The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hatuwezi Kuendelea Kuona Kashfa za Wengine Kama Chanzo cha Furaha Yetu

Natamani tujitafakari kama taifa, na kujiuliza, je, huku tulipo na tunakotaka kuelekea, kwenye matumizi haya ya mitandao ya kijamii, ni kuzuri?

subscribe to our newsletter!

Matumizi ya mitandao ya kijamii yamezidi kukua na kuongezeka sana hapa nchini Tanzania, yakichangia kwenye mabadiliko chanya kwenye sekta mbalimbali, iwe ni za kiuchumi, kijamii au, zaidi, kisiasa.

Harakati za kudai utawala bora, maisha bora kwa Watanzania, utawala wa kisheria, haki za watu, na hata kuelezea kero mbalimbali, zimekua zikifanyika sana kupitia mitandao ya kijamii kama vile X, zamani Twitter, Instagram, Telegram, Whatsapp na mitandao mingine ya kijamii, na kwa kiasi chake harakati hizi zimezaa matunda mengi mazuri. 

Tumeshuhudia, kwa mfano, Watanzania wakitumia mitandao ya kijamii kuhimiza waliotekwa warudishwe, au miundombinu ya barabara iboreshwe. Kwa lugha nyepesi, jamii ile ya mtaani sasa haikutani tena kwenye vijiwe vya kahawa, au kwenye ofisi za vyama vya siasa, au mikutano ya hadhara. Kwa sasa watu tunakutana kiganjani!

Lakini kama kulivyo na mazuri mengi yanayotokana pale mitandao ya kijamii ikitumika sawasawa, kuna athari nyingi sana pia zinazoendelea kutokea kwa matumizi mabaya ya mitandao hiyo, na moja kati ya matumizi hayo mabaya ni kile ninachokitafsiri kama kufurahia kashfa za wengine ili kujifurahisha sisi wenyewe.

Kama wewe ni mtumiaji wa mitandao ya kijamii, basi utakuwa umeshuhudia siku za hivi karibuni vichwa vya habari kama vile Ayker Achafua Hali ya Hewa, Kuna ‘Connection’ ya Ayker Imevuja, au Leo Ayker Anapikwa Twitter,  vimekuwa vikisambaa kwenye mitandao hiyo na, kwa bahati mbaya sana, kushabikiwa na walio wengi.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Wanasiasa Wanawake Wanaikimbia Mitandao ya Kijamii?

Vichwa hivi vya habari vimekuwa vikivutia zaidi wasomaji kwenda kwenye kurasa za mitandaoni kuangalia je, hicho walichotegemea kweli kimewekwa kwenye ukurasa husika? 

Je, mapishi yanayosemwa ni kweli yapo au mapishi hayo siyo makubwa sana kwa kipimo chao? Na hii imekua kiasi kwamba kwa sasa ni moja wapo ya mapato makubwa sana nchini, huku watu wakiwa hawaoni soni tena kwa kuuza taarifa zako. 

Inashangaza? Hatukuyategemea? La Hasha! Katika jamii hii inayokutana kiganjani kuna watu wa aina mbalimbali: wenye makuzi tofauti, imani na mienendo tofauti, lakini ambacho hakibadiliki ni utu wetu na ubinadamu wetu. 

Ile hulka ya kibinadamu kutamani kusemeshwa na kutendewa kwa upendo hatuivui tukiingia mitandaoni; zile familia zetu zinazotutegemea hatuziachi tukiingia mitandaoni. Ile hulka ya kuhitaji faragha zetu zilindwe na zitunzwe bado tunatembea nazo hata tukiwa kwenye jamii hii ya mtandaoni.

Leo natamani tuwafikirie wale waathirika ambao mara nyingi hawahusiki moja kwa moja kwenye magomvi yetu mitandaoni, lakini wanajikuta wamehusishwa kwa namna moja au nyingine kwenye ugomvi. Hapa nawazungumzia wale watoto, wenza, wazazi na marafiki wa hawa waathirika. 

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kujenga Jamii Yenye Mtazamo Chanya Kwa Wanawake wa Makundi Maalumu?

Je, kuna muda huwa tunajiuliza hali zao zikoje? Binti, au kijana mdogo, anaenda shule anakutana na watoto wenzie wakimwambia kwa kushangilia kwamba wameona connection ya baba au mama yake, au wazazi kule kijijini wanaomtegemea huyo kijana wao wakiamshwa na maneno ya majirani kuhusu kuona utupu au kusoma kashfa za mtoto wao. 

Na bahati mbaya sana mara nyingi kama ni tuhuma Watanzania hatusubiri zikanushwe, au kusikia upande wa pili. Sisi tutatembea na kashfa hiyo na utenzi tutaitungia, kashfa tunayo na tunatamba nayo!

Labda kwa kuwa hapa nchini kwetu hayajawahi ripotiwa matukio ya watu kujitoa uhai kwa sababu ya hizi kashfa na connection za mitandaoni ndiyo maana jamii inashangilia. 

Kwa mataifa kama Marekani, Korea Kusini, Afrika Kusini na kwingineko kumekua na ripoti za kuongezeka kwa matukio ya watu kujiua yanayosababishwa na uonevu na kashfa za mitandaoni. 

Je, kama taifa, tunasubiri kufikia hatua hii ili kuona uzito wa janga hili? Ule utu na Utanzania wetu uko wapi? 

SOMA ZAIDI: Mange Kimambi, Naomba Tuzungumze Kidogo

Maana tulitarajia ule upendo wa Kitanzania tunaokesha kuuhubiri tungeuonesha kwenye kukemea kwa nguvu matukio kama haya, lakini ni kinyume chake. Leo likes na comments za kushangilia zinatokana na taarifa mbaya zinazoandikwa.  

Taifa bora lenye watu wenye kipato linajengwa kwa watu wenye utimamu wa akili unaosababishwa, mbali na mambo mengine, na utulivu kwa kufahamu kwamba utu wao unalindwa na faragha zao zinaheshimiwa. 

Hatuwezi kujenga taifa bora tukiwa na jamii ambayo kashfa na connection ni moja ya vyanzo vikuu vya furaha kwa watu wake. Tutaendelea kushikana mashati na kuraruana kutafuta nani anayeturudisha nyuma bila kuona kwamba sisi, kwa nyakati tofauti, tumekua tukirudishana nyuma wenyewe kwa wenyewe. 

Natamani tujitafakari kama taifa, na kujiuliza, je, huku tulipo na tunakotaka kuelekea kama taifa, kwenye matumizi haya ya mitandao ya kijamii, ni kuzuri? 

Nafahamu kuna hoja za kuwepo kwa adhabu na sheria kali lakini kabla hatujafika huko, tujisahihishe kwa kutokua wawezeshaji wa hawa wanaokosea. Turudi kule ambapo tukiamua, kama wanajamii wa mitandaoni, bila kashfa, wala matusi, wala connection, tunajenga hoja zenye kuifanya Serikali iweze kuchukua hatua.

Ayker Peter ni mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia aikapeter2420@gmail.com au @AykerP katika mtandao wa X. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *