Ikitokea kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kuwa na utaratibu wa kuushirikisha umma juu ya orodha ya vitabu alivyosoma kwa mwaka, kama afanyavyo Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama, natamani Kusadikika cha Shaaban Robert kitabu kiwe moja ya vitabu katika orodha yake ya kwanza.
Siwezi kupindisha maneno juu ya hili, kweli natamani sana asome pia kitabu changu, Jinsi Ya Kurudi Nyumbani. Kama mwandishi, huwa naona haya kutangaza kitabu changu, japokuwa kadri siku zinavyoendelea ndivyo ninavyobadilika katika eneo hilo. Ila aibu itabidi zikae pembeni kwani siwezi muonea haya Rais Samia. Hata hivyo, kwa leo ninaipigia debe Kusadikika na si kitabu changu.
Kiongozi wa nchi anayesoma huakisi jamii inavyosoma. Na kama jamii haisomi, basi anao uwezo wa kuwahamasisha wananchi kufanya hivyo. Baada ya kuisoma Kusadikika, nimetamani kila kiongozi katika ngazi ya Serikali, sekta ya umma na binafsi, asome hiki kitabu na kukipitia mara kwa mara katika uongozi wake.
Watu wengi hudhani kwamba wanaweza kupata hekima ya uongozi, mawaidha ya maisha, tafakuri ya maadili na mambo yafananayo na hayo kupitia vitabu vinavyoongelea mambo hayo kwa ile lugha ya Hatua Tano za Mafanikio, au Njia Saba za Uongozi bora. Lakini siy kweli.
Ipo siri kubwa iliyojificha katika uandishi wa kubuni. Siyo tu kwa kumpa mwandishi nyenzo ya kutumia nguvu ya ubunifu aliyopewa na Mungu, lakini pia humpa msomaji uwanja wa kudadavua mambo ambayo yameandikwa kwa lugha ya picha, mafumbo, ucheshi, na kadhalika.
SOMA ZAIDI: ‘Kufikirika’ ya Shaaban Robert na Uhalisia Usiyopitwa na Wakati
Na bila shaka, Shaaban Robert aliweza kung’amua hilo. Maana katika Kusadikika anatumia hadithi kuelezea hali ya maisha halisi. Kama ilivyo katika kitabu chake kingine, Kufikirika, mwandishi anatupeleka kwenye ulimwengu uishio katika fikra tu, japokuwa ukianza kusoma habari za nchi hiyo unaanza kujiuliza kama kweli huko ni Sadiki au ni mahali fulani ambapo umeshawahi kufika.
Mwandishi anasema katika utangulizi wake kuwa Kusadikika ni nchi ambayo kuwako kwake hufikirika kwa mawazo tu. Tena nchi hiyo iko katikati ya mipaka sita. Kaskazini imepakana na Upepo wa Kaskazi, Kusini kuna Upepo wa Kusi, Mashariki kuna Matlai na Magharibi kuna Upepo wa Umande. Kwa juu imepakana na Mbingu, na kwa chini imepakana na Ardhi.
Fundisho
Simulizi inamwangazia jicho Karama, raia mmoja wa Kusadikika. Anaingia matatani baada ya kukusudia kuwa mwanasheria wa kwanza Kusadikika. Waziri wa Kusadikika, aitwaye Majivuno, analileta jambo hili kwa Mfalme. Ana hoji, kwa nini Karama afanye hivyo bila ruhusa ya Serikali?
Halafu, kama ameanza na tamaa ya kuwa mwanasheria, kesho yake atataka kuwa diwani, kisha waziri, baadaye atataka na ufalme pia. Yaliyoanza kama mambo madogo huwa makubwa!
Kama ilivyo katika Kufikirika, mwandishi anajaribu kuonesha kwamba kuna tofauti za kitabaka katika jamii. Japokuwa Karama analetwa mbele ya mfalme, sheria za Wasadikika hazimpi nafasi mshtakiwa kujitetea.
SOMA ZAIDI: Laiti Kama Ningepata Nafasi ya Kumhoji Shaaban Robert
Akifika mbele ya Mfalme, anasikiliza na kukubali hukumu. Si hivyo tu, katika baraza hilo la Mfalme walikuwepo pia watoto wao, matajiri na watu wengine maarufu.
Hata hivyo, jambo la tofauti lilitokea kwake. Aliomba siku sita za kujitetea, akakubaliwa. Katika kujitetea kwake, Karama anaikumbusha Serikali ya mfalme watu mbalimbali walioondoka Kusadikika, wakiwa wametumwa na nchi yao kwenda ng’ambo katika safari zilizohatarisha maisha yao.
Lakini kwa sababu ya mapenzi yao kwa nchi yao, walijitoa mhanga ili kujifunza wengine wanaishije huko duniani. Waliporudi nyumbani, pamoja na mengi mema waliyoleta kama mafunzo, hawakupewa heshima waliyostahili. Badala yake walibezwa, wakatukanwa na hata kufungwa.
Kwa upande mmoja, simulizi hii inaonesha ujasiri wa Karama katika kutetea fikra zake ambazo zilionekana kuwa ngeni na hatarishi kwenye jamii ya Kusadikika. Kuna mengi ya kujifunza katika ujasiri huo.
Hata hivyo, hadithi hii ni zaidi ya jambo hilo. Katika kitabu hiki, mwandishi anaongelea sana hali changamani ya ubinadamu. Wema na ubaya, upendo na chuki, ukarimu na choyo, haya yote yanaishi kama fila na lila ndani ya moyo wa mwanadamu, na hivyo ndani ya jamii.
SOMA ZAIDI: ‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania?
Anasema, “Lila na Fila hawatangamani. Kinywa cha Lila kikisema, sikio la Fila hujidai halisikii; jicho la Lila likiona, lile la Fila hujifanya halioni; moyo wa Lila ukijilainisha kwa mapenzi na huruma, ule wa Fila hujifanya mgumu kama jiwe lisilo maisha kwa chuki na uadui.” (uk, 28).
Hivi karibuni, kumekuwa na msemo unaotajwa sana na vijana – YOLO (You Only Live Once), ukimaanisha kuwa mtu huishi mara moja tu kwa hiyo tule bata la kutosha. Ponda mali, kufa kwaja.
Karama anasisitiza sana umuhimu wa kuwa na jamii inayoona mbele na kujijenga sasa kwa ajili ya vizazi vijavyo. Anasema kushusu Wasadikika, “Andao lolote kwa ajili ya wakati ujao yalikuwa si juu yao, ingawa walijua barabara kuwa watu watakaoishi katika wakati huo walikuwa si wengine ila waototo wao wenyewe. . .” (uk. 43).
Hata hivyo, Karama anaweka wazi kuwa zipo kanuni ambazo lazima zifuatwe ili watu waone mafanikio katika maisha. Mojawapo ya kanuni hizo hufuata msingi unaotambua kuwa “Ulimwengu uliumbwa kabla ya wakaaji wake.”
Anatoa mfano kwa kusema, “Ukitaka biashara ya vitabu isitawi watu hawana budi kufunzwa kusoma kwanza. Kusoma kusipotangulia vitabu vizuri vitaonekana vibaya.”
Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.