The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hatutegemei Shirika Kubwa la Habari Kama ZBC Lifanye Makosa ya Kizembe ya Lugha

ZBC, ambalo ungedhani lingekuwa na uwezo na utashi wa kuwa na mhariri mahususi wa lugha, haliwezi kutegemewa kufanya makosa ya lugha yatokanayo na uzembe na kukosekana kwa umakini.

subscribe to our newsletter!

Lugha inapotumika kwa matlaba ya umma, au kundi kubwa la watu, hupaswa kutumika kwa usahihi wa usanifu na ufasha wake. Kuibananga lugha katika tasnia ya habari hudhihirisha upeo na weledi hafifu wa wanahabari na hivyo kuchangia katika kuifundisha lugha kinyume na usanifu wake, hasa kwa wageni wa lugha hiyo.

Kwa mfano, taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa Instagram wa gazeti la Nipashe, Machi 22, 2024, ina kichwa cha habari kinachosomeka hivi: ‘Kombi’ mpya wanafunzi wa kidato V & VI zagawa wadau.

Kuna makosa mengi ya kiusanifu na kiufasaha kwenye kichwa cha habari hiki. Kwanza tunaweza kujiuliza, katika Kiswahili kuna neno kombi? Mwandishi hapa amechukua neno la Kiingereza, combination, na kulifupisha na kulifanya ni neno la Kiswahili. 

La kusikitisha zaidi, hata kwenye Kiingereza chenyewe, hakuna ufupisho wa neno hilo kwa namna hiyo. Neno sahihi hapa ni tahasusi.

Kosa jengine ni kuacha neno cha linalosimama kutengeneza kivumishi cha a-unganifu cha nomino kidato. Hivyo kwa maneno, kauli yake inasomeka kidato V & VI badala ya kidato cha tano na sita.

SOMA ZAIDI: ZBC, HabariLeo Waongeze Umakini Matumizi ya Kiswahili Fasaha, Sanifu

Vilevile, kuna kosa la kisarufi la kuacha kiambishi wa- kinachosimamia urejeshi wa mtendwa katika neno zagawa baada ya kiambishi za- ambacho hapa kinasimamia upatanishi wa kisarufi wa ngeli ya I – ZI ya nomino tahasusi ambayo Nipashe wameiita kombi, na wakati huohuo kinasimamia njeo ya wakati wa mazoea kwa kudondoshwa kwa kiambishi na- ambacho kingelifanya kazi ya njeo ya wakati uliopo. 

Neno hili lilipaswa kusomeka zawagawa au zinawagawa. Kwa ujumla, kichwa hiki cha habari kilipaswa kusomeka: Tahasusi mpya wanafunzi wa kidato cha V & VI zawagawa wadau. Usomapo maelezo ya kichwa hicho cha habari utagundua makosa mengi zaidi.

Niseme kwamba kubainika kwa makosa makubwa na mengi katika kichwa cha habari chenye maneno machache ni ishara ya umilisi hafifu wa lugha kwa wanahabari husika. Wageni, au wanaojifunza lugha, huingiziwa maarifa yasiyo sahihi ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili.

ZBC yanishangaza

Kinachoshangaza zaidi ni kuona hata mashirika makubwa ya habari kama vile Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), ambalo ungedhani lingekuwa na uwezo na utashi wa kuwa na mhariri mahususi wa lugha, yakifanya makosa haya, ambayo mengi ni ya kizembe sana.

Kwa mfano, mnamo Februari 15, 2024, ZBC walichapisha tangazo lililohusu kutolewa bure kwa huduma ya matangazo ya vifo katika mwezi huu wa Ramadhan. Katika tangazo hili kuna sentesi inayosomeka: Tunaomba ushirikiano wenu katika kufanikisha dhumuni hili. Kosa lipo katika neno dhumuni.

SOMA ZAIDI: Uchanganyaji R na L na Makosa Mengine ya Kiswahili Yafanywayo na Wanahabari

Kimsingi, mwandishi amelazimisha kutengeneza umbo la umoja katika neno ambalo halina umbo la umoja, yaani madhumuni, ambalo, kama ilivyo kwa madhehebu, maelewano, maradhi, masihara, maliwato, mahakama, maji na mengineo, halina umbo la umoja. 

Maneno hayo hubaki kama yalivyo kiothografia na kifonolijia katika hali zote, za umoja na wingi.

Wanahabari na watumiaji wengine wa lugha hulazimisha maneno hayo kuwa katika umoja kama yalivyo maneno kama vile jiwemawe, embe maembe, gari magari, tofali matofali, na kadhalika. 

Kisichofahamika ni kwamba katika maneno haya kiambishi ma- ni kiambishi cha wingi kilichoambikwa katika mizizi ya maneno hayo, mizizi ambayo ikibaki pekee huwa ndiyo maumbo ya umoja wake.

Katika maneno yaliyopo kwenye mfululizo wa mifano ya neno madhumuni, ma ya mwanzo katika maneno hayo si kiambishi, ni silabi, /ma/, miongoni mwa silabi zinazounda maneno hayo. 

SOMA ZAIDI: Umahiri, Weledi wa Hayati Mwinyi Katika Kiswahili Unatupa Tanbihi Gani?

Maneno hayo yote ni mofu huru. Hivyo, hayagawanyiki katika mofu tegemezi. Ikitokea hivyo hupoteza maana. Kimsingi, haiyumkiniki umoja wa maradhi kuwa radhi, maji kuwa ji, au mahakama kuwa hakama. Iweje madhumuni kuwa dhumuni?

Kutozingatia ufasaha na usanifu wa lugha kunaweza kusababisha kutumia misamiati isiyokuwamo katika lugha husika na hivyo kusababisha utata wa tungo na pengine msikilizaji, au msomaji, kutofahamu kile kilichokusudiwa kuwasilishwa. 

Kujirudia

Kinachosikitisha ni kwamba makosa haya hutokea kwa kiwango kikubwa sana na kwa kujirudia kiasi ya kunipelekea kuhitimisha kwamba si makosa ya bahati mbaya. Tukibaki hapo hapo ZBC, kwenye taarifa yake ya habari ya Machi 1, 2024, nilistaajabishwa mno na makosa yaliyopo katika muhutasari wa habari uliyokuwa ukipitishwa chini ya televisheni. 

Baadhi ya taarifa zake zilisomeka hivi: Hospitali Binafsi Waakiwa Kukaa na Serikali Kutoa Huduma NHIF na Kuharishwa Ratiba Kunaharibu Mipango ya Timu.

Katika taarifa ya kwanza, kosa lipo katika neno waakiwa. Hakuna msamiati huu katika lugha ya Kiswahili. Kwa sababu hiyo, tungo hiyo haiwezi kuleta maana iliyokusudiwa, hasa pale isomwapo na wasiyo weledi wa Kiswahili. Kuna kosa pia la upatanishi wa kisarufi hata kama neno hilo lingeandikwa kwa usahihi wake.

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Nomino hospitali ipo katika ngeli ya I – ZI. Hivyo, kitenzi chake kilitakiwa kuanza na kiambishi i- katika hali ya umoja na zi- au za- katika hali ya wingi. 

Kutumika kwa kiambishi wa- katika kitenzi kinachokusudiwa kupatanishwa na nomino hospitali kunaashiria kuwa hospitali ni watu na si taasisi. Jambo ambalo si sahihi. Hospitali ni taasisi, si watu. Hivyo, taarifa hii ilitakiwa kuandikwa Hospitali Binafsi Zatakiwa Kukaa …

Katika taarifa ya pili, umakini hafifu wa mwandishi umesababisha kutumia msamiati harisha wenye maana tafauti kabisa na msamiati akhirisha ambao hasa ndiyo uliyokusudiwa, na hivyo kuifanya tungo hiyo kutoa maana nyengine isiyokusudiwa na mtoa taarifa. Usahihi na ufasaha wake ulitakiwa kuwa Kuakhirishwa Ratiba …

Mtazamo potofu

Makosa kama haya hayategemewi kabisa kufanywa na mashirika ya habari makubwa kama haya ambapo taarifa huanza kwa mwandishi, kisha kupita katika hatua mbalimbali hadi kumfikia mharii na baadaye mtangazaji ukiwa ni ya kuisoma, ambaye hufanya maandalizi ya kina kabla ya kuisoma na kuitangaza hadharani.

Wanahabari kuwa na mtazamo potofu dhidi ya nafasi ya lugha katika tasnia yao, kunasababisha makosa makubwa mno. Makosa hayo huathiri mustakbali wa lugha, utamaduni na jamii husika. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunasisitiza Matumizi ya Kiswahili Sanifu, Fasaha Katika Tasnia ya Habari?

Makosa haya ambayo kwa hakika mengine ni ya uzembe na kutokuwa makini, au kutojali, wakati mwengine huenda mbali zaidi na kusababisha kupotoka kwa ujumbe unaokusudiwa au kutopatikana kabisa kwa mantiki zilizofumbatwa katika taarifa husika.

Mimi nadhani ipo haja kwa wanahabari kuipa uzito lugha na nafasi yake ya pekee katika tasnia yao. Kama lugha ndiyo mtaji wao, basi ni muhimu wanahabari watanabahi kuwa kuibananga na kuivuruga ni kuharibu bidhaa yao.

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts