The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Siku ya Wanawake Duniani: Kesho Yenye Usawa Inaanza na Leo Yenye Ujumuishi

Siku hii itukumbushe masaibu ambayo watoto wa kike na wanawake, wakiwemo wale waliopo kwenye sekta za kilimo na madini, wanapitia.

subscribe to our newsletter!

Siku moja kwenye pita pita zangu mitaani nilikutana na binti mmoja, rafiki yangu wa siku nyingi, mfanyakazi wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA). 

Wakati tukijadili mawili matatu tukawaona maafisa wa Benki ya Taifa ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). Binti yule akaniambia, “Hivi karibuni na sisi wachimbaji wadogo tunakwenda kuzindua benki yetu.”

Zilikuwa habari mpya kwangu, nikamuuliza, “Kwa hiyo, benki ya wachimbaji itatoa mikopo kwa wachimbaji kwa kutumia leseni za uchimbaji kama dhamana za mikopo?” 

Binti yule akanijibu, “Sidhani, unajua uchimbaji mdogo una mazingira magumu ya dhamana yanayosababishwa na uhaba wa taarifa za kijiolojia, kwa mfano, mkopaji asipolipa, benki wanarudishaje hela yao? Kwa kuuza leseni? Nani atanunua leseni ili akachimbe kwenye eneo ambalo wenzie hawajapata kitu?”

Sikuridhika na jibu lake, nikamuuliza tena, “Lakini ni benki ya wachimbaji, inabidi izingatie muktadha wa wachimbaji wadogo.” Ni kama vile alijua nitakachosema, akatabasamu na kunijibu, “Suala sio kuwazingatia wachimbaji wadogo, suala ni kanuni za biashara ya benki.” 

SOMA ZAIDI: Wanawake Wajitosa Kwenye Sekta ya Madini Licha ya Changamoto Wanazopitia

“Pengine tujiulize ni hatua gani zinachukuliwa na Serikali ili kufanya utafiti wa kijiolojia ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa za kijiolojia na kuacha kuchimba kwa kubahatisha?,” alihoji dada yule. “Pasi na kufanya hivyo, wanawake waliopo kwenye uchimbaji mdogo watahangaika siku zote kupata mitaji, hawatakua na kufikia uchimbaji wa kati ama kuwa wachimbaji wakubwa.”

Taratibu mazungumzo yetu yakahamia kwenye usalama mahali pa kazi. Binti yule akaniambia: “Wanawake waliopo kwenye kilimo wapo kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa yasiyoambukizwa, ikiwemo saratani, kwa sababu ya hatari zitokanazo na matumizi ya viuatilifu vyenye sumu kali. 

“Vivyohivyo, kwa wanawake waliopo kwenye uchimbaji mdogo wa madini, nao wapo kwenye hatari kubwa za kiafya zinazosababishwa na matumizi ya kemikali zenye sumu kama vile zebaki wawapo kwenye usafishaji wa dhahabu. Mara nyingi wanawake hufanya shughuli hizo bila kuwa na vifaa kinga.”

Nilielewa hoja yake, nikamjibu: “Hawa wanawake wanaposema waajiri wao hawawapi vifaa kinga, waajiri wao husema wanawake hawataki kutumia vifaa kinga. Tunafanyaje hapo?” 

Kwa mara nyingine, ni kama vile alijua nini nitajibu, naye akaendelea, “Kila mmoja husema anawapenda wanawake lakini sio wote huonyesha upendo wao kwa matendo. Kujali ndio lugha ya upendo inayosikiwa na viziwi na kuonwa na vipofu. Upendo wetu kwa wanawake waliopo kwenye kilimo na uchimbaji mdogo wa madini ni mkubwa kuliko hizi sababu tunazozitoa hapa. Ni wajibu wetu kuwalinda hawa wanawake, kwa sababu athari hizi haziwaathiri wao pekee bali watoto pia, ikiwemo ambao bado hawajazaliwa.”

SOMA ZAIDI: Hii Ndiyo Ajenda Kuu ya Wakulima Wadogo Wanawake Barani Afrika

Baada ya kuyasema hayo alifungua simu kuita gari. Nikamkatisha kwa kusema, “Unaondokaje kabla hatujajadili suala la wanawake na sekta ya uchimbaji mkubwa wa madini, mimi na wewe tumekwenda kwenye migodi mikubwa, na tumekuta idadi ndogo sana ya wanawake. Zile imani potofu kuwa wanawake wawapo kwenye siku zao hufukuza madini hazina nafasi kule kwenye uchimbaji mkubwa ila bado idadi ya wanawake ni ndogo.” 

Nikahitimisha kwa kumuuliza, “Unafikiri ni kwa nini?” Akanijibu kwa haraka, “Ili tufikie ushiriki sawa wa wanawake na wanaume kwenye uchimbaji mkubwa wa madini ni lazima tupate idadi sawa ya wanawake na wanaume kwenye taaluma kama vile uhandisi na jiolojia.”

Wakati natikisa kichwa kuashiria kukubaliana naye, alikuwa akiendelea kufafanua jibu lake kwa kusema, “Tumekuta idadi ndogo ya wanawake kwenye uchimbaji mkubwa wa madini kwa sababu kuna idadi ndogo ya wanawake kwenye taaluma za sayansi kama vile uhandisi na jiolojia wawapo vyuoni. 

“Halafu usisahau kuwa kuna idadi ndogo ya wanawake kwenye masomo ya sayansi wanapokuwa sekondari. Tutaweza kulitibu hili kwa kumruhusu binti kuota ndoto, na kuwa na mfumo wa elimu unamruhusu kuota na kuilea ndoto yake. Bila kufanya hivyo hatutapata wanawake tunaotamani kuwaona kwenye migodi mikubwa. Je, binti aliyepo Ludewa, mkoani Njombe, anaweza kuota kuwa mjiolojia angali anasoma kwenye shule isiyo na umeme, makataba, maabara, kompyuta na huduma ya mtanadao?”

Sikuwa na jibu la kumpa, mara gari aliloita lilifika, na dereva wake alikuwa mwanamke, binti mdogomdogo kama yeye. Nikajisemea na nafsi yangu, “Kweli mtandao umeibadilisha dunia. Miaka michache iliyopita huduma ya usafiri mjini ilikuwa taxi tu, hakukuwa na Uber wala Bolt, wakati huo madereva taxi wote walikuwa wanaume.”

SOMA ZAIDI: Bei Duni, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Vilio Vikubwa vya Wakulima wa Mwani Z’bar

Taratibu nikaelekea kwenye kituo cha daladala, mara nikakumbuka binti yule alivyosema, “Ni mpaka pale tutakapomruhusu binti kuota ndoto na kuwa na mfumo wa elimu unaoilea ndoto yake hata itakapotimia.” Niliyatafakari hayo huku nikiwaza tutawezaje kumruhusu binti kuota ndoto kubwa angali sheria yetu inasema aolewe akiwa na miaka 14? 

Nikajiuliza tena, tuliwaza nini kumpa cheti cha ndoa binti ambaye hatuwezi kumpa leseni ya udereva? Tulimruhusuje kuchagua mume angali hawezi kupiga kura ya kuchagua diwani? Kama hawezi kuamua masuala ya kiraia anawezaje kuwa mwanandoa?

Licha ya shauku yangu kubwa ya kuchochea mabadiliko yatakayolinda usawa kati ya mwanamke na mwanaume, ninapowaza kuwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 bado haijafanyiwa marekebisho ili kuufanya umri wa kuolewa kwa binti kuwa miaka 18, naishiwa nguvu. 

Nakosa motisha ninapokumbuka kuwa kulikuwa na kesi, na Mahakama iliamuru kufutwa kwa vifungu kadhaa vya sheria ili kuzilinda ndoto za mabinti dhidi ya wanaume wanaotaka kuwaweka ndani kabla ya kufikisha umri wa kupewa namba za NIDA.

Nikiwa nimesimama kwenye daladala, napokea maelekezo ya kondakta anayenitaka nirudi nyuma na wengine weweze kusimama kwenye daladala hiyo iliyojaa. Nashikilia bomba huku najiuliza tena, “Kwa nini Serikali haijepeleka muswada bungeni ili ufanyiwe marakebisho kufuta uhalali wa ndoa za utotoni?”

SOMA ZAIDI: Ni Upi Mtazamo wa Wakulima Wadogo Juu ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi?

Hata hivyo, nikaimbia nafsi yangu kuwa, “Leo ni siku ya wanawake ulimwenguni, siku hii ikawe chachu kwangu na wengine wote kupigania mabadiliko yenye kuleta usawa na ujumuishi bila kuchoka. Tuutafsiri upendo wetu kwa wanawake kwa kuutafuta usawa.”

Nilipofika nyumbani nikajisemea tena, “Siku ya wanawake si karibu inaisha? Kwa hiyo ikiisha, ndiyo mapambano yameisha? Yanaishaje bila ushindi kupatikana?” 

Nikajijibu mwenyewe, “Kila siku nitakayofungua macho yangu na kuwaona wanawake, kwangu itakuwa siku ya wanwake duniani, itakuwa siku nyingine ya kufanya kila linalowezekana ili kuutafuta na kuupata usawa kati ya wanaume na wanawake.”


Clay Mwaifwani ni mwanasheria na mdau wa usimamizi dumivu wa rasilimali za maliasili. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 758 850 023 au claymwaifwani09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *