The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Kufikirika’ ya Shaaban Robert na Uhalisia Usiyopitwa na Wakati

Chapa yake ya saba ikichapishwa mwaka 2018 na Mkuki na Nyota, Kufikirika ni moja kati ya kazi za fasihi zilizompatia heshima kubwa mwandishi wake, Shaaban Robert, na kuendelea kuakisi jamii halisi ya Kitanzania.

subscribe to our newsletter!

Kufikirika ni nchi ya ajabu. Japokuwa Shaaban Robert, mwandishi wa riwaya hiyo mashuhuri, hasemi waziwazi, jamii hii inaonekana kama mahali ambapo ukoloni haujawahi kufika, na lugha ngeni vilevile haijulikani. 

Jiografia ya Kufikirika inatafakarisha. Kaskazini imepakana na nchi ya Anasa. Kusini ipo nchi ya Majaribu. Mashariki kuna Bahari ya Ufaulu na Magharibi safu ya milima ya Jitihada. 

Inasemwa kuwa ramani ya nchi hiyo ni adimu kwani nchi hiyo haiandikiki ila hufikika kwa mawazo tu. Sasa, utapanda basi gani au ndege gani kufika huko, mimi sijui. Kufikirika ni mahali ambapo ukiangalia mambo kwa harakaharaka utadhani kuwa raia wa nchi hiyo wanaongea lugha moja tu – uzalendo. 

Hata hivyo, ukianza kuchunguza kwa undani utagundua kuwa vinavyoonekana kwa nje kama huo uzalendo, vimefunika maslahi binafsi, tamaa, matumizi mabaya ya madaraka, na kadhalika. Utagundua kwamba kuna mambo yanavyopaswa kuwa, na kuna jinsi yalivyo. Shida inaanzia hapo.

Uzalendo

Neno hili ‘uzalendo’ halijatajwa waziwazi. Lakini simulizi inaonesha jinsi ambavyo ni jambo la muhimu sana kwa Wafikirika. Lakini uzalendo ni nini? Kusema tu – ndiyo mzee? Kuwa tayari kuwadhuru watu ili maslahi ya watu wachache yaweze kutimizwa? Kutumia vibaya rasilimali za umma, uongozi usiojali haki za raia wake, na kuwalaani wote wasiokubali kurubuniwa kwa ajili ya wachache ‘wenye nguvu’? Mwandishi anatupa mengi ya kutafakari.

SOMA ZAIDI: Ni Wakati Tuitendee Haki Kumbukumbu ya Maisha ya Siti binti Saad

Mfalme wa Kufikirika anachorwa kama mtu aliye mzalendo nambari moja. Tunapokutana naye kwa mara ya kwanza, tunamuona kama mtu mwenye moyo mweupe, anayewapenda wananchi wote wa nchi yake na kuwajali kwa usawa, asiyethubutu hata kuwaza kuwa uvunjifu wa sheria ni jambo linaloweza kutokea Kufikirika; ni mnyoofu kwa kweli.

Hata hivyo, yeye ndiye wa kwanza ambaye uzalendo wake unapimwa. Mkasa mzima umebebwa na kitu kimoja – ugumba wa Mfalme na utasa wa Malkia. Sio tu ugumba wao, lakini haswa kuelemewa na shauku ya Mfalme ya kupata mtoto. 

Pamoja na kwamba anatambulishwa kwetu kama kiongozi asiye na hila, kila mwanadamu ana kivuli. Na cha kwake kinaanza kuonekana vema pale anapolivalia njuga swala hili.

Hitaji lake lamfanya ajione hana thamani. Anajivua nguo mbele ya wananchi wake, na kuwaambia kuwa japokuwa jambo hili laweza kuonekana kama jambo la faragha, maji yamemfika shingoni. 

“Maskini mwenye mtoto namwona kuwa ni bora kuliko mimi na pengine moyo wangu huona wivu juu yake.” (uk. 3) Na tena anasema, “Nimefanya kazi nyingi njema za kusaidia maendeleo ya nchi ya Kufikirika, lakini hata hivyo naona sijafanya kazi bora kwa sababu sijapata mtoto bado.”

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunahitaji Kusoma Vitabu Vingi Zaidi vya Kiswahili?

Mchele unamwagwa penye kuku wengi. Jambo la faragha linakuwa la wananchi wote. Na kwa sehemu, hoja ya Mfalme ni kuwa huyu si mtoto tu wa kawaida bali ni mrithi wa ufalme wa Kufikirika. Hivyo basi, linakuwa sasa ni jambo la kitaifa au tuseme linalohusu mustakabali mzima wa ufalme.

Mfalme anawaita waganga wa kila aina waweze kumtatulia tatizo lake – waganga wa mizizi, makafara, mazinguo, hirizi, mashetani na hata wanaotabiri. Baada ya kupitia tabu nyingi za kiganga, hatimaye njia inapatikana. 

Lakini je, Mfalme atayaweza masharti ? Inahitajika kafara ya damu ya wanadamu wawili – Mwerevu na Mjinga. Hapo ndipo ulipo mtego.

Ukombozi wa kifikra

Ili Mfalme aweze kutekeleza masharti aliyopewa, ilimpasa kuvunja sheria. Kwani sheria za nchi zilipinga kafara hii. 

Lakini ili asivunje sheria, ilimpasa kubadilisha sheria; na ili sheria ibadilishwe, Baraza la kushauri Serikali lilipaswa kupitisha mabadiliko hayo ya sheria kuwa damu ya mtu ni halali kumwagwa kafara kama imebidi mtu au watu kuchinjwa kwa sababu ya kuokoa maisha ya Mfalme, Malkia, mtoto au jamaa wa nyumba ya ufalme.

SOMA ZAIDI: Laiti Kama Ningepata Nafasi ya Kumhoji Shaaban Robert

Hapa ikawa dhahiri kwamba kwenye jamii hiyo kuna tabaka la wanaostahili kuishi, na wanaostahili kufa ili wengine waishi; tena kuna tabaka la wenye haki ya uhai na wengine ambao walio na haki za uhai wanapoamua kwamba wasio na haki hiyo wanapaswa kufa, basi huwa hivyo; kuna tabaka la watawala na wale walio watawaliwa.

Tunawaona wakuu wa Baraza la kushauri Serikali kama watu wenye nguvu sana ndani ya nchi ya Kufikirika. Baraza hilo lina washauri 30, wakiwemo Mkuu wa Baraza ambaye ni Waziri Mkuu wa Serikali, mawaziri sita, wasimamizi wanne, makadhi wanne na katibu mmoja kwa upande wa Serikali. 

Viongozi wa dini wanne, wanasheria watatu, wanachuoni watatu, mahatibu watatu, na mkulima mmoja upande wa raia.

Waziri Mkuu wa Kufikirika anasema waziwazi kuwa “kafara ya damu ya mtu ni jambo dogo, si kubwa la kumfadhaisha Mfalme.” (uk 32). Tena, anaongeza kuwa wao kama viongozi wamepewa “heshima kubwa ambayo haijawahi kutokea” (uk. 34) na “fahari ambayo nchi yoyote ulimwenguni bado kuwapa washauri wake.” (uk. 35)

Kuna namna fulani ya kujipendekeza inayojitokeza miongoni mwa watu wanapotaka kujikomba kwa mwenye nguvu. Zama hizi tunaita hali hii uchawa. Chawa yuko radhi ajivunjie heshima, ila atekeleze lile analoona litamfurahisha bwana mkubwa.

SOMA ZAIDI: Zubayda Kachoka Lakini Ally Saleh Anaendelea Kupambana Zanzibar

Wale ambao hawakukubaliana na Waziri Mkuu wa Kufikirika, kibaraka wa Mfalme, walikaripiwa kuwa “walikuwa ni wajinga wa historia na kuwa hawakustahili hata kidogo heshima ya uanachuoni wala ya uanachama wa baraza la Serikali ya Kufikirika.” (uk. 36)

Lakini yupo mtu mmoja aliyejulikana kama Utubusara Ujingahasara, anaonekana akijibadilishabadilisha. Kila alipojibadilisha, alihitaji kutumia akili yake vizuri ili aweze kujikwamua kutoka katika hali iliyokuwa ngumu kwa wakati huo. 

Kwa sehemu kubwa, Shaaban Robert anasema kwamba ni mabadiliko ya fikra yatakayoweza kumwokoa mwanadamu.

Thamani ya mwanamke

Japokuwa haangazii suala hili kwa undani, mwandishi anagusia thamani ya mwanamke. Kuna mahali katika simulizi, maisha yaliwakutanisha bwana mmoja Mwerevu na mwengine Mjinga. 

Iliaminika kwamba, Mwerevu alikuwa mtu mjanja anayeweza kushinda mambo kwa hoja na Mjinga alikuwa hana upeo mkubwa wa mambo. Lakini walipokutana na kuketi pamoja, ilikuwa kinyume chake.

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili

Katika mabishano, Mwerevu, ambaye alikuwa ni mjinga, akasema, “Mimi mwerevu sioni njia ya kujiokoa. Huwaje, wewe mvaa koja la ushanga shingoni kama mwanamke kupata njia! Huna sifa zaidi ya ujinga.” 

Jibu la Mjinga, ambaye ni mwerevu, anamjibu kwa upole kwamba, “Hapana haja ya kudharau mwanamke. Wanawake ni malaika… Mwanamume kumgeuza mwanamke ni ubishi usiosaidia kitu katika msiba wetu…”

Kwa mantiki hiyo, kuwa mwanamke si tusi; ni heshima.

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *