The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sababu Zinazowanyima Walemavu Haki za Kidijitali Tanzania Zatajwa

Wadau wanakubaliana juu ya haja ya kuendelea kupigania mabadiliko kwenye sekta ya haki za kidijitali nchini ili watu wenye ulemavu waweze kunufaika na haki hizo.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Kundi la watu wenye ulemavu limetajwa kuwa miongoni mwa makundi yaliyo nyuma katika kufurahia haki za kidijitali, hali ambayo wadau wa haki hizo nchini Tanzania wanadhani inahitaji hatua za dharura ili kuweza kukabiliana nayo, huku wakitaja sababu kadhaa zinazowanyima watu wenye ulemavu haki hizo.

Haki za kidijitali ni zile haki za binadamu na kisheria ambazo zinawaruhusu watu kufikia, kutumia, kutengeneza na kuchapisha maudhui ya kidijitali au kuwa na uwezo wa kufikia na kutumia kompyuta, vifaa vya kielektroniki au mitandao ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa Zaituni Njovu, Mkurugenzi Mtendaji wa Zaina Foundation, shirika lisilo la kiserikali linalojikita na utetezi wa haki za kidijitali nchini Tanzania, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kuwawezesha watu wenye ulemavu kufurahia haki hizi kwani hali ilivyo sasa hairidhishi.

Njovu alitoa tathmini hiyo wakati akiongea na The Chanzo pembezoni mwa mafunzo ambayo Zaina Foundation, kwa kushirikiana na Paradigm Initiative, asasi ya kiraia ya nchini Nigeria inayojihusisha a utetezi wa haki za kidijitali, iliandaa kwa wabunge, waandishi wa habari na wawakilishi kutoka asasi za kiraia yaliyolenga kuchagiza harakati za kutetea haki za kidijitali Tanzania.

Ukosefu wa zana muhimu

“Mtu anaweza kuwa na ulemavu wa kutokuona, yaani ni kipofu, kwa mfano, kama ni tovuti inabidi itengenezwe iwe na vifaa ambavyo vinatoa sauti,” Njovu anaeleza. “Kwa mfano, labda kwenye tovuti kuna kitu kinahusu kitu fulani,  kwa hiyo, yeye akibonyeza ile sehemu audio iwe inasema.”

Lakini hicho siyo kitu kinachofanywa na wachapishaji wengi wa maudhui ya kidijitali Tanzania, kitu ambacho Njovu anasema kinaweza kuwa kinasababishwa na watu kusahau kwamba watu wenye ulemavu wa kuona wanatakiwa wawe na audio.

Kitu kingine kinachokosekana kwenye huduma za kidijitali zinazotolewa nchini ni ukosefu wa wakalimani wa lugha za alama. Anaeleza Njovu: “Labda, kwa mfano, teknolojia ni kitu ambacho ni audio au video lakini unakuta hiyo video haina mkalimani wa lugha ya alama. Kwa hiyo, mtu ambaye hasikii anakuwa hawezi [kupata ujumbe uliokusudiwa]. Anaona lakini hakuna mtu wa kumuwezesha kuelewa.”

 

Baadhi ya watu wenye ulemavu pia hawana mikono wala miguu, kitu kinachowafanya washindwe kufurahia haki za kidijitali kwani nyingi zao zinahitaji mtu aguse ili aweze kupata kile anachokitafuta, anafafanua Njovu.

Akizungumzia hali ya kiuchumi ya watu wenye ulemavu kama moja kati ya sababu zinazowazuia watu hao wasifurahie haki hizo, Njovu alisema: “Asilimia kubwa ya watu wenye ulemavu kipato chao kinakuwa ni cha chini. Kwa hiyo, ukiangalia gharama za kununua bando labda la Sh5,000 haimalizi hata wiki. Sasa kwa mtu mwenye ulemavu akipata Sh5,000 anaona ni bora anunue chakula, ama akapate matibabu, kuliko kununua bando.”

Ubaguzi wa kisera, kisheria

Naye mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Chama cha Wanahabari Tanzania (TAMWA) Godwin Asenga aliiambia The Chanzo pembezoni mwa mafunzo hayo ya siku 4 yaliyoanzia Aprili 23, 2022, alitaja sera za nchi zinavyochangia kundi la watu wenye elemavu linavyoachwa nyuma kwenye haki za kidijitali.

Asenga anatolea mfano wa sheria inayotaka laini za simu zisajiliwe kwa njia ya vidole ambayo anadai wako watu walioshindwa kusajili laini zao kwa sababu hawana viganja na hivyo kunyimwa haki ya kufanya mawasiliano.

“Mtu kama yule ni ngumu sasa yeye kuweza kusajili laini kwa kutumia alama za vidole,” anasema Asenga. “Na ukisema wajisajili kwa kutumia majina ya mtu mwingine sheria hiyo hiyo tena mbele kuna kipengele ambacho kinaeleza ni kosa kisheria kusajili laini au kumiliki laini ambayo imesajiliwa kwa taarifa za mtu mwingine.”

Asenga anadhani ni muhimu kwa wadau kupigia kelele changamoto kama hizi ili Serikali iweze kuchukua hatua stahiki.

Mwenyekiti wa Shirika la Foundation for Disabilites Hope Michael Salali, ambaye ana ulemavu wa ngozi, anasema kundi hilo liko nyuma kiuelewa kuhusiana na matumizi ya mitandao.

Mitazamo potofu ya kijamii

“Kuwa nyuma inasababishwa na changamoto za ulemavu, mitazamo ya kiulemavu iliyopo kwenye jamii,” Salali anasema kwenye mahojiano na The Chanzo. “Jamii inaamini kwamba mtu mwenye ulemavu hawezi kushiriki shughuli yoyote. Kwa hiyo, unakuta hata matumizi ya mitandao hali hiyo inajirudia.”

Hata hivyo, Salali anasema yeye na wenzake wengine watapambana kubadilisha hali hiyo.

“Kwa sababu kwenye mitandao kuna fursa nyingi. Kimsingi sasa hivi dunia imeahamia kwenye mitandao,” anasema mwanaharakati huyo. “Fursa za kibiashara [na] kiuchumi. Sasa kundi la walemavu kuendelea kubaki nyuma maana yake linaendelea kukosa fursa muhimu zinazo patikana huko.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *