Mbeya. Wataalamu wa kilimo na viuatilifu nchini Tanzania wanaumiza vichwa kupata suluhu ya kudumu itakayotatua tatizo la konokono wanaodaiwa kuathiri mazao ya wakulima mkoani hapa na mikoa ya jirani, wakiwaacha na wasiwasi mkubwa kuhusiana na hatma yao kama wakulima na wananchi pia.
Hilo limebainika hivi karibuni wakati The Chanzo inafanya uchunguzi kuhusiana na madhila wanayokabiliana nayo wakulima kutoka kata za Utengule Usongwe, Igale na Mshewa, wilaya ya Mbeya Vijijini, ambao wamekilalamikia chombo hicho cha habari kwamba wadudu hao waharibifu wanatishia usalama wao wa chakula.
The Chanzo ilitembelea baadhi ya mashamba ya wakulima hao, wengi wao wakilima mahindi, maharage, alizeti na kahawa, na kujionea namna konokono walivyotapakaa shambani humo, wakisababisha uharibifu mkubwa wa mazao ambayo wakulima wanayategemea kwa ajili ya kula na biashara pia.
Kwenye mazungumzo yao na The Chanzo, wakulima hao waliziangukia mamlaka zinazohusika na kilimo kuchukua hatua za haraka za kuwanusuru na madhara yanayoweza kutokana na wadudu hao, wakieleza kwamba wakati konokono wamekuwepo siku nyingi, uwepo wao wa sasa ni wa tofauti na wenye kutisha zaidi.
“Vijana wengi tunalima bustani, unashangaa unanunua mbegu ya Shilingi 300,000, unaotesha vizuri kwenye kitalu, halafu unaipeleka shambani wanakuja konokono, wanakukatia,” Aroni Thomasi, 32, alilalamika. “Inafika hatua hata kazi ya kilimo tunaikatia tamaa sisi kama vijana.”
SOMA ZAIDI: Mwenye Kiwanda Rungwe Adaiwa Kuchelewesha Malipo ya Wakulima 13,000 wa Chai
Jophrey Donard, 35, mkulima mwingine aliyechoshwa na wadudu hao, aliiambia The Chanzo: “Yaani wakilamba mfano nyanya chungu, au nyanya, zinanyauka, halafu ni wengi, hata ukiokota namna gani yaani inakuwa ni kazi bure tu.”
Kwa mujibu wa Adeni Mbuba, mtaalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), akizungumza na waandishi wa habari hapo Machi 26, 2024, konokono hao waligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 2019 kufuatia utafiti mdogo uliofanywa na taasisi hiyo.
Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Mbuba alisema kwamba mabadiliko ya tabianchi yanahusika kwa kiwango kikubwa na uwepo wa konokono hao, akisema wakati mamlaka zinatafuta suluhu ya kudumu dhidi yao, wakulima wanaweza kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na konokono na athari zinazotokana na wao.
“Kukabiliana na changamoto hii, tumekuja na mbinu mpya zitakazowasaidia wakulima kukabiliana na hawa wadudu,” alisema Mbuba kwenye mkutano huo na waandishi wa habari. “Na tumewaelekeza wakulima namna ya kutumia mbinu hizi na tunaamini kwamba, kama watazitumia ipasavyo, zitawasaidia kupunguza tatizo hili.”
Mbinu hizi ni kama vile kuhakikisha mashamba yanakuwa safi na kuwatokomeza konokono kwa kutumia chumvi, au maji yaliyochanganywa na sabuni. Mbuba alisema pia kwamba wakulima wanaweza kupambana na konokono kwa kumwagilia majivu au chumvi kwenye mashamba yao pamoja na kutumia mbolea.
SOMA ZAIDI: Bei Duni, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Vilio Vikubwa vya Wakulima wa Mwani Z’bar
Lakini wakulima wameiambia The Chanzo kwamba wakati wanazikaribisha mbinu hizi wanazoshauriwa kutumia, wanaiomba Serikali kubuni viuatilifu vitakavyowasaidia kuwatokomeza konokono mara moja na milele.
Afisa Kilimo wilaya ya Mbeya Vijijini, Gidion Mapunda, aliiambia The Chanzo kwamba anawaelewa wakulima wanaoteswa na wadudu hao, lakini alishauri kwamba wakati Serikali inaendelea kutafuta suluhu hiyo ya kudumu, wakulima hao wafuate ushauri waliopewa na wataalamu ili kukabiliana na tatizo hilo.
Naye Lusille Ryaluu, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi kutoka Mamalaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, ameiambia The Chanzo kwamba mamlaka hiyo inaona ambavyo konokono wanavyofanya uharibifu katika mashamba, akisema kwamba wanachukua hatua mbalimbali kutatua changamoto hiyo.
“Konokono hawa wanapenda kukaa juu kama kwenye miparachichi, kahawa, na hata kwenye mahindi pamoja na migomba,” Ryaluu alisema. “Kuna kiuatilifu kinatumika japo kwa kiasi kidogo, kinaitwa kono bait.”
“Hiki kiuatilifu kinaangamiza konokono wale wakubwa,” aliongeza mtaalamu huyo. “Bado hatujabaini kama kinaweza kuangamiza mayai na wale wanaoanguliwa kwa sababu wale kokonokono wakubwa wanafuata ile harufu na pale anapokigusa wanakufa.”
SOMA ZADI: ‘Tunaona Ina Tija’: Alizeti Kuwaondolea Adha ya Korosho Wakulima Liwale?
“Tunaendelea kuchunguza, na wakati tunaendelea kufanya hivyo, tunawahimiza wakulima wafuate ushauri wanaopewa na wataalamu,” aliongeza Ryaluu.
Modesta Mwambene ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Mbeya. Anapatikana kupitia mwambemo@gmail.com.