The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Tunasisitiza Matumizi ya Kiswahili Sanifu, Fasaha Katika Tasnia ya Habari?

Suala la matumizi mabovu ya Kiswahili katika vyombo vya habari, hasa vya Tanzania, limeshitadi na kukithiri mno. Sababu za makosa haya zinaweza kuwa nyingi, ikiwemo kukosekana kwa weledi wa lugha miongoni mwa waandishi wa habari.

subscribe to our newsletter!

Tukirejelea fasili ya lugha, tunagundua kuwa inashtamili na mambo makuu sita – sauti, mwanadamu, nasibu, mfumo, jamii na mawasiliano. Sauti ni vitamkwa (/a/, /b/, /m/, /k/, /p/, /i/) nakadhalika. Lugha humuhusu mwanadamu pekee. Wanyama wana sauti lakini si lugha, ingawa kwazo wanawasiliana wao kwa wao. 

Lugha ni nasibu kwa kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kiashiria na kiashiriwa. Kwa mfano, hakuna uhusiano kati ya neno kiti na kifaa chenyewe kinachorejelewa. Hii ndiyo maana kifaa hicho hicho hurejelewa kwa neno au dhana tafauti kutoka lugha moja hadi nyingine.

Kadhalika, lugha huhusishwa na jamii fulani kwa uzao wake. Majina ya lugha takribani zote yamejengwa kwa majina ya jamii husika. Kwa mfano, Wajerumani, lugha yao ni Kijerumani, Wahindi – Kihindi, Waingereza – Kiingereza, Waswahili – Kiswahili na mifano mingine katika utaratibu kama huo.

Katika fasili ya lugha, kuna dhana ya mawasiliano, ikiwa na maana kwamba lengo kuu la lugha ni kuwafanya watumiaji waweze kuelewana na kuwasiliana, yaani msikilizaji au msomaji apate ujumbe unaokusudiwa na mzungumzaji au mwandishi. Pamoja na hayo, tunapaswa kuzingatia dhana ya ‘mfumo’ iliyopo katika fasili ya lugha. 

Kwa muktadha wa lugha, mfumo hukusudiwa utaratibu maalumu wa mpangilio wa sauti ili kupata – silabi – mofu – neno/maneno – tungo – sentesi – kifungu cha habari na hatimaye kupata maana iliyokusudiwa.

Kwa kuzingatia misingi hii, ndipo tunapopata tawi maalumu la lughawiya – isimu fafanuzi/sarufi– linaloshughulikia masomo ya fonolojia (sauti), mofolojia (maumbo), sintaksia (tungo) na semantiki (maana). Mtumiaji wa lugha akishindwa kuzingatia misingi hii, hufanya makosa katika lugha, hatimaye kusababisha ama kutofikiwa kwa mawasiliano au ujumbe wake kueleweka kinyume na makusudio yake.

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru wa Mwanafasihi, Fasihi Haiwezi Kuwa Chombo cha Ukombozi wa Umma

Katika nyakati tulizonazo sasa, tunashuhudia dunia ikiendelea kwa kasi ya ajabu, huku ikichochewa zaidi na tekinolojia ya habari na mawasiliano katika miktadha mbalimbali, ikiwemo elimu, tafiti, diplomasia, habari, siasa, uchumi na mingineo.

Nyenzo kuu ya tekineolojia hii ni lugha na watumiaji wakubwa ni wanahabari, wakiwemo wa televisheni, redio, magazeti na vyombo vya habari vya mtandaoni. Wanahabari wanaweza kuwa wahariri, watangazaji au waandishi. 

Kwa minajili hii, ni wazi kuwa wanahabari wanapaswa kuwa makini zaidi wanapotumia lugha katika utangazaji na uandishi wao. Makosa ya usanifu na ufasaha wa lugha hayategemewi kufanywa na watumiaji rasmi wa lugha, hususan wanahabari.

Kiswahili na habari

Macho yetu ni shuhuda wa idhaa mbalimbali za televisheni za kitaifa na kimataifa zikitangaza habari, kuchambua kadhia mbali mbali za ulimwengu na kuendesha vipindi kadhaa kwa lugha ya Kiswahili. Hali ni hiyo hiyo kwa upande wa masikio yetu yakishudia idhaa za redio nchini na nje ya Afrika. 

Hii ni kusema kwamba Kiswahili ni lugha iliyovuka mipaka ya ulimwengu katika tekinolojia ya habari na mawasiliano. Vyombo vya habari vya kimataifa vikiwemo BBC, VOA, DW, Sauti ya China na vinginevyo vinatumia lugha ya Kiswahili. Kwa vyombo vya habari vya nchini na Afrika Mashariki, takriban vyote vinatumia lugha ya Kiswahili.

Pamoja na Kiswahili kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika tasnia ya habari ulimwenguni, bado kinakabiliwa na changamoto kubwa ya kutumiwa visivyo sahihi kulingana na kanuni zake za kiufasaha na kiusanifu. Tunashuhudia wanahabari wengi wakifanya makosa mengi na ya mara kwa mara katika utangazaji na uandishi. 

SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria

Jambo la kusikitisha zaidi ni pale tunapoona vyombo vya habari vya Tanzania kuwa mstari wa mbele katika matumizi mabovu ya Kiswahili fasaha na sanifu. Matarajio ya wengi ni kuwa wanahabari wa Tanzania wawe mstari wa mbele katika matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha. Inatarajiwa wanahabari nchini Tanzania wawe kigezo na mwalimu wa Kiswahili kwa mataifa menginge ulimwenguni. Lakini hali haiko hivyo.

Tunashuhudia makosa mengi ya matamshi; ujumuishaji na utenganishaji wa maneno isivyostahiki; uongezaji, ubadilishaji na upunguzaji wa viambishi na vitamkwa; matumizi ya msamiati nje ya muktadha; uchanganyaji wa Kiswahili na Kiingereza; matumizi ya lugha za mitaani; matumizi mabaya ya alama za uandishi; miundo ya sentesi na makosa ya kimantiki. Hapa nitatoa mifano michache.

Katika kipindi cha Kapu la Michezo cha ZBC cha Januari 24, 2024, mtangazaji alisikika akisema: “Zimesalia siku tatu kushuhudia pambano hili ambalo litakaloweza kupiganwa…” Katika kauli hii kuna makosa mengi ya kiusanifu. 

Kwanza kiambishi lo– ambacho kina dhima ya o-rejeshi ya nomino ‘pambano’ kimejirejea katika kivumishi ‘amba’ na kitenzi kisaidizi (TS) ‘weza’. Ilitosha kwa msemaji kutumia kiambishi hicho katika neno moja tu. Kiambishi cha o-rejeshi kinapoambikwa katika kiwakilishi au kivumishi –amba, hakirejewi tena katika kitenzi kinachofuata. 

Pili, ni kosa la kimantiki ambalo hupendelewa sana na wanahabari katika matumizi ya lugha. Kosa hili ni matumizi ya kitenzi kisaidizi (weza) pahala pasipostahiki. Kimsingi, haileti maana kusema ‘pambano litaweza – kutokea, kupiganwa, kusimama, nakadhalika. Hakukuwa na haja ya kutumia kitenzi kisaidizi katika sentesi hii. 

Usahihi ni kuwa msemaji alitakiwa kusema, “Zimesalia siku tatu kushuhudia pambano hili ambalo litapiganwa…” au “Zimesalia siku tatu kushuhudia pambano hili litakalopiganwa…”

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Katika kipindi hicho hicho, mtangazaji alisema pia “…ili uweze kulishuhudia pambano hili bila ya kuhadisiwa.” Kosa la kimatamshi limetokea katika neno hadisiwa. Usahihi wake ni hadithiwa. Makosa ya namna hii hujitokeza sana katika vinywa vya wanahabari na wakati mwengine kuathiri hata maandishi yao. 

Makosa haya, pamoja na kuwa mingine hutokana na athari ya lugha za kikabila, hutokana na umilisi mdogo wa lugha. Kwa mfano, maneno yenye kitamkwa /dh/ mara nyingi husikika yakitamkwa kwa /z/. Maneno hayo ni fedha, dhahabu, dhalili, dharau, dhibiti, dhambi, dhihaka, dharuba/dharba, radhi na mengineo.

Katika kipindi cha Wekeza Tanzania cha TBC1 cha Januari 24, 2024, mtangazaji alisikika akimuuliza mgeni wake: “Ukitathmini miaka mitatu iliopita na tulipo sasa, tunaendeleeje?” Kosa lipo katika kitenzi ‘tunaendeleeje’. 

Ufafanuzi wa matumizi ya kiambishi je– kinapotumika kama kiulizi mwishoni mwa kitenzi, ni mrefu. Lakini kwa ufupi, ikiwa kitenzi kitabeba kiambishi cha wakati (li- me- na- ta-), kiambishi tamati maana cha kitenzi hicho kitabaki kama kilivyo.

Kwa mfano, muulizaji anaweza kuuliza “Tunaendeleaje? Utafikaje? Wamesemaje? Alisomaje?” Katika maneno haya, viambishi tamati maana (a-) vimebaki kama vilivyo kabla ya kiambishi kiulizi (je-) kwa sababu vitenzi vimeambikwa viambishi vya njeo. 

Ikiwa vitenzi havitakuwa na kiambishi cha njeo, kiambishi tamati maana kitabadilika na kuwa (e-) kabla ya kiambishi kiulizi je-. Hivyo, kwa mifano iliyotangulia hapo juu itakuwa: “Tuendeleeje? Ufikeje? Wasemeje? Asomeje?”

SOMA ZAIDI: Hatua Zilizobaki Ili Kiswahili Kiwe Lugha ya Kufundishia Tanzania

Kwa ufafanuzi huo, tutakuta kuwa kauli ya mtangazaji ilikuwa na makosa kwa kubadilisha kiambishi tamati maana (a-) na kuwa (e-) katika kitenzi ambacho kina kiambishi cha njeo (na-). Hivyo, alitakiwa kusema, “Ukitathmini miaka mitatu iliopita na tulipo sasa, tunaendeleaje?”

Lengo la lugha ni mawasiliano?

Tumewahi kueleza kuwa lugha huzungumzwa, husemwa na hutumiwa. Tunaweza kusamehe makosa ya lugha pale lugha hiyo inapokuwa katika mazungumzo ya kawaida. Yawe ya sauti au maandishi. Hali haiwezi kuwa hivyo katika lugha ya usemaji na utumiaji. 

Lugha ya usemaji hujumuisha lugha ya utangazaji, uhubiri, hotuba, nakadhalika.  Lugha ya utumiaji huhusisha matumizi ya lugha katika uendeshaji wa shughuli rasmi kama vile za kiserikali, kibunge, mikataba, sheria, sayansi, elimu, habari, uandishi na nyinginezo.

Bila ya shaka lugha hukusudiwa kufikisha mawasiliano baina ya watumiaji. Hata hivyo, dhana hii inachukuliwa tafauti na baadhi ya wadau wa Kiswahili wanaohalalisha makosa ya usanifu na ufasaha wa Kiswahili kwa kisingizio cha kuwa lengo ni kuwasiliana. 

Hapa tunaweza kuhoji masuala kadhaa. Ikiwa lugha ni mawasiliano tu na hivyo hakuna haja ya kuzingatia usanifu na ufasaha, kwa nini tunafundisha misingi ya sarufi ya lugha? Kwa nini tunafundisha misingi ya uandishi; insha, matangazo, makala, barua na habari? Kwa nini tunatengeneza kamusi? Kulikuwa na haja gani kukisanifisha Kiswahili?

Tunaamini kwamba tumesanifisha Kiswahili na kuendelea kufundisha stadi zake katika ngazi zote za elimu kwa lengo la kuifanya lugha hii itumike kwa namna moja katika shughuli rasmi. Tunayafanya haya ili lugha itumiwe kwa ufasaha na usanifu wake. Kama haya ni kweli, kwa nini tutumie kisingizio cha mawasiliano kuhalalisha matumizi mabovu na yasiyo sanifu ya Kiswahili hata katika shughuli rasmi?

SOMA ZAIDI: Matokeo Kidato Cha Nne 2023: Somo La Kiswahili Laendelea Kuongoza Kwa Ufaulu

Wasichofahamu wengi ni kuwa hata hayo mawasiliano hayatoweza kufikiwa ikiwa watumiaji wa lugha hawakuzingatia usahihi na usanifu wake. Hapa tuchukue mfano mmoja. 

Kwa mfano, mtu akikusudia kutoa ujumbe kuwa Serikali imefanikiwa kudhibiti dawa za kulevya, lakini akasema, “Serikali imefanikiwa katika uthibiti wa dawa za kulevya nchini.” Sentesi hii inatoa tafsiri kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kuthibitisha dawa za kulevya zinapoingia au imethibitisha kuwa dawa za kulevya zipo nchini.

Kinachodhihiri hapa ni kuwa kosa la kimatamshi katika neno dhibiti kutamkwa thibiti limesababisha kutoa maana na ujumbe tafauti na makusudio ya msemaji. Je, hapa mawasiliano yamefikiwa? 

Inafaa ifahamike kuwa lengo la lugha si kufikisha mawasiliano tu, bali mawasiliano yaliyokusudiwa yafikiwe. Sentesi hii, licha ya kutoa maana isiyokusudiwa, pia inaweza kusababisha migogoro mikubwa katika nchi. Hapa ndipo tunapoona athari kubwa ya kutozingatia matumizi sanifu na fasaha ya lugha.

Maendeleo katika lugha

Suala jingine linalotumiwa kama kisingizio cha kuhalalisha makosa ya lugha ni pamoja na dai kuwa lugha lazima ikue, iendelee na ibadilike kulingana na mabadiliko ya mwanadamu. Hakuna anayeweza kupingana na ukweli wa kauli hii, lakini maendeleo ya lugha hayapaswi kuwa kibali cha kuiharibu lugha. 

Usanifishaji ni miongoni mwa maendeleo makubwa ya lugha yoyote duniani. Lakini hatujiulizi kuwa usanifishaji hulenga matumizi sanifu na fasaha ya lugha licha ya kuwa ni maendeleo?

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili

Tunachosisitiza hapa ni kuwa lugha ina sanaa na sayansi yake. Maendeleo ya lugha katika sanaa (fasihi) yanaweza kuchupa mipaka ya usanifu na ufasaha. Katika sayansi ya lugha, lazima kuwe na misingi, kanuni na taratibu zinazoiongoza lugha. 

Katika muktadha huu, maendeleo ya lugha lazima yazingatie misingi ya lugha hiyo. Maendeleo ya lugha nje ya misingi, taratibu na kanuni zake, si maendeleo bali ni uharibifu na udhalili wa lugha na watumiaji wake na zaidi kuharibu hata utamaduni wa lugha yenyewe.

Kukua na kuendelea kwa lugha kunakozungumziwa hapa kunahusisha zaidi lugha yenyewe. Hata hivyo, kuongezeka kwa watumiaji, maeneo na matumizi kunahesabiwa pia kama sehemu ya ukuaji na uendeleaji wa lugha. Tunapojikita katika lugha yenyewe, tutawafikiana kuwa kuna utaratibu na njia maalumu zinazoanzia kwenye vitamkwa, silabi, viambishi, maneno na hata tungo.

Kadhalika, kuna utaratibu maalumu wa uundaji wa msamiati na istilahi mpya. Kuwapo kwa utaratibu huu kunadhihirisha kuwa mabadiliko na maendeleo katika lugha ni jambo lisiloepukika. Ilifahamika kuwa lugha itahitaji istilahi na misamiati mipya kutokana na mabadiliko ya kila siku. 

Kuwekwa kwa utaratibu wa lugha kukidhi mahitaji na kuendana na mabadiliko na maendeleo kunatubainishia ulazima wa maendeleo ya lugha kuzingatia misingi ya sayansi ya lugha husika. Hivyo, maendeleo ya lugha si kigezo cha uharibifu wa lugha.

Suala la matumizi mabovu ya Kiswahili katika vyombo vya habari, hasa vya Tanzania, limeshitadi na kukithiri mno. Vilio vya wataalamu na wadau mbalimbali vinasikika katika mijadala mbalimbali. Sababu za makosa haya zinaweza kuwa nyingi mno. 

SOMA ZAIDI: Watanzania na Kilio cha Samaki Kwenye Maji Katika Kiswahili

Umilisi, ama weledi, hafifu wa lugha na stadi zake kwa wanahabari wengi waweza kuwa sababu kuu ya makosa haya. 

Nyingine ni pamoja na kuiga mifumo ya lugha ya Kiingereza, lugha za vijiweni kuingilia matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha, kasumba ya Kiswahili hakina kwao, kutofahamu utamaduni wa lugha ya Kiswahili, kutokuwa na somo maalumu la Kiswahili na habari kwa wanafunzi wa Mawasiliano ya Umma na Uandishi wa Habari katika vyuo vikuu vingi nchini, kukosekana kwa wahariri maalumu wa lugha katika vyombo vya habari na mwamko mdogo wa kujifunza kwa wanahabari wengi.

Kwa kuliona hili, kila Jumanne katika wiki, kutakuwa na safu maalumu hapa The Chanzo. Safu hii itakuwa ikijadili makosa mbalimbali ya lugha ya Kiswahili yaliyogunduliwa katika vyombo mbalimbali vya habari katika wiki nzima. Makosa hayo yatabainishwa na kuchambuliwa kisayansi na kisha kubainisha usahihi wake. 

Napenda kuwaalika na kuwakaribisha wasomaji wetu na wadau wa Kiswahili katika safu hii. Aidha, napenda kutoa wito kwa wanahabari wote nchini kufuatilia safu hii ili iwe mwanzo wa kujifunza na kubaini makosa ya Kiswahili sanifu na fasaha katika vyombo vya habari. Asaa ikawa mwanzo wa mwarubaini wa gonjwa hili na pengine, kwa kiasi kikubwa, tutapunguza, kama si kuondoa kabisa, makosa hayo.

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *