Mtwara. Serikali imetetea uamuzi wake wa kuanzisha tahasusi za masomo ya dini kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita, huku Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akisema kwamba uamuzi huo unalenga kuwapa wanafunzi chaguzi nyingi zaidi kwenye kujiendeleza kimasomo.
Mkenda alitoa utetezi huo kwenye mahojiano maalumu aliyofanya na The Chanzo hapo Aprili 13, 2024, huku maoni ya Watanzania yakiwa yamegawanyika kuhusiana na hatua hiyo, ambapo baadhi ya wananchi wamehoji Serikali ina maslahi gani kufundisha masomo ya dini kwenye taifa linalojitambulisha kama halina dini.
“[Kufundisha] dini ni matakwa ya watu, na Serikali inaakisi matakwa ya jamii,” alisema Mkenda, ambaye pia ni Mbunge wa Rombo (Chama cha Mapinduzi – CCM). “Masomo haya yapo siyo tu Tanzania, [na] tulifanya utafiti kabisa na asilimia karibia 93 ya sampuli ambayo ilitumika [ilisema] wafundishwe.”
Mnamo Machi 20, 2024, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, alitangaza kuwa Serikali imeongeza tahasusi mpya 49 kutoka tahasuasi 16 zilizokuwepo na kufanya kuwe na jumla ya tahasusi za masomo 65 ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika kwa wanafunzi wa kidato cha tano watakaojiunga Julai mwaka huu.
Tahasusi hizo 65 ziligawanywa katika makundi saba ambayo ni tahasusi za sayansi jamii, tahasusi za lugha, tahasusi za masomo ya biashara, tahasusi za sayansi, tahasusi za michezo, tahasusi za sanaa na tahasusi za masomo ya dini.
SOMA ZAIDI: Mkenda: Vyuo Vikuu Vinahitaji Kweli Mijadala, Lakini Siyo ya Kiharakati Pekee
Baada ya kutangazwa, kundi la tahasusi za masomo ya dini ambalo ndani yake kuna tahasusi nane liliibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau mbalimbali, wengi wakihoji ni nini kiliisukuma Serikali kufikiria kuanzisha tahasusi hizo. Wengine, hata hivyo, walitetea uamuzi huo, wakisema hakuna ubaya kwa Serikali kufundisha dini.
Kwenye mahojiano yake hayo na The Chanzo yaliyofanyika pembezoni mwa hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam, Mkenda aliwatoa hofu wale wenye mashaka, akisema Serikaliinajua inachokifanya.
Mkenda alisema mchakato wa kuanzisha tahasusi hizo ulianza tangu mwaka 2010 ambapo watalaamu na watafiti wa Serikali waliliangalia suala hilo kwa kina na kupelekea kupatikana kwa tahasusi 74 lakini hazikutolewa kwa ajili ya kuanza kutumika hadi hivi sasa walipoamua kufanya hivyo.
Profesa Mkenda anadai kuwa mwanafunzi anachagua tahasusi ya kusoma baada ya kujua atafanya nini baada ya kumaliza masomo yake na katika suala hilo wapo baadhi ya wanafunzi ambao wanamalengo ya kuwa viongozi wa dini na ndiyo maana waliamua kutoa fursa hiyo.
“Hulazimishwi kuchagua [tahasusi]” Profesa Mkenda anasisistiza. “Ni hiari yako kabisa na pengine unapochagua somo la dini unaweza ukawa umejipunguzia fursa nyingi zaidi za kwenda vyuo vikuu na [wanafunzi] wanafahamu na wanaelezwa.”
SOMA ZAIDI: Shule, Vyuo Vikuu Viwaelimishe Wanafunzi Badala ya Kuwatahinisha
“Kwa sababu ukitaka kwenda kusoma baadhi ya masomo vyuo vikuu utakuta hili la dini pengine halitahesabika, litakusaidia kupata A, lakini halitakusaidia kwenda kusoma chuo kikuu.”
Kwa mujibu wa Mkenda, masomo ya dini yatafundishwa kwenye shule ambayo itakuwa na mwalimu aliyekidhi vigezo vya kufundisha somo husika kwa sababu anadai kuwa wapo baadhi ya watumishi hao ambao licha ya kusoma masomo ya kawaida lakini pia walisoma na masomo ya dini.
Hatufundishi imani
Mnamo Machi 24, 2024, akitolea ufafanuzi suala hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dodoma kuwa masomo ya dini hayatafundisha imani ya dini fulani bali maarifa na falsafa ya dini fulani, hali ambayo itatoa fursa kwa mwanafunzi kusoma somo lolote la dini.
“Tahasusi za masomo ya dini hazifanya kitu chochote kipya,” alisema Matinyi. “Kwa sababu masomo ya dini yalikuwepo katika nchi yetu katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Kilichokuwa hakipo ni kutengenezea tahasusi na kilichopo pale lile ni somo kama taaluma kwa maana kwamba hata mtu asiyekuwa na dini anaweza kufanya somo mojawapo la dini ama maarifa ya Kiislamu au ya Kikikristo.”
“Wala haizuii mwanafunzi Mkristo kufanya somo la Kiislamu au mwanafunzi wa Kiislamu kufanya somo la Kikristo kwa sababu unachojifunza pale ni maarifa, ni falsafa ya kinachofundishwa katika imani fulani. Ndiyo maana tuna Wanazuoni duniani ambao wamesomea dini mbalimbali na wanaandika masuala ya kifalsafa na kufanya tafiti. Kwa hiyo kinachofundishwa pale siyo imani ila maarifa ya hiyo dini.”
Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com. Habari hii imehaririwa na Lukelo Francis.