April 18, 2024, Bunge lilipitisha bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mwaka wa fedha 2024/25. Bajeti hii ya Trilioni 10.1 ni ongezeko la takribani Bilioni 981 kutoka kwenye bajeti ya mwaka 2023/24.
Katika mwaka huu wa fedha 2024/25, bajeti ya TAMISEMI inachukua takribani asilimia 24 ya bajeti yote ya Serikali ingawa kwa ujumla bajeti hii haina utofauti sana na bajeti ya mwaka 2023/24. Eneo ambalo limepata ongezeko kubwa ni eneo la mishahara, hasa mishahara ya watumishi wa halmashauri ambayo bajeti imeongezeka kwa takribani Bilioni 919.
Uchambuzi wetu, unatoa alama katika vipengele mbalimbali vya bajeti kwa madaraja matatu A ikionesha inaridhisha, B inaridhisha ingawa ina changamoto na C ina changamoto za msingi.
Sehemu ya kwanza tuliyoiangalia ni utoaji wa fedha, ambapo kwa miaka mitatu kati ya mwaka wa bajeti 2020/21 mpaka 2022/23, kwa wastani fedha zilizoombwa kwenye bajeti zimekuwa zikifika kwa asilimia 88. Eneo hili uchambuzi wetu unatoa alama A, japokuwa fedha hazikupelekwa zote na kumekuwa na makusanyo yanayoongezeka katika taasisi zilizo chini ya TAMISEMI.
Kwa mwaka 2022/23, taasisi chini ya TAMISEMI zilipangiwa kukusanya Trilioni 1.012, taasisi hizi ziliweza kukusanya Trilioni 1.021 ikiwa ni asilimia 101 ya ukusanyaji.
Eneo la pili tuliloangalia ni utoaji wa taarifa wa bajeti iliyopita, eneo hili tumetoa alama B, kwa sehemu kubwa bajeti imeweza kutoa mrejesho wa kutosha kuhusu vipaumbele vya bajeti 2023/24.
Eneo la tatu tuliloliangalia ni muundo wa taarifa ya bajeti, kwa mwaka huu eneo hili tunalipa alama C. kwa kulinganisha na miaka ya nyuma, muundo wa taarifa ya bajeti haujafanikiwa kuweka kiurahisi vipaumbele mbalimbali vya bajeti.
Kwa mfano, wakati bajeti zilizopita ziliweza kuonesha fedha taslimu zilizopangwa kwenda kwenye vifaa tiba, madarasa, gharama ya vitabu, zahanati; kwa sasa bajeti imeweka fedha kwa ujumla ujumla.
Jambo hili linafanya kuwa vigumu kwa mwananchi kuweza kufuatilia kipaumbele kimoja mpaka kingine kwa kutumia bajeti na hata kuelewa kiurahisi maendeleo wanayoyategemea. Moja ya eneo ambalo limeweza kuoneshwa kwa upekee ni katika ujenzi wa barabara, ambapo bajeti ya Bilioni 841 imetengwa.
Eneo la nne tuliloangalia ni baadhi ya mapungufu na changamoto zilizoonekana kwenye Wizara na namna ambavyo bajeti imeweza kukabiliana na mapungufu hayo. Katika eneo hili, uchambuzi wetu unatoa alama B.
Moja ya changamoto kubwa inayotajwa kwenye taasisi za Serikali za Mitaa ni ubadhirifu, ambapo ripoti ya CAG imeonesha baadhi ya halmashauri mfano Mpimbwe, Shinyanga zimekuwa zikikumbwa na kashfa za ubadhirifu. Taarifa ya bajeti imeweza kuonesha kuwa Wizara inalizingatia eneo hili kwa kutoa mafunzo na taratibu za kinidhamu.
Wizara inaeleza katika mwaka 2023/24 watumishi 225 walichukuliwa hatua za kinidhamu, kati yao wakurugenzi ni 13, wakuu wa idara 30, watumishi wa sekta ya ujenzi 15, sekta ya afya nane (8) na 159 wa kada nyingine.
Eneo lingine ambalo Wizara imeonesha kulifanyia kazi ni Mikopo ya asilimia 10 ya vijana, watu wenye ulemavu, wanawake na wazee. Serikali inategemewa kuanzisha utarataibu wa majaribio ya kutumia benki katika halmashauri zipatazo kumi, huku katika halmashauri zipatazo 174 utaratibu ulioboreshwa utatumika.
Katika eneo hili serikali inategemea kutoa mikopo yenye thamani ya Bilioni 227.96 ikijumuisha, shilingi bilioni 63.24 zilizotengwa na halmashauri mpaka sasa na bilioni 63.37 ambazo ni fadha za marejesho ya mikopo ambayo halmashauri imeendelea kupokea. Kiasi kingine kinatokana na makadirio ya mapato katika mwaka wa fedha 2024/25.