Undani wa mwanadamu ndiyo haswa sanaa ya ushairi. Ushairi si maneno tu, ni kitu kinachoishi ndani yetu; kina uhai. Lugha na maneno ni vyombo tu vya kuelezea ushairi ambao tunauishi. Na tena, kila mtu anauishi uhalisia huo; japokuwa si kila mtu anayeweza kutumia maneno kuuelezea.
Shaaban Robert, moja kati ya washairi nguli kuwahi kutokea hapa Tanzania, alikuwa fundi katika hilo. Na kama vile ambavyo ushairi ni undani wa mwanadamu, ushairi wenyewe una undani wake pia, undani ambao unauhisi kwa lugha isiyotamkika kwa lugha za wanadamu bali lugha ya moyo.
Kwa mtu anayependa kusoma, kuandika na kuyaelewa mashairi kwa undani, Sanaa ya Ushairi, kilichoandikwa na Shaaban Robert na kuchapishwa na Mkuki na Nyota mwaka 2023, kikichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1971 na Nelson, ni moja ya vitabu ambavyo lazima awe navyo katika maktaba yake.
“Ushairi ni namna moja ya sanaa muhimu katika masomo,” mwandishi anaeleza kwenye kitabu hicho kidogo chenye kurasa 79 tu. “Masomo bila ya ushairi ni sawa na Misri bila ya Nili. Zaidi ya hayo, ushairi ni maumbile ambayo mtu huzaliwa nayo.”
Shaaban Robert anaielezea sanaa ya ushairi kwa kuainisha namna mbalimbali za kuandika mashairi – mashairi ya mizani, yale yenye kipimo au vipimo, matamko ya herufi au silabi; mashairi ya vina, yenye mlingano wa sauti kati ya na mwishoni mwa kila mstari wa ubeti; mashairi ya kutupa vina, yale yasiyokuwa na vina; tenzi, shairi lenye bahari katika mstari wa mwisho wa kila ubeti; na guni, ambayo hujulikana kwa dosari ya mizani na ila katika vina.
Simulizi
Anahitimisha utangulizi wake kwa kueleza umuhimu wa kuwepo kwa kitabu kama hiki. Kama kawaida yake, Shaaban Robert anatumia simulizi kufafanua hoja yake. Simulizi yenyewe inamhusu Mfalme na Malkia wa nchi fulani.
SOMA ZAIDI: ‘Utubora Mkulima’ na Funzo la Kuwekeza Nguvu Katika Kuipendezesha Nafsi Yako
Siku moja, Mfalme alitaka wanawake wa mjini wawe kama wa porini – wakakamavu na wanaostahimili ugumu wa maisha kwa kuzaa bila msaada wa mkunga na kuwa na uwezo wa kuinua jembe na kulima hapohapo! Alitaka wawe wanawake jasiri kama vile tunavyowaita siku hizi super woman.
Malkia akaona isiwe tabu. Akamwagiza yule aliyekuwa anasimamia bustani ya Mfalme, kuwa bustani isilimwe. Ilipoanza kuwa na mwonekano mbaya, Malkia akaulizwa. Naye alikuwa na utetezi.
“Ua la porini pengine hupita ua la bustani kwa uzuri na manukato lakini halihitaji uangalifu wa mtu,” alieleza Malkia kwenye utetezi wake. “Ua la bustani hutaka sana kutunzwa kama wanawake wa mijini walivyo.”
Hali kadhalika, mwandishi anasema kuwa, “… uzuri wa masomo humea vema katika bustani ya ushairi. Pasipo kuitunza bustani hii uzuri wa masomo yetu haukamiliki.”(uk. viii).
Mawaidha ya maisha
Mashairi ya kitabu hiki yanajadili masuala mbalimbali ya jamii, yakitoa mawaidha kuhusu maisha, kujenga tabia njema, mahusiano na watu, uongozi, na mapenzi.
Japokuwa katika utangulizi mwandishi anaonesha nia ya kufundisha mbinu za kishairi, kwa kiwango kikubwa jina la kitabu linaakisi hulka, ama utashi, mwa mwanadamu. Shaaban Robert anatumia mashairi mengi kuuelezea undani mwa mwanadamu – uzuri wake, ubora wake, fikra zake, furaha yake, wema wake.
SOMA ZAIDI: ‘Kusadikika’ ya Shaaban Robert na Nasaha Njema za Maisha
Moja ya mashairi yanayonivutia sana katika kitabu hili ni Anasa Bora (uk. 41). Mwandishi anampamba binadamu kwa lugha ya kupendeza. Mwandishi anasema:
Mtu ni anasa bora,
Kwa haki hana kifani
Ana wingi wa busara,
Umbo na mwendo wa shani.
Kwa matendo ni sogora,
Wala hana mshindani.
Kwa fahamu ni imara,
Ajua siri za ndani.
Ni upeo wa ibura,
Pambo la ulimwengu.
Kwa vile tunavyomjua mwanadamu, tunavyojijua, sisi ni mavumbi tu. Twaamini kuwa mavumbini tulitoka, nako tutarudi. Lakini mwandishi aliona kwa jicho lingine, uzuri alioumbiwa mwanadamu na Mwenyezi Mungu. Anauona undani wa mwanadamu na kutumia shairi kama chombo tu cha kuwasilisha anachokiona. Na katika ubeti mwengine anasema:
Duniani kamuweka
Na tunu nyingi idadi.
Tunu zisizo mpaka,
Kama ana jitihadi,
Juu aweza kuruka,
Mtu kiumbe wa sudi;
“Juu aweza kuruka” ni mstari ambao umebeba maana nyingi. Juu kwa maana ya kwamba nafsi ya mwanadamu inaweza kukabiliana na changamoto, kushinda mawazo hasi na hata kuwa na nguvu; au jinsi ambavyo mtu anaweza kushinda hali ngumu za maisha – umasikini, hali yoyote duni katika mazingira yake – na kuinuka kimaisha; au kuashiria jinsi mwanadamu anaweza kuwa na maarifa mengi hata kuweza kupaa katika mawingu kwa vyombo maalumu viwe katika namna ya ya mwili au ya roho.
SOMA ZAIDI: ‘Kufikirika’ ya Shaaban Robert na Uhalisia Usiyopitwa na Wakati
Udhaifu wa mwanadamu
Kwenye Tamu Yangu (uk. 52), mwandishi anaweka wazi undani wake; udhaifu wake, maumivu yake, hafichi wala hajitengi na hali ya ubinadamu, kiumbe yuleyule aliyetukuka mwenye uwezo wa kuruka juu anao:
Mashaka yangu nitaeleza,
Asaa Mungu akapunguza,
Nina uchungu mwingi naweza,
Ulimwengu umeniumiza,
Si mwenye fungu katika meza.
Kwenye kitabu chake cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, Shaaban Robert anaelezea jinsi washairi walivyomshambulia baada ya kuchapisha shairi lake la Ujane gazetini, linalohusu maisha yake.
Anawajibu washairi mbalimbali, akiwemo Bwana Palla, ambaye pia anamjibu katika mashairi kadhaa kwenye Sanaa na Ushairi, likiwemo, Fundi hawi Mwanafunzi, Kuoa Kumelazimu, na Swali Langu ni Ujane.
Kwa namna fulani, Shaaban Robert anaendelea kuonesha jinsi ushairi ulivyo kitu kilicho na uhai. Ushairi ni mazungumzo, ni majibizano kati ya fikra na fikra. Ushairi hauishi katika ombwe, kama vile ambavyo mwanadamu haishi hivyo.
SOMA ZAIDI: Ni Wakati Tuitendee Haki Kumbukumbu ya Maisha ya Siti binti Saad
Ushairi unahitaji kuhusiana na mashairi mengine, japokuwa shairi lina uwezo wa kuishi peke yake kwa kujitegemea. Hata hivyo, inaleta maana kubwa zaidi pale ambapo shairi lingine linapaza sauti yake kunena na kuishi nalo.Anamwambia Bwana Palla katika Swali Langu ni Ujane (uk. 67):
Wengi mwangoja mapenzi, huku mwatafuna nyama;
Tukiwaita wazinzi, mwenda kwenye mahakama,
Adili hamziwezi, mwajivutia heshima!
Swali langu ni ujane si namna ya kuoa.
Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Kàzi nzuri sana ila watu wetu ha2asomi kazi hizi.