The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ajali za Barabarani Zinavyoangamiza Vijana Tanzania

Wadau wahimiza mabadiliko ya sheria ili kudhibiti wimbi la ajali kwa vijana

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Novemba 7, 2002, ilikuwa ni siku nzuri na ya furaha kwa Margareth Magabilo, 43, ya kurejea nyumbani kwao Kondoa mkoani Dodoma baada ya kumaliza muhula wa masomo.

Hata hivyo, furaha hiyo iligeuka kumbukumbu isiyosahaulika maishani mwake wakati akielekea nyumbani kutokea chuoni Hombolo kutokana na ajali iliyo msababishia ulemavu wa kudumu.

Ajali hiyo ya gari aliipata akiwa na umri wa miaka 22 tu iliyosababisha kutolewa fuvu la kichwa la mbele na kupata changamoto ya pingili za uti wa mgongo hadi sasa.

Margareth, mjane na mama wa watoto wawili wa kiume anayeishi mkoani Dodoma kwa sasa, alisema ajali imempa pigo kubwa kwenye maisha yake.

“Ajali ilinisababishia changamoto kubwa, napata maumivu makali kwenye mishipa ya fahamu,” alieleza Margareth kwa huzuni wakati wa mahojiano haya.

“Nashindwa kutembea vizuri na kuweza kufanya majukumu yangu,” aliongeza huku  akiwa akijifuta machozi.

Margareth Magabilo (43) alipata ajali ya gari mwaka 2002 kuelekea kwao wilayani Kondoa ,iliyosababisha kutolewa fuvu la kichwa la mbele na kupinda kwa pingili za uti wa mgongo.

Alisema alikuwa pia akipata maumivu makali kwenye uti wa mgongo. Aliporudi hospitali kufanya vipimo vya MRI ilibainika pingili za uti wa mgongo zimepinda.

“Sehemu ya kifua mbele kuna namna fulani kama kuna kibyongo kutokana na kwamba nililala chali tu kwa muda mrefu. Siwezi kulalia ubavu wa kulia wala wa kushoto. Nimekuwa ni mtu wa kutegemea msaada wa watu mbalimbali,” aliongeza mama huyo kwa huzuni.

Mamia wapoteza maisha barabarani

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), ajali za barabarani ni miongoni mwa sababu namba moja ya vifo kwa watoto wa umri kati ya miaka 5 hadi 14 pamoja vijana wa umri kati ya miaka 15 hadi 29 ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa.

Jumla ya Watanzania 886 walipoteza maisha kati ya Januari na Novemba mwaka 2022 kutokana na ajali za barabarani wakiwemo vijana, huku wengine 573 wakiachwa na majeraha kwenye ajali 1,422 zilizorekodiwa na Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi.

Ajali hizo ziliongezeka kutoka 1,177 zilizorekodiwa kati ya kipindi cha  Januari hadi Agosti 2022. Hii ina maana kuwa ndani ya miezi mitatu kulitokea ajali mpya 245.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliyowasilishwa mwezi Februari 2023 katika Bunge la 12, watu 382 wameripotiwa kupoteza maisha kutoka mwezi Oktoba hadi Disemba 2022, vifo vinavyoelezwa kuongezeka kwa asilimia 4.1 kutoka idadi ya watu 367 waliokufa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2021, huku chanzo kikubwa kikitajwa ni ajali za barabarani zilizotokea katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi hicho.

SOMA ZAIDI: Ajali za Barabarani Zilivyoteketeza Maisha ya Watanzania 2022

Margareth ni sehemu ya watu waliopata ajali akiwa kijana mdogo. Majeraha na makovu yaliyobaki kwake yamekatisha ndoto zake. Amekuwa ni mtu wa kulala kitandani wakati wote. Watoto wake wa kiume ndiyo wanaomuhudumia anapohitaji baadhi ya huduma kutoka kwao.

Si Margareth peke yake aliyekutana na madhila haya ya ajali za barabarani kwani wako vijana wengi nchini waliokutana na masaibu hayo.

Alhumani Dady mwenye umri wa miaka 27 yeye alijikuta kwenye wakati mgumu baada kuvunjika mguu wake wa kulia Julai 7, 2020, wakati akiendesha bodaboda kutoka Chamwino kuelekea Kisasa Sheli jijini Dodoma.

“Hiace haikunionesha ishara kama inasimama kuchukua abiria, kwa kuwa nilikuwa naendesha kwa mwendo mkubwa nilishindwa kujihami, nikaligonga gari, nikapata majanga makubwa sana, nikavunjika mguu,” alieleza kijana huyo.

Alhumani Dady mwenye umri wa miaka 27 alipata ajali ya bodaboda mwaka 2020 iliyosababisha kuvunjika mguu wake wa kulia na kuwekewa chuma kwa takriban mwaka mmoja .

Majanga juu ya majanga

Alizimia kwa saa tatu baada ya kupata ajali, akajikuta yupo hospitali fahamu zake ziliporejea.  Alipofanyiwa  vipimo iliamuriwa kuwekewa chuma kwenye mguu wake wa kulia ambacho ameishi nacho kwa takriban mwaka mzima.

Kabla ya kupata ajali, Dady alikuwa akiingiza kiasi cha Shilingi 25,000 kwa siku, hivyo kusababisha kupoteza mapato ya Shilingi 9,125,000 ndani ya mwaka alipokuwa akiuguza majeraha yake.

“Asilimia kubwa sisi vijana ajali tunazisababisha sisi wenyewe, sheria hatuzifuati,” alieleza kwa kujutia kosa lake.

“Tunaendesha kwa mwendo mbovu, kuna alama za barabarani zinazoonyesha tusitembee spidi 30 lakini tunalazimisha tutembee mpaka spidi 80. Gari linapokwenda kusimama pembeni unashindwa kujizuia, unajikuta umeligonga kwa sababu ya mwendo mkali,” alisema.

SOMA ZAIDI: Mbeya Katikati ya Mtanziko wa Kulinda Maslahi ya Kiuchumi na Kujikinga na Ajali za Barabarani

Ajali aliyoipata imempa funzo na hatamani kupata madhila aliyoyapata hapo awali.

“Ushauri wangu vijana wenzangu waviheshimu vyombo vya moto. Tuziheshimu sana sheria za barabarani. Mimi nimekutana na majanga kama haya nikateseka kwa muda mrefu,” alishauri kwa majuto makubwa.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kwamba zaidi ya watu milioni 1.35 hufariki kwa ajali za barabarani duniani, huku wengine milioni 20 hadi 50  wakiachwa na majeraha na ulemavu wa kudumu.

Daladala zikiwa zimepaki eneo la stendi ya sabasaba kusubiri abiria

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, takriban ajali nane kati ya 10, sawa na asilimia 76, husababishwa na makosa ya kibinadamu kama ilivyomtokea Dady, huku takriban ajali mbili kati ya 10 zikisababishwa na matatizo ya kiufundi. Ni asilimia nane tu ya ajali kati ya 10 husababishwa  na sababu za kimazingira kama ilivyotokea kwa Margareth.

Ajali yamkosesha kujiunga na jeshi

Alex Mhando, 50, baba wa mtoto mmoja, alipata ajali ya gari mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 18 tu akitokea Dodoma kuelekea jijini Dar es Salaam baada ya basi alilokuwa akisafiria kupoteza muelekeo kwenye mlima.

“Ajali imenipa changamoto ya kuwa mlemavu na imesababisha malengo yangu kupotea,” alisema Mhando huku akinitazama usoni akiwa amekaa kwenye kiti.

“Kwa sababu wakati ule nilikuwa na malengo ya kuingia jeshini, nikakatisha ndoto zangu ambazo nilikuwa nimezipanga muda mrefu,” aliongeza Mhando.

Alisema mtu anapopata ulemavu inamkosesha fursa nyingi ikiwemo kupata kazi kutokana na kupata ulemavu.

Alex Mhando (50) alipata ajali ya gari mwaka 1997 ambayo ilipoteza ndoto zake za kuwa mwanajeshi

“Unapotolewa kiungo ni changamoto, huwezi kufanya kazi kama mtu mwingine alivyo mzima,” alisema.

Vijana kwa sasa ndiyo kundi kubwa linaloongoza kuendesha vyombo vya moto ikiwemo bodaboda huku baadhi wakipuuza kufuata sheria za usalama barabarani, ikiwemo kuvaa vifaa kinga kama kofia ngumu (Helmet).

Tabia waluwalu za vijana katika kuendesha vyombo vya moto zinahatarisha maisha yao, ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Wengi wanaopata ajali barabrani ni bodaboda

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ilisema kwa upande wa Idara ya Mifupa wanaolazwa wodini ni wagonjwa kati ya sita mpaka 10 kwa siku, wengi wao wakiwa ni wa ajali za barabarani zinazotokana na bodaboda.

Kwa upande wa majeruhi  wa ajali wanapokea kati ya watu 180 mpaka 300 kwa mwezi.

Daktari Bingwa wa upasuaji kitengo cha mifupa Dk Samuel John alisema mbali na kupokea walioanguka kutoka kwenye miti, wanaohusika na ujenzi, wenye umri mkubwa  asilimia 50 ya watu wanaowalaza  ni vijana wanaotokana na ajali za bodaboda.

“Kiafya tunasema tunatakiwa tuanze kwenye kinga. Kwa nini wanapata ajali? Elimu zaidi ikitolewa kwa upande wa kinga, upande wa kuzuia, watu wa bodaboda wawe wanaendesha kwa uangalifu,” alisema Dk John wakati wa mahojiano haya.

SOMA ZAIDI: MOI Yapokea Wastani wa Majeruhi Sita wa Ajali za Bodaboda kwa Siku

Lole Peter, aliyefanya kazi ya udereva tangu mwaka 1989, alisema madereva wengi vijana hawajali wanapokuwa barabarani.

“Kuna watoto wengine huwa wanajisifia kwamba kwao kuna uwezo fulani wanajua watakachofanya, wanasema mzee atakuja kunitoa tu,” alieleza dereva huyo akiwa katika kituo cha daladala sabasaba.

Kwa miaka Donasian Magayane amekuwa dereva wa daladala alisema vijana wengi wanajikita kwenye uendeshaji wa bodoboda kwa ajili ya njaa.

“Anakuwa hana uzoefu wa kutembea barabarani matokeo yake anasababisha ajali barabarani,” alisema Donasian.

Abiria walieleza madereva bodaboda wengi hawana muda wa kupumzika. Uchovu unachangia kutokuwa na ufanisi mzuri wa kuendesha vyombo vya moto wanapokuwa barabarani.

“Wangepata muda wa kupumzika wangekuwa wanafanya kazi vizuri na wangekuwa wako makini sana barabarani,” alieleza Omari Mohamed.

Asha Mwakyonde alisema vijana wana mihemko na hulka wanapokuwa barabarani hivyo kuhatarisha usalama wao.

“Wenyewe wanachowahi ni kuwahisha abiria na kuja kuchukua abira, usalama wao unakuwa ni mdogo. Muda mwingine sisi abiria tunaopakiwa tuna tabia ya kushinikiza watuwahishe. Ile ni hatari na ni kosa kwa sisi abiria ambao tunatumia chombo hicho,” alisema Asha.

Sheria mpya muarobaini wa ajali

Mackphason Buberwa, Wakili na Meneja Miradi  kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alisema wanadhani ni muhimu mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani yakaangalia makundi maalum kama vijana kwa maana ya kutilia mkazo kutokana na kundi hilo kuathirika kwa kiwango kikubwa na ajali za barabarani.

“Kwa sababu,  sheria siyo kali za kuwabana, vijana wengi wanakuwa hawana elimu ya usalama barabarani, hivyo wanajikuta wanaingia kwenye matatizo kwa kiasi kikubwa, sheria  zibadilishwe kuwabana zaidi,” alisema Buberwa.

Mtendaji Mkuu wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania Augustus Fungo anasema ipo haja ya kuwa na mkakati wa kitaifa au sheria inayodhibiti zaidi usafiri wa bodaboda na bajaji.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Unapaswa Ufikirie Mara Mbili Kabla Ya Kutumia Usafiri wa IT

“Bodaboda anapokosea na kulipishwa faini ya Shilingi 10,000 hata haimuumi kwa kumpunguzia faini,” alisema Fungo.

“Tumefanya kama vile ni haki kila mtu kuendesha chombo cha moto barabarani jambo ambalo siyo sawa. Mtu akishindwa au kama hawezi kufuata sheria za barabarani ni vyema tumfanye akatafute kazi nyingine za kufanya,” alisema Fungo.

Alisema kinachopaswa kufanyika ni kupiga marufuku kabisa usafiri wa bodaboda kama nchi nyingine au kuufanya uendelee kuwa halali. Kwa kuwa usafiri huo umehalalishwa na kuwa chanzo cha ajira kwa watu wengi, hivyo inapaswa kuwepo na mpango wa kitaifa wa kuimarisha usafiri huo.

“Kwanza kabisa kwa  kuwatambua kujua wako wangapi, wako wapi na kuwasajili kwenye kanzi data maalumu. Kwa hapa, Serikali ijenge mfumo ambao bodaboda watasajiliwa kwenye kila halmashauri nchini,” alishauri Fungo.

Tekinolojia itasaidia kudhibiti ajali za barabarani

Wakati wadau wa sheria wakihimiza mabadiliko ya sheria, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Usalama katika Usafirishaji na Mazingira kutoka chuo cha NIT kilichopo jijini Dar es Salaam Patrick Oforo Makule  alisema mara nyingi ajali zinapotokea zinasababishwa na makosa ya binadamu na si masuala ya kiufundi.

‘’Siyo masuala ya kifundi ambayo labda niseme ni kifaa pikipiki pengine imekuwa na hitilafu ya kiufundi, hapana, ni maamuzi yale ya kibinadamu,” alisema Makule wakati wa mahojino haya.

“Kwa hiyo, dawa ya hayo maamuzi ya binadamu ni kuwatengeneza na kuwapatia elimu. Shida kubwa ipo kwenye tabia na mtazamo kuwabadilisha wale vijana waweze kufanya kama wanavyofundishwa,” aliongeza.

Kuhusu tekinolojia kudhibiti ajali za barabarani, Makule alisema inaweza kwani kwa nchi zilizofanikiwa zimetumia teknolojia kudhibiti ajali.

“Kwa mfano, kama kuzuia spidi vipo vifaa vinafungwa kwenye gari vinasaidia kuzuia spidi. Maana yake kama mtu anaongeza mwendo ambao ni hatarishi, chombo chenyewe ni tekinolojia aidha inamuonya au inazuia hiyo spidi. Tukiwa na uwezo tekinolojia itatusaidia sana [kudhibiti ajali],” alihimiza.

Suluhu ya kudumu ya kudhibiti ajali za barabarani

Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma linasema suluhu ya kudumu ya kudhibiti ajali za barabarani ni kuendelea kutoa elimu kwa vijana na vijana kuwa wasikivu wanapopewa mafundisho ya namna ya kuzingatia sheria za barabarani.

“Wanapoendesha bodaboda wavae kofia ngumu  [Helmet], ikitoea bahati mbaya amepata ajali ataweza kujikomboa kwa njia moja au nyingine anaweza asiumie,” alisema Kamanda wa Jeshi la Polisi Martine Otieno alipo kuwa akifanya mahojiano haya katika eneo la kituo cha polisi.

Alishaurii vijana kwenda maeneo sahihi  kupata mafunzo kama vile VETA kupata ujuzi wa kuendesha vyombo vya moto.

“Wakija kwenye vyuo vyetu vya polisi tunazo shule za udereva tuna wafundisha kuendesha magari na  pikipiki. Badala ya kwenda kwenye vyuo ambavyo vimesajiliwa kupata mafundisho wao wanachukuana mitaani, basi jioni anaingia barabarani,” alisema.

Zinapotokea ajali Kamanda Otieno alisema taifa linapata athari kubwa kwa kupoteza nguvu kazi ya taifa zaidi kundi la vijana.

“Wengi wanakua wameumia wanapata ulemavu matokeo yake ndio nguvu kazi inapungua. Na shughuli nyingine zinashindwa kuendelea kwa sababu vijana ndiyo nguvu kazi inapaswa kutumika kwa maendeleo ya taifa,” aliongeza.

Hatua  zilizo chukuliwa na Serikali kudhibiti ajali

Mnamo Februari 10, 2023, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni akiongea na waandishi wa  habari jijini Dodoma alisema Serikali inachukua hatua mbalimbali kupunguza ajali, ikiwemo kuangalia mfumo mzima wa utoaji leseni nchini  baada ya kuona kuna upungufu katika aina ya utoaji wa mafunzo ya udereva.

“Tunadhani kuna haja ya kupaangalia zaidi je, mafunzo yanayotolewa kwa madereva wetu yanaenda sambamba na wakati uliopo, yanakwenda sambamba na mazingira na mabadiliko ya teknolojia ya wakati huu?” aliuliza Masauni.

Mbali na uhakiki wa leseni, Masauni alisema wanataka kufanya uhakiki wa madereva, hususan wa mabasi na malori nchi nzima Ili madereva wote wanaoendesha yale mabasi ya abiria na malori yanayoenda masafa mbali wasajiliwe kwenye mfumo wa LATRA.

Pia, alisema kuanzia hivi sasa wanaanza operesheni kufuatilia nyendo za madereva wa magari yote usiku na mchana, hususan kwenye barabara kubwa.

“Tunapokwenda kushughulikia mifumo na taratibu za utoaji wa leseni, yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha utoaji leseni bila kuwa na utaratibu atashugulikiwa,” alionya Masauni.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *