The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Madereva Wanaobadili, Kukatisha Ruti Wawakera Abira Dar. LATRA Waonya

Polisi, LATRA wasema huo ni uvunjifu wa sheria na kanuni; wataka wananchi watoe taarifa kwa mamlaka husika.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wanaotumia huduma ya usafiri wa daladala katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam wamelalamikia tabia za madereva wanaobadili na kukatisha ruti zao kinyume na utaratibu.

Wakitoa malalamiko yao hayo, baadhi ya abiria hao wamedai kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na utamaduni wa madereva wa daladala kubadili ruti, hali ambayo wameeleza kuwa ni kero kwa wengi na kuwa inasababisha usumbufu.

Amina Hassan, Mkazi wa Goba, anasema amekumbana na jambo hilo kwa nyakati tofauti.

“Siku nikiwa Mbezi kuelekea Mawasiliano nilipanda gari lakini nikashangaa kondakta anasema hawaendi huko,” alilalamika Amina.

“Siyo jambo jema,” alisema. “Ni usumbufu. Maana tulikuwa tumeshapanda na kukaa watu kama wanne, wote tulikuwa tunaenda njia ya kuelekea Mawasiliano. Wengine walipanda waliposikia inaenda Kawe kupitia Goba.”

Amina anasema kuwa utaratabu uliozoeleka unajulikana kulingana na magari yalivyoandikwa lakini amedai kuwa madereva na makondakta wakiona abiria wengi wanabadili ruti.

Amedai pia kuwa awali walizoea kuwa tatizo hilo hutokea usiku kuanzia mida ya saa tatu lakini kwa sasa jambo hilo limekuwa sugu na hufanyika muda wowote.

Naye Kennedy Jackson, mtumiaji mwengine wa daladala, ameeleza kwamba amekuwa akikutana na changamoto hiyo mara kwa mara siku za hivi karibuni, hasa akiwa kwenye kituo cha daladala Kawe akiwa anaelekea Buza.

“Kwa hapa siku hizi suala la kubadilisha ruti imekuwa kawaida,” alisema. “Magari yameandikwa Kawe/Buza lakini kondakta anasema gari mwisho wake Buguruni na tulishushwa pale yeye akabeba abiria wa kurudi Kawe.”

“Jambo hili limekuwa likipelekea ubishani kwetu na hao madereva. Kama hawaendi kwenye ruti walizoandika kwenye magari yao basi wabadilishe hata maandishi yanayoonesha ruti,” aliongeza mwananchi huyo.

Doreen Bryson, mfanyabiashara mdogo, anasema changamoto hiyo imewahi kumkwamisha kufika kwa wakati eneo alilopaswa kukutana na mmoja wa wateja wake.

SOMA ZAIDI: Karibu Tanzania, Nchi ya Madalali

“Ilinikwaza sana,” anaeleza. “Siku moja nikapanda gari la Buza kutokea Makumbusho lakini kondakta akawa anatangaza kituo cha mwisho ni Buguruni. Mimi nikadhani ni ujanja tu maana tumezoea maana wanafanya hivyo usiku.”

Baada ya kufika Buguruni na daladala kusimama wakiwa wamebaki wanne tu ndani ya gari huku wakiwa tayari wamelipa nauli, kondakta akaondoka wakabaki na dereva ambaye alisisitiza kuwa pale ndiyo ilikuwa mwisho wa safari na ndipo Doreen na abiria wenzake wakalazimika kutafuta gari lingine.

“Mteja alipoona nimechelewa akaniambia nimkute Mbagala,” alisema. “Kwa kweli niliumia maana nilitakiwa kuwahi kurudi Makumbusho. Nililazimika kupanda bajaji baada ya kushuka Kwa Mama Kibonge lakini ilikuwa hasara kwangu.”

Madereva, kondakta wajitetea

Kwenye mahojiano na mwandishi wa habari hii, madereva wametoa sababu mbalimbali ambazo husababisha wakati mwingine kubadili ruti ghafla.

Hassan Jabir ni dereva wa daladala zinazotokea Kawe kwenda Mbezi Louis aliyeniambia kwamba licha ya kuwa wanatambua ruti zao lakini wanaweza kuamua kubadili ruti kwa mara chache kutokana na mazingira tofauti.

“Tunazo ruti ambazo tumepangiwa lakini kuna wakati unaweza kukuta siku hiyo hakuna abiria na sehemu ambayo hutakiwi kwenda ikawa abiria wapo na magari yanayoelekea huko hayapo, hivyo lazima uchangamkie hiyo nafasi, lakini haitokei mara kwa mara,” alisema.

“Au kuna wakati tunafanya hivyo tukigundua njia ya ruti yetu ina foleni na hapo tokea asubuhi hatujapata kitu na jioni tunatakiwa kurudisha pesa ya bosi – hapo lazima tutafute namna, ndiyo kama hivyo unachepusha ruti,” anaongeza Hassan.

SOMA ZAIDI: Ajali za Barabarani Zinavyoangamiza Vijana Tanzania

Anna Paul ni kondakta wa daladala za kutoka Buza kwenda Kawe. Yeye anasema kuwa kuna wakati hutumia mbinu ya kuwaambia abiria kuwa gari inaishia Buguruni ili kuangalia uwezekano wa kupata abiria wapya kutoka Buguruni kwenda Buza au kuamua kurejea.

“Kuna wakati ili upate chochote lazima uwe mjanja,” anasema Anna. “Ndiyo maana tukiwa tunapakia pale Kawe mara nyingi tunatangaza kuwa magari yanaenda Buguruni ili tupate abiria wanaoishia Buguruni na tunapofika hapo kunakuwepo abiria wa Buza.”

“Kwa hiyo, kimahesabu na sisi tunakuwa tumepata kuliko tunapotangaza moja kwa moja Kawe/Buza,” anaongeza. “Hapo ukipakia umepakia, unakuta watu wanapanda hakuna kushuka mpaka Buza au kutoka Buza mpaka Kawe.”

Polisi, LATRA waonya

Hata hivyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salam (ZTO), ACP William Mkonda amesema kuwa kwa upande wao wamekuwa wakisimamia utaratibu na wanaobainika kwenda kinyume wamekuwa wakichukuliwa sheria.

“Sisi kazi yetu ni kusimamia sheria na taratibu, lakini ruti wanapangiwa na LATRA,” Mkonda alieleza kwenye mahojiano maalum. “Tunapobaini wanavunja huo utaratabu tunachukua hatua kwa kushirikiana na LATRA na hili limekuwa likifanyika.”

LATRA ni kifupi cha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, mamlaka ya Kiserikali yenye wajibu wa kupanga na kusimamia ruti za daladala.

Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano LATRA, Salum Pazi, amesema kubadili ruti ni kinyume na sheria na taratibu na kuwa wanaofanya hivyo wanakiuka sheria hizo.

SOMA ZAIDI: MOI Yapokea Wastani wa Majeruhi Sita wa Ajali za Bodaboda kwa Siku

Pia, ameeleza kuwa wemekuwa wakitoa elimu kwa raia ili wanapokumbana na mazingira ya aina hiyo watoe taarifa ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Wanaofanya hivyo wanavunja sheria; hawaruhusiwi kufanya hivyo na sisi tunafuatilia na kufanya kaguzi kuwachukulia hatua wanaofanya hayo makosa,” alisema Pazi.

“Tunao wakaguzi wanaofanya ukaguzi wa kushutukiza japo hawezi kuwa kila sehemu kila wakati, lakini ukibainika unachukuliwa hatua na tayari baadhi tumewachukulia hatua,” aliongeza.

LATRA wanasisitiza wananchi wanaokabiliana na mazingira ya aina hiyo kuripoti matukio hayo kwa kupiga simu namba 08001100019 ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

Anthony Rwekaza ni mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia anthonyrwekaza9@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *