The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zubayda Kachoka Lakini Ally Saleh Anaendelea Kupambana Zanzibar

Saleh, gwiji la utangazaji kutoka Zanzibar, anasema amedhamiria kuyanyoosha yote yaliyopinda kwenye jamii kupitia uandishi wake.

subscribe to our newsletter!

Kinachoonekana juu ya ukurasa wa kwanza ni kanga ya kijivu iliyochakaa, ina kiraka upande wa kushoto na imechanika upande wa kulia. 

Mvaaji yuko pekupeku na rinda la kanga hiyo limeandikwa Zubayda Kachoka, maneno ambayo ni jina la kitabu hiki cha Ally Saleh kilichozinduliwa kwenye Tamasha la Vitabu Zanzibar, Oktoba 20 mpaka 22, 2023, visiwani humo.

Saleh si mgeni masikioni mwa wengi Tanzania, akifahamika miaka mingi kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari. Saleh alikuwa mwandishi wa redio ya BBC Idhaa ya Kiswahili kwa muda mrefu kabla ya kustaafu mwaka 2013 na kuingia kwenye siasa. 

Alikuwa Mbunge wa Jimbo la Malindi kisiwani Unguja kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kati ya mwaka 2015 na 2020. Kwa sasa, Saleh ni mwanachama wa chama cha upinzani, ACT-Wazalendo ambacho pia ni mshirika wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inayotawala Zanzibar.

Jina la Saleh, unaweza kusema, ni kisawe cha uanaharakati. Ukilisikia, unapata picha ya mtetezi wa maslahi ya wanyonge, sauti ipazwayo kwa ajili ya haki za binadamu na maendeleo ya jamii kwa ujumla. 

SOMA ZAIDI: Tamasha la Vitabu Zanzibar: Kitovu cha Vipaji Vipya?

Kwa hiyo, siyo ajabu kuwa katika mkusanyiko huu wa hadithi 13, Saleh anaangazia masuala mbalimbali yanayowachosha watu kwenye jamii. 

Katika kulithibitisha hili, mwandishi anasema kwenye utangulizi wa kitabu kuwa, “Mkusanyiko huu [wa hadithi] ni wa madai na kupaza sauti. Iwe ni haki, iwe ni kutimizwa wajibu, iwe ni kupokwa urithi, utamaduni na utambulisho.”

Saleh hakuanza leo kuandika vitabu. Mbali na kuwa mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii kwenye vyombo vya habari, Saleh ameandika vitabu mbalimbali vikiwemo La Kuvunda: Na Hadithi Nyingine (2016) na Jumba Maro (2005) kwa upande wa hadithi. 

Saleh pia ameandika vitabu vya mashairi na wasifu, ikiwemo Maisha ya Bi Kidude na Maisha ya Haji Gora.

Hadithi fupi zilizomo kwenye Zubayda Kachoka ni pamoja na Weleo Jini, Bwan’Jogoo, Mazonge, Babu, Siku Moja, Chezea Ndevu na Zaituni. Zingine ni Zubayda Kachoka, 18-22, Imamu wa Ging’ingi, Kiunga-uzi, Bibi wa Baghani, na Siri ya Mtungi

Vitendo vya dhuluma

Kwenye Weleo Jini, Bwan’Shaaban amechoshwa na vitendo vya dhuluma alivyofanyiwa na kijana Sumaili ambaye watu wanamhisi kuwa ni jini maana hajulikani alipotoka wala anapokwenda. 

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru wa Mwanafasihi, Fasihi Haiwezi Kuwa Chombo cha Ukombozi wa Umma

Na siku Bwan’Shaaban anapojenga urafiki na mtu huyu anayetiliwa mashaka, habari zilimfikia “saatauli-khabar,” au wengine wanamwita Bwa’Khalfan muuza kahawa, alihoji kuwa, “Mnataka kupindua Serikali wenzangu?”

Saleh analeta matukio yanayoshangaza na kutafakarisha kidogo. Kwenye Mazonge, Kheir amechoshwa na ahadi za uongo alizopewa na Mazonge baada ya “kumpa” mchumba wake aitwaye Bi. Mwanakwetu, kwa makubaliano ili amuoe. 

Mazonge, ambaye anatajwa kuwa ‘mtu wa Kusini’ ana sifa ya kutokuwa mwaminifu kama ‘watu wa Kusini’ walivyo, kwani pale ambapo Kheir alipohitaji Mazonge atunze ahadi yake, hafanyi hivyo. 

Mazengo anamwambia, “Mimi nimeweza kukwambia kwa kuwa najua wewe muungwana. Siamini mtu yeyote duniani anaweza kukubali, ila wewe unaweza kukubali. Sisemi nitakulipa, lakini nitathamini uungwana wako kadri ya maisha yangu, na utaona siku yoyote ile itapokuwa wajibu wangu kwako.” 

Unaweza kujiuliza, huku Kusini ni wapi, Pemba? Usipotulia vizuri unaweza kukurupuka. Kwani hadithi hizi ni kama mafumbo, ni sitiari zilizojaa mafunzo mengi ndani yake. Kwa juujuu yaonekana kama kinaongelewa kitu kimoja, lakini ukisoma kwa makini, unaweza kupata maana nyingine.

Ubaguzi na rushwa

Hadithi inayobeba jina la kitabu imemulika mazungumzo ya Zubayda na mama yake, Bi. Sauda. Zubayda mwenyewe ni msichana wa miaka 25, mwenye watoto wawili lakini, kama anavyosema mwenyewe, “Utasema nimezaa peke yangu.” 

SOMA ZAIDI: Furaha, Matumaini Vyatawala Tukio la Watunzi, Wapenzi wa Kazi za Fasihi Dar

Mazungumzo yao yanaakisi masuala mbalimbali ya ubaguzi, rushwa, ukandamizaji na matumizi mabaya ya madaraka. 

Mohammed Ghassani, mwandishi na mchambuzi, anasema katika dibaji ya kitabu hiki kuwa, “Uteuzi wa jina Zubayda Kachoka, licha ya kuwa jina la moja ya hadithi zilizomo, ni ishara ya watu waliochoka na mfumo uliooza na unaotoa harufu kali ya vundo inayomkirihisha kila mmoja. 

“Zubayda, akiwa mwanamke na kijana, ni alama ya walio wengi kwenye rika na jinsia yake, ambao ni watendwa wa mfumo huu uliooza, ambao wamechoka nao na ambao wanapambana nao kuuondosha na vundo lake.”

Saleh anafafanua zaidi kuwa aliandika kitabu hiki kwa sababu kuna mambo mengi kwenye jamii ambayo hayasemwi. 

“Nilitaka kuonesha kwamba kuna mambo mengi hatuyasemi,” mwandishi huyo aliniambia hivi karibuni. “Mpaka mtu awe kachoka ndiyo anasema. Kwa mfano, mtu inawezekana anapigwa na mumewe kila siku. Lakini akifika kuchoka, atasema: Jamani, mi napigwa. 

SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria

“Mtu ambaye amechoka na wanasiasa. Iko siku atasema: Jamani, tunawapeni kura kila siku. Nilitaka kuwaambia wanajamii kwamba yapo haya maeneo ambayo watu wamechoka lakini hatuyasemi mpaka tufike hapo.”

Mazungumzo kuliko matendo

Kwa upande mwingine, pengine ndipo udhaifu wa mkusanyiko huu ulipojificha. Kitabu hiki kimejaa mazungumzo zaidi kuliko matendo. 

Wahusika wengi wanakaa kitako na kuongea, kila mmoja akitaka kuyatoa yale yaliyoko moyoni mwake. Hakika, kuongea ndiko kupona!

Kwa mtazamo wa Saleh, hali ya uchofu imeshapitiliza Zanzibar, hususan kuhusu uchaguzi wa viongozi wa kisiasa. Katika hadithi ya Bwa’ Jogoo, mhusika mkuu Bwa’ Jogoo anahamia kwenye mtaa akiwa na jogoo lake.

Anajidai mbabe kwa kuhakikisha kuwa jogoo lake ndilo linashinda kila kunapokuwa na shindano, ambalo yeye mwenyewe ndiye aliyelitaka. Hii ni picha ya kinachoendelea Zanzibar, anasema Saleh. 

“Bwa’ Jogoo alikuwa mtu ambaye alitaka jogoo wake kila siku ashinde,” Saleh aliniambia nilipomdadisi kuhusu hadithi hiyo. “Akiona jogoo mwingine kachipukia tu, anataka apigane nayee. 

SOMA ZAIDI: Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?

“Hata kama huyo jogoo hayuko tayari kupigana, anasema nakupa wiki mbili uje tupigane. Lakini shindano likiisha, akishinda, anakuja anamuua jogoo wako, au anamchoma, anafanya vyovyote vile. 

“Kwa hiyo, kama alikuwa hataki, anataka apigane kwa kushinda tu, lakini siyo kwa kushindwa. Watu walipochoka, wakajikusanya.”

Licha ya kuwasanifu wahusika wake wote kwenye kitabu chake kama watu waliochoka, Saleh alinihakikishia kwamba yeye mwenyewe bado hajachoka, akisema anaendelea na harakati zake za kujenga jamii iliyobora zaidi ya sasa.

“Mimi sijachoka na ndiyo maana naendelea kila mara [na mapambano],” alinihakikishia Saleh. “Mambo mengi yamenifika, lakini silalamiki mimi. Mimi nayafanyia kazi. Siyo kama watu wengine. Kitu kama hakifai, nakifanyia kazi ili kuwaambia watu life goes on.”

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *