The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tuitumie Sekretarieti ya Maadili Kuwawajibisha Viongozi

Tukiiandikia Sekretarieti kwa uwingi wetu tutawaamsha hata waliolala; Tutapiga kelele na kupata matokeo bila kutumia nguvu au kuumizwa.

subscribe to our newsletter!

Wajibu wa wananchi kusimamia maadili ni wa kisheria. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampatia kila raia wajibu wa kuchukua hatua kuhakikisha ulinzi wa sheria. Raia anaweza kuchukua hatua za kimahakama kuomba amri itakayosaidia kulinda Katiba na sheria za nchi. Tumefungua kesi nyingi za kikatiba kupitia kifungu hicho.

Hata hivyo, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Namba 13, 1995, imeweka mfumo maalum wa malalamiko. Raia yeyote anaweza kufungua shauri mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya kiongozi wa umma. Msingi ni kukiukwa kwa maadili, kiapo au miiko ya uongozi – kama nilivyoeleza katika makala tangulizi.

Sekretarieti imeanzishwa kupitia kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Kazi zake ni kupokea matamko ya viongozi wa umma chini ya sheria na Katiba, mathalani, kuhusu mali na migongano ya maslahi. Katika hili, Sekretarieti ina nafasi ya kukagua na kujiridhisha juu ya uhalali wa matamko hayo.

Pia, Sekretarieti inapokea malalamiko kuhusiana na kukiukwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Ili kufanya hivyo, itachunguza, au kumhoji, mtu yeyote ili kusaidia uchunguzi, au uamuzi wa suala lililoko mbele yao. Sekretarieti, kwa maelekezo ya Kamishna wa Tume na kwa amri ya Mahakama, inaweza kuchunguza taarifa za kibenki za kiongozi yeyote wa umma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataajiri maofisa wa Sekretarieti na kuwaapisha viapo vya usiri wanaposikiliza mashauri ya maadili ya viongozi wa umma.

Maofisa wa Sekretarieti wana kinga wanapofanya kazi zao, kwa nia njema. 

SOMA ZAIDI: Teuzi za Watu Wasio Waadilifu Zinawapa Motisha Viongozi Kutumia Vibaya Ofisi za Umma

Ni kosa kuwazuia kufanya kazi yao, au kuwapa taarifa za uongo, na adhabu yake ni faini isiyopungua Shilingi milioni moja ama kifungo cha mwaka mmoja jela, au vyote.

Malalamiko

Malakamiko kuhusu kukiukwa kwa maadili kwa viongozi wa umma yatawasilishwa kwa Kamishna wa Sekretarieti, kwa njia ya maandishi. Malalamiko yatakuwa na taarifa za kutosha kuhusu suala husika. Ni juu ya mlalamikaji kuweka jina, saini na anuani yake.

Malalamiko dhidi ya Mawaziri au Wakuu wa Mikoa yatawasilishwa kwa Rais kwa njia ya maandishi. Rais atatoa nakala ya malalamiko kwa mlalamikiwa – Waziri au Mkuu wa Mkoa, ambaye atatakiwa kutoa ufafanuzi ndani ya siku thelathini.

Malalamiko dhidi ya Rais yatawasilishwa kwa Kamishna. Kamishna atayawasilisha kwa Rais na kwa Spika wa Bunge – ambaye atayawasilisha katika Kamati ya Kudumu ya Bunge. Itakuwa ni juu ya Kamati ya Bunge kuchunguza na kutoa majibu.

Hata hivyo, siyo rahisi kueleweka kwamba Rais anaweza kushitakiwa. Lakini sheria imeelekeza kwamba Rais anaweza kushitakiwa Bungeni. Kukiwa na sababu ni vema kujaribu kuitumia fursa hii na kuona matokeo yake.

SOMA ZAIDI: Tusiruhusu Uholela wa Matumizi ya Mamlaka ya Kipolisi

Malalamiko dhidi ya viongozi wengine wa umma yatawasilishwa kwa Rais na Spika wa Bunge. Malalamiko kumhusu Kamishna mwenye wajibu wa kupokea na kusikiliza malalamiko yatapokelewa na Kamishna na kuwasilishwa kwa Rais.

Kama kiongozi wa umma ataona tuhuma za kimaadili dhidi yake, anaweza kutoa taarifa kwa maandishi kwa Kamishna kuomba suala lipelekwe mbele ya Baraza. Kamishna atamfahamisha Rais na Spika, na, kwa kushauriana na Mwanasheria Mkuu na Jaji Mkuu, ataunda Baraza kuchunguza tuhuma hizo.

Rais atateuwa Baraza lenye wajumbe watatu kwa kushauriana na Kamishna. Baraza litafanya kazi na kutoa taarifa kwa Kamishna ndani ya siku 45. Kamishna atawasilisha nakala kwa Rais na Spika, kwa mamlaka ya nidhamu ya kiongozi, na kiongozi mwenyewe. Aidha, Spika anatakiwa kuwasilisha nakala kwa Bunge ndani ya siku saba.

Kiuwajibikaji, Kamishna anapaswa kuwasilisha ripoti ya utendaji wa Sekretarieti, ikiwemo kesi zilizosikilizwa na Baraza, kwa Rais – ambaye ataiwasilisha Bungeni.

Tuitumie Sekretarieti

Wananchi tumekuwa wazito kuchukua hatua dhidi ya viongozi, hata pale ambapo kunakuwa na sababu chungu nzima za kufanya hivyo. Nikiangalia idadi ya mawakili wanaofanya kazi katika eneo la sheria za umma hawawiani na mahitaji yaliyopo. Niwe makhsusi katika eneo la kesi za maslahi ya umma. Tunaweza kuwahesabu.

SOMA ZAIDI: Mahakama Tanzania Isikwepe Wajibu Wake wa Kusimamia Utoaji Haki

Hivi karibuni, Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, alikaririwa akisema siku hizi hasikii kesi za maslahi ya umma. Japo kauli yake haiakisi ukweli kwa kuwa mwaka 2020 ilitungwa sheria kuzuia kesi hizo kufanyika kirahisi, ninadhani, alikuwa anatoa wito kwa wadau kuangalia suala hilo kwa upya.

Kwa wananchi hali ni mbaya zaidi. Sina takwimu lakini naamini hakuna kesi nyingi mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, licha ya kuwa na matukio mengi sana ya kimaadili.

Nilifuatilia kesi ya aliyekuwa Meya wa Ubungo Boniface Jacob dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda mbele ya Sekretarieti. Jacob alimshitaki Makonda, sasa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kwa tuhuma za kughushi vyeti. Kwamba, kwa tuhuma hiyo uadilifu wake ulikuwa matatani. Hata hivyo, kesi ile iliisha kimagumashi.

Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama cha upinzani ACT-Wazalendo, ameiandikia Sektretarieti kuhusu maadili ya viongozi. Licha ya matokeo, ni vema kuitumiaa mifumo ya uwajibikaji ili, vilevile, tupate fursa ya kuiimarisha na kuwakumbusha viongozi kuwa sisi ni jamii iliyostaarabika tangu 1961 tulipopata uhuru.

Tuna visa vingi vya viongozi ambao maadili yao yanasadikika. Tukiiandikia Sekretarieti kwa uwingi wetu tutawaamsha hata waliolala. Tutapiga kelele na kupata matokeo bila kutumia nguvu au kuumizwa.

Wito wangu ni tutumie nafasi na mamlaka yetu kama wananchi kutaka uwajibikaji na heshima ya utawala wa sheria. Tutumie mifumo na sheria zilizopo kurejesha heshima ya utumishi na uongozi wa umma.

Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts