The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau Watia Neno Matukio ya Watoto Kujinyonga: ‘Jamii Imetelekeza Wajibu Wake’

Wanatoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwa karibu na watoto, pamoja na kusikiliza na kufanyia kazi hisia na mawazo yao.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Wito umetolewa kwa jamii kuhakikisha inakuwa karibu na watoto kwa lengo la kusikiliza na kuzifanyia kazi hisia zao ili kuweza kulimaliza tatizo la watoto kuchukua uamuzi wa kujinyonga, wakidhani hiyo ndiyo suluhu ya matatizo yanayokuwa yanawakabili kwa wakati huo. 

Aidha, halmashauri mbalimbali nchini zimeshauriwa kuongeza idadi ya vituo vya ushauri nasaha kwa ajili ya kusogeza fursa ya msaada wa kisaikolojia karibu na wananchi kwa lengo la kusaidia kutatua suala la mgandamizo wa mawazo ambalo limekuwa likiwasumbua watu wengi, kitu ambacho huwasukumua kujitoa uhai. 

Haya yote yamebainishwa na wadau mbalimbali waliozungumza na The Chanzo kufuatia utafiti wake mfupi unaoonesha kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio mengi ya watoto kujinyonga kwa sababu mbalimbali, hali ambayo si nzuri na inahitaji kuchukuliwa hatua. 

Kati ya Machi 2023 hadi Aprili 2024, The Chanzo imebaini uwepo wa matukio 13 ya watoto kujinyonga yaliyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.  

Matukio hayo yaliyothibitishwa na Jeshi la Polisi yalihusisha sababu mbalimbali, zikiwemo ugomvi na familia, mtoto kutopewa baadhi ya mahitaji, mtoto kutazama filamu za kutisha pamoja na hasira baada ya kutokubaliana na maamuzi ya wazazi. 

SOMA ZAIDI: Utajuaje Kama Mwanao Anafanyiwa Ukaliti wa Kingono?

“Kuna changamoto kwa jamii kutosikiliza hisia za mtoto,” anasema Jenipha Kalman ambaye ni mratibu wa elimu kutoka shirika lisilo la kiserikali lililojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto la C- Cema.  

“Wazazi wengi huwa tunapata mshituko pale ambapo unasikia mtoto wako amepigwa, amevuninjika, au mtoto wako amepata ajali,” anafafanua mdau huyo. “Hapo ndiyo mtu anapata mshtuko na uamsho juu ya suala la mtoto. Lakini mzazi hazingatii hisia zile mtoto anakuwa nazo. Fikiria mtoto anarudi nyumbani hana furaha, ameamua kujifungia ndani, mzazi anaona ni suala la kawaida. Hapana, hilo siyo suala la kawaida.”

“Kwa hiyo, wazazi, walezi, wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla tushirikiane wote katika kuangalia tabia za mtoto,” Kalman anashauri. “Chochote kile mtoto anachokipitia kinaanzia kwenye familia. Chochote kile ambacho mtoto anakifanya kinaanzia kwenye hisia. Kwa hiyo kama tusipozingatia hisia za mtoto tutapoteza watoto wengi sana.” 

Baltazari Komba ni MKurugenzi Mtendaji wa shirika linalotetea haki za wanawake, vijana, watoto na walemavu la Faidika Wote Pamoja (FAWOPA) kutoka mkoani Mtwara. Yeye anaeleza kuwa tatizo la watoto kujinyonga litakoma endapo kama kwenye jamii kutakuwa na vituo vingi vya ushauri nasaha ambavyo vitatumika kuwahudumia watoto wenye msongo wa mawazo. 

SOMA ZAIDI: Mzazi, Hakuna Ushahidi Kwamba Viboko Vinasaidia Katika Malezi ya Mtoto Wako

“Jamii inatakiwa kuwa na malezi yenye muongozo wa namna gani mtu anaweza kuhimiri mkandamizo wa mawazo na ni kwa namna gani anaweza kuhimili matatizo ya kisaikolojia yanapomkumba,” Komba aliiambia The Chanzo kwa njia ya simu.  

“Na kwenye halmashauri itengwe kabisa bajeti kuhakikisha kwamba hawa maafisa ustawi wa jamii wanapata majukwaa ya kuzungumza na wananchi kuhusiana na msaada wa kisaikolojia na mkandamizo wa mawazo ambao umekuwa tatizo kubwa sana kwenye jamii ambapo [watoto] wanakutana nalo na hawajui waende wapi?” aliongeza mdau huyo.

Komba anaendelea kusema, “Serikali yetu na wadau kama vile mashirika yasiyokuwa ya kiserikali inatakiwa kuliangalia hili kama tatizo linalokuja juu sana. Hata hivi vituo vya afya vinavyojengwa kwa wingi sana hapa nchi vinatakiwa kuwa na hiyo idara ya ushauri wa kisaikolojia kwa wananchi.”

Ripoti ya haki za bianadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2023 inaonesha haja ya watoto kuangaliwa kwenye suala la afya ya akili baada ya kubaini kuwa tatizo hilo limechanga watoto kuchukua uhai wao wenyewe. 

Ripoti hiyo ilionesha kuwa kwa mwaka huo wa 2023 matukio ya watu, hasa vijana, kujiua yaliongezeka ambapo robo ya matukio hayo yawahusisha watoto walioamua kujinyonga kwa sababu mbalimbali. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Muhimu Mzazi Kumuomba Mtoto Wake Msamaha? 

Mmomonyoko wa maadili

Kwa upande wa Sheikh Ponda Issa Ponda, ambaye ni Katibu wa Shura ya Maimamu Tanzania, ameshauri jamii kuendelea kulinda maadili mema kwa sababu  kwa sasa kuna tatizo kubwa la mmomonyoko wa maadili, suala ambalo anaamini limepelekea watoto kuona na kujifunza mambo yasiyofaa, ikiwemo jinsi ya kujitoa uhai. 

Sheikh Ponda ameenda mbali zaidi na kueleza kuwa mfumo wa maisha uliopo sasa umemsahau mtoto kwa kumuacha awe huru kuona kitu chochote, jambo ambalo anadhani halina afya kwa kwenye makuzi yao. 

“Haya mambo ya kujinyonga na mengine mengi [watoto] wanayaona na yanaoneshwa kwenye sinema kabisa,” anasema Ponda. “Kuna michezo ya kufyatua bastola na michezo ya watu kuiba [watoto wanaona].”

“Filamu kama hizo zipo kwenye jamii na watu kwa kuwa hawana maadili wanazichukua wanapeleka kwenye familia na zinaonyeshwa kwenye telesheni. Kwa hiyo, hivi ni vitu ambavyo tunatakiwa tuwe navyo makini, kwamba filamu inayokuja ikaguliwe [ili kufahamu] kwamba [filamu] hiyo inamuelekeza mtu upande gani? Kuna wenzetu wanafanya huko kwenye mataifa mengine.

“Saa nyingine [sinema hizo] zinaonyesha mtu alikuwa na msongo wa mawazo, amebanwa na maisha magumu, akajinyonga, hata vikundi vya kuigiza navyo vinacheza michezo ya namna hiyo. Kwa hivyo, ina maana kwamba haya wanayoyafanya watoto watoto wetu ni mambo ambayo wanayona katika jamii,” Sheikh Ponda anasema.


Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com. Habari hii imehaririwa na Lukelo Francis.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *