The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

LATRA Itupie Jicho Bei za Vyakula Kwenye Vituo vya Abiria wa Mikoani

Nani kama siyo msafiri atalipa Shilingi 4,000 kwa vipande vya chips kavu unavyoweza kuvihesabu kwa macho na kipande kimoja cha nyama ya kuku iliyopoa?

subscribe to our newsletter!

Katika mazingira ya safari ambayo msafiri hana chaguo jingine zaidi ya pale basi linaposimama, msafiri huyo tayari anakuwa na nafasi ndogo sana ya ushawishi wa bei na maafikiano ya kibiashara kabla ya kununua bidhaa au huduma fulani. 

Mazingira ya safari yanamfanya mtoa huduma ya chakula, kwa mfano, kuwa na nafasi ya juu ya kuamua kuuza chakula chake kwa bei aitakayo, hata kama tafsiri ya bei hiyo ni uonevu kwa msafiri na faida isiyo ya haki kwa muuzaji. 

Swali ni je, nani anachagua vituo vya chakula vya mabasi ya mikoani? Je, anapochagua vituo hivyo huwa anazingatia vigezo gani? Je, hali ya kipato cha Mtanzania wa kawaida dhidi ya bei za vyakula kwenye vituo hivi ni kigezo kimoja wapo kabla mpanga vituo hajapanga abiria kutoka mikoa hii watakula kituo hiki ama kile? 

Labda tujiulize kutokea kona nyingine. Je, ni nani anadhibiti bei za vyakula kwenye vituo hivi? Je, ni kweli kwamba wauzaji wa vyakula wameachwa wapange bei za vyakula vyao kwa namna wanavyotaka kutajirika? Nauliza maswali haya kwa sababu bei za vyakula kwenye vituo hivi, kwa karibu sehemu zote nchini, siyo bei ya soko.

Ni wazi kwamba iwapo mabasi ya mikoani yatapitiliza, vituo hivi vitalala na vyakula vyao. Hii ni kwa sababu waenda kwa miguu, ama wakazi wa maeneo jirani, hawawezi kulipa gharama za vyakula ambazo vituo hivi vinatoza. Hii ni wazi kwa sababu hakuna bei ya soko na huduma inayotolewa haiendani na gharama.

Hakuna chaguo

Nani atalipa Shilingi 4,000 kwa vipande vya chips kavu unavyoweza kuvihesabu kwa macho na kipande kimoja cha nyama ya kuku iliyopoa? Hakuna, isipokuwa msafiri ambaye dereva wa basi alilopanda, kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, ama kwa maelekezo ya bosi wake, ameamua kuwaleta abiria wale hapo, watake watanunua, wasitake watanunua. Hawana chaguo!

SOMA ZAIDI: Usafiri wa Umma Unaweza Kuwa Rafiki Zaidi kwa Watu Wenye Ulemavu?

Ni kawaida vituo hivi kuuza vinywaji laini, kama vile maji na soda, kwa bei ya juu kuliko bei iliyozoeleka sokoni. Wauzaji wanauza kwa bei wanazoamka nazo siku hiyo, nani anajali? Msafiri atalipa tu. 

Wakati msifiri anahesabia hela mfukoni huku akijiuliza ni lini bei ya soda na maji ilipanda, dereva wa basi anapiga honi nyingi kuashiria muda wa kula umeisha, kawia uachwe na basi, utaomba lift kwenye lori.

Hali hii imekuwapo siku zote. Inaendelea kuwa jinsi ilivyo kwa sababu kila mmoja anadhani hili jambo halimhusu. Pengine swali la msingi ni je, tunayo mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu? Jibu ni ndiyo, tunayo na inaitwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

Nani haijui LATRA? Ipo, na kila siku inasikika ikipanga nauli na masaa ya mabasi kusafiri. Je, LATRA haijui kuwa wanaosafiri ni watu na watahitaji kula wawapo njiani? 

Kama LATRA inaheshimu haki ya abiria kupata chakula njiani, haioni haja ya kuratibu mazingira ya biashara ya chakula kuwa mazingira ya haki ili wasafiri wanunue chakula kwa bei ya soko? 

SOMA ZAIDI: Madereva Wanaobadili, Kukatisha Ruti Wawakera Abira Dar. LATRA Waonya

Nani anafaidika na hizi faida zisizo za haki wazipatazo wauza vyakula kwenye vituo hivi? Mimi sijui, lakini hoja ya msingi ni kuwa tuliacha majukumu yetu kwa Serikali ili isimamie tusinyonywe. 

Serikali isilale

Serikali, kupitia mamlaka zake kama vile LATRA, haipaswi kufumba macho kama vile hakuna kinachoendelea angali ni dhahiri kuwa wasafiri wananyonywa. Ningeambiwa nitumie mfano wa ng’ombe, ningesema wanakamuliwa maziwa mpaka damu!

Umewahi kusafiri ikafika muda wa kula ukawaona wasafiri wenzako wasio na fedha za kutosha jinsi wanavyotia huruma kwa kushindwa kumudu gharama za vyakula kwenye vituo hivi? Ni jambo la kusikitisha sana. Kwa huruma, unaweza kumsaidia mtu leo ama kesho lakini hutatatua tatizo. 

Tatizo la msingi ni kuwa wafanyabiashara ya chakula kwenye vituo hivi wameachwa wapange bei kwa namna wanavyotaka na bei hizo zinaumiza wasafiri, hasa Watanzania wengi wenye vipato vidogo. Hivyo, namna pekee ya kuwasaidia Watanzania hawa ni kuwaondoa kutoka kwenye makucha ya unyonyaji. 

Serikali imejenga vituo vya mabasi vya mikoa vya kisasa, na vina migahawa yenye kuuza vyakula kwa bei ya soko, inagharimu nini kuwaambia abiria tukifikia stendi ya mkoa fulani tutakuwa na dakika kadhaa kila mmoja anunue chakula cha kuendana na kipato chake? 

SOMA ZAIDI: Karibu Tanzania, Nchi ya Madalali

Kwa nini abiria walazimishwe kula kwenye migahawa ya kibwanyeye ambayo wengi wao kwenye maisha yao ya kila siku hawamudu gharama za vyakula kwenye migawaha ya aina hiyo? 

Kama madereva wa mabasi yetu, na mabosi wao, wanafikiri huku stendi kutatuchelewesha, kwa nini wasitushushe kwenye migahawa yenye kuuza vyakula kwa bei ya soko? 

Labda tujiulize, kwa nini migahawa hii ambayo tunalazimishwa kula isituuzie vyakula kwa bei ya soko? Kama wenye mabasi wanapewa bei elekezi za nauli, kwa nini wenye migahawa wasipewe bei elekezi za vyakula? 

Unyonyaji

Lengo la kutaka udhibiti kwenye biashara ya chakula kwa wasafiri siyo kuifanya Serikali mwamuzi wa biashara baina ya watu, hapana. Lengo ni kulinda haki ya abiria ya kupata chakula wawapo safarini. Siyo tu kupata chakula, bali kupata chakula kwa utaratibu unaoepuka unyonyaji kati ya mtu na mtu. 

Waswahili wanasema, tembo hazidiwi na mkonga wake, na mimi nina imani LATRA hawazidiwi na watoa huduma ya chakula kwa abiria. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Unapaswa Ufikirie Mara Mbili Kabla Ya Kutumia Usafiri wa IT

Kwa kusema hivyo, natoa rai kwa LATRA kuingilia kati suala hili kwa vitendo thabiti, hasa msimu huu wa mwisho wa mwaka ambao Watanzania wengi wanasafiri kurudi makwao. 

Watu wasafiri na wale vyakula wavipendavyo kwa kulipa bei ambayo wangelipa bila manung’uniko kama wasingekuwa wakisafiri. Hili ni la kwenu ndugu zangu wa LATRA.

Clay Mwaifwani ni mwanasheria na mdau wa usimamizi dumivu wa rasilimali za maliasili. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 758 850 023 au claymwaifwani09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Ulilosema ni la kweli kabisa,wasafiri wanapigwa hela za hovyo,vyakula vibovu vingine vimelala,ikiwemo wachuuzi wanaouza stendi,mfano clips za viazi na ndizi za pale shinyanga stand,vinatiwa chumvi nyingi sana,hatari kwa figo,ikizingatiwa kila rika linanunua,iko haja wanaozitengeneza washauriwe kupunguza chumvi sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *