michuano hii lilifikiwa kwenye kikao cha Baraza Kuu la Mawaziri wa Michezo na Vijana wa nchi mbalimbali za Afrika waliokutana nchini Senegal mwaka 1963 ambapo Congo-Brazzaville ilipewa jukumu la kuwa mwenyeji wa michuano ya mwanzo na kwamba iliazimiwa kuwa itakuwa ikifanyika kila baada ya miaka minne.

Aprili 22, 1965, Kamati ya Tanzania Amateur Athletic Association (TAAA) ilikutana jijini Dar es Salaam ambapo ilijadili na kutoa orodha ya awali  ya wanamichezo, au Tanzania’s Possibles kama orodha hiyo ilivyoitwa, watakaoweza kushiriki michuano hiyo. Katika orodha ya awali ya TAAA iliyokuwa na wanamichezo 11, jina la Theresia Dismas, aliyekuwa mwanafunzi Kowak, halikuwemo. 

Majina yaliyokuwemo ni: M.H. Chabanga (Dar es Salaam  800M); Omary Abdallah (Dar es Salaam 5,000M); Blas Peter (Dar es Salaam 1, 500M); M. Josiah (Arusha 400); V. Lubuva- (Dodoma 5,000M); P. Rugaimukamu (Bukoba- Pole Vault); James Wanda (Tabora- Mkuki); Paschal Mfyomi (Dar es Salaam-Maili  6); Bertha Victor (Mwanza- Mkuki); Mary Thomas (Kuruka Juu); na Edith Mhuto (Dar Es Salaam- mita 80 Kuruka Vihunzi).

Baadaye, orodha ya awali ilichambuliwa kama karanga na katika mchujo wa mwisho wa washiriki wa Tanzania kwenye michuano hiyo, TAAA ililazimika kutumia kigezo kilichoainishwa kwenye Kanuni za Kamati ya Ufundi ya All Africa Games ambacho kilieleza, kwa kimombo, “All participants must have broken the minimum standards between March 31, 1964 and April 1965.”

Kigezo hicho kilipotumika, na pia kwa kuzingatia suala la gharama, majina mengi yaliyokuwemo kwenye orodha ya awali yalisambaratishwa. Jina la Theresia likawemo kwani alikidhi kigezo hicho. Wanamichezo wengine wanne  walipenya kwenye mchujo huo mkali uliofanywa na TAAA ambayo ilitayarisha orodha mpya iliyokuwa na wanamichezo wafuatao: Norman Chihota; Omary Abdallah; Mwaisoni; Mary Thomas; na Theresia Dismas.

Stamford Nkondola ndiye alikuwa mkuu wa msafara. Aidha, kwenye msafara huo alikuwepo pia Halifa Abdallah ambaye alikuwa Afisa wa Michezo. Wanamichezo wote waliopata fursa hiyo adimu ya kuliwakilisha taifa walifanya matayarisho makubwa na walipewa na Serikali  kila msaada waliohitaji.

Hayawi hayawi huwa. Hatimaye, Theresia na wanamichezo wenzie waliochaguliwa kuliwakilisha taifa, waliondoka nchini kwenda Congo-Brazzaville kushiriki michuano hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu.

Wanamichezo hao wa Tanzania walijiapisha kuwa aslan abadan lazima wakaandike historia kwa kutwaa medali baada ya wenzao kushindwa kutwaa medali yoyote kwenye michuano ya Jumuiya ya Madola 1962 na ya Olimpiki 1964. Serikali iliwapatia suti na vifaa vingine kwa ajili ya michezo hiyo na kisha kuwakabidhi bendera ya taifa.

Theresia aupiga mwingi

Jumapili ya Julai 18, 1965, Alphonce Massemba Debat, wakati huo akiwa Rais  wa Congo-Brazzaville, alifungua rasmi michuano hiyo kwenye uwanja wa taifa wa nchi hiyo uliojaa hadi pomoni. Kwa hakika zilikuwa ni sherehe za kukata na shoka zilizofana vilivyo. 

Wanamichezo wa mataifa yote 30 yaliyoshiriki walipita mbele ya Rais huyo na kuzunguka uwanja. Wanamichezo wa Tanzania, wakiwa nadhifu ndani ya suti zao, walikuwa ni miongoni mwa wanamichezo hao.

SOMA ZAIDI: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria

Michuano ilipoanza kutimua vumbi, wanamichezo wa Tanzania walijitahidi sana lakini walikutana na upinzani mkali kutoka kwa wanamichezo wa mataifa mengine.

Theresia, aliyekuwa mrusha mkuki na ambaye hakuwemo kwenye orodha ya awali ya washiriki wa Tanzania iliyoandaliwa na TAAA Aprili 22, 1965, baada ya kuona wenzake waliomtangulia wakiwa wameangukia pua, alifanya jitihada kubwa ili alitoe kimasomaso taifa lake. Wahenga walinena, penye nia, pana njia. Hatimaye, Theresia alikonga nyoyo baada ya kuupiga mwingi.

Theresia, akitambua taifa linamtegemea, alifumba macho, akasali na kisha akauvurumisha mkuki umbali wa mita 40.24. Mshindani mwingine, Helene Okwara wa Nigeria, alitupa umbali wa mita 40.30. 

Hivyo, Helene akamzidi Theresia kiduuuchu kwa mita 0.6 tu. Helene akatwaa medali ya Dhahabu wakati Theresia akatwaa ile ya Fedha. Mshindi wa tatu alikuwa Angelina Anyikwa kutoka Nigeria aliyetupa umbali wa mita 39.48.

Nderemo, shangwe, vifijo na hoihoi zilitamalaki kwa wanamichezo wa Tanzania pamoja na viongozi walioambatana na Theresia kutokana na mafanikio hayo makubwa. 

Wanamichezo wa Tanzania, wakiwa na furaha kubwa na bashasha baada ya mmoja wao kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupata medali, waliwasili nchini baada tu ya michuano hiyo. Wanamichezo hao walialikwa Ikulu na Rais Julius Nyerere ambaye alimpongeza sana Theresia kwa kuliheshimisha taifa lake.

Kutokana na Theresia kuandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuliheshimisha taifa kwa kupata medali ya kwanza, alichaguliwa kuwa ‘Mwanamichezo Bora wa Mwaka 1965.’ Huyo alikuwa mwanamama wa kwanza kutwaa tuzo hiyo nchini.

Shindano la ‘Ladies First’

Kutokana na mwamko mdogo wa wanawake kwenye riadha licha ya mwanamke kuwa Mtanzania wa kwanza kuipatia Tanzania medali, Juma Ikangaa, mmoja wa wanariadha bora kabisa kuwahi kutokea nchini, mwaka 2017 aliasisi shindano kwa ajili ya wanawake, lililopewa jina la Ladies First Athletic Event. Shindano hilo bado linaendelea ingawa lilisimama kwa miaka kadhaa kutokana na janga la UVIKO-19.

Kwenye mazungumzo yake na mimi yaliyofanyika Februari 13, 2024, Ikangaa aliniambia: “Niliona licha ya mwanamke Theresia kuwa Mtanzania wa kwanza kutuletea medali, ushiriki wa wanawake umekuwa mdogo sana, hivyo nikaanzisha shindano baada ya kupata udhamini wa JICA [shirika la ushirikiano wa kimataifa la Japan].”

Theresia, kwa upande wake, baadaye alikuja kuolewa na raia wa Kenya. Wawili hao waliishi Marekani na kisha Kenya. Mwaka 2015, akiwa Kenya, Theresia alihabarisha kilichojiri mwaka 1965.

SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni

“Daima sitaisahau michuano ya All Africa Games ya mwaka 1965,” Theresia alisimulia. “Mimi wakati nashinda nilikuwa binti mdogo tu. Wakati ule, hamasa ya michezo ilikuwa kubwa sana na tuliandaliwa kwelikweli. Wachezaji hatukuipa kipaumbele fedha bali tuliamini medali ndiyo kila kitu.”

Kwa kweli, mwanamama Theresia Dismas ni shujaa wa taifa hili. Ni imani yangu kwamba kupitia makala haya, Watanzania wengi sasa wamemjua kwani, naamini, asilimia 99 walikuwa hawajawahi hata kumsikia.

Hata hivyo, nimalizie makala haya kwa kutoa rai kwa kamati ambayo huwa inapendekeza majina ya Watanzania wanaostahili kupewa tuzo siku ya Uhuru wa Tanzania Bara Disemba 9, ikiwapendeza walijumuishe jina la shujaa huyu.

Pia, anatoa rai kuwa ushauri kuntu uliotolewa na rais wa zamani wa riadha duniani, Sebastian Coe, hapo Machi 3, 2021, ufanyiwe kazi, ambapo alisema: “Litakuwa jambo jema kama Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ikawa na jumba la makumbusho ya wanamichezo mahiri walioliletea sifa taifa la Tanzania.”

Theresia, ambaye kwa sasa anaishi Uingereza na wanae, ni mmoja kati ya wanamichezo hao!

Mzee wa Atikali ni mwandishi na mchambuzi kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 754 744 557. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts