Kwa mujibu wa mapokeo na makabrasha ya historia ni kwamba kwenye vita kuu ya pili ya dunia, 1939 – 1945, moja ya silaha ya maangamizi waliyotumia Serikali ya Ujerumani dhidi ya Waingereza na Wabelgiji ni kombora aina ya V-2.
Awali ya hapo, silaha nyingine, pasi na shaka yeyote, ilikuwa ni kuwagawa wananchi, kukaba koo vyama vya upinzani na kudhoofisha asasi mbalimbali za kiraia, kueneza propaganda kwa wananchi na mahasimu wao. Hizi ni baadhi tu ya mbinu maarufu zitumikazo sana hadi leo na dola za kidikteta.
Kimsingi, katika vita hiyo, Wajerumani walionesha makucha yao ya ukatili bila utu, yaani kimkakati kabisa, walidondosha makombora takribani 4,300 na kuua mamilioni ya watu wasio na hatia. Wengine walijeruhiwa na kubakwa; wengine walipata ulemavu na mfadhaiko wa akili wa kudumu.
Pia, Waafrika wengi waliotumikishwa, bila ari wala hiari, katika vita hii ya kibeberu wanasimulia kwa uchungu mkubwa kadhia na madhila ya vita hiyo. Ni bahati mbaya, vita kemkem za aina hiyo bado zinaendelea sehemu mbalimbali duniani.
Naam, mataifa yenye nguvu kiuchumi na kinyuklia yanaweza kuufuta ulimwengu kwa mpepeso tu wa macho yao. Tafsiri yake ni kwamba, mfumo na itikadi za uliberali-mamboleo unahitaji vita na mauaji kama oksijeni ili uweze kustawi!
SOMA ZAIDI: Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini
Sasa, yayumkinika, katika mahojiano na mtengenezaji mmoja wapo wa makombora hayo ya vita, kwa jina la Wernher von Braun, mfiadini-mkereketwa na mtetezi wa chama dola cha Kinazi, alipoulizwa kama dhamira ilimsuta na kumtesa kwa kutengeneza silaha iliyotumika katika mauaji makubwa kama yale, alisema hapana.
“Mimi natengeneza mabomu, lakini uamuzi wa wapi hayo mabomu yakaue siyo wangu,” alijibu von Braun, ambaye ni mhandisi kitaaluma, bila tabu. “Hata hiyo dhamira yenyewe siijui ni kitu gani, kile mimi nafuata ni maagizo kutoka juu kwa mkuu wangu, Adolf Hitler, na kuyatii tu.”
Basi, mnamo mwaka 1945, mkono wa sheria uliwatia hatiani wote waliohusika na mauaji, walifunguliwa mashtaka na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Dhambi yao ni kutii na kutekeleza sheria katili na mbovu kiimla.
Mafunzo
Kuna mafunzo lukuki kwenye hadithi hii fupi, moja ikiwa ni umuhimu wa mtu kuongozwa na dhamira, au nia, yako sahihi. Ikiwezekana ukiri kwa kudra na kadri ya imani yako, kuwa hutakubali kamwe kufanya jambo unalojua ni kosa, au baya, hata kama lipo kisheria. Hivyo, katika muktadha na mustakabala huu, chagua daima uaminifu kuliko utii kipofu.
Kabla ya kutekeleza uamuzi wowote, jenga tabia ya kujisikiliza na kujitafakari kwanza kuhusu madhara ya matendo yako. Nionavyo mimi, maamuzi yetu mengi hapa Tanzania, lakini hasa viongozi wetu Serikalini, ni ya kukurupuka, mhemko, uchawa na ushabiki wa kisiasa.
SOMA ZAIDI: Mvutano Kati ya Mungu na Shetani Unaweza Kueleza Hali ya Sasa Tanzania?
Hata mipango yetu mingi kama nchi, mathalani, inakwama, kwa sababu siyo ya kitafiti, siyo jumuishi na shirikishi vya kutosha, wala endelevu.
Rai yangu kama raia, tunahitaji kuwa na ukomavu wa dhamira. Hili ni muhimu zaidi na la kwanza, kabla ya kuwa hata na sheria mama, yaani Katiba Mpya. Kuwa na dhamira safi, pamoja na dai la Katiba kama muundombinu, au framework, wa kujiongoza ni muhimu sana.
Lazima tufike mahali tuenende kwa haki, kufuata utawala bora na uwajibikaji hata kama hakuna mtu anatuona, anatusifia, au sheria inatulazimisha. Ifike mahali, tujidadisi kwa kina, kwa nini, kwa mfano, pamoja na sheria nyingi tulizonazo, bado makosa ya kimakusudi yanatendeka?
Utii na kuapa juu ya Katiba zetu, una thamani gani kama Serikali yenyewe ndiyo ya kwanza kuvunja sheria hizo? Je, tunajenga mahusiano gani kati ya Serikali na wananchi ikiwa ahadi zinazowekwa hazitimizwi?
Je, tunatarajia wananchi kuwa na imani na viongozi waliowadhamini kuwawakilisha kama hawatimizi majukumu yao? Kwa nini wananchi wengi hawaamini tena chaguzi zetu na hawapigi kura?
SOMA ZAIDI: Sakata la Bandari: Je, Serikali Imepoteza Imani ya Wananchi?
Hakika maswali ni mengi kuliko majibu. Uhuru uko wapi pale Serikali kuu inapoingilia utendaji kazi wa Mahakama, Bunge na hata ‘kuua’ kimkakati vyama vya wafanyakazi na vyombo huru vya habari?
Ukweli ni kwamba, uzembe na baadhi ya maamuzi ya kisiasa,unaleta umaskini na kuongeza ugumu wa maisha kwa Watanzania. Mfano, utitiri wa kodi na tozo mbalimbali, huduma mbovu kwenye afya, umeme na elimu, uwekezaji na ubinafsishaji holela wa taasisi za umma.
Jambo lingine, mpaka sasa fedha nyingi sana zimetumika kuunda tume mbalimbali ili kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuboresha haki jinai na demokrasia nchini, lakini mpaka leo, hakuna maboresho yeyote ya msingi yametokea.
Haya yote yanaonesha dharau na kukosekana kwa nia, au dhamira, ya dhati kutoka kwenye tabaka la watawala katika kuleta maendeleo ya kweli nchini.
Uasi wa kiraia
Mwanafalsafa wa Kimarekani, Henry D. Thoreau, aliamini kwamba uasi wa kiraia, siyo wa kijeshi, ni hali ya kutokutii sheria batili na kukataa kuzifuata kwa sababu ni sheria kandamizi. Wajibu wa kutokutii hizo sheria, hata kama ni za miungu, siyo kukosa heshima, uzalendo au ni uhaini fulani, bali ni ukomavu wa kisiasa.
SOMA ZAIDI: Teuzi za Watu Wasio Waadilifu Zinawapa Motisha Viongozi Kutumia Vibaya Ofisi za Umma
Ni kuwa na dhamira huru kama ambavyo walikuwa nazo watu maarufu kama John Rawls, Mahatma Gandhi, Yesu wa Nazareth na Martin Luther King waliotumia uasi wa kiraia katika kushinikiza mageuzi chanya kwenye jamii zao.
Kwenye miaka ya 1960, baadhi ya vijana wa Marekani waliandamana na kuchoma mabango ya mwaliko wa kwenda kupigana vita na Vietnam, wakieleza kwamba walipinga ile vita na hivyo wasingeweza kusaliti dhamira zao dhidi ya mauaji ya raia wasio na hatia.
Walisadiki kwamba, kama raia, hasa vijana, wana haki ya kuongozwa na siasa safi, huduma za kisheria rafiki na taasisi bora.
Katika mazingira yetu hapa Tanzania, bado kuna utabaka mkubwa kati ya watawala na watawaliwa, kati ya wenyeheri na walalahoi. Mahusiano kati yao bado ni ya kiuoga na kujipendekeza. Watawala wanajiona kama masultani fulani, wajuaji wa kila kitu na hawana la kujifunza na kuwajibika kutoka kwa wananchi.
Mnamo mwaka 1975, akiongea na wafanyakazi, Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania, alisema: “Utii ukizidi unakuwa woga, na uoga siku zote huzaa unafiki na kujipendeza, na mwisho ni mauti. Kujenga mazoea ya kutii viongozi, hata katika mambo haramu, ni dalili ya woga na kukaribisha udikteta.”
SOMA ZAIDI: Barua kwa Askari wa Jeshi la Polisi Tanzania: ‘Mmepoteza Imani Yetu Kwenu’
Hivyo, kama wananchi, tuna wajibu wa kukataa mazingira yeyote ya kuabudu watawala na kuogopana. Wito wa umma wa Watanzania, iwe binafsi na kupitia vyama vyao na taasisi za kiraia, ni pamoja na kuishinikiza Serikali kuleta mabadiliko ya kina, kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Na katika hili bado tuna safari ndefu ya kuelimishana na kuhamasishana kuhusu haki zetu na uwezo wa kutumia nguvu yetu ya kikatiba. Maendeleo ya kweli na endelevu, popote duniani, yataletwa na wananchi wenyewe na siyo na fadhila ya rais wa nchi.
Lazima wananchi wajengewe uwezo na kuwa na ‘hasira’ ya kujiletea maendeleo yao wenyewe.
Isaac Mdindile ni mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira. Kwa mrejesho anapatikana kupitia ezyone.one@gmail.com au Twitter kama @IsaacGaitanJr. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.
One Response
Asante sana Kwa kutukumbusha kua na ukomavu wa dhamira na kama vijana kutokua na woga usio na tija linapohusu swala la maendeleo na kua na mpango mikakati tulivu na hoja thabiti.