Machi 6, 2024, chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, kupitia Mkutano Mkuu wa chama, kilifanya uchaguzi wa viongozi wapya ambao wataongoza taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kwenye uchaguzi huo, Dorothy Semu alimsinda Mbarala Maharagande na kuwa Kiongozi wa Chama, akichukua nafasi ya Zitto Kabwe aliyehudumu nafasi hiyo kwa muongo mmoja.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu pia walimchagua kwa kura nyingi za ndiyo Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, akichukua nafasi ya Juma Duni Haji, mwanasiasa mkongwe aliyejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho mwishoni mwa mchakato.
Ingawaje viongozi wengine wengi walichaguliwa kwenye mkutano huo mkuu, swali ambalo wengi wanajiuliza ni iwapo Dorothy Semu, mwanamama aliyeacha utumishi wa umma na kujiunga na siasa za upinzani, ataweza kushika majukumu ya uongozi kama vile mtangulizi wake, Zitto Kabwe, alivyofanya.
Kutoa jibu la uhakika kwa sasa ni jambo lenye changamoto. Kabwe amejijengea sifa kama kiongozi wa kisiasa tangu mwaka 2005 alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza, na amekuwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri na anayetambulika na umma.
SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Kwa Nini ACT-Wazalendo Tumeamua Kuwa na Ofisi?
Semu, ingawa ameshikilia nyadhifa mbalimbali ndani ya chama tangu mwaka 2015 – Waziri Mkuu wa Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT-Wazalendo, Kaimu Mwenyekiti wa Chama Taifa, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Katibu Mkuu, Katibu wa Fedha na Katibu wa Sera na Utafiti –bado jina lake halijulikani sana miongoni mwa Watanzania walio wengi.
Kupitia nyadhifa hizo, ni dhahiri kwamba Semu ana ufahamu mzuri wa masuala ya chama, na huenda kuwa ni bora kwa chama kuhama kutoka kwa uongozi wa kisiasa kwenda kwa uongozi wa utendaji.
Hii inaweza kusaidia katika kuimarisha misingi ya chama kwa kiwango cha taasisi badala ya kuendeshwa kwa muktadha wa utashi wa kiongozi wa sasa.
Kwa hoja iliyotolewa hapo juu, ninatofautiana na wale wanaotaka kufanya ulinganisho kati ya Semu na Kabwe. Semu hakuteuliwa kwa lengo la kuwa ‘Zitto Kabwe wa pili.’ Amechaguliwa kwa kusudi la kujenga nguvu ya chama kama taasisi.
Mafanikio yake katika kutekeleza jukumu hili yataonekana kadri wakati unavyosonga mbele, lakini changamoto yake ya kwanza ni kukiandaa chama kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Mitihani
Mtihani pekee wa Kabwe unalenga katika jambo moja tu: kumpa nafasi mrithi wake kufanya kazi bila kuingiliwa na kiongozi wa awali.
SOMA ZAIDI: Ni Zipi Fursa, Changamoto za Ukuaji wa ACT-Wazalendo Kama Chama cha Upinzani?
Mara nyingi, ni changamoto kwa kiongozi aliyeondoka kuwaacha wengine waendeshe taasisi bila kuingilia kati, kwani wanaweza kuwa na tamaa ya kuona vitendo vinavyofanana na vile walivyofanya wao wenyewe, au hata kujaribu kudhibiti maamuzi ya kiongozi mpya.
Ili taasisi iwe imara na Semu afanikiwe, ni muhimu sana kwa Kabwe kuvuka mtihani huu.
Othman, ambaye wafuasi wake hupenda kumwita OMO, pia ana mtihani wa kipekee. Kama Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mtu aliyezoea mazingira ya utumishi na siasa za Zanzibar, anakabiliwa na changamoto ya kubadilika na kuwa kiongozi anayeshughulika na masuala ya Muungano kwa pande zote.
Hii siyo jambo dogo, hasa kwa kuzingatia jukumu lake kubwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambalo linahitaji uzingativu wa kina katika masuala ya Zanzibar.
Hata hivyo, anawezaje kubadilika kidogo na kuhakikisha kwamba anatumia lugha inayojumuisha wanachama na wananchi wa pande zote za Muungano?
SOMA ZAIDI: Upi Mustakabali wa ACT-Wazalendo Kwenye Siasa za Upinzani Tanzania?
Hili ni swali muhimu ambalo linahitaji kuzingatiwa kwa umakini. Hapa ndipo Othman atakapohitaji msaada mkubwa kutoka kwa msaidizi wake kwa upande wa Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita.
Kwa afya na uhai wa chama, ni lazima Othman Masoud Othman aonekane na aeleweke na pande zote za chama.
Kupokezana uongozi
Mwisho, niseme kwamba ACT-Wazalendo wameonyesha kielelezo bora cha mchakato wa kupokezana uongozi katika ngazi ya juu ya chama. Sera yake ya kuwaenzi viongozi wake wastaafu itakuwa msukumo kwa viongozi wakuu wa chama kuepuka ukiritimba na kutaka kung’ang’ani madaraka.
Hii inatokana na ukweli kwamba viongozi hawa wanajua kwamba watatunzwa wanapostaafu na bado watakuwa sehemu ya muundo wa maamuzi ya chama. Kabwe amesisitiza mara kadhaa kwamba lengo la chama ni kujenga taasisi imara badala ya kutegemea mtu mmoja.
Kabwe na Duni watajiunga moja kwa moja na Kamati ya Uongozi wa Chama, ambayo inajumuisha wajumbe wa Kamati Kuu pamoja na viongozi wakuu wa zamani wa chama.
Hii ni hatua muhimu ambayo itahakikisha kwamba kama taasisi, ACT-Wazalendo itaweza kuendelea kunufaika na utajiri wa uzoefu kutoka kwa viongozi mbalimbali waliohudumu kwenye chama hicho hapo awali.
SOMA ZAIDI: Ripoti ya CAG: ACT-Wazalendo Yapendekeza Njia Nne Kudhibiti Ubadhirifu Serikalini
Hata hivyo, mafanikio ya mchakato uliokamilika kwa kupatikana safu mpya ya uongozi ndani ya ACT-Waalendo hayatapimwa tu kulingana na matokeo ya uchaguzi uliopita, bali pia kwa jinsi chama kinavyoendelea kutekeleza majukumu yake bila hitilafu yoyote.
Ufanisi wa mchakato wa kupokezana uongozi utapimwa katika miezi ijayo, na wachunguzi wengi wa masuala ya kisiasa watakuwa macho kuona mwelekeo wa hali hii.
Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au Twitter kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Ingekuwa Iran, ningesema sasa Zitto ni Ayatollah na Semu ni rais tu wa sirkal. Hata hivyo, nawatakia kila la heri.
Nkwazi Mhango