The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Simulizi za Wapiga Debe Wanawake Stendi ya Magufuli: ‘Sisi Siyo Mateja’

Kuhusishwa na vitendo vya kihalifu, kama vile wizi, na unyanyasaji wa kingono vimetajwa kama changamoto kuu zinazowakabili akina mama hao.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Maimuna Shaaban amekuwa akifanya kazi ya kupiga debe kwa kipindi cha miaka kumi sasa, akianzia Stendi ya Mabasi Ubungo na sasa anafanyia shughuli zake katika Stendi ya Magufuli baada ya stendi hiyo kuondolewa Ubungo na kupelekwa huko Mbezi Louis jijini hapa.

Maimuna, 40, anajivunia kazi yake hii anayoifanya kwa mapenzi makubwa, akisema hakuna kazi nyingine ambayo imekuwa ikimsaidia kuendesha maisha yake na yale ya watoto wake watatu mbali na kupiga debe.

“Mtoto wangu mkubwa wa kike ndiyo ameingia chuo mwaka wa kwanza, lakini huko kote alipopita pesa za kumsomesha na kuwapa mahitaji zimetoka kwenye kazi hii,” Maimuna aliieleza The Chanzo ilipokutana naye kwenye eneo lake la kazi. “Hii ni kazi yangu, naipenda kwani ndiyo inayonipa heshima.”

Maimuna siyo mwanamke pekee aliyeamua kujiingiza kwenye kazi ya kupiga debe ili aendeshe maisha yake. Janeth Elias ni mama wa watoto wawili ambaye amekuwa akifanya kazi hii kwa muda wa miaka sita sasa, akisema kazi hiyo imekuwa ikimpatia kipato kinachomsaidia kuendesha familia yake.

“Mimi hii kazi naiheshimu sana. Imenipa maisha. Bila hivyo, ningefanyaje?” Janeth, 36, alimweleza mwandishi wa makala haya. “Nakumbuka mwaka 2016, kuna kiwanda nilikuwa nafanyakazi wakapunguza watu. Sikuwa na sehemu ya kwenda. Ndipo mwenzangu mmoja alikuwa ajenti pale Ubungo wakati stendi ipo kule. Akanivuta kule, nikaanza kupata chochote.” 

SOMA ZAIDI: Usafiri wa Umma Unaweza Kuwa Rafiki Zaidi kwa Watu Wenye Ulemavu?

Janeth, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, anasema hakuwa na namna bali kuifanya hiyo kazi kwa ari yote maana alikuwa na mtoto mdogo aliyehitaji matunzo na baba yake hakuwa na utayari wa kumshughulikia.

“Nilizoea kazi hiyo, hata mwaka 2020, nilipojifungua mtoto wa pili, nilitulia nyumbani nikiwa na biashara yangu ya genge,” anaeleza Janeth kwa sauti inayoashiria ufahari. “Baada ya hapo, nilirejea tena, nipo mpaka sasa, na kwenye genge langu nimeweka mtu anaendelea.”

Rushwa ya ngono

Kama Janeth alilazimika kuingia kwenye kazi ya kupiga debe baada ya kupunguzwa kwenye kiwanda alichokuwa akifanyia kazi, kwa Salome Moh’d* ilikuwa ni kutaka kutunza heshima yake kama mwanamke kwa kukataa kutumia mwili wake kama tiketi ya kupata kazi.

Salome, 41, aliiambia The Chanzo kwamba matukio ya unyanyasaji wa kingono yamekithiri katika Stendi ya Magufuli, akiwataja maajenti kama wahusika wakuu wa vitendo hivyo vya kiudhalilishaji ambavyo vimekuwa vikilaaniwa kwa kurudisha nyuma maendeleo na ustawi wa wanawake walio wengi nchini.

“Wanataka wakutumie wanavyotaka, haja yao ikiisha wanakutimua [kwenye kazi], wewe jiulize, akishafukuzwa [mwanamke] anaenda wapi?” alihoji mama huyo. “Lazima uje kuungana na sisi hapa ambao tumekataa kabisa rushwa ya ngono.”

SOMA ZAIDI: Madereva Wanaobadili, Kukatisha Ruti Wawakera Abira Dar. LATRA Waonya

Salome anaeleza kwamba rushwa ya ngono imetamalaki katika stendi hiyo kiasi ya kupewa jina la Interview, au Usaili, kwani utayari wa mwanamke kutoa rushwa ya ngono ndiyo kigezo kikubwa cha kupata kazi tofauti na ile ya kupiga debe katika stendi hiyo.

“Kuna kipindi mpaka yaliibuka matukio ya ubakaji na ukifuatilia wahusika ni wao, lakini nani wa kusema?” alieleza Salome, akisema kwamba kuna watu ambao wanajulikana kama ‘Tembo’ au ‘Wazee wa Kitengo’ wanaojihusisha na vitendo hivyo.

The Chanzo ilimuuliza Salome, ilikuwaje mpaka yeye akaja Stendi ya Magufuli kutafuta kazi na kuishia kuwa mpiga debe?

“Mimi nilianza kufanya kazi hii baada ya kibanda changu kubomolewa kupisha upanuzi wa barabara pale stendi ya chini ya daladala Mbezi,” alijibu mama huyo. “Mimi nina watoto watatu na hii kazi ndiyo inafanya niwatunze maana mimi ndiyo baba [na] ndiyo mama, na ukiangalia, kwa asilimia kubwa ya wanawake tuliopo hapa, ndiyo tunatunza familia. Wengine ni wajane, wengine wameachiwa watoto. Mimi mnavyoona hapa sina mume, nafanya majukumu yangu, natunza watoto.”

Kupiga debe

Kwa wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam, wapiga debe ni watu ambao hukutana nao kwenye vituo vingi vya daladala, kazi yao kubwa ikiwa ni kuwaita abiria waingie kwenye gari fulani. Hapa Stendi ya Magufuli, wapiga debe husaidia makampuni ya mabasi kupata abiria, wakipata malipo fulani kwa kila abiria wanayepeleka.

SOMA ZAIDI: ‘Inatuumiza Sana’: Nyakua Nyakua ya ‘Nyau’ Kariakoo Yawakwaza Machinga

Licha ya wao kujiona kama watu wanaopambana na ugumu wa maisha, wakitafuta riziki za kutunza familia zao, kwa wananchi walio wengi wapiga debe hawana taswira nzuri. Sababu kadhaa hupelekea hali hii, kubwa ikiwa ni vitendo vya kihalifu, kama vile wizi, ambavyo vimekuwa vikihusishwa na wapiga debe.

Hali hiyo, ikichanganyikana na uwepo wa watu wanaosadikika kuwa ni waathirika wa matumizi ya madawa ya kulevya, maarufu kama ‘mateja,’ imeifanya kazi ya kupiga debe kuwa miongoni mwa kazi zinazodharaulika sana, huku wengi kati ya wanaofanya kazi hiyo wakishindwa kupewa heshima wanayostahiki.

Hapa Stendi ya Magufuli hali siyo tofauti sana kwani kumekuwa na malalamiko makubwa miongoni mwa watumiaji wa stendi hiyo kuhusiana na uwepo wa wapiga debe katika eneo hilo, hali inayoisukuma menejimenti ya stendi hiyo kutafakari mbinu za kukabiliana na uwepo wa wapiga debe hao.

Kwa mfano, Meneja wa Stendi hiyo, Isihaka Waziri, licha ya kukiri kwamba wapiga debe katika stendi hiyo wamekuwa na msaada kwa abiria, alidokeza changamoto za uwepo wa matukio ya wizi yanayowahusisha wapiga debe, hali inayowasukuma kudhibiti kazi hiyo.

“Kwenye stendi yetu wapo wapiga debe na siku hizi kumekuwepo na wimbi kubwa,” Waziri aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano. “Wale ambao wamekuwa na tabia ovu, ikiwemo wizi na uhalifu, tunawachukulia hatua kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, lakini [wapiga debe] wengi wamekuwa na msaada [kwa abiria].”

Changamoto

Maimuna alikiri kwa The Chanzo kwamba mtazamo huu hasi wa jamii juu ya kazi yao wao kama wapiga debe ni moja kati ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo na ambazo wanachukua mikakati ya makusudi kuhakikisha utatuzi wao.

SOMA ZAIDI: LATRA Itupie Jicho Bei za Vyakula Kwenye Vituo vya Abiria wa Mikoani

“Tumeanza kushirikiana kwa pamoja, tunapogundua kati yetu kuna ambaye ametenda jambo lisilo sawa, tunatoa taarifa kwa watu wa ulinzi shirikishi,” alisema Maimuna. 

“Watu wenye hiyo tabia wanajulikana lakini tunatoa taarifa ili wasitudhuru,” aliongeza. “Lakini wanaofanya hivyo mara nyingi ni wale wa kujichomeka [na] kujifanya nao ni wapiga debe kumbe kuna wanachokitaka.”

Maimuna pia aligusia changamoto nyingine wapiga debe wanawake wanakibiliana nayo kwenye stendi hiyo, akisema: “Unaweza kumuhudumia abiria, yeye akawa anakuchukulia kama unajiuza. Baada ya hapo anaanza kukutongoza, anakuona kama malaya. Sasa hii ni changamoto kama huna msimamo.”

Kwa upande wake, Janeth alilalamikia “kuvamiwa” kwa kazi yao na watu wenye nia tofauti na kupiga debe, akisema hali hiyo imeifanya kazi yao kuwa ngumu maradufu kwani watu hawawachukulii kama wachapa kazi bali kama vibaka.

“Wengi wamekuwa wakijipachika kwenye kazi hii kwa sababu hakuna usimamizi,” Janeth alisema. “Kikubwa, tunatakiwa kuwekewa utaratibu wa maeneo ya kukaa na wale wenye tabia tofauti wachukuliwe hatua kali za kisheria.”
Anthony Rwekaza ni mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia anthonyrwekaza9@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Ujumbe mzuri nadhani utakuwa umewafikia walengwa Maimuna,Janeth na wengine wametoa ushuhuda nadhani watakuwa mabalozi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *