The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uchanganyaji R na L na Makosa Mengine ya Kiswahili Yafanywayo na Wanahabari

Ni afadhali vyombo vya habari vikafanya makosa makubwa ambayo yanaweza kugunduliwa kuwa yanatokana na uhaba wa maarifa husika; ni aibu kwao kufanya makosa madogo madogo na ya kizembe.

subscribe to our newsletter!

Bila ya shaka, tutakubaliana kuwa Kiswahili ni lugha adhimu sana na ni utambulisho wa taifa la Tanzania. Halikadhalika, ni lugha inayoitambulisha Afrika Mashariki na Afrika nzima. Kutumiwa vyivyo sahihi na bila ya kuzingatia usanifu na ufasaha wake, hasa katika vyombo rasmi vya habari, ni kukidunisha, au, kama wasemavyo wengi, ni kukibananga.

Athari ya matumizi ya Kiswahili kisicho sanifu na fasaha haiithakili lugha pekee, bali hata jamii, utamaduni na zaidi kukinza mawasiliano na ujumbe unaokusudiwa kutolewa, hususan kwa wale wasikilizaji na wasomaji ambao Kiswahili kwao ni lugha ngeni au ya kujifunza. 

Kwa minajili hii, tunapokosoa matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha katika vyombo vya habari hatukusudii kutuhumu, kulaumu wala kushutumu vyombo hivyo, bali ni kwa mintarafu ya kuilinda lugha hii adhimu, jamii na utamaduni wake. Halikadhalika, kuyalinda mawasiliano ya umma ili ujumbe unaokusudiwa na wanahabari ufike kama ilivyokusudiwa.

Makosa katika lugha, kama ilivyo katika nyanja yoyote ile, hayawezi kumaliza. Yanatokea kila uchao na yataendelea kuwapo siku hadi siku. Pamoja na ukweli huo, si busara kuendelea kuyaacha pasi na kuyaibua na kuyasahihisha ili yasiwe ni yenye kujirudia hayo kwa hayo. 

Makala hizi zinalenga kutoa elimu kwa watumiaji rasmi wa Kiswahili, hususan wanahabari, ili taarifa zetu zijengwe katika misingi ya lugha bora, sanifu na fasaha. Hatimaye, mawasiliano yafikiwe kwa ukamilifu wake.

Kiswahili magazetini

Leo tuanze na gazeti la MwanaHabari. Katika ukurasa wa mbele wa gazeti hili la Februari 6, 2024, kuna taarifa inayomuonesha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda. Taarifa hii inasomeka hivi: “Tuungane na Rais Samia kupambana na dhuruma kwa wananchi.” Chini ya taarifa hii kuna mada ndogo inayosomeka: “Makonda awataka wananchi kuendelea kutoa kero na malalamiko bila uwoga.”

Ukurasa wa mbele wa gazeti la MwanaHabari unaoonesha habari yenye mapungufu ya kisarufi ya lugha ya Kiswahili. PICHA | SCREENSHOT.

SOMA ZAIDI: ZBC, HabariLeo Waongeze Umakini Matumizi ya Kiswahili Fasaha, Sanifu

Katika taarifa hii kuna makosa makubwa mawili ya kisarufi. Moja ni kosa la ubadilishaji wa fonimu, au kitamkwa, katika neno dhuruma. Mwandishi ametumia kitamkwa /r/ badala ya /l/. Inawezekana kosa hili linatokana na athari ya lugha ya kikabila ya mwandishi. Hata hivyo, tunaweza kujiuliza ikiwa mwandishi hasomi taarifa za magazeti au vyombo vingine? 

Nafasi ya mhariri iko wapi katika taarifa hii? Athari za lugha ya kikabila zinaweza kuchukuliwa kama dharura ya kukosea katika lugha ya mazungumzo. Haiwezi kuwa hivyo katika lugha ya maandishi. Msamiati huu ulitakiwa kuandikwa dhuluma. Makosa ya namna hii hujitokeza sana hasa katika vitamkwa /l/ na /r/, /f/ na /v/, /s/ na /th/, /z/ na /dh/ na vinginevyo.

Kosa la pili ni la uongezaji wa viambishi. Kosa hili lipo katika neno uwoga. Kisichozingatiwa ni kuwa si kila nomino inapaswa kuekewa kiambishi (u-) mwanzoni, kama ilivyo katika masikini – umasikini; nafsi – ubinafsi; pendo/mapenzi – upendo; sawa – usawa, nakadhalika. 

Nomino kama woga, tafauti, mauti, mwelekeo haziwi uwoga, utafauti, umauti, uelekeo, ingawa wengi wanafanya kosa hili kwa kisingizio cha mazoea. Nomino sahihi ya kiuambishaji ya kitenzi ogopa ni woga. Kadhalika, tunaweza kutumia msamiati hofu ambao kwa kukaribiana kwake kimaana na msamiati woga unaweza kutumika kama kisawe.

Katika habari iliyochapishwa na gazeti la Mwananchi la Februari 7, 2024, inayohusu kadhia ya kuakhirishwa kwa mahojiano kati ya Wasafi TV na Tundu Lissu, kuna kifungu cha habari kinachosomeka hivi:

“Mapema leo Februari 7, 2024 Lissu alifika ofisi za Wasafi Tv kuhoji sababu za kuahirishwa kwa mahojiano naye, ambayo tayari yametangazwa kuanzia jana na kwenye mitandao ya kijamii.”

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunasisitiza Matumizi ya Kiswahili Sanifu, Fasaha Katika Tasnia ya Habari?

Katika kifungu hiki, kumejitokeza kosa la kimantiki na kiufasaha kutokana na matumzi yasiyo sahihi ya kiunganishi na. kwenye kifungu cha maneno “…ambayo tayari yametangazwa kuanzia jana na kwenye mitandao ya kijamii.” Kwa kawaida, kiunganishi hiki hutumika kuunganisha ama neno na neno, tungo na tungo au maana na maana. Bila ya shaka, msomaji anaweza kukanganywa na maana ya tungo hii.

Hii ni kwa sababu hakuna muktadha wa kimaana, au kisemantiki, wala wa kimuundo, au kisintaksia, uliyounganishwa katika kifungo cha maneno cha kabla na kile cha baada ya kiunganishi na. Kutokana na mkanganyiko huu, usahihi wa kifungu hicho cha maneno unaweza kuwa katika namna tafauti kulingana na kutofahamika kwa makusudio ya mwandishi:

Ikiwa ilikusudiwa neno na kutumiwa kama kiunganishi (U), basi ilitakiwa ama kuunganishwa na dhana ya kutangazwa (kitenzi) au jana (kielezi) – dhana awali. Kwa bahati mbaya, baada ya kiunganishi hakukujitokeza kitenzi (T) wala kielezi (E). Kwa mfano, ilitakiwa kuwa:

…ambayo tayari yametangazwa kuanzia jana na yalisubiriwa kwa shauku…

…ambayo tayari yametangazwa kuanzia jana na leo…

Kwa njia nyingine, ilitakiwa kutanguliza kutaja vyombo visivyokuwa mitandao ya kijamii, vilivyotangaza, ili kukipa uhalali kifungu cha maneno kwenye mitandao ya kijamii kilichopo baada ya kiunganishi na. Kwa mfano, …ambayo tayari yametangazwa kanzia jana kupitia redio na telivisheni na kwenye mitandao ya kijamii.

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Ikiwa neno na limekusudiwa kutumika kama kihusishi (H), basi ilitakiwa kihusishi kwenye kiondoke katika tungo hiyo. Kwa muktadha huu, tungo ilitakiwa kuwa …ambayo tayari yametangazwa kuanzia jana na mitandao ya kijamii. Au …ambayo tayari yametangazwa kuanzia jana kwenye mitandao ya kijamii. Yaani, kama ilikusudiwa kihusishi, ilipaswa kutumiwa kimoja tu, kati ya na au kwenye.

Makosa ya upatanisho wa kisarufi

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Kimataifa ya China, CRI Kiswahili, Februari 6, 2024, yanapatikana maneno haya: Njiwa aliyekamatwa na askari ya India akishukiwa kuwa…” Katika kauli hii kuna kosa la upatanishi wa kisarufi katika askari ya… 

Ukurasa wa Facebook wa CRI Kiswahili unaoonesha habari yenye mapungufu ya kisarufi ya lugha ya Kiswahili. PICHA | SCREENSHOT.

Kwa kawaida, maneno katika tungo za Kiswahili huambatanishwa kwa upatanishi wa kisarufi na neno kuu –nomino au kiwakilishi– linalozungumziwa katika sentesi husika. Mara nyingi upatanishi huu huzingatia aina ya ngeli ya nomino husika au kiwakilishi chake. 

Nomino askari ipo katika ngeli ya kisintaksia ya A – WA. Maneno yote yaliyo katika ngeli hii hutumia kihusishi wa badala ya ya. Kwa hivyo, usahihi wake ilitakiwa kuwa – aliyekamatwa na askari wa India.

Sababu ya kosa hili inaweza kuwa ni kutumiwa kwa msamiati usiyo sahihi. Inavoonekana, mwandishi alikusudia askari kwa maana ya taasisi. Kimsingi, askari ni mtu na taasisi ni kama vile polisi, jeshi, nakadhalika. Inawezekana mwandishi alikusudia polisi ya India.

SOMA ZAIDI: Matokeo Kidato Cha Nne 2023: Somo La Kiswahili Laendelea Kuongoza Kwa Ufaulu

Habari nyingine ni ya Azam TV, iliyochapishwa katika mtandao wake wa X, Feb 11, 2024, ikizungumzia tukio la ajali la msafara wa Makonda. Taarifa hii ina kifungu kinachosomeka:

“Katika ajali hiyo, magari 13 yaligongana na kusababisha majeruhi kadhaa wakiwepo Mbunge wa jimbo la Tandhahimba, Katani Ahmed Katani na Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Bahati Geuzye.”

Kosa lipo katika neno wakiwepo. Mwandishi ametumia kiambishi tamati kijenzi cha urejeshi (po-) ambacho hurejelea pahala au wakati. Kwa kutumia kiambishi hiki, maana ya kifungu cha habari hii hupotoka. 

Badala ya kutoa tafsiri ya miongoni mwa majeruhi, inatatoa tafsiri ya miongoni mwa watu waliyokuwa wapo katika eneo la tukio. Kiambishi sahihi kilichotakiwa kutumiwa katika muktadha huu ni (mo-) ambacho kwa hapa hufanya kazi ya ujumuishi. Hivyo, ilitakiwa kuandikwa …na kusababisha majeruhi kadhaa wakiwemo…

Mdharau mwiba humchoma

Yawezekana makosa haya yakaonekana ni madogo na hivyo labda kusingekuwa na umuhimu wa kuyabainisha. Pengine inaweza kuwa hivyo, lakini nadhari zetu zinapodhani makosa haya ni madogo zisisahau kuzingatia ukweli uliyofumbatwa na methali isemayo haba na haba hujaza kibaba na bandu bandu hwisha gogo.

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili

Tutawafikiana pia, kuwa kosa dogo la imamu huwa na uzito kuliko kubwa la maamuma. Vyombo vya habari kama Mwananchi, MwanaHabari, Azam TV na vingine ni vikubwa na vina hadhi ya juu. Ni afadhali vyombo hivi kufanya makosa makubwa ambayo yanaweza kugunduliwa kuwa yanatokana na uhaba wa maarifa husika. Vyombo kama hivi ni aibu kufanya makosa madogo madogo na ya kizembe.

Kwa minajili hii, ni aula kuyabainisha makosa hayo, kuyachambua na kuyasahihisha. Ni wajibu wetu kuziba ufa kwa kuchelea uzito na kashikashi za kujenga ukuta. Asaa ikawa dawa ya kupunguza makali kama si kuyatokomeza kabisa maradhi haya ya ajabu na aibu.

Tukutane wiki ijayo safu hii, tukijaribu kuchambua na kusahihisha makosa ya Kiswahili sanifu na fasaha yanayofanywa na vyombo mbalimbali vya habari. Usiache kuniandikia pale unapotanzika na lugha unayokutana nayo kuwa ni Kiswahili fasaha na sanifu au la, katika usikilizaji na usomaji wa taarifa mbalimbali za vyombo vya habari.

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *