The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Tunahitaji Kusoma Vitabu Vingi Zaidi vya Kiswahili?

Hatuwezi kukuza fasihi yetu ikiwa hatusomi vitabu vyetu.

subscribe to our newsletter!

Mwishoni mwa mwezi Januari, nilialikwa na kikundi kidogo cha wasomaji vitabu ambao walikuwa wamesoma kitabu changu cha mashairi kinachoitwa Jinsi ya Kurudi Nyumbani, ambacho walikisoma kwa pamoja mwishoni mwa mwaka 2023. Mezani walikuwa wameketi vijana, wasomi, wengi wao wakiwa na umri kati ya miaka 25 na 40 mwanzoni. 

Wamejiwekea utaratibu wa kuzungumza kwenye kundi sogozi la WhatsApp na kila mwezi wao huchagua kitabu kimoja cha kusoma na kukijadili. Kikao kilifanyika kwenye mgahawa mmoja maarufu eneo la Masaki, ambao ulikuwa umejaa harufu ya kahawa na kupendezeshwa na vitabu ambavyo watu huweza kuazima – kitu ambacho ni cha kipekee jijini Dar es Salaam.

Mjadala mkubwa ulijikita kwenye shairi la Unaolewa ini? Shairi hilo linasema: 

Wameshaniuliza sana, unaolewa lini?
Mimi ninahoji, inawahusu nini?
Mume angekuwa ananunuliwa dukani mbona ingekuwa raha
Ningekuwa nimeshampata nami nimepatikana
Tumepatana na ndoa tumefungana.

Mwanamume mrefu kidogo
Maji ya kunde hivi
Mwenye pesa kidogo
Mcha Mungu hivi.

Mmeshaniuliza sana, unaolewa lini?
Miaka thelathini inakaribia
Haya sasa, thelathini na tano na sina bwana
Utadhani nisipoolewa siwezi kupumua, eti?
Na mwenye ndoa mwamuuliza, mbona hazai?
Anayezaa mwamuuliza, mbona majike
Na mwenye majike mwamuuliza, nguo gani hizo kuwavalisha?
Mtuache!

Mtazamo wa mwanamke

Kwa sehemu, niliandika kitabu hiki kwa sababu nilitaka kusoma kitu ambacho sijakiona sokoni. Kwa sehemu, nilitaka kunakili mawazo na fikra zinazoakisi jinsi wanawake wanavyopitia hali mbalimbali za maisha katika muktadha wa kuwa mwanamke mweusi, Mwafrika, Mtanzania, mama na kadhalika, ambazo sijaona katika vitabu vya Kiswahili. 

SOMA ZAIDI: Laiti Kama Ningepata Nafasi ya Kumhoji Shaaban Robert

Je, kitabu hiki kinaakisi mtazamo wa kila mwanamke? Hapana. Lakini nilitaka mtazamo huu pia unakiliwe kimaandishi na kuwa chanzo cha mijadala. Wapo waliokisifia, na wapo waliokibeza. Hata hivyo, katika usiku huu wa kukijadili, niliona kuwa nilikuwa nimefanikiwa, kwa sehemu.

“Wewe ni jasiri. Asante kwa kuandika,” aliniambia Billy Luomba, 25, anayesomea shahada ya kwanza ya udaktari Hubert Kairuki Memorial University na mmoja wa wasomaji siku hiyo ambaye alikuwa mwanamume pekee mezani. Kwa kiwango fulani, mawazo ya wengine yalifanana na ya Billy. 

Mwanakundi mmoja ambaye ni mwanasheria alisema, yeye hakuwahi kudhani kwamba anaweza kusoma mashairi tena kwa Kiswahili. Lakini, kitabu changu kilimfanya aone kwamba kumbe anaweza, na siyo vigumu kama alivyowaza awali.

Japokuwa klabu hii ya vitabu imekuwa hai tangu mwaka 2016, kitabu changu ni kitabu cha kwanza kilichoandikwa kwa lugha ya Kiswahili walichosoma kama kundi. Entesh Melaisho, 32, mmoja wa waanzilishi wa klabu hiyo, anafafanua kwamba huwa mtu mmoja anachagua kitabu cha kusoma kwa mwezi husika kisha anakuwa na jukumu la kusimamia taratibu za kukutana na mjadala kwa ujumla. 

Kwa hiyo, watu huchagua vitabu kutokana na aina ya vitabu wanavyopenda kusoma binafsi.

“Mimi binafsi nimeathiriwa na msisitizo niliopata kutoka kwa walimu wa kuzungumza na kusoma kwa Kiingereza tangu shuleni,” alisema Entesh. “Tangu ukiwa shule unahimizwa kuboresha Kingereza. Kwa hiyo, unasoma vitabu vya Kingereza zaidi. Japokuwa ninasoma vya Kiswahili, siyo sana. Sivifahamu vingi.”

SOMA ZAIDI: ‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania?

“Hivi karibuni matukio kama Kalaam Salamu inayoandaliwa na kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota na kufanyika mara moja kwa mwezi, yamenisaidia kuvijua zaidi vitabu vya Kiswahili na waandishi pia,” aliongeza Entesh. “Pengine wachapishaji na wauzaji wana kazi kubwa zaidi ya kutangaza vitabu vya Kiswahili ili tuvijue na kuvisoma.”

Entesh aliongeza kuwa, vitabu vya Kiingereza vinapatikana kwa urahisi mtandaoni pia, au katika mfumo wa sauti, jambo ambalo linamfanya yeye kama mlaji kuvipata kwa urahisi. Hali hii siyo ya kipekee kwa kundi hili. Yapo makundi mengine yaliyoanzishwa miaka ya hivi karibuni yenye majina – kama Hekima Book Club, Umoja Book Club, Taswira, na kadhalika– au yasiyo na majina. 

Kusoma Kiswahili

Nilipata bahati ya kusomwa na Hekima Book Club (Dar) mwaka 2022 na tawi lao jipya la mjini Arusha limepanga kusoma kazi yangu mwezi Agosti mwaka huu. Jambo hili linanifurahisha sana kama mdau wa vitabu na kama mwandishi. 

Hii inatokana na ukweli kwamba ukisomwa katika kundi, kazi inazidi kufahamika, lakini pia unapata kipato hata kama ni kidogo, kama mwandishi. Lakini ukiangalia orodha ya vitabu vilivyosomwa na makundi haya katika kipindi cha nyuma, au wanavyopanga kusoma, utagundua kwamba vitabu vya Kiswahili havijapewa kipaumbele.

Marc Ngotonie, 31, anayeendesha podcast ya More than 30 With Marc inayoangazia masuala ya vijana na mchango wao katika jamii kupitia sanaa, anasema tofauti za kimatabaka katika jamii zinachangia hali hii. Kuna namna fulani msomi akisoma kitabu cha Kiingereza anaonekana ‘mjanja,’ ana fikra pana za dunia, lakini akishika kitabu cha hadithi cha Kiswahili anaonekana ‘mswahili.’ 

“Kama nikiwa na marafiki kumi na wote wanasoma vitabu vya Kingereza, nitataka nikubalike,” anasema Marc. “Na mimi nitasoma wanavyosoma wao.” Marc anaongeza kuwa kazi kubwa inatakiwa kufanyika na waandishi wenyewe, wachapishaji na wadau wengine wa vitabu vya Kiswahili katika kuvitangaza na kufanya usomaji wa vitabu vya Kiswahili kuwa kitu ambacho watu wanajivunia.

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili

Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wasomaji wanaofungua kurasa zinazohusu vitabu katika mitandao ya kijamii, na wengine wanaweka orodha za vitabu walivyosoma mwishoni mwa mwaka. Viongozi wa kisiasa kama Zitto Kabwe wamekuwa maarufu sana kwa miaka mingi katika hili. 

Kwengine ulimwenguni, orodha ya vitabu ya aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama husubiriwa kwa hamu, huku klabu za vitabu zinazoongozwa na watu mashuhuri kama ile ya Oprah Winfrey zikiwa na mashabiki sana. Kuwa kwenye orodha hiyo kwa mwandishi kuna maana kubwa. 

Kwanza, ni jambo la kutia moyo kuwa mtu maarufu kama huyo amesoma kazi yao; lakini pia, wasomaji wengine hufuatilia ili waweze kununua na kusoma. Kwa bahati mbaya, wasomaji wengi wa hapa nyumbani hawazingatii uzito wa orodha zao. 

Pengine, hawadhani kuwa watu wanaweza kutamani kusoma wanachosoma; au labda, hawadhani kwamba kuna umuhimu wowote wa kusoma vitabu vya Watanzania zaidi na kuvitangaza kupitia orodha zao.

Ni kweli, kukiwa na kampeni kubwa ya kutangaza wasifu wa mtu mashuhuri kama Rais mstaafu au kiongozi fulani, basi watu wengi watataka kusoma na kuonekana wamekisoma kitabu hicho. Watu wataulizana mtaani: vipi, wewe umesoma? Na ili uonekane uko makini, itabidi usome. 

SOMA ZAIDI: Zubayda Kachoka Lakini Ally Saleh Anaendelea Kupambana Zanzibar

Ni jambo zuri na lapaswa kuendelea lakini vipo vitabu vingi sana vya Watanzania wa kawaida, na vya simulizi za aina nyingine. Je, tuishie kusoma wasifu na tawasifu za wanasiasa tu? Hatuwezi kukuza fasihi yetu kwa jinsi hii. Tukiwa katika vikundi au klabu, tunayo nafasi ya kuambukizana hamu ya kusoma vitabu vya aina tofauti na ile tuliyozoea.

Ngumu kubadilika

Christian Bwaya, 42, Mhadhiri wa Saikolojia na Unasihi, Chuo Kikuu cha Dodoma anakiri kuwa kuwafanya watu wabadilike tabia si kazi ndogo. Yeye alianzisha klabu ya usomaji mwaka 2015. Klabu hiyo imejaa wasomi. Japokuwa amejaribu kushauri vitabu vya aina nyingine visomwe, vikiwemo vya Kiswahili, jitihada zake hazijafua dafu. 

“Inawezekana umasikini unachangia aina ya vitabu tunavyosoma,” Bwaya anasema. “Hatuoni maana ya kusoma kama burudani. Watu wanapenda vitabu vyenye majibu ya matatizo yao; vitabu vyenye ujumbe wa wazi unaoleta suluhisho na wenye uhalisia wa maisha wanayopitia.”

“Kwa bahati mbaya, sio Watanzania wengi wanaoandika vitabu vya aina hiyo na wale wanaofanya hivyo, huleta fikra ambazo zimeanzia kwa mtu mwengine aliyeandika kwa Kingereza,” anaongeza Bwaya. “Ukimwambia mtu, tusome mashairi, anakwambia yatanisaidia nini?”

Wanasema, Rumi haikujengwa kwa siku moja. Tunahitaji pa kuanzia. Miaka ya nyuma kulikuwa na vuguvugu lililohamasisha usomaji lililovuma sana wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19, Mjue Mtunzi. Tukio moja walilofanya liliwavutia wasomaji zaidi ya 500 ambao walikutana na waandishi wa vitabu na kununua vitabu vyao pia. 

Pengine, ni muda kwa makundi mbalimbali kama hilo kuamka, kupanga mikakati ya namna ya kuwafikia hadhira kwa upya. Pengine ni muda wa kutathmini jinsi ya kutumia mitandao ya kijamii, orodha za mwaka za watu maarufu, klabu maarufu za vitabu, kutangaza kazi zetu kibunifu. 

SOMA ZAIDI: Tamasha la Vitabu Zanzibar: Kitovu cha Vipaji Vipya?

Lakini pia, jambo hili linahitaji wasomaji wenye malengo binafsi na nia ya kukuza fasihi ya Kiswahili. Wale wenye kurasa za kusoma vitabu huko Instagram na kadhalika, wawe na malengo ya kuongeza idadi ya vitabu vya Kiswahili wanavyosoma kila mwaka. 

Kama ilikuwa sifuri, iongezeke iwe moja; kama ilikuwa tano iongezeke iwe kumi. Wito huu ni kwa klabu za kusoma vitabu vilevile. Hatuwezi kukuza fasihi yetu ikiwa hatusomi vitabu vyetu. Ni wakati wa kubadilika!

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Hii imenifurahisha na kunitia moyo, umeandika vizuri sana, nimetamani niandike kwa kingereza maana ndo lugha iliyokuja kichwani, lakini ntabaki lugha mama. Asante kwa uchambuzi huu, na hongera kwa kazi yako nzuri ya mashairi kwenye kitabu chako cha Jinsi ya Kurudi Nyumbani. Kazi yako ina akisi maisha ya wanawake wengi sana Tanzania na Afrika kwa ujumla, kiasi gani mwanamke anayo mengi moyoni lakini hawezi kusema, umefungua njia. Ni kweli lazima tuanzie mahala, umeongeza jiwe kwenye msingi uliojengwa na waasisi wa lugha. I am super proud of you sister. keep up.

  2. Asante sana kwa makala hii. Mimi ni mwandishi nimeandika pamoja na wenzangu kitabu kiitwaacho KARAGWE, HISTORIA, MILA na DESTURI. Kabla ya kuandika watu walikuwa wanauliza sana kitabu cha aina hiyo. Baada ya kitabu kutoka watu hawapnekani na walionunua bado hawajamaliza kusoma japo wanasema kitabu kinavutia ila muda wa kusoma kitabu cha page 300 wanaona haupatikani. Ila nimepata changamoto nyingine kwamba wanatamani kingekuwa cha kiingereza. Kwa bado tuna kazi ya kufanya ili kuhuisha usomaji wa vitabu!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *