Mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter, umekuwa ni jukwaa la mijadala mtambuka. Mimi ninafuatilia zaidi masuala ya haki za binadamu na hivyo kushuhudia namna kukamatwa kwa mtumiaji maarufu wa mtandao huo, Sukununu, kulivyozua mjadala wenye viashiria vya sheria na haki.
Sukununu amekuwa katika ‘ligi ya peke yake’ dhidi ya watu binafsi na wanasiasa kupitia maandiko yake. Ninakiri, kuna utata usiyo na athari katika maoni yake. Mwitikio wa watumiaji wenzake wa X kufuatia kukamatwa kwake, hata hivyo, umenipa sababu ya kutafakari sana namna tunavyochukulia mambo kama taifa.
Kwa mfano, baadhi ya watumiaji wa X walistaajabu kusikia Sukununu atapewa msaada wa kisheria baada ya mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kutafuta taarifa zake na kuonesha nia ya kumpatia kijana huyo msaada huo. Mshangao wa watumiaji wa X haushangazi. Ni kutokana na upungufu wa taarifa, na pengine, kumradhi, maarifa.
Kimsingi, kila mtu ana haki ya kupata msaada wa kisheria. Niliandika kwa ufupi katika akaunti yangu ya X kwamba siyo ajabu watuhumiwa wa makosa ya jinai kutetewa na wakili. Nitafafanua wajibu wa wakili kwa ufupi.
Wajibu wa mawakili
Wakili anawajibika kwa Mahakama kuisaidia kufikia uamuzi wa haki. Mfumo wetu wa kisheria unawaachia wadaawa, yaani mlalamikaji na mshitakiwa, nafasi ya kuendesha kesi zao. Mahakama inakuwa katikati kama mwamuzi tu.
SOMA ZAIDI: Mahakama Imdhibiti DPP Kuondokana na Kero ya Futa Kesi, Kamata, Shitaki Upya
Mara chache Mahakama itaelekeza utaratibu au uwasilishaji, lakini haiwajibiki kumuepusha mdaawa na hatari, kujenga au kubomoa kesi yake. Kwa misingi hiyo, wakili anatarajiwa kuisaidia Mahakama kuona miisho ya haki.
Vilevile, wakili anawajibika kwa jamii na mteja wake. Huu ni wajibu wenye mkanganyiko. Wakati mwingine siyo rahisi kuoanisha maslahi, hususani pale jamii inapoona fulani ni mhalifu. Ukimtetea mtu huyo utaonekana unalinda mhalifu. Lakini mawakili wamefunzwa mbinu za kulinda maslahi ya pande zote.
Wajibu wa wakili ni kusaidia kuhakikisha taratibu za kufikia uamuzi zimefuatwa, kwa upana, kulinda haki za mtuhumiwa wakati anaposhitakiwa. Wakili yuko kwenye nafasi bora kuona kama taratibu za ukamataji na upekuzi zilifuatwa, kama maelezo ya onyo yalichukuliwa kwa hiyari, na zaidi. Haya yote yana athari katika matokeo ya kesi.
Pia, katika mashitaka ya jinai, wakili anasaidia kuonesha endapo mashitaka yamethibitishwa bila kuacha mashaka. Kiwango hicho cha uthibitisho ni muhimu sana kufikiwa kwa kuwa, bila hivyo, siyo rahisi kupata hatia, au ikapatikana inaweza kuwa ya ‘kimagumashi.’
Wakili ataionesha Mahakama kama ushahidi haujatosheleza. Kwa mantiki hiyo, atamuepusha mtuhumiwa na adhabu asiyostahili. Raia asiye na wakili anaweza kufanya hivyo lakini siyo mara zote.
SOMA ZAIDI: Mahakama Tanzania Isikwepe Wajibu Wake wa Kusimamia Utoaji Haki
Kwa kufahamu umuhimu wa msaada wa kisheria, Mahakama na Serikali huwapangia mawakili kuwatetea, au kuwawakilisha, watuhumiwa wa mashitaka ya mauaji. Shabaha siyo tu kumuepusha mtuhumiwa na jela bali kuisaidia Mahakama kutenda uamuzi wa haki.
Zaidi, maadili ya mawakili yanawazuia kuwabagua watuhumiwa, isipokuwa penye mgongano wa kimaslahi. Kwa hiyo, tukisema mtuhumiwa huyu asitetewe, yule atetewe, tutakuwa tunapalilia ubaguzi na kuua dhima na wajibu wa mawakili kwa Mahakama.
Polisi wazingatie sheria
Jeshi la Polisi limekuwa likishutumiwa kufanya kazi bila kufuata sheria na taratibu. Kikawaida, haitarajiwi mtuhumiwa anyakuliwe au kutekwa, au ateswe ili kupata kiri ya kosa, ama kumkomoa.
Taarifa nilizozithibitisha ni kwamba Sukununu alinyakuliwa, hakukamatwa; alitwaliwa katika oparesheni maalum dhidi yake. Waliomtwaa hawakujitambulisha, hawakuwa wamevaa sare, na hawakumfahamisha haki zake akiwa chini ya ulinzi.
Sukununu hakupewa haki zake kama mtumhumiwa. Mathalani, alishikiliwa zaidi ya masaa 48, na hakushitakiwa kwa wakati. Muda wote hakuwasiliana na ndugu au wakili. Hakutibiwa – kufuatia kipigo. Kuruhusu polisi wafanye haya bila kuhofia uwajibikaji ni kuhalalisha matumizi mabaya ya mamlaka.
SOMA ZAIDI: Tukiwa Tunaadhimisha Wiki ya Sheria, Tuwafikirie Wanaoendelea Kusota Gerezani Bila Kutiwa Hatiani
Vilevile, inadaiwa Sukununu alipigwa sana, siyo tu ili akiri makosa wanayomtuhumu nayo, bali kwa kumkomoa. Hii, kwa bahati mbaya sana, siyo habari mpya kwani polisi mara nyingi wameshutumiwa kutesa watuhumiwa. Hata hivyo, hali hii haitakiwi kuzoeleka.
Kutesa watuhumiwa wakiwa mikononi mwa polisi ni kuondoa mantiki nzima ya kuwa na Mahakama. Adhabu na anayeitoa, vyote sio halali. Polisi wadhibitiwe.
Tunatarajia mtu akikamatwa ashitakiwe mahakamani, tena kwa uharaka, ili haki zake na za wanaomshitaki zilindwe. Huwezi kusema unatenda haki wakati mshukiwa amepigwa, ameteswa na ametendewa kama mhalifu kabla ya kukutwa na hatia. Polisi siyo Mahakama; katika kesi wao ni mashahidi tu.
Ni hatari kuiacha Serikali itumie sheria na mabavu bila udhibiti. Kuwapa polisi idhini ya kutesa, kuteka, na kufungua kesi dhidi ya mtu yeyote kwa kuwa inadhaniwa ni mkosaji, ni kuhalalisha matendo na hatua zao kwa wasio wakosaji. Ni vema taratibu zizingatiwe.
Tulinde uhuru wa maoni
Tunahitaji kuheshimiana na kulinda vidole vyetu visiathiri wengine, hususani tunapotumia mitandao ya kijamii. Vilevile, tunahitaji kuvumiliana. Hadi naandika, hakuna kipimo sahihi cha uhuru wa maoni, isipokuwa kanuni ya asili ya kutomuumiza mwenzako.
SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania
Mwamko wa kuwashughulikia watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaoingia katika mgogoro na Serikali hauamaanishi nia ya kutokomeza uhalifu; ni kwamba ‘wakubwa’ tu hawajafurahia kushikwa sharubu.
Ndiyo maana masuala yanayowahusu watu binafsi Serikali haihangaiki nayo. Sheria zinatumika kiupendeleo dhidi ya wakosoaji, au watu wanaogusa maslahi fulani yaliyotengwa.
Nihitimishe kwa kusema – kila raia ana haki ya kutendewa kama mtu huru hadi atakapokutwa na hatia. Kwa hiyo, matendo yote yanayomomonyoa uhuru wa mtu kabla hajakutwa na hatia ni batili, kinyume cha sheria, na hayafai kuungwa mkono.
Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.