The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Laiti Kama Ningepata Nafasi ya Kumhoji Shaaban Robert

Sidhani kama kuna mwandishi yeyote ambaye nimewahi kumsoma aliyemwelezea mke wake kipenzi kwa jinsi alivyofanya Shaaban Robert.

subscribe to our newsletter!

Nasema hili kwa utani, japokuwa ninamaanisha – sidhani kama kuna mwandishi yeyote ambaye nimewahi kumsoma aliyemwelezea mke wake kipenzi kwa jinsi alivyofanya Shaaban Robert. Kwa lugha ya siku hizi tunaweza kusema, ajengewe sanamu yake pale Posta!

Huyu bwana alimpenda mke wake. Kumpenda huko, na kumwelezea huko kwa uzuri na uwazi kimaandishi kuna maana kubwa sana. Mwanaume anayemzungumzia mkewe kwenye kadamnasi ni wa pekee. Na tena upekee huo ni mkubwa zaidi kama atachukua kalamu na kuandika kuhusu mkewe kwa mapambo yote ya lugha, bila kujizuia. 

Cha kusikitisha ni kwamba mke aliyepambwa alikuwa amefariki. Pengine alipokuwa hai alipata kufurahia mashairi na barua za mumewe. Katika kitabu chake cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza 1971 na Mkuki na Nyota, Shaaban Robert ameambatanisha shairi aliloliita Amina, aliloandika baada ya kifo cha mke wake huyo kipenzi. Baadaye, alioa tena.

Lakini upendo wake katika familia haukuishia kwa mkewe tu. Mwanzoni mwa kitabu hicho Shaaban Robert anamwandikia binti yake, Utenzi wa Hati, na kijana wake wa kiume, Utenzi wa Adili, aliowapata na mke wake wa kwanza, akiwaasa kuhusu mambo mbalimbali, jambo ambalo nadhani walilifurahia katika maisha yao. 

Lakini ukarimu huu wa maneno haukuanza na yeye. Wakati fulani alipokuwa akihama kituo cha kazi, kutoka Tanga kwenda Mpwapwa, wafanyakazi wenzake walisema maneno mazuri kuhusu yeye. Maneno ya wakili wa Mudir wa Forodha yalinukuliwa:

Uhamisho wa Shaaban Robert toka idara yetu si hasara ndogo. Twasikitika kuwa uhamisho wake hauzuiliki. Kila jitihada iliyofanywa kuzuia jambo hili haikufaulu kwa sababu wakuu kuliko sisi wameamua jambo hili. Basi imebaki kwetu kuomba apate heri aeendako. Tunataka akakariri matendo mema aliyotenda katika idara yetu pia akafanikiwe zaidi. Ingawa hatakuwa kati yetu tena lakini jina lake litadumu katika kumbukumbu zetu. Katika kumbukumbu hizo jina hilo litakuwa zuri na jipya siku zote. Kwa heri, Shaaban!

Yalimgusa maneno hayo kiasi kwamba Shaaban anasema: “Nilikuwa nimezoea kusikia maneno mazuri kama haya mara kwa mara. Baba yangu alikuwa mmoja wa mahatibu wema sana katika wakati wake. Lakini mara hii maneno yaliyosemwa yalinipenya katika moyo wangu kwa sababu yalikuwa na mchanganyiko wa furaha na huzuni.’ (uk. 47). Kwa hakika, tunda halidondoki mbali na mti wake na kila kitu kina chimbuko lake.

SOMA ZAIDI: ‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania?

Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini kina sehemu mbili – Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. Katika sehemu ya kwanza, mwandishi anaanza kuelezea maisha yake akiwa na umri wa miaka 27 kwani lipo andiko lingine lililoangazia kipindi cha nyuma yake; anafafanua hilo kwenye Utangulizi wa kitabu. 

Kama jina lake linavyosawiri, sehemu ya pili imeangazia maisha yake baada ya kutimiza miaka hamsini. Ndani ya kitabu hiki, Shaaban Robert anaongelea mapenzi, ndoa, familia, kazi, na mahusiano yake na wanajamii wengine – haswa washairi.

Upekee wa uandishi wake

Shaaban Robert haogopi kuonesha undani wake kimaandishi. Ujane wake, majonzi yake, kukerwa kwake, upweke wake, lakini pia ubaba wake, uaminifu wake, furaha yake, na ujumla wa maisha yake. Kwake yeye, hakukuwa na kitu cha muhimu zaidi ya kutunza heshima ya jina lake. 

“Niliona mamia ya watu waliouza roho zao kwa vitu hivi [utajiri/mamlaka] lakini pato lao lote lilikuwa ni uharibifu wa majina yao,” anaandika kwenye ukurasa wa nne wa kitabu hicho. “Ukosefu wa jina zuri ni ukiwa mkubwa duniani.” Na kwa hakika, jina lake limeishi na kuvuma hata baada ya maisha yake.

Kwa kiwango kikubwa, Watanzania tuna utamaduni wa usiri katika jamii yetu. Ila uandishi wa Shaaban Robert una namna fulani ya uwazi, ambao unamfanya avutie. Anavyoandika na unapomsoma, anakua kama mtoto mdogo ambaye hajui kuongopa. Shaaban Robert anaeleza lililo jema juu yake kwa uwazi, na lililo baya pia. 

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili

Si hivyo tu, bali anaonesha moyo wake pale ambapo ulikuwa na furaha na huzuni. Pale penye kicheko na jeraha. Na haogopi kuufunua ubinadamu wake kwako. Uandishi ni tendo la kujifunua, kukaa uchi kwenye ukurasa. 

Ni hali hii ya kuwa mkweli inayomfanya msomaji aguswe na uandishi wako na kubaki na alama inayodumu; ahisi kwamba kuna mwanadamu mwingine aliye na hisia kama zake – furaha, hofu, hasira, nakadhalika.

Changamoto

Nilijikuta nikitoa chozi niliposoma kuhusu changamoto alizozipitia Shaaban Robert kama mwandishi. Safari hii ya uandishi ina mambo mengi. Yapo ya kufurahisha, kama pale unapoona kwamba uandishi wako umepokelewa vizuri; na yapo ya kuvunja moyo. 

Ule uthubutu wake, kutokukatishwa tamaa, kulinipa faraja kuwa changamoto zipo lakini hatuna budi kuzishinda. Kwenye sura ya ‘Upigishaji Chapa,’ Shaaban Robert anaelezea nyakati ambazo kipato kilikuwa hakitoshi, pesa ya kuchapa ilisuasua, wapiga chapa walikuwa wasumbufu, wengine hata wakawa wanampa pato dogo kuliko uhalisia wa mauzo, basi tabu tupu! 

Nikawaza, ingekuwaje leo hii kama maandishi ya Shaaban Robert yasingetufikia kwa sababu ya pesa? Kwa sababu ya changamoto za wachapaji? Ingekuwa ni huzuni ambayo tusingeijua. Nalo linahuzunisha.

SOMA ZAIDI: Zubayda Kachoka Lakini Ally Saleh Anaendelea Kupambana Zanzibar

Navutiwa kusoma na kufahamu kuwa mwandishi huyu aliandika kwa sababu alikuwa na mapenzi ya dhati kwa fani ya uandishi. Si pesa au umaarufu uliomfanya akajipinda na kuweka maneno kwenye karatasi ili yasomwe na hadhira, la hasha. Bali ni moyo wa kutaka kuwasilisha mawazo yake, moyo wa kutaka kuzungumza na sauti yake isikike.

Kama ningeweza kumhoji

Japokuwa anajifunua bila kujivunga, anajiwekea mipaka kuwa taarifa hiyo iwe ni ukweli wake. 

“Kwa kuwa muda wangu wa kufanya kazi katika idara hii sasa ni mwaka mmoja tu adabu yakataza kusema mengi kuliko niliyoona,” Shaaban Robert anaandika katika ukurasa wa 63. “Nasimulia habari ya maisha yangu na matokeo yaliyohusu maisha hayo peke yake. Sina haki ya kwenda ng’ambo ya mipaka ya mambo yasiyohusu hadithi nisimuliayo.”

Nilipokuwa nasoma, nilitamani kuwa ningekuwa hai kipindi hicho. Siyo ili niwe mke wa tatu wa Shaaban Robert, la hasha! Ila kuna mengi ambayo hakuyafunua kwa uwazi wake ambayo nilitamani kuyasoma. 

Sio kwamba alificha kitu, lakini nilitamani kupata ufafanuzi zaidi juu ya masuala mbalimbali na haswa yale ambayo yalihusu muktadha wa ulimwengu wa wakati huo. Shaaban Robert anafunua picha ya maisha yake katika muktadha wa ukoloni, ubaguzi wa rangi, Vita Kuu ya Pili ya Dunia, vitu ambavyo huvioni sana katika fasihi yetu andishi kwa mtazamo wa mtu mweusi.

Alipokuwa akiandika, alikuwa anawataja watu kwa rangi zao. Alipotumia ‘wafanyakazi wenyeji’ mara ya kwanza, sikuelewa maana yake. Wenyeji wa wapi? Mpaka baadaye aliporudia, na kusema ‘wafanyakazi wenyeji wenzangu’ (uk. 41), na kisha sehemu nyingine akaweka bayana kuwa walikuwa ni Waafrika weusi, ndipo nilipoelewa kwamba alikuwa anaelezea utambulisho wake kwa muktadha wa rangi. 

SOMA ZAIDI: Tamasha la Vitabu Zanzibar: Kitovu cha Vipaji Vipya?

Kitu ambacho pengine ni nadra kufanya hivyo kwa zama za leo. Sura ya ‘Abiria Cheo cha Pili’ ina mgogoro mkubwa sana ambao kiini chake ni ubaguzi wa rangi. Sura hii inaangazia safari yake kutoka Mpwapwa Julai 1944 kwa usafiri wa lori, ambapo kulikuwa na abiria Waafrika na Wahindi. 

Kama simulizi ya maisha yake ikitengenezwa kuwa filamu, basi sehemu hii itawapa watazamaji matumbo joto. Lakini tena, aligusia jinsi ambavyo Vita Kuu ya Dunia iliathiri maisha yao huku Afrika. Hali ya uchumi uliathirika (uk. 61), kukawa na uhaba wa baadhi ya vitu kama bati na saruji(uk. 53). 

Nikasema kumbe sasa watu wanasema, kila kitu kimesababishwa na vita vya Ukraine, sio jambo lililoanza leo. Ama kweli, kila kilichopo kimewahi kuwa.

Kama ningeweza kukaa chakulani na watu watano, walio hai au wafu, nafikiri wa kwanza angekuwa bibi yangu, Bibi Esther. Tangu nikiwa mtoto mdogo, nilihuzunika kwa kukosa kumjua mtu ambaye nimepewa jina lake lakini sifa zake haziishi midomoni mwa watu. Hiyo ni simulizi ya siku nyingine. 

Lakini wa pili, bila shaka, atakuwa Shaaban Robert. Sijui ni yule wa Maisha Yangu kijana mdogo, au wa Baada ya Miaka Hamsini ambaye ameshakula chumvi ya kutosha. Lakini najua, nitafurahia kila neno litakalotoka mdomoni mwake usiku huo. 

Wengine wangekuwa Siti Bin Saad, Bibi Titi Mohamed na mwanangu, Jasmine Mainda-Rose. Tukutane wiki ijayo ambapo nimedhamiria kudurusu kitabu kingine cha Shaaban Robert, kutoka kwenye orodha ya vitabu vyake kadhaa vilivyochapishwa na Mkuki na Nyota kama sehemu ya kusheherekea miaka 50 ya urithi wa fasihi, ambayo ni miaka 50 tangu Shaaban Robert atutoke duniani (1962-2012).

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *