The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fahamu Dalili za Ugonjwa wa Presha ya Macho Kwa Watoto na Watu Wazima

Ugonjwa huu huwapata watu wazima na watoto, japo zaidi ni kwa watu wazima wenye umri kuanzia miaka 35, wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, pamoja na wale wenye historia ya ugonjwa kwenye familia zao.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Imebainika kuwa asilimia 10 ya wagonjwa wote hapa nchini wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na matatizo ya macho, hugundulika kuwa na ugonjwa wa shinikizo la macho au presha ya macho (Glaucoma).

Haya yameelezwa na daktari bingwa wa magonjwa ya macho wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Sarah Ludovick wakati akiongea na The Chanzo katika Maadhimisho ya Wiki ya Shinikizo la Macho Duniani yaliyofanyika Machi 11 hadi 16, 2024.

Ugonjwa huu unapompata mtu kwenye macho yake kunakuwa na hali ya kuharibika kwa neva ya kuona inayounganisha jicho na ubongo. Hii husababishwa na presha kubwa ndani ya jicho.

“Unaweza kusababishwa na mkandamizo wa shinikizo la maji maji ndani ya jicho.” Anasema Dkt. Sarah  “Hivyo kusababisha kupotea kwa uoni taratibu taratibu na mara nyingi huo uoni unaanzia kupotea  pembeni kuelekea katikati.”

Nchini Tanzania inakadariwa kuwa na watu milioni 1.86 wenye matatizo ya uoni kwa kiwango cha kati na juu. Huku watu takribani 620,000 wanatajwa kuwa na ulamavu wa macho.

Ugonjwa wa presha ya macho huwapata watu wazima na watoto, japo zaidi ni kwa watu wazima wenye umri kuanzia miaka 35,  wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, pamoja na wale wenye historia ya ugonjwa kwenye familia zao.

SOMA ZAIDI: Jitihada Zaidi Zinahitajika Kuwakinga Watanzania Dhidi ya Magonjwa Yasiyoambukiza

Chanzo kingine kinachotajwa kupelekea ugonjwa huu ni pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya dawa za macho kama vile za matone yanayoangushiwa kwenye macho.

“Mgonjwa anapoumwa tatizo lolote la macho anakwenda kwenye maduka ya dawa bila kupata ushauri kutoka kwa daktari wa macho.” Anasema Dkt Sarah “Hivyo dawa hizi mara nyingi huwa na viambata ambavyo vinaweza kusababisha shinikizo la macho zikitumika vibaya.” 

Dalili za shinikizo la macho kwa watoto na watu wazima

Kwa hatua za awali kwa watu wazima ugonjwa huu huwa hauoneshi dalili zozote lakini kadiri siku zitakavyozidi kwenda, mtu anaweza kupata shida ya uoni taratibu.

SOMA ZAIDI: Fanya Hivi Mtoto Wako Akipata Tumbo la Chango

“Na mara nyingi uoni huanza kupotea kwa pembeni halafu unafuatia uoni wa katikati,” alisema Dkt. Sarah. “ Tatizo linavyozidi kuwa kubwa kioo chake cha jicho anaanza kuona ukungu. Pia anapata maumivu ya kichwa sana. Na katika mwanga mkali anakuwa anaona rangi ya upinde.” 

Kwa upande wa watoto wadogo dalili hutokea katika wiki ya kwanza ya kujifungua. Mtoto hushindwa kuhimili kuangalia mwanga, hivyo muda mwingi huwa amefunga macho. 

“Mzazi aonapo dalili hii baada ya wiki ya kwanza ya kujifungua anatakiwa amuwaishe mtoto hospitali. Pia anakuwa na tabia ya kutoa machozi mengi kwenye macho wakati mtoto huyo anakuwa halii.”

SOMA ZAIDI: Hii Ndiyo Njia Bora Ya Kukabiliana Na Magonjwa Yasiyombukiza

Inaelezwa kuwa tatizo hilo litakavyozidi kuendelea kwa mtoto, kioo cha jicho lake huanza kubadilika rangi na kuwa cheupe. Tatizo hili lisipotibiwa mapema mtoto huweza kupoteza uoni kabisa.

“Ni vizuri kuwahi matibabu mapema kabla ya dalili kutokea kwa kufanya uchunguzi mapema kwa sababu shinikizo la macho ni ugonjwa wa kudumu. Hivyo basi matibabu yake yanatakiwa kuwa endelevu.”

Tiba ya shinikizo la macho

Ugonjwa huu una tiba. Dkt. Sarah alibainisha kuwa tiba zake ziko kwa hatua kutokana na daktari atakavyokuwa amemfanyia uchunguzi mgonjwa.

“Tiba hizi zinapatikana kuanzia ngazi ya hospitali za rufaa ya mkoa, hospitali za kanda na hospitali za taifa. Matibabu haya ni dawa za matone ambapo yanakuwa ni endelevu au upasuaji kulingana na vile daktrai ataona” alibainisha Dkt. Sarah.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

  1. Mjomgwa wa presha ya macho ataitajika kutumia dawa kwa muda gani hadi apone? Mimi nimeanza matibabu juma hili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts