The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Usafiri wa Umma Unaweza Kuwa Rafiki Zaidi kwa Watu Wenye Ulemavu?

Watu wenye ulemavu wamelalamikia kuachwa na daladala na kukosa viti wakiwa ndani ya daladala miongoni mwa changamoto nyingine nyingi wanazopitia.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Watu wenye ulemavu jijini hapa wamelalamikia manyanyaso na usumbufu wanaopata kila wanapotumia usafiri wa umma, hususan ule wa daladala, huku wakitoa wito kwa mamlaka za nchi kuingilia kati ili kuwapunguzia adha wanazokutana nazo wanapotumia huduma hiyo muhimu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii kwa nyakati tofauti, watu waishio na ulemavu wamelalamikia kukosekana kwa mazingira rafiki kwenye usafiri wa umma, ambayo hujumuisha mabasi yaendayo mikoani, hali waliyosema inawasababishia usumbufu wa hali ya juu.

Miongoni mwa malalamiko wananchi hao waliyaibua ni pamoja na kuachwa na daladala; kukosa viti wakiwa ndani ya daladala; kunyanyapaliwa na madereva na makondakta kwa kuitwa ‘jiwe’ kwa sababu hawalipi nauli; kunyanyaswa kingono kwa walemavu wanawake; miongoni mwa changamoto nyingine nyingi wanazokutana nazo.

Gervas Pastory, 58, ni mlemavu wa miguu ambaye amelalamikia daladala nyingi kuacha kuwabeba watu wenye ulemavu kutokana na ukweli kwamba raia hao huhitaji msaada ili waweze kupanda usafiri huo wa umma, kitu ambacho daladala nyingi hudhani ni usumbufu.

“Wakati mwingine wakitukuta vituoni hawatupakii, wanatuacha, maana wanajua mpaka ubebwe, upandishwe, na wanaona kama wanapoteza muda,” Pastory, baba wa watoto sita na mkazi wa kwa Mtogole, Temeke, anasema. 

SOMA ZAIDI: Wadau Wahimiza Ufikishwaji Elimu ya Uzazi kwa Vijana Wenye Ulemavu

“Madereva wengine wakishajua hatulipi nauli wanatuacha vituoni makusudi,” alibainisha Pastory kwenye mazungumzo hayo. “Sasa tunaomba Serikali itazame namna ya kutusaidia ili kuepukana na changamoto za namna hii; tunaumia sana lakini hatuna jinsi ya kujisaidia. Uchumi wetu siyo mzuri ningesema hata ninunue bajaji.”

Pendo Baraka, mlemavu mwengine wa mguu, anasema amelazimika kujichanga na kununua bajaji yake ili kuepukana na usumbufu aliokuwa anaupata anapotumia usafiri wa umma, hususan muda wa kwenda kazini. 

Pendo, mama wa watoto wawili anayeishi Goba, Dar es Salaam, anasema alikuwa anaweza kukaa kituoni mpaka akachelewa kazini, hali iliyokuwa inamfanya ahisi aibu kwa bosi wake. 

Bosi anakuonaje?

“Nilikuwa natoka nyumbani Goba saa moja kasorobo asubuhi kwenda maeneo ya Mbezi Beach Makonde, nafika saa mbili na nusu asubuhi au tatu, watu wanakuwa wameshaanza kazi,” Pendo, 38, anasema. “Fikiria hapo bosi kama siyo muelewa anakuonaje?”

Pendo amewasihi wamiliki wa usafiri wa umma, madereva, na makondakta waache kuwaangalia watu wenye ulemavu kama mzigo, mtazamo ambao anasema huwaongezea mzigo watu hao wenye mahitaji maalum na kufanya maisha yao yazidi kuwa magumu.

SOMA ZAIDI: ​​Madereva Wanaobadili, Kukatisha Ruti Wawakera Abira Dar. LATRA Waonya

Fredrick Msigara ni Mkuu wa Kitengo cha Ujumuishwaji wa Haki za Watu Wenye Ulemavu Kwenye Michakato ya Kimaendeleo, Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam, ambaye amezungumzia mateso wanayopitia watu wenye ulemavu wanapotumia mabasi ya mikoani.

“Kuna wakati mnapata huduma za chakula unatakiwa kwenda haja,” alisema Msigara ambaye pia ni mlemavu. “Wakati mwingine watu wenye changamoto ya ulemavu hujibana kwa kushindwa kutoka nje wakihofiwa kuachwa au kutumia muda mwingi; hii kibaiolojia ina madhara. Wengine wanaamua kutokunywa maji au kitu chochote ili kuepuka kushuka.”

Msigara pia amesema pia ili kukabiliana na chanagamoto hiyo inayoweza kuwatokea wakiwa wanasafiri, baadhi ya watu wenye ulemavu wanalazimika kusafiri na makopo kwenye gari ili ikitokea wanahitaji kupata huduma ya haja ndogo wanamaliza humo humo. 

“Jiulize, hii ni salama kweli?” anahoji Msigara. “Je, kwa wanawake mbinu hii ni rafiki kwao hata tukisema iwe hivyo?”

SOMA ZAIDI: ‘Nimeamua Kuacha Kesi, Nibaki na Binti Yangu’: Masaibu ya Waathirika wa Udhalilishaji Walemavu Zanzibar

Diana Mwakatundu ni mjasiriamali mwenye ulemavu na mkazi wa eneo la Tegeta Kwa Mpemba, Dar es Salaam, ambaye ameziomba mamlaka za jiji kuzimulika changamoto wanazokutana nazo kwenye usafiri wa umma ili waweze kufanya utaratabu wa kuzitatua.

“Natamani njia zote zingekuwa na mwendokasi lakini ndiyo hivyo haiwezekani,” Mwakatundu, 68, alimueleza mwandishi wa habari hii. “Siku hizi nikitaka kwenda kwenye daladala nalazimika kutafuta kijana anisaidie.”

Mwendokasi yapigiwa mfano

Mwendokasi umeelezewa kwa hisia tofauti na watu wenye ulemavu waliohojiwa kwa ajili ya habari hii, wengi wao wakipongeza namna miundombinu ya usafiri huo ilivyotengenezwa, wakisema imetengenezwa kwa kuzingatia mahitaji na maslahi yao.

Pia, mwendokasi ni eneo ambalo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Jonas Lubago, amezitaka mamlaka za nchi kuliangalia na kujifunza inapobuni miundombinu kwa ajili ya usafiri wa umma.

“Mfano mzuri wa kujifunza kuhudumia watu wenye ulemavu tunao hapa hapa Tanzania, hatuna haja ya kwenda kujifunza mbali sana,” Lubago alisema. 

“Tunaona miundombinu ya mwendokasi jinsi ilivyo,” aliongeza. “Hiyo ndiyo miundombinu ambayo ni fikivu. Popote duniani utakapoenda ambapo wanazingatia sana mazingira ya watu wenye ulemavu miundombinu yao iko kama hii ya mwendokasi.”

SOMA ZAIDI: Sababu Zinazowanyima Walemavu Haki za Kidijitali Tanzania Zatajwa

Mbali na kurekebisha miundombinu, SHIVYAWATA inashauri pia utengenezwe mwongozo wa usafiri wa umma utakaosisitiza uwepo wa magari yatakayokuwa yanakidhi matakwa ya abiria wenye ulemavu, kitu ambacho itakuwa ni kigezo ili gari iweze kutoa huduma.

“Pia, na sisi [wawakilishi wa watu wenye ulemavu] tunatakiwa kuhusishwa kwenye ukaguzi wa magari yanayokuja na kupewa vibali kutumika kama usafiri wa umma kuangalia viwango vya ufikikaji na mambo mengine,” Lubago alisema. 

“Kwa sababu kukosekana kwa vyombo vinavyotoa ripoti za mara kwa mara kwamba mabasi ya kampuni hii yakoje, hata kama tukiyalaumu, tukayasifia, tunaona ni mazuri na yanafikika vizuri na kuwaambia watu wetu wenye ulemavu wapande zaidi hayo,” aliongeza.

Mitazamo chanya

Francis Mugasa ni Mwenyekiti wa Umoja Wa Haki za Wasafiri Tanzania anayekiri kwamba sekta ya usafiri Tanzania siyo bora kwa wasafiri na hata walemavu, akitolea mfano wa muundo ya mabasi ya mikoani na daladala ambayo anasema hakuna miundombinu rafiki kwa walemavu kuingia na viti vya magurudumu.

SOMA ZAIDI: Simulizi ya Mapambano ya Mama Mwenye Ulemavu: Uzazi Katika Umri Mdogo, Kazi, Mapenzi, Familia na Ndoa

“Tunapendekeza vyombo vyenye leseni za kusafirisha abiria watambue kwamba watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii na miundombinu ya stendi na vyombo vya usafiri viendadane na mazingira ya kuwajali watu wenye ulemavu,” anashauri Mugasa. “Pia, tuna wazee nao wanahitaji kupewa upendeleo maalum.”

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu ambayo imebeba dhamira mbalimbali ikiwemo kusimamia haki zao. 

Kwa mfano, Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) unasisitiza juu ya ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika jamii.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Tanzania ina jumla ya walemavu wa kutembea milioni mbili, huku asilimia 39.3 kati yao wakiwa ni wanaume na asilimia 60.7 ni wanawake.

Anthony Rwekaza ni mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia anthonyrwekaza9@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *