Dar es Salaam. Asasi za kiraia 21 zinazofanya kazi za utetezi wa haki za binadamu na ardhi zimeitaka Serikali kusitisha mara moja operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu wakazi wa vijiji nane jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na badala yake ipeleke haraka misaada ya kibinadamu kwa familia zilizoathirika.
Katika tamko lao hilo lililotolewa Mei 9, 2024, asasi hizo za kiraia zimeeleza kuwa operesheni iliyoendeshwa na Serikali kwa kutumia Jeshi la Polisi, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, imegubikwa na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu vilivyopelekea wananchi kuachwa bila makazi.
Tamko hilo linakuja siku chache tangu kuripotiwa kwa zoezi la kuvunja nyumba za wakazi jirani na uwanja wa ndege wa KIA kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni sehemu ya zoezi la upanuzi wa uwanja huo wa kimataifa wa ndege.
Katika operesheni hiyo zimeripotiwa taarifa za wananchi kuachwa bila makazi, huku baadhi ya wazazi wakiwa hawajui watawahifadhi wapi watoto wao wadogo achilia mbali mali walizopoteza.
Mgogoro huu unahusu wananchi takribani 22,000 kutoka vijiji vya Majengo, Malula, Samaria, Sanya Station, Mtakuja, Tindigani, Chemka na Kaloleni ambavyo vipo katika wilaya za Hai, mkoa wa Kilimanjaro na wilaya ya Meru, mkoani Arusha.
Licha ya vijiji hivyo kuwepo kisheria tangu miaka ya 1970 na kuwepo kwa ushahidi wa makazi ya wananchi hata kabla ya ujenzi wa uwanja wa KIA mwaka 1971, kwa nyakati tofauti wakazi wa vijiji hivyo wamekuwa wakiambiwa kuwa ni wavamizi na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Wakati Serikali na KIA ikiwaona wananchi wa vijiji hivyo nane kuwa ni wavamizi wa eneo hilo, wananchi hao waliovunjiwa nyumba wanaeleza kuwa uwanja huo wa ndege ndiyo umewakuta na siyo kama inavyosemekana kuwa wao ni wavamizi
Amos Nassar, mkazi wa kata ya KIA, akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam TV mara baada ya kuvunjiwa nyumba yake, Mei 8, 2024, alieleza kuwa amekuwepo katika eneo hilo analotakiwa ahame kwa miaka zaidi ya 60.
“Kwa sasa najiendea tu,” alisema Amos alipohojiwa na kituo hiko cha televisheni. “Nikatafute mahali pa kulala na hizo mbuzi zangu nachunga.”
Chimbuko la mgogoro
Mwaka 1969 wakati Serikali ya awamu ya kwanza ilipoamua kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa kanda ya kaskazini kwa ajili ya kukuza utalii kwenye kanda hiyo, ilikutana na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi ambao wengi walikuwa ni jamii ya wafugaji kwenye eneo ulipo uwanja wa KIA leo.
SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro
Hatua hiyo ilimlazimu Rais wa wakati huo, hayati Julius Kambarage Nyerere, kwenda kuzungumza na wananchi hao na kuzihakikishia jamii hizo za wafugaji kuwa ardhi yao itakuwa salama, hivyo Serikali ilichukuwa hekari 460 tu kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa KIA uliozinduliwa mwaka 1971, na eneo lilobaki liliendelea kuwa eneo la makazi ya wananchi ambao wengi wao walikuwa wafugaji.
Chokochoko za kuibuka kwa mgogoro tena zilianza Agosti 1985 kufuatia kamati za ushauri wa mkoa wa Kilimanjaro na Arusha kushauri eneo la uwanja wa KIA kutanuliwa, huku wakazi waliozunguka uwanja huo wakituhumiwa kuwa ni wavamizi.
Hali ya kutoelewana baina ya wakazi hao wanaouzunguka uwanja wa KIA na Serikali iliendelea, na kwa mara kadhaa sakata hilo likitua Bungeni na wakati mwingine viongozi wa kisiasa na wa Serikali kwenda kuzungumza na wananchi hao.
Sura mpya ya mgogoro
Imebainishwa kuwa mgogoro baina ya KIA na wananchi wa vijiji hivyo ulichukua sura mpya kuanzia mwaka 2022 baada ya kampuni iliyokuwa inaendesha uwanja wa KIA ya Kilimanjaro Airport Development Company (KADCO) na Kampuni ya Viwanja vya Ndege ya Oman (Oman Airports) kuingia mkataba wa uendelezaji wa uwanja wa KIA, wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Oman Juni 12 mpaka 14, 2022.
Miezi mitatu baada ya kusainiwa kwa mkataba huo zoezi la upandaji wa vigingi vya mipaka lilifanywa na Serikali, huku viongozi wa Serikali, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakidaiwa kufanya ziara za mara kwa mara kuwataka wananchi hao wahame huku akitoa ahadi za kifuta jasho.
Jambo lililowaacha na mshangao wadau wa haki za binadamu ni eneo la upanuzi wa uwanja huo kutoka hekta 460 mpaka hekta 11,447.7. Wadau hao wanashindwa kuelewa lengo la upanuzi huo ikizingatiwa kwamba uwanja wa ndege mkubwa duniani unaohudumia watu wengi zaidi wa Hartsfield Jackson Atlanta nchini Marekani una eneo la hekta 1,902.
SOMA ZAIDI: CCM Yadaiwa Kupora Ardhi ya Wanakijiji Kilimanjaro
Zoezi la upandaji vigingi lilifuatiwa na zoezi la kutoa ‘kifuta machozi’ ambacho Serikali ilidai ni fidia kwa wakazi wa vijiji hivyo. Katika uchunguzi uliofanywa na asasi za kiraia zinazofanya kazi kwenye eneo la haki ardhi umegundua kwamba zipo familia zililipwa fedha ndogo sana licha ya kumiliki ardhi, wakitolea mfano familia yenye eneo la takribani ekari tano kulipwa shilingi 5,778.
Christan Masyaa, ambaye ni mmoja wa wananchi waliovunjiwa nyumba na kuhojiwa na vyombo vya habari amesema pamoja na ahadi iliyotolewa na Serikali kwamba watalipwa fidia, yeye hajapokea chochote na nyumba yake imevunjwa.
“Serikali wamenivunjia nyumba na bado hawajanifidia,” alisema mama huyo ambaye anaonekana hana nuru tena usoni mwake. “Walitakiwa walipe makaburi, miti, nyumba ili tuweze kutafuta eneo la kuishi.”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema kuwa nyumba zinazovunjwa ni zile za wananchi waliolipwa fidia na kuhama katika makazi yao, huku akidai kuwa wanaolalamika kuvunjiwa nyumba zao waache uongo akidai kwamba asilimia 96 ya wananchi wameshachukua hela ya fidia.
“Wale ambao hawajachukua kabisa, waende wakachukue hela zao,” amsema Babu. “Uwanja wa ndege unahitaji kuendelezwa na uwanja wa ndege una hati ni wa Serikali”
Kutokana na hali hiyo, asasi hizo za kiraia zimependekeza Serikali kuunda tume huru itakayochunguza ukiukwaji huo wa haki za binadamu. Asasi hizo pia zimetaka viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro na wilaya za Hai na Meru kuwajibishwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu uliotendeka.