Kwa muda mrefu nimekuwa nikifuatilia jinsi kampuni ya Azam Media inavyozungumziwa na wadau wa soka na hasa mamlaka husika, yaani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB); ni kama zinaona zimeshushiwa neema ambayo hazikustahili.
Yaani ni muda wa kuishukuru Azam Media kwa kununua haki za matangazo ya televisheni ya mechi za Ligi Kuu na Championship na kuhimiza shukrani hizo zitolewe na vyombo vingine vinavyojishughulisha na mchezo huu pendwa nchini.
Hakuna shaka kwamba Azam Media imefanya makubwa na imeleta mapinduzi makubwa katika soka tangu ilipoingia na kuanza kurusha moja kwa moja Ligi Kuu mwaka 2013. Na imekuwa ikiboresha dau lake kila mkataba unaposainiwa upya.
Hakuna ubishi kwamba Azam Media imefanya kile ambacho nchi nyingi za Afrika zimeshindwa kufanya na sasa inapanua wigo wake hadi kwa nchi jirani kuendeelea kutupa burudani pana zaidi.
Mkataba wa sasa wa matangazo ya Ligi Kuu umezipa ahueni zaidi klabu zetu kwa kuangalia kiasi ambacho zinapata kila baada ya miezi mitatu, nadhani Shilingi milioni 40, ambazo kwa kweli si haba ukizingatia kuwa klabu zina wadhamini wao binafsi na zina mdhamini wa jumla wa Ligi Kuu, ambaye ni benki ya NBC.
SOMA ZAIDI: Utitiri wa Marathoni Unakisaidiaje Chama cha Riadha Tanzania?
Ilichofanya Azam Media ni kutungua macho tu kuhusu upande huu wa vyanzo vya mapato. Wakati wa mazungumzo ya Azam na TFF kuna klabu zilikuwa hazielewi kabisa zinawezaje kutengeneza fedha kwa kutumia matangazo ya televisheni ya moja kwa moja, lakini tulipowapa mkurugenzi wa masoko aongee nao, viongozi walishangaa jinsi fursa zilivyo nyingi.
Lakini kutokana na viongozi na watendaji wa klabu kubadilika kila mara, ile elimu waliyoipata siku ile haijatekelezwa na bado klabu zinaendelea kuingalia Azam Media kama mfadhili aliyeshushwa na Mungu badala ya kuchacharika kutumia fursa ya matangazo ya moja kwa moja kutengeneza vifurushi vyake kwa ajili ya kuwauzia wadau wengine.
Kwa jinsi hali ilivyo, ni kama mamlaka za soka zinasubiri Azam Media iboreshe mkataba wake na si wao kukaa chini na kuangalia watawezaje kuboresha na kuipa kampuni hiyo mpango wao wa mkakati ujao wa kuuza haki za matangazo ya televisheni.
Uzoefu kwengineko
Kwa wenzetu, ambao wengi hawataki tulinganishwe nao eti kwa sababu wako kiwango cha juu zaidi, mpango wa mauzo ya haki za televisheni huanzia Ligi Kuu, yaani waendeshaji wa ligi kama ile ya England (Premier League), ya Hispania (La Liga) ya Ujerumani (Bundesliga) au ya Italia (Serie A).
Hawa ndiyo hutengeneza vifurushi, au bidhaa, kwa ajili ya kuuza kwa kampuni tofauti. Na kabla ya kwenda kwa wanunuzi, Ligi Kuu huitisha kikao cha klabu zote na kuwaeleza mkakati huo na zikishakubali ndipo zabuni hutangazwa.
SOMA ZAIDI: Mpira wa Miguu Sasa ni Sekta Muhimu, Uratibiwe
Mkataba wa sasa wa matangazo ya Ligi Kuu umezipa ahueni zaidi klabu zetu kwa kuangalia kiasi ambacho zinapata kila baada ya mwezi, yaani Shilingi milioni 40, ambazo kwa kweli si haba ukizingatia kuwa klabu zina wadhamini wao binafsi na zina mdhamini wa jumla wa Ligi Kuu, ambaye ni benki ya NBC.
Walionunua haki hizo ni pamoja na televisheni ya Sky, ambayo ilinunua vifurushi vinne kati ya vitano na kampuni hiyo itaonyesha mechi 215 kila msimu, wakati Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limeendelea kushikilia haki za picha za matangazo ya matukio makubwa, au highlights, huku TNT ikichukua mechi 53.
Vifurushi hivyo ni kama vile zile mechi za Jumapili ambazo zimebatizwa jina la Super Sunday kuanzia saa 10:30 Jumapili, kifurushi ambacho kimechukuliwa na Sky ambayo, kwa mara ya kwanza, itaonyesha moja kwa moja mechi 10 za siku ya mwisho.
Kifurushi kingine ni cha mechi za Jumamosi kuanzia saa 12:30 jioni na mechi mbili za katikati ya wiki kilichochukuliwa na TNT, huku Mechi ya Siku, au Match of the Day, kikibakia katika matukio makubwa na kikichukuliwa na BBC.
Kwa mujibu wa mpango huo wa Ligi Kuu, kampuni zinaweza kununua hadi vifurushi vinne tu, kitu ambacho kinapanua wigo kwa kampuni nyingine kuwa washirika wa mashindano hayo maarufu duniani.
Tuamke
Kwa hiyo, kazi ya TPLB ni kuangalia vifurushi hivyo vinajumuisha nini na kama mazingira yetu yanawezesha mkakati huo kufanyika.
Mfano, kama kuna kampuni inayoweza kufanya uzalishaji, au production, mkataba utenganishe uzalishaji na haki za matangazo ili Azam Media ijigawanye na hivyo TPLB iweze kubuni vifurushi zaidi ya matangazo ya moja kwa moja na hivyo kujipatia fedha nyingi zaidi, huku ikipata washirika wengi zaidi wa kusaidiana nao kusambaza burudani hiyo katika nchi ambayo wananchi wake wana wendawazimu wa soka.
SOMA ZAIDI: Baraza la Michezo Lifikirie Kuandaa Olimpiki Yetu Kwanza
Kwa hiyo, badala ya kusubiri kuletewa sahani ya dhahabu mezani na kutumia muda na nguvu nyingi kujaribu kuonyesha jinsi wanavyoshindwa kueleza kwa ufasaha shukrani zao kwa Azam, ni muda sasa umefika kwa TPLB na TFF kuanza kufikiria zinawezaje kuboresha mkataba wa matangazo ya moja kwa moja ili kujiongezea kipato na kupanua wigo wa washirika wake, ambao zamani waliitwa wadhamini.
Ni kweli Azam Media wanapaswa kushukuriwa sana, lakini soka ni biashara kubwa ambayo inatoa fursa nyingi za kujipatia fedha. Ni muhimu kwa wahusika kuangalia fursa hizo bila ya kukwaruzana na Azam, ambaye ni mshirika mkuu, kwa ajili ya kuendeleza soka letu.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
2 responses
Hiki pia ni kifurushi tosha
Timu za ligi husika ziamke na kuunga mkono taarifa hii kwa maslahi mapana ya michezo na uendelevu na kipato cha wavuja jasho michezoni..
Tatizo Angetile Osiah ni mshauri ambaye yeye alifeli pakubwa akiwa katibu mkuu wa TFF. Kwa maoni yangu hana moral authority ya kushauri. Ukilisoma hilo andiko lake kwa ndaaaaaani antipodean TFF na TPLB. Wakati yeye alifeli.