Watoto wanapokuwa nyumbani, mara nyingi hujishughulisha na michezo mbalimbali ambayo husaidia kujiburudisha na kujenga mahusiano mazuri baina yao.
Kila hatua ya ukuaji wa watoto huleta matukio mengi ya furaha, lakini pia kuna nyakati ambazo matukio hayo yanaweza kuhatarisha usalama wao.
Swali muhimu la kujiuliza ni je, wazazi tunajua vya kutosha kuhusu elimu ya huduma ya kwanza kwa watoto pindi wanapokabiliwa na dharura nyumbani?
Ni wazi kwamba wazazi wengi hatuna uelewa wa kutosha kuhusu huduma ya kwanza kwa watoto wetu. Hivyo, wakati dharura inapotokea, mara nyingi tunajikuta tukishindwa kujua cha kufanya ili kuokoa hali ya hatari inayowakabili watoto.
Kiuhalisia, kuna matatizo mengi ambayo yanaweza kushughulikiwa kwa huduma ya kwanza.
SOMA ZAIDI: Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Ujauzito Kama Una Ugonjwa wa Kudumu
Kwa mfano, mtoto akiwa na maumivu ya muda mfupi, mzazi unaweza kutoa huduma ya kwanza kwa kuweka barafu au kitu cha baridi kwenye eneo lenye maumivu, mtoto akapumzika na kumpatia dawa za kupunguza maumivu kama vile paracetamol – kwa ushauri wa daktari au kulingana na umri wa mtoto.
Huduma ya kwanza kwa matatizo kama maumivu ya muda mfupi, majeraha madogo, pumu, au kushtuka kwa mguu au mkono ni muhimu ili kupunguza madhara, au kuzuia hali hiyo kumdhoofisha zaidi mtoto.
Hivyo, ni muhimu sana kwa wazazi, walezi, na watunzaji wa watoto kujifunza jinsi ya kutoa huduma ya kwanza.
Huduma hii ni muhimu kwa kuwa inaweza kuokoa maisha ya mtoto wakati ambapo msaada wa kitaalamu hauko karibu, au kabla ya kumpeleka hospitalini kwa matibabu zaidi.
Ili kutoa huduma ya kwanza kwa ufanisi, ni muhimu kuwa na kisanduku cha huduma ya kwanza nyumbani na hata katika gari lako, kwa wale wenye nayo. Kisanduku hiki kina zana muhimu kama vile pamba, bendeji, spiriti, na dawa za vidonge.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwajengea Watoto Wetu Misingi ya Maadili na Tabia Njema?
Pia, ni muhimu kuwa na mwongozo wa jinsi ya kutumia vifaa hivi kwa usahihi. Visanduku vya huduma ya kwanza vinapatikana katika ofisi za Shirika la Msalaba Mwekundu, maduka ya dawa, na maduka ya vifaa tiba.
Ili kuhakikisha usalama wa watoto wetu, ni wajibu wetu kama wazazi au walezi kuwa tayari kutafuta taarifa muhimu juu ya huduma za kwanza kwa matatizo mbalimbali ambayo huwatokea watoto kutokana na michezo, lakini pia kuwa na kisanduku cha huduma ya kwanza kama sehemu ya tahadhari.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.