‘Inatuumiza Sana’: Nyakua Nyakua ya ‘Nyau’ Kariakoo Yawakwaza Machinga

Machinga wanawake wamelalamikia kudhalilishwa pia na mgambo wa jiji. Manispaa yasema haijapokea malalamiko hayo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. “Kwa namna wanavyotunyakua ni kama nyau anavyomnasa panya; wanakuvizia, mara ghafla unasikia wamekukumbatia, huku mwingine akikusanya bidhaa ulizotandaza chini, au unayokuwa nayo mikononi. Hii ndiyo sababu ya kuwapa jina la nyau.”

Hayo ni maneno ya Sarah Sanga ambaye ni mfanyabiashara mdogo katika soko la Kariakoo, jijini hapa.Sarah ni mmoja ya wafanyabiashara wadogo, maarufu kama ‘Machinga,’ kwenye mitaa mbalimbali ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ambao wamedai kutozwa fedha kwa njia ya kificho na Mgambo wa Jiji, waliowabandika jina la ‘Nyau,’ wakihoji endapo fedha hizo zinafikishwa serikalini.

Machinga hao wamedai kutozwa kiasi cha Sh1,000 hadi 2,000 kwa siku kila mmoja, huku wengine nao wakidai kutozwa kiasi cha Sh10,000 kila Jumamosi.

Wengi wao wamedai kuwa mizigo yao ikikamatwa na kufikishwa kwenye ofisi za machinga zilipo Mtaa wa Wapemba hutozwa kiasi kikubwa zaidi kisichopungua Sh10,000, kwenye zoezi linalofanyika kila siku, huku zaidi ya watu hamsini hukamatwa kwa siku moja.

Mfanyabiashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Idrissa Hammad ameeleza kuwa baada ya Serikali kutangaza utaratibu wa kuwaondoa kwenye mitaa mbalimbali, kundi la Mgambo wa Jiji walianza kuratibu zoezi la kuwakamata na kushikilia mali zao mpaka wanapolazimika kutoa pesa kwa wahusika.

“Serikali ilipotangaza kutuondoa, walikuwa wakija Mgambo wa Jiji wanatutimua tuache mali zetu ili wasitupige virungu,” anasema Hammad. “Lakini mali zetu zilikuwa zinaharibiwa, huku nyingine wakizipeleka kwenye ofisi zao, na ukienda huko lazima fedha ikutoke ndipo mali zinaachiwa.”

Idrissa ameongeza pia kwamba baada ya jambo hilo kuzoeleka, Mgambo wa Jiji wamekuwa wanakusanya kiasi cha Sh1,000 hadi 2,000 kila siku kutoka kwa machinga wanaopanga bidhaa zao kando ya barabara ili wasiwasumbue.

Udhalilishaji

Sarah Sanga ni mwanamke anayefanya biashara ya kuuza nguo za ndani za kike sokoni hapo. Anasema amekamatwa zaidi ya mara kumi na Mgambo wa Jiji na ametozwa zaidi ya Sh100,000 bila kupewa risiti ya malipo hayo ambayo huelezwa kuwa ni faini.

Sarah ameongeza kuwa utaratabu ambao hutumika kukamata unadhalilisha wanawake wengi kwa kuwa zoezi hilo, kwa kiwango kikubwa, hutekelezwa na mgambo wa kiume, huku pia mali zao nyingine zikiharibiwa na kupotea katika harakati za kukamatwa na baada ya kufikishwa kituoni.

SOMA ZAIDI: ‘Hakuna Biashara’: Machinga Old Airport Mbeya Waeleza Masaibu Yao

“Tunakuwepo unaona nyau [mgambo] ameshakuvamia, anakukumbatia, huku mwingine akikusanya bidhaa ili usilete makeke,” Sarah alimwambia mwandishi wa habari hii.

“Kwa mara zote nilizokamatwa imekuwa hivyo hivyo; nakamatwa na nyau wa kiume, ukijaribu kujitetea unaweza hata kupigwa lazima uwe mvumilivu. Sasa utafanyaje? Unakubali tu. Lakini tunaumia zaidi maana kuna wakati bidhaa zetu zinapotea zikiwa mikononi mwao na wakati wa ukamataji ambao ni kama kuvamiwa,” alilamika mama huyo.

Aidha, kijana Hamad Musa anasema kuwa changamoto ya kutozwa hela hiyo imekuwa kama biashara halali. Amedai kuwa kwa sasa jambo hilo limekuwa endelevu, akitolea mfano watu kukamatwa na kupelekwa kwenye ofisi zao na kutozwa fedha.

“Hili suala wameligeuza kama biashara; wakiamka tu wanakuja kutunyakua ili wajipatie hela, sijui hata hela tunayoitoa inaenda wapi maana hawatoi hata risiti,” Musa alisema.

“Wanaweza wakakukamata leo ukatoa hela, wakakukamata kesho ukatoa hela, yaani wao siku hizi kazi yao ni kuchukua mizigo yetu ili tutoe hela,” aliongeza. “Inatuumiza sana.”

SOMA ZAIDI: Kuna Ugumu Gani Kwa Serikali Kuwasikiliza Wamachinga?Musa anahoji pesa inaenda wapi kama wanatozwa bila kupewa risiti. Amesema kuwa kuna pesa nyingi inapotea kutokana na mazingira ambayo amedai kuwa yamezungukwa na rushwa.

“Wewe jiulize, kama hii fedha haiingii serikalini, unadhani ni mamilioni mangapi yanapigwa kwa kila machinga?” anauliza mfanyabiashara huyo.

“Tuchukilie Machinga mia tano kila Jumamosi wakitoa Sh10,000 inakuwa kiasi gani kwa mwezi? Hapa Serikali inaweza kuwa inapoteza pesa nyingi sana,” Musa alibainisha.

Musa pia amesema kuwa baadhi ya machinga wanaoshindwa kutoa fedha wamejikuta katika hali ya kutoelewana na Mgambo wa Jiji, jambo linalosababisha ugomvi na visasi.

“Kuna mtu alipigwa na hao mgambo mpaka akapata majeraha kisa aligoma kutoa fedha,” alisema. “Ukigoma kutoa hela, au kwenda ofisini kwao, jiandae kuharibiwa mali zako au kupigwa; siku hizi wametujengea visasi.”

Hawafuati utaratibu

Hata hivyo, Katibu wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Augustino Atanas Choga, alimwambia mwandishi wa habari hii kwamba upo utaratibu wa kamatakamata, lakini ni utaratabu ambao unatekelezwa kwa wanaokiuka taratibu wanazozisimamia.

“Utakuta wengine wanalazimisha kukaa kwenye maeneo ambayo hayatakiwi, kwa mfano, pembezoni mwa barabara, sehemu ya mwendokasi au sehemu ambazo zimepigwa marufuku,” Choga alisema. “Utakuta watu wanalazimisha ndiyo maana wanakamatwa kutokana na kuvunja taratibu.”

Aidha, Choga alidai kwamba pesa hiyo ambayo inadaiwa kutozwa kwa machinga hao hutumika kuendesha ofisi yao, na kuwa gharama inayotozwa ni ya kwaida na haina uhitaji wa kutoa risiti.

SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hili la Wamachinga Linanisononesha Sana

“Kwa haya unayoyaona sijui wengine kulalamika wanaonewa, kulalamika ni kawaida. Masuala ya msingi yanayofanyika ni kuangalia na kusimamia taratibu. Tukiwachukua hao tunawatoza faini, wanatulipa kwa ajili ya kuendesha ofisi kwa kuwa hatuna chanzo kingine cha mapato,” Choga alisisitiza.

Katibu huyo pia aliongeza kuwa, “Tukikukamata kwa mara ya kwanza, unapewa angalizo, kwa maana kwamba mzigo wako tunakaa nao wiki tatu. Baada ya hapo, tunakukabidhi nenda kaendelee kwenye sehemu rasmi. Ukirudia, tunachukua mzigo wako na wewe unaweza ukakaa ndani miezi sita.”

Choga amesema kuwa wanazingatia haki za binadamu katika ukamataji kwani watuhumiwa wa kike hukamatwa na mgambo wa kike na kuwa utaratabu wa ukamataji ni Rafiki.

Ameeleza pia kuwa baadhi ya mgambo ambao hubainika kukiuka utaratabu, ikiwemo kupokea rushwa, au kutumia nguvu, wamekuwa wakiwachukulia hatua kwa kuwafukuza kazi.

Hata hivyo, mwandishi wa habari hii alijionea kwa macho yake baadhi ya mgambo kuchukua pesa katika mazingira ya kificho. Mwandishi pia alishuhudiwa machinga wa kike wakikamatwa na mgambo wa kiume.

Ni ukaidi wao wenyewe

Kufuatia madai hayo, Mkurugenzi Mawasiliano wa Halmashauri ya Jiji la Ilala, Tabu Shaibu, amesema kuwa hawajapokea malalamiko ya aina yoyote kutoka kwa Machinga wanaodaiwa kutozwa faini hizo.

SOMA ZAIDI: Machinga Aliyevua Nguo Kuzuia Meza za Wenzake Kuhamishwa Afunguka

“Serikali imeshaeleza msimamo wake kuhusu Machinga kuondoka kwenye maeneo ambayo siyo rasmi kwao, kama kuna wanaodai kutozwa hela, sijui rushwa, ni ukaidi wao, lakini sisi hatuna taarifa zozote za wao kukumbana na changamoto kwa kuwa hatutambui uwepo wao,” alisema Shaibu.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka eneo la Kariakoo wamedai kuwa zoezi la kuwaondoa Machinga kwenye maeneo mbalimbali haliwezi kufanikiwa kama limegeuzwa sehemu ya baadhi ya watu kujipatia fedha.

“Sasa hivi hata waliokuwa wameondoka wanarejea kwa kuwa mtu anajua atatoa pesa yake na hatasumbuliwa na mgambo kama ilivyokuwa mwanzo,” anasema Rosemary, mfanyabiashara mdogo eneo la Kariakoo. “Nadhani kuna jambo litakuwa linaendelea [na] sijui kama wahusika wanajua.”

Anthony Rwekaza ni mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia anthonyrwekaza9@gmail.com.

One Response

  1. Kusema ukweli kero za migambo wa jiji kariakoo ni uchafu mtupu, pamoja ma kwamba wapo kisheria lakini njia wanazo tumia haziendi sambamba na sheria Bali waitwe wavamizi au waporaji.
    1- Nchi iliyo huru na inatumia sheria ktk utekelezaji wa shughuli zake haiwezi kuwa na watumishi waoga wasiojiamini , maana unapotumia nguvu na vurugu kutekeleza majukumu Kila siku ni kuizaririsha Nchi.
    Taifa letu linawatu wanaozingatia adabu na itii, ila muundo wa vyombo vya mamlaka ya serikali ndio hupandikiza chuki na jeuri kwa kushindwa kutumia sheria na utaratibu mzuri wa kutekeleza majukumu.

    2-Tunaomba ofisi ya mkoa ilala , pamoja na uongozi wa watekelezaji wa nyakuanyakua( migambo wa jiji) itoe elimu hadhara kwa watu , piteni na vipaza sauti fundisheni watu , hasa kwa kutoa utaratibu wa siku na namna wanavyoteleza majukumu Yao, hii namaanisha kwamba , Kuna migambo wanao ingia kuchukua pesa kwa wananchi ki magendo,siku ambazo ofisi haipo kazini, wanavizia wanajipanga watatu, wawili wanapita kuchukua pesa kwa wananchi. Hili swala nilishihudia kwa macho yangu nikiwa kibanda Cha kisajiri raini wakipita siku za jumapili wakidai pesa Tena kwa kutishia kujenga ufitini kama mtu hataki kutoa.

    Wananchi wanatoa pesa kwa woga kuogopa kesho wakiwa kazini watabeba biashara yangu, pia katika makindi hayohayo ya migambo , Kuna watu wanajenga urafiki na baadhi ya machinga hasa kwa kujiwekea vilinge maalumu vya kuchukua pesa kwa mda maalumu ni kama kirafiki kwahiyo hao machinga hawaguswi hata wawe barabarani.
    Ombi langu ni hili. kwakuwa Kila ofisi inaongozwa na sheria, na katika ofisi Kuna mikakati mbalimbali ya utekelezaji majukumu ya kiofisi, tunaomba itengeneze mpango kazi ambao utasaidia kujenga urafiki kwa wananchi, Toeni mbiu kwa wananchi juu ya utaratibu wa kamatakamata na utozaji wa faini kwamba nani anatakiwa apokee fedha, na wapi pakilipia, wakati Gani na siku maalumu za kazi kiofisi.
    3.waajiriwa wa migambo jiji: ofisi iwe na mkakati wa kutambua sifa , nidhamu ya waajiriwa hasa migambo wanaoingia mitaani kukamata kamata wafanya biashara, Kuna baadhi ya wengine hawafai kabisa kuwepo ktk ofisi hiyo maana tabia zao ni kinyume na taratibu , kwahiyo wanaipatia sifa mbaya ofisi.Kwahiyo napendekeza hilo kuwapo na mkakati maalumu wa kiofisi wa kuchunguza mienendo ya askari wake ili kubaini utovu wa nidhamu unao haribu sifa za majukumu, hii itasaidia sana kumfanya raia afanye kazi kwa utii zaidi, kwahiyo ofisi isitazame kupata faini tu Bali iwepo ktk kudumisha amani, uzalendo na kukuza wafanya biashara ili kuongeza tozo kwa uchimi wa taifa, Kuna migambo wengine hawafai kabisa kuwepo ktk ofisi hiyo kwa namna tu wanavyoteleleza majukumu bila kuzingatia sheria.
    Ahsanteni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts